Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada usiku wa deni haukawii kukucha.” Baada ya siku mbili za michango mizuri sana ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge, nianze hitimisho langu kwa kuahidi kuwa ingawa hapa nitajibu kwa kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala yaliyoibuliwa, lakini nikuahidi kwamba michango mingi ina tija na tunaandaa utaratibu ili tuweze kuijibu kwa maandishi michango yote ambayo imeulizwa na Waheshimiwa Wabunge. Naomba nichukue pia fursa hii niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, nitajenga matumaini katika mioyo ya Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge waniruhusu niingie katika vifua vyao ili nipunguze mazito waliyoyabeba ya changamoto mbalimbali za migogoro ya aina mbalimbali inayohusu Wizara yetu. Natambua kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa amezungumza kuhusu changamoto, ndovu akataja kwa jina lingine watu wakacheka kidogo, lakini nikuthibitishie, nitaingia katika mioyo ya kila Mbunge, kwa sababu natambua kwamba Waheshimiwa Wabunge hawa wanafanya kazi kubwa ya kuzungumzia maslahi ya wananchi wetu katika maeneo yao. Kwa hiyo niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niseme tu mambo yafuatayo kwamba wananchi wetu waliotupa heshima ya kuwa katika Bunge hili Tukufu sisi pamoja na Chama chetu Tawala, yako mambo wanayoyahitaji sisi kama Serikali tuyafanye. Kwa muda mrefu Wizara yetu hii Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miongo mingi sana wamepita Waheshimiwa Mawaziri wengi sana na kila nyakati ambazo Waheshimiwa Mawaziri wakisimama nyakati hizi za bajeti mambo mengi yanayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge imekuwa ni changamoto changamoto, changamoto kila siku ni changamoto katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, hata yale mambo ambayo yanatuletea tija katika Utalii Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyasahau hawayazungumzi kwa mapana yake, kwa sababu Wizara hii toka nyakati za Baba wa Taifa mwaka 1961 mpaka nyakati hizi za Rais wetu wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na changamoto, changamoto, changamoto. Sasa nadhani wakati umefika na lazima tuseme kwamba wakati ni sasa kuhakikisha kwamba sisi kama Wizara tunajipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba tunazimaliza changamoto zote ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumza ili tutakapokutana hapa mwakani tusizungumze tena changamoto, tuzungumze namna tutakavyoweza kukuza utalii wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge nikushukuru sana wewe, niwashukuru Maafisa pamoja na Wenyeviti wote wa Kiti chako kwa kusimamia vyema mijadala hii kuhusu Wizara hii kwa siku hizi zote mbili. Niendelee kutoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, mdogo wangu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuchambua na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea na kuchambua michango kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, lakini pia tumechambua michango ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia 57 na Mheshimiwa Mbunge mmoja amechangia kwa maandishi, jumla michango 58 tumeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujielekeza kqwenye baadhi ya hoja, chambilecho wahenga, “mcheza kwao hutuzwa”. Napenda kusema hapa nakuunga mkono Watanzania wenzangu kuipongeza Timu ya Yanga, lakini vile vile nimpongeze sana Rais wa Yanga, Engineer Hersi Said kwa kuendelea kuitangaza vyema nchi yetu nje ya mipaka ya Tanzania na dunia kwa ujumla kwa kushika nafasi ya pili kwenye Fainali za Kombe la Shirikisho Barani Afrika sambamba na kutoa Mfungaji Bora na Golikipa Bora wa mashindano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua hii imeiwezesha brand ya Tanzania kuzidi kujulikana katika mataifa mbalimbali na hivyo kuchochea hamasa za watalii na kutoa mataifa mbalimbali kwenye vivutio vyetu Tanzania. Kwa ushindi huo Wizara yangu inatoa offer, inatoa offer kwa wachezaji na viongozi wa klabu ya Young African baada ya kazi hiyo ngumu tutaratibu pamoja na viongozi wao kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu tutaufanya watakapokuwa mapumziko. Sambamba na hilo, naomba nichukue fursa hii kuwakaribisha mashabiki wote wa Yanga kwenda kujumuika pamoja na wachezaji wao katika safari hiyo katika tarehe itakayotangazwa na utaratibu utakaowekwa ziara hiyo tunaomba ipendekezwe iitwe kwa jina la The CAf Finalist Royal Tour. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi na shukrani maalum ziende kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kujitoa kwake tumeeleza humu jinsi filamu ya Tanzania the Royal Tour ilivyoleta mafanikio lukuki hapa nchini, lakini siyo tu kwa watalii kuongezeka lakini pia nchi yetu sasa ni kivutio cha mastaa mbalimbali na watu mashuhuri duniani wamekuwa wakija hapa nchini na wanaendelea kujakutokana na juhudi hizi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wageni wetu hawa wanapenda faragha yao na tunazingatia hilo mara zote lakini wapo ambao wameridhia jamii yetu iweze kutambua Tanzania kutuunga mkono kwa kupitia filamu ya Royal Tour, hivi ninavyozungumza leo hii naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba hivi juzi tumepokea wageni kutoka nchini Marekani; mtoto wa aliyekuwa Rais wa Marekani, mtoto wake na familia yake wapo hapa nchini Tanzania, bwana Donald Trump Junior yupo hapa nchini Tanzania amekuja kuunga mkono jitihada za Serikali na atakuwepo nchini kwa mapumziko ya siku kadhaa na nitamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aridhie ili kesho niweze kukutana naye kuzungumza ni namna gani wanaweza kutuendeleza katika biashara hii ya utalii hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya hoja za Kamati na Wabunge; Kamati yako lakini na Wabunge wengi zaidi ya 14 wakiwemo Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Tecla Mohamedi Ungele, Jacqueline Ngonyani Msongozi, Jeremiah Mrimi Amsabi, Simon Songe, Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Deus Clement Sangu.

SPIKA: Samahani Mheshimiwa Waziri, hawa ni akina nani?

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, hawa ni Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye baadhi ya maeneo.

SPIKA: Kanuni zetu haziruhusu. Ahsante sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, tunao Wabunge wengi waliochangia kwenye baadhi ya hoja na wamechangia kwa hisia sana. Nichukue fursa hii kwanza kabisa kusema mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zetu, TANAPA, TAWA, Ngorongoro, pamoja na TFS zinaongozwa na Jeshi la Uhifadhi, Jeshi Usu. Jeshi hili la Uhifadhi ni Jeshi ambalo limepewa mafunzo ya kutosha, Jeshi hili la Uhifadhi ukiangalia utaratibu wa kijeshi na Waziri wa Ulinzi angekuwepo hapa angenisaidia, ni jeshi la pili baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kama sijakosea.

Mheshimiwa Spika, Jeshi hili lina mafunzo ya kutosha, kwanza niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao pengine wanaweza kujaribu ku-undermine uwezo wa jeshi hili basi watambue kwamba jeshi hili ni jeshi ambalo lina mafunzo ya kutosha na kwa kuwa jeshi hili lina mafunzo ya kutosha, kero za Wabunge hapa kila aliyekuwa anasimama anazungumzia kuhusu ndovu.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi kwamba kila panapotokea wafugaji wameingia ndani ya Hifadhi, wenzetu wa Jeshi la Uhifadhi wanachukua hatua za haraka sana na kila ambapo pengine wananchi wananingia kwenye Hifadhi, Jeshi la Uhifadhi linachukua hatua za haraka sana, lakini kelele zote za Waheshimiwa Wabunge hapa ndani ya Bunge kuhusu wanyama hawa wakali kuingia kwenye maeneo ya wananchi, lazima tukiri kwamba hatua za haraka zinachelewa kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa na kwa bahati nzuri sana Jeshi la Uhifadhi chini ya TANAPA, TAWA, Ngorongoro linaongozwa na Majenerali wa Jeshi ambao walifanya kazi kubwa sana kwenye Taifa hili, kazi nzito sana kwenye Taifa hili, tunatambua tuna kazi kubwa ya kufanya kuendelea kuliimarisha jeshi hili, lakini naomba nitoe maelekezo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, nimekwishakaa na Viongozi wa maeneo haya wa Ngorongoro TAWA, TANAPA na TFS lakini pia nimeshawakutanisha na viongozi mbalimbali wa Chama Tawala wanaotoka kwenye maeneo ya wananchi, tumekwishakubaliana kwamba Kiongozi yoyote wa Uhifadhi katika eneo lake iwapo Waheshimiwa Wabunge wataendelea kupiga kelele kwenye maeneo hayo na kiongozi huyo akaendelea kubaki ofisini, maana yake ni kwamba yule Kiongozi wa Taasisi ile mimi nitashughulika naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishakubalina, kila mmoja wetu afanye kazi zake, kama tunaweza kuchukua hatua za haraka dhidi ya wafugaji wanaoingia ndani ya Hifadhi vilevile tuchukue hatua za haraka kuwaondoa wanyama wakali katika maeneo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo zone zetu za kila Hifadhi na tumekwisha kufanya kikao. Nikuthibitishie mimi ni tofauti kidogo na ninaposema namaanisha, kiongozi yoyote wa Uhifadhi ambaye yupo kwenye eneo lake na kunakuwepo na kelele za wananchi yeye kushindwa kushuka kwa wananchi kukaa na kuzungumza nao, maana yake huyo hanifai katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nichukue fursa hii kwanza kutoa pole kwa wananchi wote ambao wamepata madhara mbalimbali katika maeneo yote na ndio maana ningetamani sana hata kuwataja Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wamezungumza kwa uchungu sana, kila Mheshimiwa Mbunge kwa namna alivyozungumza na hatuna sababu ya kuwa na changamoto hizi hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tunavyo vitengo vyetu mbalimbali tunatambua panapokuwepo na changamoto mara nyingi Wizara ya Maliasili na Utalii ndio inayoguswa lakini tunajipanga vizuri na wenzetu wa TAMISEMI kwa sababu katika kila Wilaya nchi hii tunao Maafisa Wanyamapori, lakini swali la kujiuliza ni kwamba hawa Maafisa Wanyamapori kila wilaya wanafanya kazi gani? Kwa sababu hata tukiwauliza Waheshimiwa Wabunge hapa pengine hata hawawajui Maafisa Wanyamapori kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo misingi ambayo Baba wa Taifa aliianzisha. Katika nyakati za Uhuru tulikuwa na Afisa Wanyamapori kila Kata na kwenye vijiji, lakini hapo katikati mambo kidogo yakabadilika na leo hii hatuna Maafisa Wanyamapori kwenye vijiji na kwenye Kata na kwenye Tarafa, lakini hili tumekwishalizungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishatuagiza ili tuandae mpango mkakati ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kupata Maafisa Wanyamapori katika meneo yetu hayo ya vijiji na maeneo ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosisitiza hapa, tutamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na wenzetu tutakaa ili tuweze kuzungumza, kuona uwezekano hawa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya warudishwe kwenye Wizara hii ili niweze kuwashughulikia vizuri katika maeneo yao. Tunatambua yako maeneo Maafisa Wanyamapori wanafanya kazi nzuri sana, kwa mfano kule Tunduru aliyekuwepo Afisa Wanyamapori akifanya kazi nzuri sana lakini baadaye wakamhamisha, Mbunge wa Tunduru analalamika, sababu za kumhamisha mambo tu ya hovyohovyo ambayo hayaeleweki. Tumemwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naye ameridhia kuhakikisha kwamba Afisa yule aliyehamishwa kutoka Tunduru, arudi Tunduru akafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba changamoto hii imeleta vilio kwa wananchi katika baadhi ya maeneo na hata leo tunapozungumza kule Bariadi kuna mwananchi amekanyagwa na tembo muda tunapozungumza kule Bariadi. Kwa hiyo tunatoa pole kwa wananchi, lakini pia tunatambua kwamba changamoto hii ya wanyama wakali inaleta changamoto pia hata mpaka kwetu. Hivi karibuni wiki mbili zilizopita askari wetu kule Ngorongoro amechomwa na ndovu na kufariki. Kwa hiyo ni changamoto ambayo ipo pande zote mbili, lakini tumeandaa mpango mkakati wa kuona ni namna gani tunakwenda kumaliza changamoto hizi, mpango wa miaka kumi (2020 mpaka 2024).

Mheshimiwa Spika, mpango huu mkakati umeainisha hatua za muda mfupi na hatua za muda mrefu ambazo tutakwenda kupambana ili kuweza kuhakikisha kwamba changamoto hizi tumezimaliza. Aidha nichukue fursa hii kama ambavyo nimesema kuwaomba wenzangu wakati huu utakuwa mgumu kidogo katika Wizara hii, tunataka kila mmoja wetu afanye kazi kwa uweledi. Kila mmoja wetu afanye kazi kwa uweledi huku tukitanguliza ubinadamu mbele, nadhani hii lugha imeeleweka vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe Maafisa wetu katika maeneo mbalimbali tufanye kazi kwa uweledi tufanye kazi usiku na mchana na kauli yangu hapa ni kwamba hawa ni Askari Jeshi, maana yake tunataka kuona wakifanya kazi usiku na mchana, wakifanya kazi wakati wa jua, wakifanya kazi wakati wa mvua kuhakikisha kwamba wamekwenda kumaliza tatizo na migogoro mbalimbali ya wanyama wakali kuingia katika maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, lipo eneo lingine lenye migogoro, kati ya maeneo ya Hifadhi. Suala hili pia limegusiwa na Kamati ya Bunge lako Tukufu pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumza jambo hili. Wewe mwenyewe ni shahidi kwamba Baraza la Mawaziri liliwateua Waheshimiwa Mawaziri Nane kwenda kuzunguka na kupita katika maeneo mbalimbali. Nakiri kabisa kwamba Waheshimiwa Wabunge hapa wamezungumza, yako maeneo ambapo pengine tunapaswa kuendelea kupita zaidi ili tuzungumze na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu, Baraza la Mawaziri ni kikao cha juu kabisa cha Serikali cha maamuzi. Sasa wapo Waheshimiwa Wabunge hapa wamelalamika kwamba yapo maeneo ambapo hakuna migogoro, wananchi wameridhia yale maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amekwishasema hapa, sasa kama maamuzi yamefanywa na Baraza la Mawaziri na kuna watendaji katika Serikali kule chini ambao walipaswa kutoa matamko na mpaka leo hii hawajatoa matamko, maana yake wanakinzana na maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ni Mheshimiwa Rais mwenyewe, maamuzi haya yamekwishafanywa, yako maeneo ambapo hakuna migogoro, ni jukumu la wale watendaji waliokasimiwa mamlaka na Mheshimiwa Rais, kutoa matamko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tumetoa mpaka tarehe 28 Mwezi wa Sita ili Waheshimiwa wanaohusika kwenye maeneo yao, yale yasiokuwa na migogoro kutoa matamko mara moja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amekwishalizungumza hili. Yako maeneo ambapo Baraza la Mawaziri limerejesha maeneo kwa wananchi. Kwa hiyo, sababu hii tunawataka wale wanaohusika watoe maelekezo ili yale matamko yaende yakawasaidie wananchi kwa sababu Mheshimiwa Rais ameridhia kwenda kuwagawia maeneo yale wananchi. Kwa hiyo, niwaombe waliokasimiwa mamlaka maeneo hayo kuhakikisha kwamba wamelitekeleza eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni tuhuma za askari wa uhifadhi kutumia nguvu na ubabe na mabavu. Baadhi ya Wabunge walizungumza hili, wamechangia katika eneo hili, naomba nisiwataje kwa misingi ya kanuni, wameeleza malalamiko kuhusu eneo hili na niwathibitishie tumekubaliana kufanya kazi kwa uweledi.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri ngoja nikuweke huru, ukiorodhesha ndio kanuni inakatakaza, kama unamjibu Mbunge na hoja yake mahususi huyo uliyemchagua inaruhusiwa, yaani vile ulivyokuwa unaorodhesha Wabunge waliochangia ndio kanuni inakataza. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Wabunge wamezungumza hivi kwamba kuna matumizi ya mabavu lakini nichukue fursa hii kama ambavyo nimesema, ndani ya hifadhi zetu kuna mengi. Tunao pia wafugaji ambao wanaingia ndani ya hifadhi na silaha za moto, lakini pia tunao watu wanaoingia na silaha za moto ndani ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mambo mengine uridhie tu nisiyazungumze hapa, lakini nimepokea hoja hii ambayo imezungumzwa na Mheshimiwa Kasheku Musukuma pamoja na Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, akituomba twende kufanya mapitio ya Sheria ya Uanzishwaji la Jeshi la Uhifadhi na nimtaarifu kwamba Wizara yetu inaendelea kufanya reform kubwa sana. Tunaendelea kufanya mapinduzi makubwa sana kwenye sekta zetu zote na nimtaarifu tu kwamba hakuna mlango utakaobaki bila kufunguliwa katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwishaanza kufanya mapitio ya sheria mbalimbali, tumekwishaanza kufanya mapitio ya kanuni mbalimbali, zipo kanuni ambazo zinaingiliana, zipo kanuni ambazo zinakinzana, lakini zipo kanuni ambazo hazitoi tafsiri sahihi iliyotolewa na sheria. Kwa hiyo, niwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tutakwenda kulipitia na niko tayari baada ya Bunge hili nitakaa na Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi pamoja na Mheshimiwa Ally Juma Makoa pamoja na Mheshimiwa Festo Richard Sanga na Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah ili niweze kupata ushahidi wa yale mambo ambayo wameyazungumza kuhusu askari ambao wanafanya vitendo kinyume na utaratibu wa Jeshi la Uhifadhi na iwapo nitapokea ushahidi huo tutachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutachukua hatua pale ambapo tunaona kabisa kuna vitendo vya hovyo vya uonevu, tutachukua hatua dhidi ya askari wote ambao wanafanya vitendo hivyo. Pia nilitaarifu tu Bunge lako Tukufu kwamba tunaendelea na vikao na pengine tarehe 11, 12 tutafanya vikao na Wenyeviti wa Bodi TANAPA, Ngorongoro, TAWA pamoja na TFS; ili tuweze kujadiliana kwa pamoja kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa jeshi hili la uhifadhi. Ili tuweze kujiridhisha katika maeneo yenye mapungufu na tuweze kuyarekebisha katika maeneo hayo. Niwaahidi tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tutakapokutana hapa mwakani haya mapungufu yote itakuwa ni makofi tu na furaha kwa kweli. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mingi katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mifugo kutaifishwa na kutozwa faini. Kwa hotuba yangu kuu nilinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akitoa hotuba ya Arusha Manifesto ambapo alisisitiza kwamba uhifadhi ni lazima tuamue. Sisi kama Taifa ni lazima tuamue na lazima tuseme ukweli kwamba kuna haja ya kulinda hifadhi zetu. Mheshimiwa Baba wa Taifa alisema kwamba, Taifa lolote bila uhifadhi si Taifa na akayaomba Mataifa mbalimbali kuhakikisha kwamba tunashirikiana nao katika uhifadhi. Hivyo, naomba nisisitize kwamba tuna kila sababu ya kulinda hifadhi zetu kwa ajili ya vizazi vya leo na vizazi vya kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutambue tu kwamba hifadhi zetu zinachangia katika pato la kigeni zaidi ya asilimia 25 pamoja na kwamba kiasi hiki ni kidogo sana lakini lazima tukiri kwamba kwenye mchango katika Pato la Taifa ni karibu asilimia 21 na kwenye fedha za kigeni ni asilimia 25 naomba nirekebishe hilo kidogo. Kwa hiyo, tuna kila sababu ni kwa nini tuzilinde hifadhi hizi na niwaombe Waheshimiwa Wabunge pale ambapo tunajadili kuhusu uhifadhi basi kila mmoja wetu arejee kwenye kauli ya Baba wa Taifa aliyoitoa wakati ule wa Arusha akitoa hotuba yake kwenye Arusha Manifesto.

Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize hapa tena, kama Taifa ni lazima tukubali kwamba tunazo sheria, tunazo kanuni na sheria hizi kwa mfano sheria kuhusu TANAPA zimetoa miongozo za kutaifisha mifugo baada ya maamuzi ya Mahakama na kama kuna ushahidi wowote kwamba kuna afisa yeyote anataifisha mifugo bila uamuzi wa Mahakama, basi nipewe taarifa hizo ili tuweze kuzifanyia kazi mara moja.

Mheshimiwa Spika, utaratibu uliopo ni kwamba Mahakama ndio hutoa maamuzi wakati wa utaifishaji wa mifugo kwa mujibu wa sheria hizi. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kama wana vielelezo vya ziada, basi waweze kunipatia ili tuweze kuona ni namna gani tutaweza kuchukua hatua katika maeneo ambapo watendaji wetu wamekuwa wakitenda mambo ambayo ni ya utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na sheria nyingine suala hili pia limechangiwa na Kamati pamoja na Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso. Nitoe tu taarifa kuwa marekebisho ya utungaji wa sheria mpya hizi za kuzipa mamlaka zaidi taasisi hizi, zimefika hatua nzuri. Tunaendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kuwa na subira kwa sababu tunaendelea kufanya mapitio na hivi karibuni tutawashirikisha wadau ili tuweze kukamilisha urekebishwaji wa sheria hizi ili kuweza kutoa mamlaka lakini pia sheria ambazo zitaenda kusaidia katika uhifadhi wa eneo letu la Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kukamilishwa kwa zoezi la Ngorongoro; nichukue fursa hii kuishukuru sana Kamati, lakini pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwenye eneo hili. Jukumu la Serikali kwa misingi ya Ibara ya nane ni ustawi wa wananchi lakini kama inavyofahamika kwamba Serikali inafanya kazi pia kwa kupita utekelezaji wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ibara ya 67 imezungumzia kwa kina sana kuhusu uhifadhi, lakini namna ambavyo tuna kazi kubwa ya kuustawisha ustawi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba, suala la Ngorongoro limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge lakini nataka niwaahidi hapa kwamba wakati natoa hoja hapa Bungeni siku ya Ijumaa nilizungumza hili kwa kina kabisa na sisi kama Serikali hatutarudi nyuma, tunatambua kwamba tunao baadhi yetu wakishirikiana na vijana wengine wa Mataifa ya nje. Tena vijana hawa wa Mataifa ya nje ndio wamekuwa wengi sana. Wakienda huko wakizunguka zunguka kwenye baadhi ya maeneo mbalimbali, Mahakama za nje ya Nchi, Mahakama za Ulaya na maeneo mengine wakijaribu kututekenya. Nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu hatutarudi nyuma kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawashukuru sana Watanzania wa Ngorongoro ambao wameridhia wenyewe kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda kwenye maeneo mengine. Sisi kama Wizara tutaendelea kupitia maelekezo ambayo Kamati imetoa. Tutaendelea kutekeleza maelekezo ambayo Waheshimiwa Wabunge wametushauri kwenye Bunge hili Tukufu ili tuhakikishe kwamba utekelezaji wa jambo hili unatekelezwa, lakini tunatambua kwamba tunaendelea kufanya mashauriano na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba jambo hili tumelitekeleza kama ambavyo tumeahidi mbele ya Bunge Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni mikakati ya kutangaza utalii. Kamati ya Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza sana kwa kina jambo hili, lakini pia katika hotuba yangu ya awali niliweka hadharani mikakati 10 ya kutangaza utalii ikiwa ni pamoja na ubunifu na teknolojia, ambavyo vitaongoza katika mchakato huu wa kutangaza utalii.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumza sana kuhusu hifadhi, lakini hatujazungumzia sana kuhusu utalii. Nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe kwa kulianza jambo hili. Niwashukuru Watanzania, niwashukuru pia wadau mbalimbali wa utalii ambao kwa kipindi kirefu sana wamefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana ya kutangaza utalii nje ya mipaka ya Tanzania lakini sisi kama Serikali sasa tumekwishalianza jambo hili. Nichukue fursa hii kuwaomba wawakilishi, Mabalozi wetu waliopo katika maeneo mbalimbali kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, tunazipongeza Balozi mbalimbali ambazo zinafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. Balozi wetu kila Nchini, Balozi wetu Nchini Afrika ya Kusini na maeneo mengine wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa, kama jambo hili likishikwa na kila Mtanzania, kila mwananchi wa Tanzania akitoka akazungumza mazuri kuhusu utalii, kuzungumza mazuri kuhusu Nchi yetu, Baba wa Taifa ameturithisha mambo makubwa, mambo mazuri amani na utulivu, lakini Taifa letu lipo katika eneo jiografia ambayo hakuna popote Afrika. Tunaamini kabisa Mwenyezi Mungu ametupa akili, ametupa na uwezo wakati ni sasa, kila Mtanzania kutoka kuzungumzia mazuri kuhusu Taifa letu. Sisi kama Wizara pia tayari tumekwishaanza mazungumzo na wenzetu ta Tripadvisor tipo advisor wenzetu wa Expedia lakini pia tunaendelea na mazungumzo na wadau mbalimbali ambao wao wana mchango mkubwa sana katika Sekta hii ya Utalii. Pia tunaendelea kuwakaribisha wadau katika Sekta ya Utalii walioko kwenye Mataifa mbalimbali duniani ambao tayari wamekwishaanza kuja kutoka China na maeneo mengine duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nikuombe hotuba yangu hii iingie kwenye Hansard ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya vizazi vya leo na vizazi vya kesho.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ufafanuzi nilioutoa pamoja na maelezo mengi ambayo nimeyazungumza na kwa sababu ya muda, naomba sasa baadhi ya hoja nitaziwasilisha kwa ufafanuzi wa hoja nyingine kwa maandishi, lakini natambua hapa kwamba wapo Wabunge wakiwemo Wabunge wa Mbarali, Ngorongoro, Serengeti, Mheshimiwa Kakunda na wengine wote waliomba tufike kwenye maeneo yao na wengine ambao sijawataja kule Nachingwea kule kwa ndugu zangu Kusini na maeneo mengine, kote nitafika kwa ajili ya kupitia na kuzungumza na wananchi ili tuweze kufanya kazi hii ambayo tumekabidhiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa ufafanuzi huo na majibu yote ya hoja niliyowasilisha na mengine nitakayowasilisha kwa maandishi, naomba yaingie kwenye Hansard ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.