Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameendelea kutulinda hadi ameweza kutufikisha siku hii ya leo ambapo tunakwenda kuhitimisha Bajeti yetu ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele wa kuhakikisha kwamba uhifadhi na dhamira yake kuu ya kuendeleza utalii inazingatiwa katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwapongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wanaendelea kuipigania sekta hii ukizingatia kwenye masuala mazima ya uhifadhi wa mazingira, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba migogoro mbalimbali iliyokuwa kwenye sekta yetu hii ameendelea kuisimamia na kuitatua kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipokupongeza wewe kwa uthubutu ambao umeuonesha kama mwanamke mwenzetu. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu kwa harakati hii unayoiendea, tuna imani na wewe na tunaamini ushindi unarudi Tanzania. Tunakuombea sana na Mwenyezi Mungu akakufanikishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa moyo wa dhati kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na nimpongeze kwa namna ambavyo ameipokea Wizara lakini kwa jinsi ambavyo ameipokea Wizara lakini kwa jinsi ambavyo ameichukua kwa muda mfupi na kuielewa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ina changamoto nyingi sana, lakini kwa muda mfupi tayari tumekwishaanza kuiona nuru na Waheshimiwa Wabunge tayari wameonesha kwamba wanakwenda kushirikiana na sisi kwa nguvu zote. Niendelee kumuahidi Bosi wangu kwamba tutashirikiana vizuri na nitampa ushikiano wa kutosha kuhakikisha kwamba Wizara hii tunaipigania na kuivusha hapa ilipo na tunaipeleka mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii ya dhati kabisa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge lakini niwapongeze sana kwa namna ambavyo wametupa ushauri, kwa namna ambavyo wametupa maelekezo, lakini kikubwa wametuonesha wapi tulipo.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa nini? Unapokuwa umevaa nguo yako unaweza ukaona umevaa vizuri na umependeza, lakini ukikutana na mwenzio akakwambia hapa kuna doa huyo anakupenda sana. Vile vile, sisi tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wametuonesha ni namna gani tunapaswa kwenda. Niwaahidi kabisa kwa moyo wa dhati kwamba, yale yote ambayo wametuelekeza, wametushauri na yale ambayo wametupatia kama mapendekezo tumepokea na tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi ya uhifadhi na hususani kulinda rasilimali za Taifa ni kazi kubwa sana na inahitaji ushirikiano wa kutosha. Kuna milima na mabonde, hizi rasilimali tulizonazo tunazozilinda, tunazitunza si rasilimali za mzaha. Tunakutana na milima, mabonde na changamoto nyingi, lakini tunaamini kwa maelekezo waliyotupatia Waheshimiwa Wabunge na kwa namna tunavyokwenda kushirikiana na wananchi kuzungumza, kushuka nao huko chini ili tukae nao kwa pamoja tutahakikisha kwamba migogoro mingi tunakwenda kuipunguza ama kuimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta yetu hii inategemewa na sekta nyingi. Ukiangalia katika maliasili hatuhifadhi wanyamapori peke yake. Hatuhifadhi kwa ajili ya utalii, lakini ndani ya sekta hii kuna sekta nyingi zinaitegemea. Sekta ya nishati, usipokuwa na eneo maalum ulilohifadhi vyanzo vya maji na kadhalika hakika sekta ya nishati haiwezi kuendelea. Vilevile tuna sekta ya mifugo, sekta ya kilimo, tuna maji, mazingira na kwenye mazao pia tuna uchavushaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunatunza haya maeno sio kwa ajili ya kuendeleza utalii peke yake ni kwa sababu tunaishi na uhai wetu unategemea sana maeneo hayo. Kwa hiyo, ningependa hili tulielewe sisi kama wawakilishi wa wananchi kwamba maeneo haya tunayatunza kwa ajili ya Watanzania wote, ni kwa ajili ya maslahi yetu wote ni kwa ajili ya uhai wetu wote Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la migogoro Waheshimiwa wameliongelea. Natambua kwamba Mheshimiwa Waziri atalifafanua, lakini pia kwa yale yote ambayo wametuelekeza tutaendelea kuyafanyia kazi na tunatamani sana migogoro hii iishe. Niendelee kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, uthubutu huu wa kutatua migogoro hii ni mwanamke jasiri na wa kwanza aliyeamua kutekeleza wazo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukikumbuka migogoro hii imekuwa na historia ndefu sana. Iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane ikaingia uwandani ikaanza kuibua migogoro. Hata hivyo, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa unyenyekevu mkubwa ameingia ndani akaamua yeye mwenye kuitekeleza. Ndani ya miaka miwili sasa hivi tunaelekea kutatua migogoro yote.

Mheshimiwa Spika, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais ndani ya mwaka mmoja tumezunguka na tumekwenda mkoa kwa mkoa, tumezungumza na wananchi, lakini hatuwezi kukataa mapungufu yapo, lakini tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna amabavyo anaendelea kutuelekeza na sisi tunaendelea kuahidi kwamba kwa ile migogoro ambayo bado ipo, tutashuka na tutakwenda kuzungumza na wananchi na kuhakikisha kwamba migogoro hii inakwisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mikakati mingi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuifafanua na kuielekeza katika Wizara yetu ya Maliasili na Utalii, tumeipokea. Kuna suala zima la kuimarisha Utalii wa Fukwe. Kwa sasa Wizara imejipanga kuanisha maeneo ambayo yanaweza kuwa mahususi kwa ajili ya fukwe. Tumeainisha fukwe hizi katika Mkoa wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Pwani na Tanga, lakini pia tunakwenda kuangalia maeneo ya Kanda ya Ziwa ili fukwe hizi sasa ziweze kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, pale ambapo kama walivyopendekeza Waheshimiwa Wabunge kwamba fukwe hizi zikimilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii basi itakuwa ni rahisi sana kwenye utekelezaji wa uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kuna wazo lingine limetolewa la Kiberenge (Utalii huu wa cable car). Kwa sasa hivi Wizara imeshaweka mshauri mwelekezi ambaye ameshaanza kufanya upembuzi, kupata mawazo ya wadau mbalimbali na kuangalia namna ya masuala mazima ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kupokea mawazo na ushauri kutoka kwa wadau. Muda wa utekelezaji ukifika na wadau watakapokuwa wameshatupatia mawazo ya kutosha, zao hili la utalii la cable car litakwenda kutekelezwa kwa nguvu zote. Tunaamini kwamba kwa sasa hivi asilimia 80 ya utalii tunategemea sana utalii wa hifadhi kwa maana ya wanyamapori. Kwa hiyo sasa hivi tunajikita sana katika kutanua wigo katika mazao mengine ya utalii ikiwemo utalii huu wa kiberenge (cable car).

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tumepata maoni mengi kutoka kwa Wabunge hususani suala zima la mali kale. Kwenye suala hili la malikale tumeanza kujitanua na hivi sasa ukienda hata Kilwa tumeshaanzisha utalii wa meli na sasa hivi tunapata watalii wengine kutoka nje ya nchi. Hii yote ni kuboresha maeneo mbalimbali ya kihistoria lakini wakati huo huo tunatanua wigo wa utalii.

Mheshimiwa Spika, sambamba na suala la utalii tumeendelea kuhamasisha masuala mazima ya uwekezaji. Kama ambavyo tumesikia kwamba sasa hivi Tanzania tuna vitanda 132,676. Hiki ni kiwango kidogo sana kwenye masuala mazima ya uwekezaji ukilinganisha na mataifa mengine. Kwa hiyo, tumekwishazindua investment forum lakini pia tumeendelea kuhamasisha wawekezaji mbalimbali na hata humu ndani wawekezaji wamo. Tunaendelea kuwahamasisha tujenge Hotel, lodge, tujenge maeneo ambayo watafikia watalii wetu ili tuweze kupanua wigo wa namna ya kuwahudumia wageni wetu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu miundombinu. Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana suala la miudombinu wezeshi ambayo inaweza ikasaidia utalii kufikika maeneo mbalimbali. Tumeshaanza kuboresha miundombinu hii ukizingatia tulikuwa tuna Hifadhi 16 za Taifa na sasa hivi tuna Hifadhi 22, maeneo haya yote tumeshaanza kutengeneza miundombinu ya barabara lakini pia tunaweka uwekezaji ndani yake ikiwemo kujenga lodges na hotels na hii ni maandalizi mazuri sana ya mapokezi ya wageni wanaoweza kuja katika hifadhi hizo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na suala zima la misitu hususani upandaji wa miti, lakini pia tumeanzisha mpango kabambe unaitwa “Achia Shoka Kamata Mzinga.” Huu ni mpango mahususi wa kuwezesha wenzetu wote ambao wanashughulika na suala zima la ufugaji nyuki wahakikshe kwamba ukataji wa miti tunaukomesha lakini tunafuga nyuki kwa kuachia shoka halafu tunakamata mzinga. Lengo ni kuhakikisha kwamba zao hili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: …na mazao mengine yanayotokana na nyuki yaweze kuboreshwa ama kulimwa kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri aliweza kuzindua mpango huo…

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)