Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kweli kama alivyotangulia kuzungumza Mheshimiwa Ndejembi hapa, Wizara ya Ardhi ni kiungo kati ya Wizara zile za Kimkakati katika kutatua migogoro mbalimbali hapa nchini. Katika mazingira ya kawaida Serikali iliona umuhimu wa kuwa na Timu Maalum ya Mawaziri Nane kupita katika maeneo yote ya migogoro nchini na ilitoa miongozo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, yale maeneo machache ambayo yamebaki, tunaendelea kuhangaika nayo kwa ajili ya kutatua ile migogoro. Niwape tu comfort wananchi kwamba wawe watulivu katika kipindi hiki cha kutatua hii migogoro ambayo kimsingi inakwenda kumalizika hasa kwenye hii mipaka ya hifadhi na wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya kawaida yale maoni yote ambayo nimesikia kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge yanayohusu hii migogoro ni maelekezo kimsingi tunayapokea kwa mikono miwili na tutatoa ushirikiano mkubwa sana kwa sababu maeneo mengi Wabunge wanasema hatushirikishwi, hatushirikishwi. Tunapokwenda uwandani hatuwapi taarifa lakini ukweli wana majukumu mengi sana ambayo wakati mwingine yanawatenga na zile shughuli za kiutendaji. Hata hivyo, ahadi tunayoitoa Wizara ya Ardhi…

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Pinda, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwijage.

TAARIFA

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Pinda. Jukumu muhimu la Mbunge ni maslahi ya wananchi, hakuna kazi yoyote ninayoweza kupewa na mtu yeyote zaidi ya kazi ya wapigakura wangu. Wawe wanatujulisha. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine mnakuwa hapa Dodoma na Kamati zenu zimepewa na Spika, mnashindwa kwenda majimboni Serikali inapokuwa inakwenda huko. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba sio kila Mbunge anakuwa sehemu ambayo Waziri yupo. Waziri anakwenda anafanya kazi yake, lakini hoja ya Msingi ni Mbunge kutaarifiwa ili hata yeye asipokuwepo awepo mwakilishi wake aweze kumpa mrejesho. Hata hivyo, hakuna uhalisia wa kufikiri kwamba kila Waziri anapokwenda kwenye ziara Mbunge atakuwepo, hakuna huo uhalisia. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hiyo malizia mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana huko ndiko nilikuwa naelekea. Nataka tu kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, wakati wote wa zoezi hili tutawarifu Waheshimiwa Wabunge na watuwie radhi kama huko nyuma walikuwa hawaarifiwi. Nia yetu ni kuongeza mshikamano katika kutatua migogoro ambayo inatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo kwa kweli tumwachie mtoa hoja ili aweze kwenda kufanya majumusiho ya mwisho kabisa. Ahsante. (Makofi)