Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika ni nyota wa mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ushahidi ni kwamba ameanza na mkakati wa Royal Tour mkakati unaokwenda vizuri na majibu tunayaona. Ameingia na mkakati wa kuhamasisha katika michezo ikiwa ni sehemu ya utalii na mkakati wa hamasa ya michezo umejibu na matokeo tumeyaona Algeria, timu yetu na vijana wetu wamefanya vizuri. Tunawapongeza sana, hatuna tunachowadai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juu ya michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge inayohusu suala zima linalohusianisha juu ya mifugo na hifadhi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumejipanga vema. Moja katika mipango yetu ni kuhakikisha ranch zetu za NARCO tutazitumia vema. wale wafugaji ambao wamekuwa wakihangaika sasa tunakwenda kuziboresha na tunaanza na pale Mkata ili wale wafugaji wanaoondoka katika Bonde la Mto Kilombero tutakwenda kuwapa eneo pale, ili ile mifugo isiadhirike zaidi, iweze kuingia katika eneo hili na iendelee kutoa mchango katika pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutatoka hapo tutakwenda na maeneo mengine ili kuhakikisha kwamba wafugaji wetu waweze kuwa na maeneo na ndio kitakuwa kipaumbele chetu cha kwanza kwa ajili ya aeneo hili la Serikali kwa maana ya ranch zetu.

Mheshimiwa Spika, la tatu, ni jambo maalum ambalo limezungumzwa hapa na Mheshimiwa Hawa Mwaifunga na Waheshimiwa Wabunge wengine kuhusiana na Msomela. Msomela inakwenda vizuri mno, hivi sasa tunavyozungumza tumejenga kituo kizuri cha maziwa na ili kuhakikisha kituo kile kiwe na tija tumehakikisha tumeunda ushirika wa wafugaji na ushirika ule tutakwenda kuwapa ng’ombe bora ili waweze sasa kupiganisha na ng’ombe walioko pale na kusudio letu waweze kukilisha kituo chetu lita 5,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, vile vile tumeenda kuwafunza namna ya kuwa na mashamba ya malisho yanakwenda vizuri mno. Tatu, tumeimarisha eneo la majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo. Tunayo mabwawa mawili; moja linajengwa na Wizara ya Maji na lingine tunajenga Wizara ya Mifugo na Uvuvi, yanakwenda vizuri na tutahakikisha kwamba yanakamilika ili kusudi watu wote wanaotoka Ngorongoro wanakuja pale Msomela waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji wa mifugo kwa usalama. Vile vile, kwa hakika kinakwenda kuwa kituo cha biashara ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)