Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa, Naibu Waziri Mheshimiwa Mary Francis Masanja na wataalam wa Wizara, taasisi zilizo chini ya Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye changamoto ya magugu vamizi katika mbuga zetu za wanyamapori na maeneo ya akiba, udahili wa wanafunzi kutoka nje katika Chuo cha Wanyamapori Mweka na fursa za utalii zilizopo katika jimbo la Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, ripoti za kiutafiti zilizofanyika katika Mbuga za Serengeti, Ngorongoro, Mapori Tengefu zimeonesha kwamba magugu vamizi yamesambaa katika maeneo mengi ya hifadhi za wanyamapori na mapori ya akiba yaliyoko nchini.

Mheshimiwa Spika, aina ya magugu vamizi hayo yaliyoko katika baadhi ya maeneo nimeayaorodhesha. Magugu vamizi yaliyoko Ngorongoro ni Azolla filiculoides (red water fern), Argemone mexicana (Mexican poppy), Datura stramonium (jimsonweed), Gutenbergia cordifolia, Acacia mearsii na Parthenium hysterophorus (famine weed); huko Serengeti magugu vamizi yaliyoonekana huko ni Parthenium hysterophorus, Opuntia stricta, Tithonia diversifolia, Lantana camara, Chromolaena odorata na Prosopis juliflora; huko mbuga ya wanyama ya Burigi Chato magugu vamizi yaliyopo ni Tegetes minuta na Argemone Mexicana; na huko Mahale Mountains National Park mmea uitwao Senna spectabilis (Caesalpiniaceae) umekuwa ni gugu vamizi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uvamizi wa magugu yaliyotajwa hapo juu, maisha ya wanyamapori katika maeneo mengi ya Hifadhi za Taifa yapo hatarini kwani uwepo wa magugu haya umesababisha athari nyingi, kubwa ikiwa ni kuua majani na mimea mingine inayoota karibu yake.

Mheshimiwa Spika, magugu vamizi hayo yana tabia inayoonesha kwamba yanapoota hakustawi kitu kingine kwa kuwa hufunika eneo lote na kusababisha kutoweka kwa nyasi na kuathiri malisho ya wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, hata ripoti moja ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali (CAG) ilionesha kuwepo kwa magugu vamizi katika Hifadhi ya Ngorongoro ambayo inahatarisha uwepo wa wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo hivi sasa kunatakiwa kuwe na mikakati dhabiti ili kudhibiti magugu haya kwani yanasambaa kwa kasi kubwa sana katika mbuga mbalimbali na maeneo ya akiba hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali iwe na mpango kazi maalum na iwekeze kikamilifu kwenye kudhibiti magugu vamizi ili kulinda ikolojia ya mbuga zetu ziweze kutoa huduma ya kuwapatia wanyama chakula.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka hutoa mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori na utalii. Ni chuo kimojawapo pekee chenye hadhi kubwa hapa Barani Afrika. Chuo hiki hutoa Shahada, Stashahada na Astashahada katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, chuo hiki hupokea idadi kubwa ya wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto ya kupokea wanafunzi kutoka katika baadhi ya mataifa ya Afrika kama Kenya na Msumbiji. Vigezo vilivyowekwa na NACTE vimekuwa vinazuia wanafunzi kutoka mataifa haya kujiunga na Chuo cha Mweka.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Wizara ikae na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na NACTE ili waangalie upya vigezo vya kujiunga na Chuo cha Mweka ili tuwe na muundo wa kuwasaidia wanafunzi kutoka nchi hizi wapate elimu kama walivyotumwa na nchi zao. Haifurahishi kuona mtu anatumwa na nchi yake kusoma shahada, na akifika ananyimwa fursa na kuambiwa asome stashahada. Jambo hili limekuwa siyo rafiki, na limepunguza idadi ya wanafunzi kutoka nje na kutunyima fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro ni mdau muhimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Ninasema hivyo kwa sababu Mlima Kilimanjaro na viunga vyake ni moja ya vivutio muhimu vya utalii ambavyo vimeipatia Tanzania heshima kubwa kimataifa. Ndani ya Mlima Kilimanjaro na maeneo yanayouzunguka mlima kuna vivutio vya aina mbalimbali vya kitalii.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Rais wetu alishiriki kikamilifu kwenye filamu ya Royal Tour iliyokuwa na kipengele cha kutangaza utalii ukiwepo Mlima Kilimanjaro. Kutokana na hili, ni vyema tukachukua tahadhari mapema ili watalii watakapoanza kumiminika kuja kutalii Kilimanjaro kama ambavyo imeanza kujitokeza wakutane na mazingira mazuri. Tusipofanya hivyo, watalii wakija wakikumbana na changamoto watapeleka sifa mbaya kuhusiana na eneo letu, na kuathiri idadi ya wageni watakaotembelea Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia kwenye suala la vivutio vya Mlima Kilimanjaro na umuhimu wa kutatua changamoto za vivutio hivyo ili kuwezesha watalii kufika maeneo hayo kirahisi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni imegundulika kwamba mti mrefu kuliko yote Barani Afrika ujulikanao kama Mkukusi umepatikana katika Kijiji cha Tema, Kata ya Mbokomu, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro. Mti huo ambao una urefu wa mita 81.5 upo ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA). Ugunduzi huo umeonesha pia huu ni mti wenye miaka mingi zaidi duniani kwa aina hii ya mti kwani una miaka 600.

Mheshimiwa Spika, mti huu umeupa heshima Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa jumla. Kugundulika kwa mti huo kumeongeza chachu ya watalii kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kwenda kushuhudia mti huo. Licha ya mti huu kuwa kivutio ambacho kinaweza kuiingizia Serikali fedha za kigeni, lakini changamoto iliyopo ni ugumu wa kuufikia mti huo. Ili kufika katika eneo la Mrusungu ambapo ndipo ulipo mti huo mrefu zaidi, ni safari ya kutembea kwa mguu kwa takribani muda wa saa nne kwenda na kurudi kwa kupita katika milima, mabonde, mito na makorongo.

Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hii, ninaishauri Serikali iboreshe miundombinu ya barabara ili kuweza kuufikia mti huo iwapo watalii watataka kwenda kuuona. Barabara ya kufika kwenye mti huu ni mbaya sana, na hii ni changamoto inayowafanya watalii wasitembelee eneo hili. Tunaiomba TANAPA isaidie ujenzi wa hii barabara katika mipango yao ya mwaka 2023/2024. Katika mwaka ujao wa fedha, TANAPA ina programu ya kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilometa 500, na kukarabati kilometa 10,500. Katika hizo barabara, tunaomba tusisahau barabara inayokwenda kwenye huu mti mrefu.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ihakikishe kuwa eneo hili linaendelezwa ili liwe na hadhi ya kuwa sehemu ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Vilevile ninaishauri Serikali itengeneze utaratibu wa kuhakikisha wanaokwenda kuuona mti wanalipa ada.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utahusu maporomoko ya maji Materuni au kwa jina lingine Mnambe Waterfalls. Maporomoko haya ni moja ya maporomoko ya maji katika Mto Mware, Kata ya Uru Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro. Maporomoko haya yanapatikana katika Kijiji cha Materuni pembezoni mwa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Maporomoko haya yana urefu wa zaidi ya mita 100.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kivutio cha maporomoko ya maji, eneo hili la utalii limekuwa maarufu kwani watalii wanaokwenda kuona maporomoko hupata fursa ya kutembelea shamba la kahawa na kujifunza jinsi kahawa inakuzwa, kuvunwa na kusindikwa. Watalii hupata fursa ya kujaribu kwa mkono yao kuchoma na kuandaa kikombe cha kahawa kwa kutumia njia asili ya Wachagga.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayokabili eneo hili ni ubovu wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka Mjini Moshi. Kutokana na ubovu wa barabara, watalii hupata shida kufika katika eneo hili. Changamoto za barabara katika maeneo yanayopeleka watalii kwenye vivutio vya Mlima Kilimanjaro zinatakiwa zipewe kipaumbele cha pekee na Wizara ya Maliasili na Utalii kwani wao ni wanufaika wakuu.

Ninaishauri Serikali iachane na kuzitegemea TARURA na TANROADS kwani mitandao yao ya barabara ni mingi, na hawajatoa kipaumbele kikubwa kwa barabara za jimbo langu kama zile za kupeleka watalii kupitia Umbwe Gate, Kidia VIP Route, Materuni Waterfalls, Mti Mtefu Kijiji cha Tema huko Mbokomu, Kanisa la Kibosho Singa, na maeneo mengine muhimu.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali, huu ni wakati wa kutumia michango ya Corporate Social Responsibility (CSR) unaotokana na mapato ya Mlima Kilimanjaro kutengeneza miundombinu ya barabara katika jimbo langu la Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Spika, baada ya michango yangu hapo juu, naunga mkono hoja.