Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu kwa Taifa lakini pia kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuungana na wenzangu ambao wamemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kuhamasisha utalii, lakini pia Mradi wa REGROW ambao wenzangu wameuzungumzia ni mradi ambao ni wa matumaini makubwa sana katika Sekta ya Utalii katika uwanda wa kusini mwa nchi yetu. Mradi huu ulitupa hamasa sana na ulitupa matumaini mkubwa lakini utekelezaji wake unasuasua sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo wakati Waziri akifanya majumuisho tunaomba atoe msimamo wa Serikali, nini hatma ya huu mradi wa REGROW hasa kwa wananchi ambao wamejikita katika Sekta hii ya Utalii. Sekta ya Utalii ni muhimu sana katika uhai wa Taifa lolote lile. Ajira za vijana, lakini uhifadhi endelevu wa mazingira unategemea sana shughuli za kiutalii endelevu. Naomba niungane na wenzangu ambao wanazungumza kwamba pamoja na mafanikio makubwa ambayo tumeyapata kwa idadi kubwa ya watalii katika nchi yetu, bado kuna nguvu kubwa tunapaswa kuwekeza katika suala la kutangaza vivutio vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili la kutangaza, haitoshi tu kuongeza bajeti lakini suala zima la ushirikishwaji wa wadau ni muhimu sana. Huu ni mchango wangu wa nne kwenye sekta hii na kwenye Wizara hii ya utalii. Nilizungumza kabla na naomba nirudie tena, Balozi zetu Mwanadiplomasia wa Kitanzania ndio mwanadiplomasia pekee ambaye anapaswa kujibu hoja za CAG, anapaswa kutafuta wawekezaji, anapaswa kutafuta watalii, anapaswa kuboresha mahusiano ya nchi. Hatuwezi kufika kwa sababu wanadiplomasia hawa hawajafundishwa marketing, hawajafundishwa utalii, customer care na si kazi yao ambayo imewapeleka katika vituo vya kazi huko nje.

Mheshimiwa Spika, nilizungumza, wakati umefika wa Serikali kuona namna bora ya kushirikisha taasisi mbalimbali ambazo zinajikita kwenye utalii, ku-station watu wao kwa gharama zao lakini wakapata nafasi katika balozi zetu, watu waliosomea utalii, kwa ajili ya kushughulika ku-promote utalii katika balozi zetu. Ukiuliza kwa nini tunashindwa wanakwambia sababu za kiusalama, sababu za kiusalama kwa nini wao wamekaa kwenye hizo ofisi?

Mheshimiwa Spika, hivi ni nini ambacho kinampa huyu Afisa wa Serikali ambaye ameajiriwa hadhi ya ziada kwamba usalama wa nchi uko salama kwa sababu yeye ameajiriwa? Kwa sababu yeye analipwa na Hazina? Kitu gani ambacho kinawafanya kuamini kwamba sekta binafsi sio wazalendo na kuwakaribisha ndani ya balozi zetu ku-promote utalii wetu kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi?

Mheshimiwa Spika, lazima tufike mahali tuaminiane. Lazima tufike mahali tuamini kwamba hata hawa ambao wako kwenye sekta binafsi wangeweza kufanya kazi kwenye sekta ya umma lakini kwa sababu sekta ya umma haiwezi kuajiri kila mtu ndio maana wameamua kujiajiri katika sekta binafsi. Mchango wao lazima uheshimike na lazima tuwape nafasi katika mawanda ambayo Serikali inaweza kuruhusu.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa katika utekelezaji wa shughuli za kiutalii, sawasawa na biashara nyingine, kodi ni nyingi sana. Compliance ambazo anatakiwa ku-comply mtu ambaye anajikita kwenye utalii ni nyingi mno kiasi ambacho haichochei watu hawa ku-comply na sheria zetu. Matokeo yake wanasuasua, matokeo yake mitaji yao inakufa na utalii wetu unashuka.

Mheshimiwa Spika, nina mfano hai utalii pale Mikumi hali ni mbaya, wafanyabiashara wanafunga ofisi zao, lakini wakati wanafunga ofisi zao tunaona idadi ya ndege zinazoshuka Mikumi inaongezeka kila siku, lakini watalii hao ambao wanashuka pale Mikumi hawaji mjini, hawakai mjini, hawaji kuangalia vivutio pale mjini. Hakuna package ambayo inawakalisha pale Mikumi. Matokeo yake Serikali inapata fedha nyingi kutoka kwa watalii, lakini wananchi na hasa wafanyabiashara ambao wanajikita kwenye shughuli za kiutalii wanakufa kiuchumi na wanaondoka kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jikumu la Serikali kuona namna bora ya kulinda wafanyabiashara wetu ambao wanajikita katika shughuli za kiutalii kama tunavyoweza kuwawezesha wakulima wengine vijana kwenye block farming na maeneo mengine. Ni muhimu sasa tukajikita kungalia namna bora ya kuwawezesha vijana ambao wamesomea utalii, shughuli za kiutalii namna ya kuwapa mtaji, namna ya kuwawezesha ili waboreshe huduma zao kwa ajili ya kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuchangia katika shughuli za kiutalii.

Mheshimiwa Spika, siwezi kumaliza mchango wangu bila kuzungumzia migogoro kati ya hifadhi na wananchi. Wenzangu wamezungumza na naomba nilikazie. Tatizo la mipaka kati ya hifadhi na wananchi limekuwa kubwa kiasi ambacho mwananchi haoni kwamba anawajibu wa kulinda hifadhi zetu na hawa ndio walinzi namba moja. Pale Mikumi tuna changamoto katika Misitu ya Palaulanga, Mkwiva, Mbeleselo na maeneo mengine. Kule Kielezo na Kitete Msindazi katika Kata ya ulenge.

Mheshimiwa Spika, tumezungumza sana, wakati umefika sasa Serikali kuona kilio cha wananchi na kilio chao ni kimoja tu wanakwambia kwamba kuna GN zaidi ya tatu ambazo zina identify mipaka kati ya hifadhi na kijiji. Ni mamlaka gani ambazo zinatoa hizi GN? Ni kwa nini hizi GN zimekuwa chanzo cha migogoro kati ya wananchi na Serikali yao?

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kero ya ndovu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)