Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami kwa utamaduni, naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara yetu ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, pia nakuponggeza na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu wewe binafsi ambaye unaomba nafasi ya Urais wa IPU, nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akusimamie na utashinda nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Namtumbo ni wahifadhi, na nimekuwa nikisema ni wahifadhi na wakulima. Kwa miaka yote tumekuwa ni watu wa aina hiyo. Ni sisi wenyewe pia tulifika mahali tuliamua kwamba tuanzishe maeneo ya uhifadhi kwenye maeneo yetu ya vijiji.

Mheshimiwa Spika, tulianzisha Wildlife Management Areas (WMAs) ambazo jumuiya hizi tulianzisha kwa kusini mwa Selous wakati ule mwaka 2007, ilikuwa inaitwa Mbalang’andu Kaskazini, na Kusini tuna Kisengue na Kimbande. Jumuiya hizi tulikubaliana hapo awali kwamba baada ya miaka 10 tutakuja kuwa na mapitio kwa ajili ya matumizi ya ardhi kwa sababu ile ilikuwa ni ardhi ya kijiji tuliiweka kwa ajili ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, miaka 10 ilishapita mwaka 2017 na wanavijiji wamekuwa wakiomba kufanyika mapitio ya ardhi kwa sababu wanahitaji ile ardhi kiasi, siyo yote kwa ajili ya kilimo. Lakini kumekuwa na danadana wasifanye yale mapitio na kuna sehemu wamefanya mapitio lakini majawabu hayaji. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali lazima tuishauri kwamba twendeni tukawaelewe wananchi mahitaji yao, ardhi yao ile waliitoa kwenye uhifadhi sasa wanahitaji kiasi kwa ajili ya kilimo. Lakini sasa hivi wanaonekana wananchi wale wa Namtumbo katika vijiji vile vyenye uhifadhi kana kwamba wao ndiyo wanataka kuvamia maeneo ya uhifadhi, kwa hiyo nguvu kubwa sana inatumika ili kuhakikisha kwamba wasiingie.

Mheshimiwa Spika, kama mtarudi mkazungumza nao kama mlivyowashawishi mwanzo, kuwapa elimu mwanzo na kukubali kufanya uhifadhi, tunaomba sana mrudi tena kuzungumza nao ili kuona ni kiasi gani na kufanya mapitio wapewe wananchi wale waweze kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tufahamu Maafisa wa Hifadhi pia, tufahamu sisi sote ni binadamu, na binadamu hasa wa vijijini kule wanategemea mapato yao ni kilimo, ndicho kinachofanya wanakidhi maisha yao kuishi katika dunia yetu hii. Kwa hiyo, lazima tufikirie hilo pia, pamoja na uhifadhi. Kwa hiyo, ushauri wangu ulikuwa huo, naomba sana tunapokwenda kule tuwasikilize wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu utalii. Balozi zetu na consuls kuu zetu zinafanya kazi kubwa ya kutangaza utalii, lakini kwenye bajeti zao Balozi na consuls kuu hakuna vifungu maalum vya kutangaza utalii, wanatumia OC zao. Siyo vibaya, lakini kutumia OC zao zile za kawaida inawawia ugumu sana kufikia malengo ya kuutangaza utalii wa nchi yetu. Kuna Ubalozi una nchi saba, lakini unahitaji usafiri uende ukatangaze maeneo hayo, hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna uhitaji wa kutangaza, fedha zinakuwa hazitoshi. Kwa hiyo, tunashauri Wizara mtenge fedha kwa ajili ya balozi zetu kuchapisha matangazo, majarida kwa lugha za kule, lakini kufanya matagazo kwenye televisheni pia. Ni muhimu sana kwenye hili kuzisaidia Balozi zetu. Hakuna fedha mahsusi zinazotumika kwa ajili ya utalii. Mimi naamini hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuutangaza utalii wetu. Nilipata bahati alikuja Spika wa India, Lok Sabha Om Birla. Uliniteua niwe mmoja wa watakaompokea na kuwa naye, lakini ulinipa kazi ya ziada kwenda Serengeti. Tulipokwenda Serengeti kule walihitaji kuona wale Big Five, waliwaona kweli, walibahatika wote, faru, a pride of 18 Alliance waliwaona kwa mara moja. Na Spika yule alishangaa kabisa, alisema katika maisha yake mpaka utu uzima hajawahi kuona simba zaidi ya mmoja, alikuwa ameona simba wale 18 live.

Mheshimiwa Spika, pia waliona nyumbu wengi, toka asubuhi wanaona nyumbu mpaka wakati wanapovuka. Wakasema walikuwa wanajua hawa nyumbu wako upande wa nchi ya pili kule, wenzetu kule wanatangaza sana, wao wanafahamu upande ule wa pili, lakini kumbe eneo kubwa la nyumbu hawa liko huku Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wahindi nao hawakuwa wanafahamu kama Serengeti ndiyo ina wanayama wengi na wale wanyama nyumbu wanakuwa wengi upande huu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tukazane sana kwenye eneo hili na hili ni pekee kwa kuwezesha Balozi zetu wazitangaze vizuri kule. Kwa hiyo ile timu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaj)

SPIKA: Haya, ahsante sana. Maliazia sentensi.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ile timu ya Spika wa Lok Sabha ndiyo imekwenda kutusaidia kututangazia kule. Kwa hiyo, tuongeze nguvu ya fedha kwenye Balozi zetu kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)