Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, angalau ni nafasi ndogo lakini naweza nikaongea machache.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri kwa hotuba nzuri inayohusiana na mambo ambayo yapo mbele yetu. Pili ninapenda niongelee sekta ya misitu. Sekta ya utalii kwa kuanzia tunaona kwamba ina mchango mkubwa wa asilimia karibu 17 kwenye Pato la Taifa. Sekta hii ya misitu inaonekana kama ni sekta ambayo mchango wake ni mdogo sana, lakini mimi nataka leo niseme bahati mbaya muda ni mfupi, nitaongea mbele ya safari. Niseme kwamba sekta ya misitu ina uwezo mkubwa wa kuchangia kwenye uchumi wa Taifa tukiweka mikakati mizuri. In fact, sekta ya utalii ni very fragile, ni tete, ikitokea shida kidogo tu inatetereka. Imekuja COVID hapa ikaporomoka, ikitokea vita inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ya misitu ndiyo sekta ambayo Wizara inatakiwa iiangalie kwa makini sana ili iwe sekta ambayo itaitegemea, ni sekta himilivu, ni sekta jumuishi, ina watu wengi, inatoa ajira kwa watu wengi, kwa hiyo wawe na mikakati mikubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, nami nataka kusema kuwa kuna mambo matatu au manne ambayo wakiyafanya sekta hii katika kipindi cha miaka mitatu kwenda minne tutaona mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, tubadilishe mtazamo na fikra. Hivi ni nani aliyesema kwamba samani, milango fremu, lazima ziwe za mninga, mvule au mpodo, nani alisema? Kuna uwezekano mkubwa tukawa na samani nzuri sana zinazotumia mbao laini.

Mheshimiwa Spika, napenda kusema wengi tumetembea hapa, tumekwenda sehemu nyingi, tumekwenda kwenye mahoteli, nitajie hoteli moja tu ambayo utakuta mlango wa mninga, hakuna! Sekta hii tupende kusema, lazima tuanzie kwanza kwenye mchakato mzima wa Serikali wa manunuzi.

Mheshimiwa Spika, tuweke permissive provision inayosema kama soft wood ina-meet kiwango na yenyewe iwe included kama sehemu ya mambo ambayo yanaweza yakatumika. Serikali ita-create demand na iki-create demand itaendelea kukua na kukua na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala zima la technology kwenye sekta hii. Tukiangalia, sisi tukivuna mti wa mbao kutoka kwenye gogo tunatumia asilimia 30 tu, iliyobaki yote inapotea. Ukiangalia tuna viwanda vingi vya kuchakata, katika viwanda asilimia 70 vyote ni mbao tupu.

Mheshimiwa Spika, kule Njombe kwa mwaka kuna semi-trailers karibu 40,000 zinazoondoka. Kwa siku kuna semi-trailers karibu 39, ni mbao tu. Tufike mahali sasa kama nchi tufanye maamuzi ya kuongeza thamani kwenye mbao, kwenye mnyororo mzima wa mazao ya misitu, tutafanyaje, tutafanya kwa kuingiza kitu tunakiita EWP (uhandisi katika mazao ya mbao).

Mheshimiwa Spika, nipende kusema tuna products nyingi sana, siyo mbao tu, tuna veneers, tuna plywood, tuna MDF, tuna boriti zile ambazo zinakuwa treated, zote hizi ni products ambazo tunaweza tukileta technology nzuri kwenye soko la mbao au kwenye industry ya mbao tutaweza kuongeza mapato kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, sasa napenda kusema technology ambayo tunaiongelea hapa ni ile ya second level, tutoe vivutio, kwanza kabisa kama Mbunge mmoja alivyosema hapa, tuangalie uwezekano wa ku-zero rate mashine zote ambazo zinakuja kwenye sekta ya mbao, hakuna hasara kwa Serikali, medium term, long term, Serikali itapata fedha zaidi, tuta-create employment zaidi katika sekta hii ya mbao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo tunaweza kufanya ni kuendelea kuiangalia hii sekta kuiondolea vikwazo na kuangalia ada na tozo mbalimbali ambazo zipo kwenye sekta. Bado kuna tozo nyingi sana kwenye hii sekta, GN Na. 59 tuiangalie kwa makini. Lakini kule Njombe kwa mfano…

SPIKA: Malizia sentensi Mheshimiwa.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, upande wa vibali watu wetu wanaosafirisha mbao wanapata taabu sana humu njiani, unatakiwa u-scan document unapoondoka, upite una-scan document mpaka unafika, vituo zaidi ya 15 kwenye destination. Kwa nini tusi-scan pale mwanzo ili biashara iendelee waka-scan mwisho kwenye destination? Kwa hiyo kwenye upande wa vibali tuliangalie kwa karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ukisafirisha mbao unatakiwa upate kibali unapotoka, lakini ukapate kibali unapouza. Kwa nini kuwe na vibali viwili? Na tunapoteza muda, tunapoteza mapato, tunapoteza ajira. Niombe sana tuiangalie sekta hii kwa makini sana na tuiongezee fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)