Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tunapowapongeza Waziri na Naibu Waziri kweli wanafanya kazi sana siyo kwamba tunawatania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naongea suala hilo hilo la tembo. Jimboni kwangu wananchi hawana raha, wananchi hawana furaha, matatizo ya tembo kwenye Jimbo la Same Mashariki naomba tafadhali haya makabrasha mawili haya yaje mbele yako apelekewe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu gani? Kama miaka mitatu hivi madhara yaliyofika mashambani kwa wananchi wangu, mpunga, mahindi, miaka mitatu, takribani miaka mitatu hata hicho mnachokiita kifuta jasho wananchi hawajapewa, sasa nianze upande wa vifo.

Mheshimiwa Spika, kabrasha hili linazungumzia vifo. Naanzia Muheza, Kenneth Edward Mazengo - Muheza, huyu alijeruhiwa tangu tarehe 24 Julai, 2022, wala Serikali haijamuangalia. Rayson Eminiel Mjema wa Kijiji cha Muheza alijeruhiwa na tembo tangu tarehe 26 Januari 2022, wala Serikali hamjampa hata senti tano. Ally Mhina Mbogo Makokane aliuawa tarehe 9 Julai, 2022 na tembo lakini Mheshimiwa Waziri mambo makubwa kama haya Serikali hamjawaona wananchi, na Zuhura Mapande wa Kijiji cha Muheza aliuawa tangu tarehe 17 Agosti, 2022 aliuawa na tembo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwepo mwenyewe Jimboni niliona aibu kwenda kumuona yule mama alivyochanwachanwa na tembo lakini Serikali hamjaona watu kama hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili kabrasha lote nililoshika mkononi hapa ni mazao ya wananchi wa Jimbo la Same Mashariki. Mimi ninahisi Mheshimiwa Waziri nisikilize vizuri, hawa tembo wangekuwa kule ndani ya National Parks wana maji ya kutosha, wasingekuja kwa wananchi huku, wangekuwa wana chakula cha kutosha wasingezunguka na kula mpaka wali uliopikwa na wananchi, angalieni vizuri ndani ya National Parks kuna hali gani?

Mheshimiwa Spika, naomba nikwambie. Naanza upande wa uharibifu wa mazao ya wananchi. Twende Kata ya Maore Kijiji cha Maore tembo wameharibu ekari 74.5 hapa ni kaya 67 zote wananchi hawakuvuna kitu, njaa. Kata hiyo hiyo ya Maore nenda Kijiji cha Mpirani ekari 21 mpunga na mahindi hapa ni kaya 21 wananchi hawakuvuna kitu. Kata hiyo hiyo ya Maore Kijiji cha Mheza kaya 367 ekari takribani 512, ekari zote hizi wananchi hawakuvuna kitu. Kijiji cha Kadando takribani kaya 54 ekeri 66, wananchi hawakuvuna kitu, tembo.

Mheshimiwa Spika, twende Kata ya Kalemawe, Kijiji cha Kalemawe kaya tisa na ekari tisa za mahindi wananchi hawakuvuna kitu. Twende Kijiji cha Makokane kaya 132, ekari 143 za mpunga na mahindi wananchi hawakuvuna hata hindi moja. Kijiji cha Karamba kaya 30, ekeri 31 mahindi, maharage, mboga za majani hawakuvuna kitu wananchi. Kata ya Nungu Kijiji cha Misufini kaya 95 ekari 145 wananchi hawakuvuna kitu. Kijiji cha Nungu kaya 33 ekari takribani 35 hawakuvuna kitu.

Mheshimiwa Spika, nikianza Kijiji kwa Kijiji kwangu ni taabu. Jimbo la Same Mashariki ni shida, nakuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja miaka miwili iliyopita, kote huku nilimpeleka hakuna kitu kimefanyika mpaka leo. Juzi nasikia Diwani anaiambia Mheshimiwa Waziri ametuma watu wake wamekuja kuona mahali pa kujenga Kituo cha Askari mimi wala hilo silipokei, wamekwenda kuona je, wamejenga? Huko ni kuona wananchi wangu wanakufa kila siku, wananchi wangu hawana mazao, hawana chakula, wana njaa, tembo.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, mimi sitaunga mkono hoja, naomba Mheshimiwa Waziri anijibu anawafanyia nini wananchi wangu kuhusu tatizo la tembo. (Makofi)