Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii. Naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kisha nikupongeze Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri unayoifanya ndani ya Bunge letu, hatimae sasa hivi unakwenda kugombea kule kwenye Mabunge ya Dunia kule. Wabunge Watanzania hatuna mashaka hata kidogo juu ya utendaji wako uliotukuka. Hakuna sehemu yoyote ile ambayo umeomba nafasi ukashindwa, kwa hiyo ndiyo maana sisi kama Watanzania tuna imani kubwa na wewe kilichobaki ni kitu kidogo tu, yaani ni nini? Ni kusema huyu ndie anaefaa kuliko wengine wote. Tunakupongeza na tunakutakia kila la kheri, Allahuma Zidna I’liman Waruzuqna Fahma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Waziri umeshapitia Wizara tatu sasa hivi, ndani ya Wizara hizo tatu hakuna Wizara hata moja ambayo imekushinda na hapa ndiyo umefunga kazi, tunakupongeza na tunakutakia kila la heri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri ni mtendaji mzuri, ni mtu msikivu ni mwanamama ambaye hajitanuitanui, ameshuka kuliko kawaida yake, hongera sana Mheshimiwa, tunampongeza pia vilevile Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na Watendaji wake wote. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kila aliyechangia amezungumzia masuala yanayohusu mnyama tembo. Mnyama tembo ni mnyama mzuri sana lakini mnyama tembo huyu, tembo ana tatizo. Tembo tunampenda huyu, tunampenda sana tembo kwa sababu tembo anatuletea kama nilivyosema pale mwanzo, pesa za kigeni. Lakini tembo huyu pamoja na uzuri wake huo mkubwa alionao, tembo huyo ana shida, tembo huyu siyo rafiki huyu kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa tumeambiwa ya kwamba tembo wameongezeka kwa kiasi kikubwa sana, tunaipongeza Serikali kwa kudhibiti majangili hatimaye kusababisha tembo kuongezeka kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kinachotokea tembo hawa wanaleta madhara kwa binadamu, ninachoomba kwa Wizara hii, yaani hapa watu wamnapiga makofi kweli kweli wakimaanisha ya kuwa lazima Serikali iweke mkakati madhubuti juu ya wanyama tembo. Mkakati madhubuti usipowekwa maana yake ni nini? tutabaki na tembo watu wataondoka, watu watakufa. Tutabaki na tembo peke yake, kweli kabisa hili siyo sawa sawa ni lazima tuliangalie kwa mapana yake makubwa. Inaonekana kama kichekesho lakini ni hatari kwa Watanzania. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa ukiachana na Wanyama tembo ambao wanaua, mimi mfano hai Jimboni kwangu Mheshimiwa Waziri sasa hivi tembo wamejaa, sasa hivi wanasaidiana na wanyama wanaoitwa fisi, wanaua watu. Nataka nikueleze tukio la watu wanne waliojeruhiwa na fisi Tarehe 10 Mwezi wa Tano Mwaka 2023 ule usiku, mmoja ameuawa na fisi na wengine watatu wamejeruhiwa wapo hospitali ya Mkoa ya Sokoine, nilikwambia Mheshimiwa Naibu Waziri wewe ni shuhuda juu ya jambo hili. Sasa si unaona wamewaambia tembo ngojea tupumzike tuwaache fisi, hii ni hatari. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumzia masuala ya tembo na kusema muweke mkakati madhubuti. Kumbe nimeambiwa nisitumie tembo, nitumie neno ndovu, ahsante, kule kwetu wanaitwa tembo. Ahsante sana haya nitatumia neno ndovu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la linalohusiana na asali ya Tabora imeshika nafasi ya pili katika Bara la Afrika. Kwa kuwa, asali yetu imeshika nafasi ya pili katika Bara la Afrika, mkakati gani uliopo ili kuhakikisha asali yetu inashika nambari moja ndani ya Bara letu la Afrika, hili ni muhimu sana kwa sababu asali ni dawa na asali ni kila kitu lazima tutengeneze mkakati madhubuti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna suala la dinasoria au yule mnyama anayeitwa mjusi. Dinasoria anapatikana huku Kusini lakini anapatikana kwenye Jimbo la Mchinga. Kwa kuwa dinasoria huyu anapatijkana kwenye Jimbo la Mchinga, Wizara ya Maliasili na Utalii tunaipongeza sana, pale Kitomanga wameshaweka kituo cha kupatia habari na Lindi Mjini pale ukifika unamkuta huyo dinasoria mrefu kuliko wengine maana yake tunatangaza utalii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu LNG. LNG italeta mabilioni ya pesa na watakaoajiriwa kutokana na LNG au watakaopata fursa ni zaidi ya watu 15,000,000. Tunajipangaje kuhusu fukwe zetu, ikiwemo fukwe za Mchinga hili ni lazima tuweke mkakati madhubuti. Tukiweka mkakati madhubuti wale watalii watakwenda kule.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia 100 tujipange kwa ajili ya LNG ili watalii wasiende huko wabaki kwenye fukwe zetu zilizopo kusini na Jimbo la Mchinga. Ahsante sana. (Makofi)