Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Minza Simon Mjika

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia. Napenda kumshukuru Mungu kwa vile amenipatia nafasi nzuri na siku njema kama hii ya leo kuweza kusimama hapa na kuongea yale niliyonayo. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Rais wetu Mama Samia, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kufanya katika nchi yetu. Ni kweli amekuwa mama wa mfano kiongozi wa mfano Rais wetu, tuzidi kumuombea awe na afya njema na aweze kutimiza maono yake kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninakushukuru sana Spika wetu kwa kazi kubwa ambayo iko mbele yako, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu asimame na uweze kushinda, hakika tunapoomba muda wote Mungu anasikia maombi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru Waziri Mchengerwa pamoja na Naibu wake, Katibu, Naibu Makatibu kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. Nimeendelea kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba kazi anayoifanya ni nzuri. Wizara hii ni nyeti sana, ina muingiliano mkubwa sana na ina ugomvi mkubwa sana, lakini Mungu awaongoze katika hilo mkubali kushauriwa na mkubali kubadilika mambo yenu yataenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Serikali yangu kwa kazi ambazo zinaendelea kwa sasa, Rais yetu Mama Samia royal tours imeleta mambo mazuri sana, tumeona wageni wengi wanaongezeka kila leo na tunapata fedha za kigeni tunashukuru kwa hilo. Pesa zile zimeingia katika maendeleo ya nchi tunapata barabara, tunajenga hospitali, tunajenga vituo vya afya na maendeleo mengine mengi nchini yanapatikana kulingana na hii ziara ya mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kuwashukuru wawekezaji wetu ambao wapo katika nchi yetu ambao wanakuja kwa ajili ya kutembelea na kutupatia fedha nyingi. Sitaki niongee zaidi kwa sababu naona muda wote ni mdogo nataka niseme habari ya Simiyu. Simiyu ina Wilaya Nne ambazo zinachangamoto kubwa sana ya tembo. Kuna Wilaya ya Busega, Bariadi, Itilima, Meatu. Wilaya hizi zinazo changamoto kubwa sana kila leo wananchi wanauawa ni hakika nadhani hata wewe Waziri taarifa hizi unazipata.

Mheshimiwa Spika, napenda niseme kwamba wananchi wa kule wamekuwa na tatizo kwa muda mrefu sana, kila siku wakinababa ni kulala nje kwa ajili ya kulinda tembo, tembo ni wengi kupita kiasi. Tembo wameleta madhara makubwa sana katika Mkoa wetu wa Simiyu, wameua akina baba, akina mama, watoto na wanafunzi wakati wanaenda shule, imefanya hata maendeleo ya baadhi ya wanafunzi kutokuwa mazuri kwa sababu hawaendi shule kwa ajili sababu ya tembo kuwa wengi kupita kiasi.

Mheshimiwa Spika, tembo hao wameleta madhara mengine ya kula chakula kikiwa shambani na kikiwa nyumbani. Tembo ni mnyama mwenye vurugu sana kwa kweli, ni ambaye kweli anavuta watalii wengi wanakuja kumuona hapa Tanzania lakini ni mnyama ambaye analeta madhara makubwa sana, amesababisha vifo vingi sana, ulemavu, ameleta njaa ameleta shida mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri napenda nikuambie kwamba katika Mkoa wa Simiyu kweli watu wengi wameuawa sana, lakini kumbuka kwamba katika Mkoa wetu wa Simiyu tunahangaika na hawa wanyama kwa muda mrefu sana. Mwaka jana tulisema walau mtupatie magari ya askari game hakuna hata gari katika Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Bariadi lakini wanyama muda wote wapo wanaingia mpaka sokoni ni muda wa kukimbia tu kina wakimama, wakibaba hawapati amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanyama hawa wamekula sana mazao unakuta katika Wilaya zetu hizo kuna njaa kubwa sana kwa ajili ya ukosefu wa chakula kwa ambao wanakaa pembezoni mwa sehemu hizi zenye wanyama hawa. Tunaomba Serikali iweze kutusaidia hili, ninaamini kiongozi wetu Waziri wewe ni msikivu, nilikuambia hata siku moja kwamba jamani mjitahidi kuleta amani hata maandiko matakatifu yanasema katika “Waebrania 12 – 14 tafuteni kwa juhudi kuwa na amani na watu wote” tunapokuwa na amani ni jambo ambalo ni jema hawa watu wanalala nje, akinamama wanabaki wenyewe nyumbani, watoto wanashindwa kwenda shule, lakini Waziri ukifika pale na Naibu Waziri wako mkawasaidia hawa watu ni jinsi gani hawa wanyama basi waweze kulindwa na watu ambao wamesomea yale mambo ili kwamba wale watu waweze kupata amani. Kweli imekuwa ni shida ni kukimbizana muda wote watu hawana hata kazi za kufanya. Mheshimiwa Waziri jitahidi kwa hilo, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Mbunge mmoja hapa amesema mimi hilo jambo kila siku nilikuwa nawaza akili kwangu, kwanini msijenge fence kwa ajili ya hawa wananyama wasiwe wanavuka kuingia kwenye makazi ya watu? Zijengwe fence kama vile yalivyo Magereza ya nchini Tanzania fence ndefu mnyama hawezi kuvuka ili tuleta amani katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, familia nyingi kule zinalia zimepoteza watoto kinababa wamefariki, kinamama wamefariki wengine wamepata ulemavu. Kwa hiyo, unakuta kwamba hata wale manyama watu wanawachukia kwa sababu ya changamoto kubwa kama zile. Waziri wetu jitahida sana kufatilia mambo kama haya. (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa hapa Jacquline Ngonyani Msongozi.

SPIKA: Mheshimiwa Jacquline Ngonyani.

TAARIFA

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa kwamba, kutokana na kadhia hiyo kwamba watoto wanashindwa kwenda shuleni lakini pia hao tembo wameweza kufika mpaka majumbani wanavuna mazao na wakati mwingine wanachua vyakula mpaka vya nyumbani wanakula.

Mimi nilikuwa nadhani kwamba sasa hawa tembo wangevunwa ili kupunguza hiyo kadhia wabakizwe wachache, hawa wachache watakaobaki waendelee kuzaa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Minza Mjika.

MHE. MINZA S. MJIKA: Naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Nilikuwa naelekea kusema kwamba kwa mfano mfugaji anapofuga anakuwa na ng’ombe wengi sana, ng’ombe wanazidi inabidi awapunguze wengine aende kuwauza mnadani apate pesa afanyie shughuli zingine za maendeleo. Hata hawa tembo wamekuwa wengi mno na ndiyo maana wanatembea huku na huku, si wavunwe wauzwe basi tupate hata fedha za kigeni? Itakuwa ni jambo jema kuliko kutesa wananchi muda wote wanakimbizana kwa ajili ya tembo, kila leo unapigiwa simu tunaomba hela ya tochi, tunaomba hela ya turubai, tunaomba pesa ya nini?

Tunaomba Waziri Mchengerwa utusaidie na tunakuomba ufike katika Mkoa wetu wa Simiyu. Ufike katika Wilaya zile ambazo zinahangaishwa na hawa Wanyama, utaona heka heka ya kinababa ambao wanayo kule, hawalali nyumbani muda wote wako porini jamani hebu tuangalie hawa watu kweli? Kuna Mheshimiwa mmoja anapenda kusema kwamba changamoto ya akili, matatizo ya akili wale watu hawawezi wakawa na akili nzuri. Kwa sababu hawatulii majumbani kwao na weka zao na familia zao, muda wote wanalala porini je, watapata amani kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kusema kwamba wanyama hawa ndiyo hatarishi sana katika Mkoa wetu wa Simiyu, hakuna mnyama mwingine mwenye vurugu kama tembo. Tunaomba Serikali iangalie kama ni kuwavuna basi wavunwe, sasa hivi wameingia katika hizo Wilaya toka mwezi Novemba mwaka jana, mpaka sasa hivi wako kule wanakula chakula shambani, wanakuja nyumbani, hata akikuta ni kubinua tu lile bati anaanza kula huyo mnyama ni mnyama mwenye vurugu sana, lakini hakuna mtu anayeweza kupiga kwa sababu wananchi wanaogopa sheria. Tunaomba Serikali basi iweze kuwavuna wanyama hao na sisi wananchi wetu waweze kuishi kwa amani na waweze kuwa na amani kama wapo katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kusema juu ya hawa wawekezaji wetu, kwa mfano Mwiba. Nashukuru kwamba si kwamba hawasaidii, wanasaidia katika maendeleo na ni wadau wa maendeleo pia. Kwa mfano, katika shule ya sekondari Paji, Mwiba ametoa baiskeli 200. Wanafunzi wamepata baiskeli ambazo zina thamani ya milioni 40 na kuendelea lakini pia wamejenga shule, wamejenga madarasa, tunawashukuru wale wawekezaji, si kwamba tunawachukia lakini kero ni kwa wale wanyama tu basi, ikitoka hiyo kero wala hatuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Mwekezaji huyo tunapenda kumshukuru sana ameamua kuanzia mwezi wa Saba wanafunzi watakula shuleni muda wote. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa huo uwekezaji, wawekezaji wetu waliyopo hapa nchini kwa ajili ya kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, Waziri Mchengerwa ninazidi kukuomba Waziri wangu endelea kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Wabunge wengi hapa wanaongea wanalalamika hilo jambo, tafadhali mtusikilize ili familia za kule ziwe na amani ili familia za kule ziwe na furaha, wanapolima wapate chakula wasije wakawa ombaomba kwa sababu ya kufirisiwa na tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)