Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi kuweza kusimama kwenye Bunge lako pia kuchangia kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Ninamshukuru sana pamoja na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa yako hii iliyopo mezani pamoja na Naibu wako Waziri. Pia niwapongeze sana Watendaji wako wa Wizara kwa uandaaji mzuri na kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya ya kuifanya Wizara hii iwe Wizara nzuri ambayo inachangia Pato kubwa la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo lakini pia nitakuwa nimefanya makosa makubwa sana nisipompongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya hususan kwenye Wizara hii. Hatujawahi kuona tokea dunia iumbwe Rais kufanya kazi kubwa mno kwa kipindi kifupi hususan kwenye Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa kweli Mheshimiwa Rais anahitaji pongezi kubwa mno na anahitaji kila pongezi, kila namna kwa namna ambavyo Rais alivyojitoa muhanga kuitangaza nchi yetu Kimataifa lakini ndani ya nchi kwenye Wizara hii ya Utalii.

Mheshimiwa Spika, leo tumeona wimbi kubwa la wageni ambao wanatoka nje, international kuja nchini kwetu Tanzania. Miaka ya nyuma tumeshuhudia kipindi kama hichi mwezi wa tatu mpaka mwezi wa sita ni kipindi cha low season lakini leo hii tunaona ndege nyingi sana ambazo zinatua ndani ya nchi kana kwamba ni kipindi cha high season. Kwa kweli anastahiki kila pongezi Mheshimiwa Rais. Ameifanya low season sasa hivi kuwa high season. Ni season nzuri tuna wageni wengi sana sasa hivi nchini kwetu namna ambavyo tayari wanavyokuja, namna ambavyo mama alivyoitangaza nchi, namna ambavyo wageni ambavyo wanavyoingia ndani ya nchi kwa ajili ya kuja kutembelea ndani ya nchi lakini pia kujifunza mambo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi nitajikita zaidi kwenye utalii wa fukwe. Ingawa nchini kwetu tuna fukwe nyingi lakini bado hatujazitumia vile ambavyo inatakiwa ukilinganisha na nchi nyingine. Utalii wa fukwe sasa hivi duniani ndiyo utalii ambao unatembelewa na wageni wengi nchini duniani. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara lazima tuweke mikakati madhubuti ili kuinua Wizara hii kwenye Sekta hii ya Utalii wa Fukwe. Mfano mzuri nilipoangalia kwenye mtandao wa BBC hivi karibuni wametoa taarifa yao 31 Machi, 2023, watalii wengi ambao wametembelea duniani ni watalii ambao wameenda kwenye fukwe ukilinganisha na maeneo mengine yoyote yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri nchi ya kwanza ambayo inaongoza kuwa na wageni wengi lakini wote wameenda kwenye fukwe ni nchi ya Brazil kwenye eneo la beach ambalo linaitwa Santos lakini pia nchi ya pili ambayo imeongoza pia kuwa na watalii wengi wameenda kutembelea kwenye fukwe ni Accra lakini pia kuna nchi ya Australia lakini kwenye tathmini yote overall Marekani ndiyo inaongoza kutembelewa na wageni wengi kwenye eneo la beach. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni wazi sasa lazima tuweke mipango mikakati ili kuhakikisha sasa tunakuwa na utalii wa fukwe. Kwenye nchi zaidi ya 30 zilizotajwa kwenye ripoti ya BBC Zanzibar imetajwa kweye eneo la Nungwi na eneo la Nungwi ni eneo ambalo limeshamiri kwenye utalii wa fukwe. Ni fursa pekee sasa hivi lazima tuwekeze huko kwenye eneo la fukwe. Watalii wengi duniani ndiyo wanakuja kwenye eneo la fukwe ukilinganisha na maeneo mengine, yote ni mazuri hayo, yote ni mazuri lakini kwenye fukwe zaidi ndiyo wanapendelea zaidi, wanapendelea zaidi ku-pleasure, kustarehe, kutembelea beach, kuota jua na mambo mengine hali kadhalika ukilinganisha na maeneo hayo ya wanyamapori pamoja na milima. Kwa hiyo, naiomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa huku kwa upande wa bara ardhi upande wa beach kwenye fukwe wameachiwa wenzetu wa Halmashauri na Serikali za Mitaa. Naiomba sana Wizara mtumie technique yoyote ile ili kuhakikisha sasa Wizara ndiyo inahodhi maeneo yale na hii Halmashauri pamoja na Serikali za Mitaa mnaweza mkatengeneza sheria na utaratibu mzuri ili ziweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Wizara ikitengeneza Tume kwa ajili ya kuchukua maeneo ya beach na kuyaendesha basi tuhakikishe kwamba tunaweka sheria na kanuni za Corporate Social Responsibility (CSR) ili vijiji ambavyo vitatoa ardhi yao kwa matumaini kwamba watahisi Serikali itaweza kuwasaidia basi mahoteli yale au wawekezaji hao wawe wanakumbuka kutoa gawio la faida kwa vijiji ambavyo vipo karibu, vitapata faida ya kujengewa mahospitali, vitapata faida za kujengewa mashule lakini pia vitapata faida vya kujengewa transportation. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze sana baada ya kuzindua hiyo filamu yetu lakini pia tuna tv yetu inaitwa Safari ambayo hiyo inamilikiwa na Maliasili, kwa hiyo niwapongeze sana kwa hiyo, lakini pia niwaambie kitu kimoja, mbali na tv sasa hivi mambo yetu haya yamehamia kwenye mitandao ya kijamii sasa hivi, tunao vijana wetu ambao wanatangaza sana kwenye utalii na ninaamini tukiwatumia vizuri nina uhakika tunaweza tukaongeza mara dufu watalii kupitia nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao vijana wetu naomba uniruhusu niwataje, yupo kijana ambaye anaitwa Yasini Jamal ni kijana ambaye ukifungua kwenye mitandao ya kijamii ana followers wengi na anauwezo mkubwa sana wa kuitangaza Tanzania kwenye issue ya kiutalii. Pia tunaye kijana wetu anaitwa Ally Jape ni vijana ambao wote wana uwezo mzuri wa kuutangaza utalii. Kwa nini tusiwachukue vijana hawa tukawafanya kama mabalozi wa kuweza kuutangaza utalii wetu ndani ya nchi? Ninaamini tukiwapa fursa hawa vijana wataitangaza sana nchi yetu kwenye sekta ya kiutalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo sasa niende kwenye eneo la pili. Watalii wengi nao wanaokuja ndani ya nchi wanavutiwa na vyakula. Kwenye eneo la vyakula bado hatujaweka mikakati madhubuti ili watalii wengi wanaokuja nchini basi wa-recognize kwenye issue ya chakula. Mfano mzuri tuna nchi nyingi sana kama India, watalii wengi wanaoenda India wanafuatilia masuala ya chakula. Ukienda Japan watalii wengi nao wanaenda Japan kwa ajili ya kufuata taste ya chakula lakini pia kwa upande wa Zanzibar, watalii wengi wanaenda Zanzibar na wao pia mbali na beach lakini pia wanafuatilia masuala ya chakula. Kwa hiyo naamini tukiweka hasa utalii wa chakula tutafanikiwa kwa asilimia 100 na ndiyo fursa yenyewe pekee hiyo tunaweza tukaitengeneza watalii wakaja wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri leo hii Zanzibar kuna tamasha ambalo linaendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja anaitwa Ayoub Mahmud. Huyu anastahiki pongezi za hali ya juu, tarehe 25 Juni, kuna tamasha Zanzibar linaitwa Zanzibar Seafood Festival. Tunaanza na tamasha mwisho wa siku matamasha kama haya yanakuwa ni sehemu ya kichocheo cha kuvutia wageni wengi nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo nchi nyingi sana zimefanikiwa kwenye matamasha haya ya kiuchumi kwenye suala hili la vyakula. Kwa hiyo nawaomba sana, naiomba sana Wizara tuangalie kwenye suala la chakula. Leo hii kuna ma-chef wengi Afrika Mashariki wamekutana walikuja kushangaa Tanzania tunapika ndizi kwa nyama ambayo duniani kote hakuna. Tukilifanya hili jambo kama ni fursa ya kiutalii tumetengeneza uchumi wetu, tumetengeneza ajira kwa vijana wetu, pia kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache ninakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii na ninaunga hoja mkono. (Makofi)