Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai lakini pia nawashukuru wananchi wa Urambo kwa kunipa ushirikano. Kabla sijaendelea naomba kwanza nikupongeze wewe mwenyewe umewapa akinamama moyo kwamba wanaweza kwa kuwa Spika lakini pia kwa kugombea nafasi kubwa ya Umoja wa Mabunge Duniani, hongera sana. Naamini kabisa watoto wa kike walioko shuleni tayari nao wanandoto kwamba siku moja wataiga mfano wa Mheshimiwa Spika wetu anaegombea nafasi kubwa sana Duniani. Mwenyezi Mungu akubariki nasi tujivune Tanzania kwamba tuna kiongozi mkubwa duniani.

MBUNGE FULANI: Halleluya! (Makofi/Kicheko)

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali inayongozwa na Mama yetu mpenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kweli kazi wanayofanya ni kubwa na inaonekana jinsi ambavyo maendeleo yanapatikana katika nchi yetu. Nichuke nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu wake, Wakuu wa Taasisi na Watendaji wote wa Wizara, kwa kweli kazi mnayo kubwa na mnaitendea haki Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama kwa niaba ya wananchi wa Urambo na hasa ambao hoja hii inawagusa ambao ni Wananchi wa Kata ya Nsenda ambako ndani yake kuna vijiji vya Lunyeta, Lutenge na Mtakuja lakini pia Kata ya Ukondamoyo ambayo ndani yake vijiji vinavyohusika ni Ifuta, Tumaini na pia Utewe. Wananchi hawa nimeshawasemea suala lao mara nyingi hii siyo mara ya kwanza na nitaomba tu Wizara ikaangalie katika kumbukumbu zake kuna barua nyingi ambazo nimeandika kuhusiana na ombi ambalo nalileta rasmi hapa mbele ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, Urambo tunategemea sana zao la biashara tumbaku lakini zao la pili ni asali. Kwa kutegemea asali sasa, tuliomba msaada wa Wizara hii hii ya Maliasili na Utalii watusaidie kutupa mashine za kuchenjua asali ili na sisi tusafirishe nje ya nchi. Tukapata watu waliokuwa wanataka asali yetu wanaitwa Follow The Honey. Walikuja na tukakubaliana nao. Tukafanya umoja wa wananchi wafugaji wa nyuki, tukatengeneza mahali pa kukusanyia asali na Wizara tulipoiomba ije itusaidie walikuja, walimtuma Mkurugenzi akaja akaona na kweli akaahidi kwamba Wizara itatuunga mkono katika kuimarisha hili zao la asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa katika harakati zile zile za ahadi ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii Serikali ikaleta Azimio hapa la kuchukua Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla. Sisi tukashukuru kwa sababu pia nasi tunapata faida. Watu wetu wananufaika na misaada mbalimbali na tunakubaliana na wazo la kuhifadhi misitu kama hii. Tatizo lililojitokeza na naomba niliweke wazi hapa, hakukua na ushirikishwaji wa wananchi. Wananchi walishtukia tu siku yenyewe tayari kuanzia leo hamuingia hapa. Imekuaje na sisi tulikua tunaishi miaka yote hii? Marufuku hamruhisiwa kuingia humu. Watu wakashangaa lakini kuna historia yake nyuma mbaya ambayo wakawa wanaikumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, 2013/2014 hawa watu walilima mazao yao yakachomwa na Tume ikaundwa, kwa kweli bado walikuwa wana uchungu wao wa mwaka 2013/2014. Kwa hiyo walipokuja tena tukasema; Hee! hii Serikali yetu vipi? Hakuna kukaa pamoja walituchomea mazao yetu tunaambiwa tu kuanzia leo hamuuingii huku. Kwa hiyo, ikaleta taharauki.

Mheshimiwa Spika, narudia tena kusema kwamba wananchi wa Urambo tunaikubali hifadhi tunachoomba kwanza ni kushirikishwa, pili ni kuelimishwa, hifadhi maana yake nini? Halafu pia nashukuru Serikali hii hii ya nchi yetu ilimtuma Mheshimiwa Hasunga, akiwa Naibu Waziri alikuja akaona, kwamba mpaka wao wa zamani ulirudidshwa nyuma baada ya TANAPA kuja kuweka mipaka yao na wana namba zao 23, 22 na yeye mwenyewe Mheshimiwa yule pale alishangaa wanafukua kwa mkono tu, wakaoneshwa kwamba jiwe letu 23, 22 mmeliruka mmeturudisha nyuma sisi lakini watu wameongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachomba, kwa heshima na taadhima Mheshimiwa Mchengerwa tunajua kazi yako ni nzuri ulipotoka, kwenye mabanda hayo tumekuta picha zako zimejaa mule, kazi uliifanya vizuri. Tunaomba wananchi wale washirikishwe, wanaomba kwa kupunguza eneo lao hawana mahali pa kuweka mizinga na alipokuja Mheshimiwa Rais Tarehe 30 mwaka jana Mwezi wa Tatu, hili pia aliliongea mbele ya Mheshimiwa Rais kwamba wanakubali kuwa na hifadhi lakini wanaomba waongezewe eneo la kuchungia mifugo yao na kuweka mizinga yao. Kwa sababu tayari tulishaweka mahali pa kukusanyia asali, walishaunda umoja wao na ninyi wenyewe kama Wizara mkamtuma Mkurugenzi akaja akaona akakubali, hasa mmetutoa tayari. Asali hatuwezi kupata tena kwa sababu mmetupungizia eneo, kwa hiyo mimi kwa sasa hivi natoa maombi tu kwako wewe ili Mheshimiwa Waziri ayachukue.

Mheshimiwa Spika, tunaomba wananchi washirikishwe, maana ya hifadhi ni nini? Ina manufaa gani kwao? Kwa undani waelewe halafu tuombe pia kwa heshima na taadhima mtupe eneo warudishe mizinga. Hawawezi sasa hivi kuweka mizinga ili wale watu ambao tulikubaliana Follow The Honey waje tuendelee kuwapelekea asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo wanaomba pia, tuna WMA yaani kuna eneo ambalo wanakuja watu kuwinda, sasa kuna madai fulani ambayo wanayo wale wananchi wa Uyumbu, WMA ya Uyumbu wanaomba kuna malipo ambayo wanahitaji ya mwaka 2021/2022 ili kurudisha mahusiano.

Mheshimiwa Spika, hatukatai kuwa na hifadhi, tunawashukuru na hili ombi tulishapeleka, kile kikundi kilichoundwa cha Mawaziri Nane walikuja lakini ndiyo walituacha hoi. Jibu lililotolewa pale lilituacha hoi, lakini bado wanaimani na Serikali yao kwamba itawafikiria ili warudishiwe eneo kiasi ili na wao waendelee kuchunga ng’ombe lakini pia na kuendelea na mizinga yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi kwa kifupi nasema tu kwamba ombi langu ni hilo, tunathamini sana hifadhi lakini bado tunaomba eneo. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)