Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu ili na mimi nipate kuchangia kwa niaba ya wananchi wa Handeni Mjini kwenye Wizara hii muhimu ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, Ilani yetu ya Uchaguzi ukurasa wa 11, ukisoma kile kipengere cha 67(a), sitakinukuu lakini nitataja kilichoelekezwa kwa sababu ya muda. Ilani inatuelekeza ifikapo 2025 tunatakiwa tuweze kuingiza fedha zinazotokana na Utalii dola za Kimarekani bilioni sita au fedha za Kitanzania karibia trilioni 14 ndani ya miaka mitano ifikapo 2025.

Mheshimiwa Spika, vilevile Ilani inatuelekeza ifikapo mwaka huu wa 2025 nchi yetu iwe imepokea au imepata Watalii milioni tano. Hali ikoje kwa sasa? Hali ilivyo kwa sasa mpaka Aprili 14 taarifa ya Serikali inaonesha kwamba tulikuwa na watalii 1,412,719 pungufu ya lengo kwa 3,500,000. Wakati huohuo inaonyesha tulikuwa tumeoingiza fedha bilioni za Kitanzania 288 ambayo hiyo ni asilimia kidogo sana ukilinganisha na lengo la bilioni sita kwa maana ya trilioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu zetu hizi wenzetu wa Maliasili hizi za kusema wanazo 1, 412,719 wanazipataje? Watalii wa Ndani kwenye hiyo 1,400,000 wako 718,299, watalii wa nje na hapa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi naomba mninukuu hilo vizuri kwa juhudi zake binafsi za kufanya tukio kubwa lile la Royal Tour na kuwavuta watalii kuja hapa Tanzania, watalii 694,420. Kwa hiyo, watalii 694,420 wameletwa na Mheshimiwa Rais kwa sababu ya Royal Tour hawa wa ndani 718,000 ndio nataka nizungumzia takwimu wanaziptaje hizi.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana, eti hata mtu akipanda basi anatoka Arusha kupitia Momera kwenda vijijini anahesabiwa ni mtalii, akipanda basi kutoka Bagamoyo au gari binafsi kupitia Saadani, Pangani yaani mimi Kwagilwa naenda Handeni nataka nipite Tanga Mjini niende msibani nahesabiwa ni mtalii.

Mheshimiwa Spika, mtu akipanda basi kutoka Arusha akapita Serengeti Ngorongoro anaenda zake Musoma anaenda kuoa huko, anaenda zake Musoma anaenda kutibiwa, anaenda zake Tarime mahindi yake yameliwa na ng’ombe anawahi, anaenda zake Mwanza anahesabiwa ni mtalii, halafu tunakuja hapa tunasema tuna watalii 1,412,000! Nimesema nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwaleta hawa 694,420, ninyi mnafanya kazi gani watalii wa kwenu wako wapi? maana hao miongoni mwao ni wasafiri, ni watu wanatoka Dar es salaam wamepanda treni ya TAZARA wanapita Morogoro wanaenda zao Mbeya mnahesabu watalii.

Mheshimiwa Spika, mtalifikiaje lengo la watalii milioni tano, mtalifikiaje lengo! Mtalifikiaje lengo hilo? Sikilizeni niwaambie ni lazima mtekeleze wajibu wenu wa kumsaidia Mheshimiwa Rais, kwenye hii habari ya utalii lazima tufanye mambo yafuatayo badala ya kuwa mnakuja hapa na kutupa takwimu kwamba kuna watalii wa ndani laki saba kumbe mmehesabu na wafugaji ambao wanahamishwa kutoka Ngorongoro wanaenda Handeni wakipita getini mnawahesabu!

Jambo la kwanza la kufanya, ondoeni VAT kwenye Airline Industry. Sikilizeni niwaambie utalii ni export, tunafanya export of service ndiyo maana tunapata Dola katika kipindi ambacho dunia yote ina msukosuko kuhusu forex hatuna fedha za kigeni za kutosha, utalii sisi ndiyo ulitakiwa utulinde tupate fedha za kigeni, acha kuhesabu mtu anakwenda mnadani kuuza kondoo amepita getini unamhesabu.

Mheshimiwa Spika, fanyeni jitihada sekta hii ituokoe, ondoeni VAT kwenye Airline maeneo yafuatayo:-

Kwanza; kwenye Ndege. Kwenye Injini za Ndege, hizi injini zinauzwa gharama kubwa sana ukitoza VAT unafanya hilo jambo linakuwa la anasa, Kwa hiyo matokeo yake Airline Industry ya kwetu iliyo ndani haiwezi ku-compete regionally, ondoeni VAT kwenye spare parts za ndege, ondoeni VAT kwenye aircraft maintenance.

Mheshimiwa Spika, hizi ndege zinasaidia wawindaji kupekewa watalii wao kwenye vituo vya kuwindia, zinasaidia watalii kutoka eneo moja kwenda jingine, sasa leo mtu amekubebea watu anakuletea unamgonga VAT! tutapata wapi mapato? Mtafikaje bilioni sita kwa mwaka? Mtafikaje watalii milioni tano?

Pili; ondoeni VAT kwenye ada za vitalu. Mtu anapokuwa amelipia kitalu kwa mwaka, amelipa ile ada ya kwanza anakuwa amekilipia kwa miaka kumi ninyi hata ile fedha ambayo anawalipa kwa miaka inayofuata mnaipiga VAT 100 percent, that’s wrong! Ilani yetu ya Uchaguzi inasema nini? Tatizo hamsomi hiki kitabu kizuri. Ilani inasema fanyeni mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo (c) ukurasa wa 112, Sheria ya VAT siyo msahafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Finance Bill, nataka tu nitoe taarifa kwamba nitashika shilingi leo kama Serikali haitaweka commitment kwenye Finance Bill inayokuja hii ili kuondoa VAT kwenye haya mambo ninayoyazungumza hapa. Tunataka fedha za kigeni, hatuwezi tukafika mahala, tutafika mahala tutashindwa hata kuagiza mafuta kwa sababu hatuna Dola, tutafika mahala viwanda vyetu vitashindwa kununua raw materials kwa sababu hatuna Dola lakini tuna nchi ambayo imejaliwa tuna kazi ya kuhesabiana tu mtu kapita anaenda Ngorongoro, mtu kapita anaenda msibani mnasema ni mtalii ameingiza nini cha forex. (Makofi)

Mwisho, watu wa mahoteli, watu wanaosafirisha kwenye tourism industry wanatozwa VAT mahala ambapo siyo sahihi kwa sababu tu ya ubovu wa sheria, ninyi watu wa maliasili na utalii hawa wanaondesha sekta ya utalii, private sector ni watu wenu, simameni muwatetee na ninyi msiwe sehemu ya kuungana kuwakandamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ondoeni VAT kwenye deposit. Sheria iliyopo ya VAT inasema hivi: The Value Added Tax imposed on taxable supply shall become payable at the earlier of (A) the time when an invoice of supply is issued; yaani mtu tu akipata mtalii kule nje akimwandikia tu invoice mnakuja mnataka VAT anaitoa wapi? Akakope? Halafu unasoma inasema: the time when consideration of supply is made yaani hata akilipa advance tu ambayo mtalii anakuja miezi sita baadae leo analipa kuwahi chumba analipa kuwahi ndege analipa, ninyi mnataka kodi we cannot work like that! Halafu we are very comfortable eti sheria iko hivyo! Sheria ni kitu gani kwani? Sheria inatungwa hapa! Kwa hiyo, tuondoeni hivi vitu. (Makofi)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kwagilwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Asya.

TAARIFA

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza kuhusiana na wadau wa utalii hasa hawa wawekezaji wa tour industry.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala zima la hawa wadau kutozwa VAT kwa sababu wageni wanapokuwa nje ya nchi ni lazima wafanye advance booking kwenye mahoteli, hoteli Sheria ukiisoma ya Utalii, hawa watu wanalipa kodi (VAT) ni mwisho wa mwaka siyo kipindi kile ambacho mgeni ana-book, kwa hiyo asipotoshe.

SPIKA: Mheshimiwa umepokea taarifa hiyo?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, anasema napotosha siipokei taarifa, nataka nimwambie nimesimama hapa nimesema nasimama kuongea kwa wananchi wa Handeni Mjini watu werevu kabisa wanaelewa ninachofanya hapa ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufanye mapinduzi kwenye hii sekta ili tumuunge mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya jitihada kubwa sana why are we lagging behind?

SPIKA: Mheshimiwa Kwagilwa muda wako umekwisha kengele ya pili ilishagonga, ahsante sana.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)