Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia uhai kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wabunge wengine kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Kwa muda mchache alioingia anaonesha uongozi, kwamba uongozi ni pamoja na kusikiliza wenzio, lakini ameshindwa kuonesha hali nyingine ambayo kwamba na yeye ni Mbunge kama Wabunge wenzake, tunakupongeza sana. Pia nimpongeze Naibu wako anafanya kazi nzuri sana. Mapungufu mengine ni ya kawaida kwenye ubinadamu lakini naamini kwenye michango hii kuna kitu amejifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwanza kwenye suala la kifuta machozi. Ili uweze kuwajibika vyema bila migogoro kwenye Wizara yako lazima uanze kufanya maboresho makubwa sana. Maboresho yenyewe ni pamoja na hizi Kanuni za Mwaka 2011. Tunaposema tunahifadhi hakuna Mtanzania asiyependa kuhifadhi ila wataona manufaa ya uhifadhi watakapoona matokeo ya moja kwa moja, na ili waone matokeo ni lazima kuwe na ushirikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili eneo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambae amekuwa anatoa miongozo mbalimbali na maelekezo ya namna ya kutatua migogoro hii bila kuacha makovu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nataka nianze kwenye kifuta machozi. Kama leo tukiacha ikabaki sura hiyo ilivyo kwenye sheria ilivyo pamoja na Kanuni tunaonesha ni namna gani Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu, sura hii siyo nzuri. Sote tunajua kwamba tunapohifadhi tunategemea kupata faida, leo tunapozungumzia utalii lazima uwekeze, unaanza kuwekeza wapi unaanza kuwekeza kwenye kuhifadhi lakini tunapohifadhi lazima mwananchi mwenyewe anaeishi hilo eneo ajue kwamba yeye ni mhifadhi namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nizungumzie kwenye maeneo machache tu kwenye hilo eneo ambalo lazima Mheshimiwa Waziri ufanye maboresho makubwa kwenye hizi kanuni. Mtu akipata majeraha ambayo anaweza akatibiwa akapona anatakiwa alipwe laki mbili, lakini mtu akipata jeraha la kudumu kwa mfano ameondolewa mkono labda alikuwa analima atalipwa laki tano. Mkono haupo kabisa analipwa laki tano, ikitokea mtu huyo ameuawa analipwa milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunataka kufananisha thamani ya mwanadamu na shilingi milioni moja, wakati unazungumza hapa kwenye hotuba yako nilikufatilia vizuri, kwamba nchi nyingine wameshaondoa kabisa suala la kifuta machozi ili uondoe kifuta machozi lazima uje na mikakati thabiti ya kuzuia wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla ya kufikiri kuondoa hicho kifuta machozi kwanza kiboreshwe wakati mnajipanga sasa kuzuia hao Wanyama. Leo Watanzania hawa wanapomuona tembo anakwenda kwenye shamba lake, anajua hata nikitoa taarifa kwa sababu yule hajapewa mafunzo na ninyi mmetuambia mmewapa watu mafunzo, yule hana mafunzo yoyote ya namna ya kukabiliana na tembo. Ni vizuri kama Taifa haya mambo inawezekana yalifaa kwa kipindi hicho, haya ni mambo ya kikoloni kabisa yamepitwa na wakati. Lazima tuanze kufikiri upya ili na huyu Mtanzania yawezekana tuliweka hizo kanuni kwa ajili ya kulinda Wanyama, lakini mimi nasema kwenye kauli mbiu yako ulisema tulirithishwa na sisi turithishe. Hatukurithishwa wanyama, tulirithishwa maeneo yenyewe ya hifadhi na wanyama ila tumerithishwa sisi binadamu siyo wanyama wamerithishwa binadamu. Kwa hiyo, binadamu alipewa nafasi ya kwanza kwa sababu tunahifadhi kwa ajili ya nani? Tunahifadhi kwa ajili ya sisi wenyewe, kwa hiyo lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa ajili ya uhifadhi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ulikuwa ni mfano mdogo kwa binadamu, nataka nije kwenye mazao. Wanasema kuanzia mita mia tano kutoka eneo la hifadhi, nikiwa ndani mita mia tano halipwi kabisa kama ikitokea wanyama wameenda kula mazao yake, lakini kuanzia mita mia tano na moja mpaka kilomita moja atalipwa shilingi elfu ishirini na tano kwa hekari moja. Leo Mheshimiwa Waziri tuambie mfuko mmoja wa mbolea ni shilingi ngapi, elfu 25 anakwenda kununua nini hata mfuko wa mbegu tu hawawezi kununua hizo ni dharau na ni mambo ya kikoloni na hayana maana kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni kilomita moja kutoka eneo la hifadhi mpaka kilomita nne kwa hekari moja mazao yake yaliyoliwa, ambayo hesabu ya kawaida tu Mheshimiwa Mchengerwa, yaani hesabu ya kawaida heka moja ile kuanzia kuandaa mpaka kuvuna ni laki saba. Ninyi mnasema ikiwa ni kilomita moja kutoka eneo la hifadhi mtamlipa fidia shilingi elfu hamsini. Kanuni za wapi ni za Watanzania kweli hizi zilitungwa na Watanzania, tulikuwa tunatunga kwa ajili ya kumsaidia nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni kilomita nne mpaka kilomita tano kutoka eneo la hifadhi, heka moja atalipwa shilingi elfu 75. Kanuni za wapi? Tulikuwa tunawatungia nchi gani? Lazima haya mambo yaboreshwe Mheshimiwa Mchengerwa hata ufanye nini kwa hali ya kawaida. Ikiwa zaidi ya kilomita tano heka moja atalipwa laki moja, tena anasema zisizidi heka tano, ukiziona tu hizo kanuni zimejikita kuwatia umaskini Watanzania. Kwa nini zisizidi heka tano? Tunataka wananchi wetu, yaani wao waanze kufikiri heka tano tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa hapa ndani tunasema lazima wafugaji waanze kufikiri kufuga kisasa, kwa nini tusifikiri kuhusu kuwekeza kisasa? Namna ya kuhifadhi hifadhi zetu? Tunapowambia Watanzania kwamba lazima waache suala la kuhama hama na mifugo yao waanze kufikiri kufuga kisasa, kwa nini sisi kama Serikali hifadhi zetu tusianze kufikiri kuhifadhi kisasa? Tutumie maeneo madogo lakini kwa uhifadhi ambao una manufaa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye ushauri, najua Mheshimiwa Mchengerwa ndiyo ameingia kwenye hii Wizara lakini tumeona maajabu yake kwenye hizo Wizara hizi mbili alikotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, lazima mambo yote mnayoyafanya yawe shirikishi. Lazima wafikiri kujenga fensi kwenye hifadhi zao. Tukibaki hivyo hivyo Watanzania wataanza kufikiri sasa kwamba ukikutana na tembo malizana nae. Kwa sababu heka yako moja imeondoka, umechukua mkopo benki halafu unaambiwa utalipwa 25,000 nani atakubali hiyo habari Mheshimiwa Waziri? Tuanze kufikiri namna ya kuwatunza hawa wanyama lakini kwa miundombinu ambayo ni rafiki na Watanzania wabaki kuendelea na shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ukija hapa utuambie ni lini utapitia hizo kanuni ambazo zimepitwa na wakati? Kanuni hizi zinaleta sura mbaya kwa Taifa letu pamoja na yote yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine, lazima muanze kufikiri inapotokea nyumba ya kwanza imeanza kujengwa kwenye hifadhi, ya pili mpaka ikawa Kijiji na uchaguzi ukafanyika akapatikana mwenyekiti wa Serikali, halafu mnakuja baadae mnasema watu hawa wapo kwenye hifadhi! Kwani Serikali ilikuwa likizo toka nyumba ya kwanza inajengwa mpaka ikawa Kijiji mpaka Mwenyekiti? Kwa bahati mbaya Serikali hiyo hiyo inatenga fedha kwa ajili ya uchaguzi hawajui kwamba Kijiji kile kipo kwenye hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hapo shule inaanza kujengwa, TANESCO wanapeleka umeme, watu wa maji wanapeleka, Serikali ni moja. Kwa hiyo, ni lazima hivi vitu muanze kutengeneza mambo ambayo yatakwenda kama uniform. TAMISEMI, Wizara ya Ardhi pamoja na ninyi lazima mkae pamoja. Pia, kuna migogoro mingine Mheshimiwa Waziri unaibeba wewe kwa sababu unaenda kwa ajili ya wanyama kumbe ni watu wengine, ni Wizara nyingine ndiyo imetengeneza imeshindwa kuwajibika, lakini kwa kuwa Serikali ni moja lazima mkae muone namna ya kumaliza jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba tuongeze vituo vya Askari. Mimi nawapongeza sana TAWA wilaya ya Nkasi wanajituma sana, wanajituma mno. Mheshimiwa Waziri, waongezee Askari, wapatie gari ili waweze kuwajibika. Kwa sababu wako kituo “A” wanaitwa kwamba tembo wamekuja mpaka watoke kule waende ni siku ya pili! inaonekana kama wao hawawathamini, kumbe ni kwa sababu mazingira yao siyo rafiki kwa ajili ya utendaji. Tunaomba tuwasidie TAWA waongezeeni bajeti lakini pia muongeze vituo. Wilaya ya Nkasi angalau tunaomba katika Jimbo langu muongeze vituo vinne kwa kuanzia ili tuweze kuondoa hii migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Sheria ya Usimamizi wa Wanyamapori lazima iangaliwe tena, tunatamani Sheria hizi tunazozitunga leo ziwe na faida kwa Watanzania zisiende kuwa kikwazo kama ilivyo sasa. Vilevile, Sheria ya Uhifadhi ya Wanyamapori iangalie upya, kwa sababu ndiyo umeingia ili uweze kuboresha vizuri majukumu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Mheshimiwa Waziri, suala la uvunaji wa tembo pamoja na wanyama wengine ikiwemo Mamba. Suala hilo limekuwa na kizungumkuti sana, ukiwauliza hawa wahifadhi wanasema kwanza hakuna sheria inayosema tuvune. Sasa kama hakuna sheria inayosema tuvune mnataka wananchi wawafundishe namna ya kuvuna? Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tukisema njooni muwaondoe mkiwaondoa leo kesho wanarudi, mmeshindwa namna ya kuwadhibiti, tofauti na hapo mtuambie kwamba mmekuwa na maeneo mengi ya hifadhi ambayo mmeshindwa kuyadhibiti. Kwa hiyo, mchague maeneo ambayo leo mnaweza kuyasimamia kikamilifu kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa kwa sababu ya muda nataka nizungumzie TFS. Hawa TFS ni watu ambao tunawahitaji sana, lakini leo huyu mwananchi wa kawaida ambaye amenunua mkaa debe moja akakamatwa barabarani, kuanzia huko alikotokea msituni anakuja kukamatwa nyumbani, hawa TFS kazi yao ni kuja kukamata au kusimamia kule ndani ili miti isivunjwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya kawaida tu hivi kweli hili eneo lina misitu na halina madawati na hao watu wanataifisha kila siku, hivi hizi mbao ambazo wanataifisha kwa nini zisiwasaidie wale watu ambao wako jirani kwenye hayo maeneo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)