Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa filamu yake ya Royal Tour tunaona watalii wanaendelea kuja nchini. Nimpongeze pia Makamu wa Rais kwamba amefanya ziara kwenye Wilaya yetu ya Ngorongoro. Kiuhalisia amefika na at least wananchi wanaona kwamba Serikali itaenda kutatua baadhi ya changamoto ambazo zipo kwenye Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, najua kwamba wakati zoezi la uwekaji wa beacons kwenye eneo la Ngorongoro eneo la Pori Tengefu la Loliondo alishatoa road map Tarehe 08 mwezi wa Sita mwaka jana. Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba baada ya eneo lile kuwekwa beacons kwa sababu ilitakiwa kushirikisha wananchi na wananchi hawajashirikishwa katika zoezi la uwekaji wa beacons, kwa hiyo, ilitakiwa kwamba baada ya zoezi lile kukamilika kwa sababu wananchi hawajashiriki, ni vizuri sasa tukakaa na wale wananchi tuone yale maeneo ambayo yameumia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mchengerwa kwa nia ya dhati, wewe siyo wa kulaumiwa leo ni wa kushauriwa kwa sababu kila bajeti ikipita tunakuja na Mawaziri wapya kwa hiyo nikuombee usiwe Waziri wa bajeti moja nikuombee uwe Waziri mpaka mwisho. Ni kwa namna gani utaweza kuwa Waziri? Ni kuepukana na machozi ya wananchi. Wizara ya Maliasili imekuwa ni sehemu ya kusababisha machozi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngorongoro tukiangalia eneo la Pori Tengefu la Loliondo baada ya kutengwa, Mheshimiwa Waziri baadhi ya maeneo, kwa mfano tukiangalia Kata ya Arash, Kata ya Piyaya, Kata ya Malambo na Kata Ololosokwan na Kata ya Soit Sambu ni Kata ambazo zimeathirika sana. Tukitolea mfano, Kata ya Arash toka eneo limetengwa Mwezi June mwaka jana mpaka Februari mwaka huu, mifugo zaidi ya 6,770 imekamatwa kwa sababu wananchi hawana eneo lingine la kulisha. Kama wananchi wangekuwa na eneo lingine la kulisha mifugo yao wasingeweza kupeleka tena katika lile eneo, mifugo zaidi ya 6,700. Ukienda Kata ya Soit Sambu vivyo hivyo, ukienda Kata Ololosokwan ni hivyo hivyo Kata Oloipiri hata jana, Kata ya Malambo Kijiji cha Sanjan mifugo zaidi ya 87 imekamatwa na kutozwa shilingi milioni nane na laki saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri, mimi nadhani tuna uhitaji uhifadhi sana, lakini uhifadhi huu ni kwa ajili ya nani? Ni kwa ajili ya Watanzania. Kwa hiyo, uhifadhi unaowaumiza wananchi tusiendekeze. Niombe Wizara hii inayoongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa, kwa nia ya dhati kabisa nikuombe tuende Ngorongoro, nitatenga muda wangu nitatembea na wewe, tuangalie maeneo yote ambayo yameathirika tuweze kuwasaidia wananchi, tuwasaidie kwa sababu haiwezekani leo, hivi Mheshimiwa Mchengerwa leo Kata ya Arash wametaifishwa mifugo 276, kaya zaidi ya 280 hawana mifugo tena, watoto wao wameacha shule waliokuwa kwenye vyuo, waliokuwa sekondari, wameacha shule. Sasa naamini kwamba uhifadhi huu siyo kwa ajili ya kuwaumiza wananchi hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kwa ujumla ukienda Kata, nikuambie tu niliuliza swali Namba 343 alijibu Naibu Waziri hapa. Alisema Kijiji cha Ngaresero hakipo ndani ya eneo la Poloreti. Mheshimiwa Waziri nipo tayari tusindikizane nikupeleke pale kama Kijiji cha Ngaresero hakijaingia kwenye Pori la Poloreti mimi nitajiuzuru Ubunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, beacon Namba 31 mpaka beacon Na. 159 zipo kitongoji cha Leparagashi, Kijiji cha Ngaresero zaidi ya kilomita tisa. Kwa hiyo, niwaombe wakati pia wa kujibu maswali hapa consult Mbunge anayehusika akupe ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ile wakati unajibu nilikuwa Ngorongoro tulikuwa na Makamu wa Rais, wananchi walikuwa wanacheka! Kijiji hicho mifugo zaidi ya mia tano wamekamatwa, hata ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngaresero ng’ombe 400 wamekamatwa, wakatozwa shilingi milioni 40. Sasa leo tukikaa tusidanganyane, ni bora tutatue matatizo ya wananchi kiuhalisia, kwa sababu utalii tunaupenda, uhifadhi tunaupenda lakini leo isiwe ni sehemu ya kuwafanya wananchi wa Tanzania kuwa maskini, iwe ni sehemu ya kuwasaidia kutatua matatizo yao. Pale tatizo linapotokea ni muhimu kukaa na wananchi tuyamalize. Naomba upange ratiba yako na tutamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Rais akuwezeshe utatue migogoro ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye Kata ya Ololosokwan, Soit Sambu, Oloipiri wananchi hawana mahindi. Tembo wameingia kwenye mashamba wamemaliza. Kutoa fidia mnatoa elfu ishirini na tano kwa heka imsaidie nani. Ni wakati muafaka pia tufikirie mtu shamba lake tembo wakila shamba zima tunakadiria tunapata gunia ngapi kwenye shamba mtu asiibiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunafikiria nimeona kwenye mipango yenu. Mnafikiria tena kupandisha hadhi Pori Tengefu la Lake Natron. Lake Natron imebeba Kata ya Ngaresero na Pinyinyi pamoja imeingia kwenye Kijiji cha Jema Kata ya Oldonyo Sambu. Ukija huku Tarafa ya Ngorongoro, kwa hiyo Wilaya nzima ya Ngorongoro itakuwa uhifadhi kwa asilimia 85. Hawa wananchi sijui watakuwawapi tena kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye suala la uhamaji wa hiari. Suala hili tulianza na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema wananchi washirikishwe kwa dhati. Kwa jinsi zoezi linavyokwenda, ushirikishwaji umekuwa hafifu. Kuna timu zimeundwa kwa ajili ya kuandikisha watu wanaoenda. Zoezi lenyewe siyo wazi, mwananchi unamfanyia tathmini halafu unakuja kuvunja nyumba yake, siku hiyo anaondoka ndiyo unaenda kumwonesha unachomlipa. Humuoneshi kabla, lakini baada ya kuvunja makazi yake yote ndiyo unaenda kumuonesha kwamba utalipwa hiki. Mwananchi hana namna lazima aende kwa sababu umeshamvunjia makazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pamoja na zoezi lote, wewe umeona kwamba sasa hivi waliondoka ni wananchi 3,010 tu, wananchi waliopo pale ni zaidi ya laki moja na kumi ambao wamebaki walioandikishwa ni watu 5,000 maana yake ukishaondoa hapo tutabaki na zaidi ya watu laki moja na elfu mbili. Halafu Mheshimiwa Mchengerwa choo ikijaa unawanyima hata, naomba kwa sababu wewe ndiyo umeingia tujaribu namna ya ku-consult jamii, tuzungumze kwa pamoja tuone namna ya kutatua matatizo, kwa sababu leo huwezi ukasema kwamba wanaondoka hao watu 7,000 halafu ndiyo zoezi limeisha. Pia, kinachotakiwa zoezi liwe wazi tusifichane. Wananchi wanahitaji kujua kwamba ni watu wangapi wanahitaji kuondoka? Leo hii tunasema kwa hiari uwazi uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora tuanzishe tena vikao tuzungumze kwa pamoja jamii ishirikishwe, wewe binafsi kama Waziri, mimi niko tayari kama Mbunge tushirikiane pamoja kufanya suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri lakini naomba masula yote ya Ngorongoro pamoja na Pori Tengefu la Loliondo tushirikiane kwa pamoja ili wananchi waache kulia. Nashukuru sana niunge mkono hoja. (Makofi)