Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naanza pia kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa mawili. Kwanza, kama ambavyo tumesema siku zote, nampongeza sana kwa matokeo chanya yanayotokana na ile Royal Tour. Tumeona ongezeko la utalii na katika taarifa imeonesha kwamba kuna ongezeko la utalii kwa asilimia 123. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuidhinisha fedha kwenda katika miradi ambayo itaendelea kuchochea na kusisimua sekta ya utalii. Kwa mfano, watu wa Iringa tunamshukuru na kumpongeza sana kwa sababu ameendelea kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa pale Iringa ambapo utakapokamilika utachochea sana utalii hasa kusini kwa maana ya Mbuga ya Mikumi na Mbuga ya Ruaha. Kwa hiyo, kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake na vyombo vyao vyote. Watu wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri alivyokuwa amefanya vizuri kwenye Wizara ya Michezo, nami napenda tu niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, alifanya vizuri kwa sababu pia ni mwanamichezo, pamoja na kuwa sasa hivi ametukimbia kwenye Bunge Sports Club, ndiye aliyekuwa namba tisa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo ya pale Mombasa ya Mabunge ya Afrika Mashariki, yeye ndiye alichukua kiatu cha dhahabu pale Mombasa, lakini baada ya kuja mdogo wake, Mheshimiwa Sanga, naona amerithi ile nafasi kutokana na majukumu mengi aliyonayo Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana. Kwa kutumia michezo, ninapenda kushauri kwamba tuendelee kutumia michezo katika kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia nafasi hii kuwapongeza sana chama cha wanaosimamia uratibu wa mshindano ya magari. Tarehe 14, Mei walifanya mashindano ya magari katika Msitu wa Sao Hill kama sehemu pia ya kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana waandaaji wa Great Ruaha Marathon. Hii ni mbio ambayo itakimbiwa Julai, 08. Yaani marathon hii itafanyika ndani ya Mbuga ya Wanyama ya Ruaha, maana yake ni katika kushirikisha michezo kuendelea kutangaza utalii. Pia Mheshimiwa Waziri na timu yako, nikuombe, kwa kutumia wataalamu wako, wako baadhi ya watu wanapendekeza na kushauri kwamba kama inawezekana na kama taratibu za kitaalamu zinaruhusu, basi kule kwenye mbuga zetu kuwe hata na viwanja vidogo vya michezo kama mpira wa kikapu, mpira wa volleyball, mpira wa pete, na hata viwanja vidogo vya kucheza mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watalii wanakuja wanatamani baada ya kutembea waende kufanya michezo ya namna hiyo. Kwa hiyo, kama taratibu za kiikolojia zinaruhusu, naomba Mheshimiwa Waziri uweze kulichukua jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuwa, kwa kutumia michezo, naipongeza sana Timu yetu ya Wanawake ya Under 17, nawapongeza Tembo Warriors, wewe mwenyewe ulikuwepo kule Uturuki, pia nawapongeza wanariadha, nitawataja baadhi tu, akiwemo Alphonce Simbu na Gabriel Geay ambao wamekuwa wakishiriki katika mashindano mbalimbali ya marathon. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na mimi nikushauri na timu yako na kupitia TTB, sina shaka kabisa na Damasi Mfugale, ni mtu ambaye ni open-minded, hebu tujaribu pia kuwekeza katika michezo kama sehemu ya kutangaza utalii. Kwa mfano, ukiwekeza kwa mwanariadha ukamsaidia vifaa, ukamsaidia training, kuweka kambi, ukamsaidia na walimu wa kuwasaidia kama timu ya watu watano, anapokwenda kushiriki kama Boston Marathon, ile tu kushiriki ni mvuto kwa Taifa letu, inaongeza kuchochea kuvutia watalii katika Taifa hili. Kwa hiyo, naomba nikuombe pia utumie michezo katika kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nijielekeze kwenye sekta ya misitu. Watu wengi wanadhani kwamba misitu ni mbao tu, lakini mimi na wenzangu kutoka kwenye maeneo ya misitu tunapenda kutumia neno mazao ya misitu. Kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu pamoja na mbao, juzi tumepitisha hapa Bajeti ya Wizara ya Nishati, wamesema watatupa vitongoji 15 kila Jimbo, maana yake ni vitongoji kama 3,000 hivi. Katika kufanikisha ndoto hiyo ya kufikisha umeme tutatumia nguzo, ni mazao ya misitu. Lakini tuna ujenzi katika Mji wetu wa Serikali, katika kujenga pale tunatumia milunda, mbao, marine board, hayo ni mazao ya misitu. Kwa hiyo hii sekta ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafinga, Mufindi na Njombe, kuna wawekezaji wakubwa ambao wametoa ajira kubwa sana kwenye viwanda vya plywood. Waheshimiwa Wabunge, niwafahamishe kwamba katika miti pia kuna utomvu, kuna makampuni yanagema utomvu, hayo ni mazao ya misitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba wanasema kwamba sekta ya mazao ya misitu inachangia asilimia tatu tu ya Pato la Taifa, siyo kweli, kwa sababu wao wanangalia tu ule mti ukishatoka kuwa mti basi wamemaliza mchango wa sekta ya mazao ya misitu. Lakini sekta ya misitu ni pana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri kutembelea uone uwekezaji uliofanywa na Serikali, lakini na makampuni na watu binafsi. Halafu nikuombe tembelea viwanda vya mazao ya misitu na baada ya hapo kutana na wadau wa sekta ya mazao ya misitu. Hapa yapo mambo ambayo mimi ninakuomba Mheshimiwa Waziri na timu yako kuweza kuyasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni suala la kurejesha kile ambacho makampuni yanakipata kwa jamii. Kwa kweli, napenda kuwapongeza sana TFS, wamekuwa wakishirikiana nasi, wametujengea mabweni, wameshiriki nasi kuboresha mazingira ya soko letu pale Mafinga, lakini makampuni ambayo yananufaika na sekta ya mazao ya misitu, bado hatujaiona Corporate Social Responsibility.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri na timu yako, mimi nawaamini sana, kama ambavyo tumefanya kwenye sekta ya madini na akina Mheshimiwa Doto, hebu tuje na utaratibu ambao hii sekta pia ya mazao ya misitu kile inachopata sehemu irejeshe kwa jamii, siyo tu wabaki TFS ndiyo warejeshe kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwaombe mshirikiane na Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Kuna hiki kitu wananchi wetu wanatuuliza mambo ya hewa ya ukaa, tunaambiwa kwamba kuna fedha nyingi duniani zimetengwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sasa sisi tumepanda miti ya kutosha, wananchi wamehamasika. Nitatoa pongezi hapa kwa wenzetu wa FDT, kwa wenzetu wapanda miti kibiashara, wamekuwa wanatoa elimu na miche kwa wananchi kama ambavyo wanatoa TFS. Wananchi wameitikia, lakini tunauliza, je, katika suala zima la hewa ya ukaa, nafasi yetu Wanamafinga, Wanamufindi, Wanairinga, Wananjome, iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe ushirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), je, na sisi, kwa sababu tunachangia sana ku-regulate haya mabadiliko ya tabianchi. Kwa kupanda miti maana yake tunachangia sana, kwenye mambo haya mazima ya kuleta oxygen na hewa safi, lakini pia tunatunza vyanzo vya maji. Kwa hiyo, nikuombe sisi kwenye kipengele hicho tutanufaika kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nitumie pia nafasi hii kuwapongeza watu wa Ebony FM Radio, katika kutimiza miaka yao 17 wamejitolea kuhamasisha kupanda miti 1,500,000. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi ambavyo hamasa iko juu sana. Tuendelee kuwaunga mkono lakini tuone wananufaika vipi na hewa ya ukaa, wananufaika vipi na hiyo CSR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REGROW, Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu nilikaa naye, nashukuru alinipa muda wa kutosha, nilimweleza. Ninaomba tumtendee haki Mheshimiwa Rais. Mradi huu wa REGROW sasa ni mwaka wa tano. Mradi huu aliuzindua Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais Tarehe 12 Februari, 2018 wadau wote na sisi watu wa Iringa na Mikoa yote ya kusini tulikuwepo katika shughuli hiyo, lakini lazima tukubaliane kumekuwa na kusuasua kwenye utekelezaji wa huu mradi. Mimi nakuamini na timu yako mkijipanga tutakavyouboresha huu mradi yako mambo ambayo yataendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona umeeleza mambo ambayo yanatarajiwa kufanyika hebu yafanyike kwa haraka. Nasi tunasema watu wa utalii Kusini, kwamba kama ambavyo tumesema Iringa ni kitovu cha utalii na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na timu yake, nawapongeza sana, wameendelea kuhamasisha lile tukio la kila mwaka la utalii kusini. Hivyo, Mheshimiwa Waziri kwa hiyo hii REGROW hebu ifike wakati, narudia kusema, tumtendee haki Mheshimiwa Rais ambaye alizindua mradi huu lakini utekelezaji umekuwa wa kusuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kama ambavyo tunafanya katika masuala mengine ya utalii, kwa mfano wageni wanavyolipa leseni ni tofauti na wanavyolipa wenyeji. Hata tunapokwenda kwenye mbuga za utalii unapoingia pale getini kama ni Mikumi, Ruaha au Ngorongoro, anavyolipa mgeni tofauti na anavyolipa mwenyeji. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la uwindaji, mimi nashauri sana wawindaji wazawa ambao wengine wanawinda for fun, wengine wanawinda kwa sababu mbalimbali, ziwe za kibiashara, hebu tuweke utaratibu kwamba kwa mfano makampuni makubwa giant tuyatengee labda asilimia 70, hawa wawindaji wazawa na wenyeji tuwatengee asilimia 30. Wao washindane kama wao na haya makampuni yashindane kama wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kiukweli wawindaji wetu ambao ni wazawa kwamba wataweza kushindana na haya makampuni ya ma-giant kutoka America, Urabuni, Ulaya na Asia? Itakuwa ni ngumu. Kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri, hawa nao wanahitaji kama Watanzania ku-enjoy na kufurahia hii nature ambayo tunayo, hii ambayo Mungu ametujalia. Kwa hiyo, ili wenyewe pia wa-enjoy, wape asilimia 30 washindane wenyewe na makampuni makubwa yape asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napongeza tena Timu ya Yanga kwa sababu ilichofanya pia imetangaza Taifa letu, imetangaza utalii, ndiyo maana nasisitiza kwamba kupitia michezo tunaweza kutangaza sana Taifa letu na kutangaza sana utalii. Wenyewe mmeona Algeria Waarabu wamelala na viatu na wameijua Yanga, wameijua Tanzania, wamelijua Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mungu atubariki sana, awabariki Watanzania, ambariki Mheshimiwa Rais, abariki kila kilicho chema kwa ajili ya Taifa letu na maendeleo ya wananchi wetu wakiwemo wananchi wa Mafinga. Ahsante sana. (Makofi)