Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nianze kwa pongezi, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anazipa kipaumbele sekta zetu za uzalishaji na hasa sekta hii ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka jana alifanya Royal Tour ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa sana kuongeza mapato kwenye hii sekta. Nami nitoe wito kwa Mawaziri wetu hawa wawili, niwakaribishe Sikonge waje wafanye Royal Tour ya kwao sasa kwa Sikonge ambayo naamini itatusaidia kutuinulia mapato kutoka kwenye hifadhi zetu na utunzaji na kutoa elimu kubwa zaidi kuhusu utunzaji wa hifadhi zetu Sikonge. Kwa hiyo, ninawakaribisha mwezi Julai au mwezi Agosti njooni Sikonge. Najua Mheshimiwa Waziri tangu azaliwe hajawahi kufika Sikonge, namkaribisha afike Sikonge kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza kwa nukuu za Katiba. Katiba yetu Ibara ya 8(1)(b) inasema: “Lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi.” Ibara ya 9(h) Katiba yetu inasema kwamba: “Aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.” Yaani ni Serikali itafanya hivyo, itasimamia hilo. Ibara ya 9(i) inasema kwamba: “Matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi.” Na mwisho 11(1) Katiba inaelekeza kwamba: “Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya kila mtu kufanya kazi halali.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesoma Biblia vilevile. Katika Biblia Isaya 32:18 unasema: “Na Watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu,” lakini Mheshimiwa Mchengerwa unafahamu katika Quran Tukufu pale Mwenyezi Mungu aliposema “Alladhi Ja’ala lakuml-ardh firshan wassama’a binaan.” Amekufungulieni ardhi kuwa kama busati na akateremsha maji kutoka mbinguni ili humo muweze kupata riziki zenu. Kwa hiyo, sekta hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya binadamu kwa sababu, hii ndiyo sekta ambayo kila binadamu anaitegemea kwa ajili ya maisha yake na humo ndiyo tunapata hewa safi na humo ndiyo tunapata kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tunazo hifadhi Tisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, hifadhi Nne za Serikali Kuu ambayo ni Iswangala, Nyahwa, Itulu Nature Reserve na Iyunga East, na misitu mitano ya Halmashauri ambayo ni Pembamkazi, Ugunda, Wala, Sikonge na Goweko, tunaelewa maana halisi ya utunzaji wa hifadhi zetu. Vilevile tuna hifadhi moja iko chini ya WMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba masuala ya kufanya kazi wananchi wetu katika misitu yetu yanakumbana na changamoto nyingi sana. Sisi tuna kazi nyingi tunazifanya kwenye misitu, kufuga nyuki, kurina asali, kuvuna miti, kuvuna uyoga, kuvua samaki kwenye mito iliyomo humo na kazi nyingine. Sasa ili mtu aingie mle afanye kazi hizi halali lazima apate kibali cha mamlaka, taratibu za kupata vibali wakati mwingine zimekuwa ngumu sana zinasumbua wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri aangalie hizi taratibu za kupata vibali kwa wananchi wetu, kufanya kazi za misitu, zirahisishwe na wananchi waelimishwe ili wapate vibali kwa njia rahisi waweze kufanya kazi zao za kiuchumi katika misitu yetu. Sheria nyingi na kanuni nyingi kwa kweli zimekuwa siyo rafiki, hilo eneo nalo lilivyo Mheshimiwa Waziri naomba lifanyie kazi kama Katiba ambavyo imeelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika misitu ya TFS ili mwananchi aingie mle kwa mfano ana kazi ya kuweka mizinga yake, ili aingie mle kwenye misitu anapewa kibali. Kibali analipia, lakini vilevile kila siku lazima alipie shilingi 2,000. Kwa hiyo, kama anaingia yeye na watoto wake wawili anaingia yeye analipa shilingi 2,000 kila siku na watoto wake wawili kila mtoto shilingi 2,000, maana yake ni kwamba, kama atakaa siku 50 anatakiwa alipe shilingi 300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi shilingi 300,000 kwa wananchi wetu wa kawaida, maskini wa vijijini, ni nyingi sana. Je, hata atakapopata mazao yake atauza apate shilingi ngapi? Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo. Kwenye Misitu ya TAWA ndiyo gharama ni kubwa zaidi kuliko hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu suala lingine ni pikipiki. Mimi nimesikiliza hoja nyingi za Serikali kuhusu kuzuia pikipiki katika misitu yetu, sawa, lakini hivi Mheshimiwa Mchengerwa nikupe wewe baiskeli utembee kilometa 200 utaweza kweli? Wananchi wetu wanapata shida kubwa sana kutembea kwa baiskeli kilometa 200 hadi 300 kwenda kwenye mizinga yao. Mimi nilikuwa naomba sana tuende na wakati, kwa nini tusiweke taratibu za unampa mtu kibali anakwambia mimi nitatumia pikipiki halafu afuatiliwe. Kama hiyo pikipiki ataitumia vibaya aadhibiwe kwa kuitumia vibaya pikipiki, lakini siyo alazimishwe kutumia baiskeli karne hii, kilometa 250, kilometa 300, akitoka kule amerina asali aweke debe lake kwenye baiskeli kilometa 200, ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa huko ni kuwatengua viuno wananchi, naomba sana hizi taratibu ziangaliwe kwa umakini na zirahisishwe na ikiwezekana hivi vyombo vya kutumiwa kwenda porini na kubeba mizigo viruhusiwe vyombo vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maombi kuhusu Jimbo. Kwanza naipongeza Serikali kwa maamuzi yake ya mwaka 2019 ambayo ni uamuzi wa kwanza wa Serikali ulikuwa ni kufuta mapori 12 ambayo yalikuwa yamekosa sifa, haya mapori yana ukubwa wa ekari 707,659 siyo jambo dogo lazima tuipongeze Serikali, vilevile Serikali ilifuta misitu 12 yenye ukubwa wa ekari 46,755 hii ni pongezi kubwa sana kwa Serikali, vilevile uamuzi ambao ni mgumu kabisa ambao Serikali iliufikia ni kuhalalisha vijiji 975 vilivyokuwa ndani ya hifadhi, huo ni uamuzi mkubwa sana, Serikali inahitaji kupongezwa sana kwa uamuzi huo. Pia kuondoa zile mita 500 ambazo zilikuwa ni buffer zone ulikuwa ni uamuzi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sikonge vijiji na vitongoji ambavyo vimehalalishwa navitaja, Miseseko kaya 533, Isenga kaya 527, Mwanzagata kaya 418, Myesuu kaya 314, Simbamdeu kaya 271, Ngakalo kaya 196, Kayemimbi kaya 193, Manyanya kaya 115, jumla kaya 2,567 zenye jumla ya wakazi 25,000 zote hizi Serikali ilisema hizi zirudi kwa wananchi. Hili jambo siyo dogo ni kubwa sana Mheshimiwa Mchengerwa, naomba simamia maamuzi haya yatekelezwe kikamilifu kama ambavyo Serikali iliamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana nimeona kwamba, kuna baadhi ya maombi yameanza kufanyika huko kupitia baadhi ya wataalam wetu wanaanza kutaka kupindua ule uamuzi. Ule uamuzi ulikuwa mzuri sana na wenye tija, haiwezekani watu wamekaa mle miaka 25 miaka 30 halafu leo hii uje uwaondoe kwa hiyo, uamuzi wa Serikali ulikuwa sahihi, ninaomba sana simamieni ili wananchi wetu waendelee kupata maslahi kama ambavyo walikuwa wametegemea kwenye uamuzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchengerwa nikuambie nakuunga mkono kwa asilimia 100 kwenye kazi zako zote, wataalam wangu kule Sikonge nawaunga mkono kwa kazi zao zote, ninachoomba tu taratibu zirahisishwe na mambo yakae vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, baada ya ziara ya Mawaziri Nane timu ya Serikali ya Wataalam, watu wa ardhi, watu wa idara ya usalama na maliasili walitembelea mipaka yote na wakakubaliana kwamba, hapa ndiyo mwisho, hawa waliozidi huku mbele wanatakiwa warudi nyuma. Sasa kule ambako walisema hapa ndiyo mwishio na wakaweka rangi ninaomba Serikali ikaweke beacon hata kesho ili wale ambao wako mbele kule tuwaelimishe warudi nyuma waache hifadhi na wananchi wa Sikonge watashirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba, misitu inalindwa vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la mwisho. Serikali iruhusu kutoa eneo la hekta 650 kwenye eneo la Bwawa la Uluwa ambalo limeingia kidogo kwenye hifadhi ya Ipembampazi. Hii hifadhi ni ya kwetu Halmashauri siyo ya Serikali Kuu ni ya kwetu Halmashauri na Baraza la Madiwani limeomba Waziri wa Maliasili na Utalii, utupe hizo hekta 650 ni eneo letu, lakini tunazingatia heshima ya kuheshimu sheria kwamba, msimamizi wetu, mlezi wetu ni Waziri wa Maliasili na Utalii, basi tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa mamlaka uliyonayo utupe hizi hekta 650 ili wananchi wajikimu kwa kulima mpunga kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alilenga eneo hilo liwe ni la mradi wa kilimo cha umwagiliaji tangu mwaka 1976 alipotembelea eneo hilo. Alizindua bwawa lile akasema mwaka 1977/1978 tutaleta fedha kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji, lakini bahati mbaya sana tukaingia kwenye vita, fedha zikachelewa, zimekuja hivi karibuni. Kwa hiyo, tunaomba sana ruhusa yako wakati utakapokuwa unahitimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Ahsante sana, naunga mkono hoja hii. (Makofi)