Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge kwa uamuzi wake wa kugombea nafasi ya Urais wa Bunge la Dunia (IPU). Mheshimiwa Tulia Ackson unastahili, unaweza, wote humu ndani tunatambua uwezo wako na tunataka dunia watambue hilo. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu, akubariki na akuwezeshe kupata nafasi hiyo ya Urais wa Bunge la Dunia. We wish you all the best. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote kwa hotuba nzuri ya bajeti lakini pamoja na kazi nzuri inayofanyika katika Wizara hii. Mheshimiwa Mchengerwa nakufahamu sana nikiwa kwenye Kamati ya Huduma nilikuona makali yako ukiwa kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na nina uhakika kwa kuwa sasa hivi unaye na Naibu Waziri ambaye ni makini mchapakazi, mnaenda kuipaisha hii Wizara, mnaenda kupaisha hizo sekta ambazo mnazisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana kipenzi chetu Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kushiriki kwenye Tanzania the Royal Tour ambayo sasa hivi imetuwezesha unaona wawekezaji wanaendelea kuongezeka, unaona watalii wanaendelea kumiminika na mchango wa utalii kwenye Pato la Taifa, umeongezeka. Tukumbuke kwamba kwa mwaka 2014 mchango wa utalii katika Pato la Taifa ilikuwa ni asilimia 4.4 tu, lakini kwa mwaka jana 2022 ulipaa mpaka umefikia asilimia 17.5. Watalii wameongezeka kutoka 1,700,000 mwaka 2021 mwaka 2022 wamefika 3,800,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema ahsante sana Mama Samia Suluhu Hassan, tunasema ahsante sana kwa mikakati mliyoweka Wizara imeanza kuzaa matunda. Ombi langu kwenu ni kwamba watalii wamekuja ndiyo sasa lazima tuweke tuhakikishe kwamba huduma wanazozipata wakiwa ndani ya Tanzania kwenye mahoteli, kwenye ndege, kwenye mbuga ni za kiwango cha hali ya juu, kusudi kesho na kesho kutwa watamani kurudi ndani aya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera tunawashukuru sana, mwaka 2018 mlipandisha yaliyokuwa mapori ya akiba yakawa Hifadhi za Taifa tukapata Burigi - Chato, tukapata Ibanda, tukapata na Rumanyika, lakini kasi ya kuziendeleza hizo hifadhi ni ndogo sana. Tulitegemea kwamba baada ya kuzipata uongozi wa Mkoa wa Kagera walihakikisha kwamba wamefanya operesheni mbalimbali, wakaondoa mifugo yote iliyokuwa kwenye hifadhi hizo na mifugo mingine ilikuwa inatoka nchi za nje, uoto ukaongezeka wa asili, Wanyama wakaanza kurudi wanyamapori lakini na Serikali mkatusaidia kutuongezea wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacholalamikia ni kwamba hatuoni kama kuna kasi ya kuziendeleza hizo hifadhi, kwa maana ya kutujengea barabara, njia zile routes, kuweka mahoteli, tunaona kwamba bado. Unakuta sehemu nyingi ndani ya hifadhi hizo hakuna mitandao. Sasa mtu ameenda kutalii amefika kule labda kapata shida akitaka kuwasiliana na mtu ambaye yuko nje ya hifadhi hawezi kwa sababu hakuna mtandao, au vijana wenyewe siku hizi wanataka wajipige picha karibu na mnyama, arushe ile picha na yule mtu aliye nje ya hifadhi aone hawezi kufanya hivyo kwa sababu hakuna mitandao. Tunaomba TANAPA itekeleze mpango mkakati wa kuendeleza hizo hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tupatiwe wataalam, kwa Mkoa wa Kagera tangu kwenye Mkoa mpaka ngazi zote za Halmashauri zote hatuna Afisa yeyote anayehusika na utalii. Kwa hiyo, utakuta mara ni Afisa Utamaduni, mara ni Afisa wa Misitu ndiye anapewa lile jukumu, yaani hatuna yule ambaye anaweza kwenda kwenye Halmashauri akatetea hata haki I mean ule mpango wa kuendeleza utalii. Kwa hiyo, tunaomba tupewe hao kusudi tuweze kuendeleza utalii Mkoani Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya mwaka jana Serikali mlituahidi kwamba sasa mnaenda kuchonga barabara kwenye hii Hifadhi ya Burigi - Chato lakini mkasema mnaenda kuanzisha utalii wa faru weupe kwenye hii Hifadhi ya Burigi - Chato. Naomba kujua kwenye bajeti hii kuna nini au kitu gani kimeshafanyika kwenye kuanzisha huo utalii wa faru weupe katika Hifadhi ya Burigi – Chato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiomba kama mkoa lakini na Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo Eng. Ezra Chiwelesa amekuwa akiliongelea sana kwamba sasa lile lango la kuingilia Burigi - Chato lipite mahali ambapo wale wataliii sasa watatakiwa wapite katikati ya Biharamulo wakati wanaenda kwenye kutalii huko Burigi - Chato. Kusudi waweze kuchochea uchumi ndani ya Biharamulo Mjini, naomba kujua huo mpango umefikia wapi na nikuombe Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha uniambie kwneye bajeti hii tulishapata hifadhi mpya zaidi ya moja Burigi - Chato ndiyo kuna mipango naiona kwenye bajeti, Je, hii Ibanda ya Kyerwa na Rumanyika ya Karagwe kuna mipango gani sasa ya kuziendeleza hizo hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tembo. Tembo wamekuwa tembo. Tembo tunawapenda, tembo ni maliasili tulipewa na Mwenyezi Mungu lakini sasa hivi wameamua kuhama kutoka kwenye hifadhi wanakuja mahali wanapoishi binadamu. Ukienda kule Missenyi kule Mabale, ukienda Karagwe kule Muramba ukaenda Kyerwa, ukaenda Ngara wanaingia kwenye mashamba, wanakula ndizi, haishii hapo hata na mgomba wenyewe anaula na anauchanachana unakuwa kama nyuzi. Wanaingia Kagera Sugar waanakula miwa ya Kagera Sugar, imekuwa ni kero, tunaomba msaada wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna nyani na ngedere. Sisi huko Uhayani huwa tunalima mahindi yanawekwa kwenye mashamba ya migomba, sasa hawavuni maana yake ni ngedere na nyani ndiyo wanakuja kuvuna. Hata ukienda pale Manispaa ya Bukoba unakuta ngedere na nyani wanatambaa hata kwenye miji, kwa sababu huku zamani kila Halmashauri ilikuwa na kitengo kinaitwa bail in control, ambapo kulikuwa na Maafisa ambao walikuwa nahusika kuwavuna, kuwaua na kuwapunguza na kuwarudisha hifadhini wale wanyamapori wakali na wale ambao ni wasumbufu wanaharibu mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hicho kitengo hakipo ndiyo maana hawa wanyama wanatawala na hakuna anayewashughulikia, tunawaomba mtuletee wataalam ambao wamesomea mambo ya wanyamapori ambao wanajua sasa ni kwa namna gani wanaweza kuwarudisha huko wanakotoka kusudi tusiendelee kuathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumebahatika na Mwenyezi Mungu akatupa vivutio vingi vya utalii. Nina uhakika kwamba kila Mkoa, kila Wilaya ikiwemo na Kagera kuna vivutio vingi, kwa sababu ya muda leo nitazungumzia vivutio vitatu tu. Mkoa wa Kagera tuna visiwa 48 ndani ya Ziwa Victoria ambavyo viko Mkoa wa Kagera. Kati ya hivyo 48 ni 27 vina watu wanaishi visiwa 21 hakuna mtu anayeishi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ni opportunity ya kuweza kuanzisha utalii. Wizara tuende mkajenge mahoteli kule tuweze kuanzisha picnic sites, tuweze kuanzisha uvuaji wa Samaki - sports fishing, tuweze kuwa na utalii wa boti, mtu anasafiri kwenye boti anaendesha mwenyewe mtumbwi, anaenda upande ule kwenye kisiwa anastarehe na kurudi. Kwa hiyo, tunaomba tufanyiwe hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunayo misitu mikubwa, tunao msitu mmoja mkubwa unaitwa Minziro, huu msitu ni mkubwa una hekta zaidi ya 25,000 na inasadikiwa kulikuwa na nyoka mkubwa sana ambaye anaishi zaidi ya miaka 209 na huyo nyoka aliweza kuishi kwa siku zaidi ya 68 bila kula chakula anakunywa labda maji tu na katika msitu huo huo, nina uhakika watu wangependa kuja kuona msitu huo unafananaje. Lakini katika msitu huo huo kuna species nyingi aina ya miti mingi mamia na mamia na kati ya hayo mamia aina 12 ya miti hiyo inapatikana Tanzania tu, kwa hiyo nina uhakika watu wengi wangependa kuja kufanya utafiti na kuiona hiyo miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vipepeo wa rangi zote, tuna aina zaidi ya 600. Wanene, wembamba, wekundu, weusi, rangi zote wanapendeza ni kivutio tosha. Tunao ndege zaidi ya specie 238 na kati ya hao hizo specie 51 zinapatikana Mkoa wa Kagera tu. Huu msitu ukiendelezwa unaweza ukatuvutia utalii na watu wengi wakaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtufungulie utalii wa fukwe, Mkoa wa Kagera kwenye Ziwa Victoria tunayo fukwe moja nzuri sana ndefu. Ukianzia kule Muleba Kusini, ukaja Kaskazini ukaenda Kusini Kaskazini ukaja Bukoba Vijijini, Manispaa ya Bukoba ukaenda mpaka Missenyi ni fukwe moja ndefu sana ina mchanga mweupe mzuri na mawe mazuri ya ajabu. Mkiweza kuuendeleza ule ufukwe unaweza vilevile ukatuvutia utalii ambao utachochea kipato cha ndani ya Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)