Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uhai kwa kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote ndani ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninampongeza Mhifadhi namba moja Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye programu ya Royal Tour na tumeona watalii wanaendelea kuongezeka ndani ya nchi yetu na naamini wataendelea kuongezeka kama vile walivyo ongezeka katika nchi ambazo zili – practice programu hii ya Royal Tour kama wenzetu wa Mexico, Poland, Ecuador na Rwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja Mkoa wa Njombe tarehe 26 Agosti, 2022 alisema kwamba itakuja phase two the hiding place of Tanzania na hii ita – cover maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha nia ya dhati ya kukuza utalii wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanda za Juu Kusini tuna vivutio vingi sana. Ukianza Iringa tuna Hifadhi ya Ruaha ambayo ina simba ambao wanatembea kwa makundi makubwa, ambayo huwezi ukaona simba hao kwenye Hifadhi zingine nchini. Vilevile ukienda Rukwa kuna maporomoko ya Karambo, maporomoko haya ni ya pili kwa ukubwa Afrika yakitanguliwa na yale ya Victoria Fall kule Zimbabwe. Ukienda Songwe tunakuta Kimondo, kivutio pekee ambapo huwezi kukiona sehemu nyingine. Ukienda Njombe unakuta Hifadhi ya Kituro ambayo ni ya kipekee ulimwenguni, lakini ukirudi huku Mbeya unakuta Kijungu, maji yanapanda mlima, utakuta Kisimba vilevile utalikuta Ziwa Ngosi ambalo lina ramani ya Afrika na lina maji mazuri yenye rangi ya bluu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fukwe nzuri Matema Beach, ukienda Ruvuma utazikuta fukwe hizi Njombe pia kule Ludewa. Ushauri wangu kwa Serikali, iendelee kuvitambua na kuvifanyia kazi vivutio vya Nyanda za Juu Kusini ili kuweza kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine Serikali iharakishe kumaliza phase one ya regrow ili ianze phase two ambayo itatoa fursa kwa hifadhi ambazo hazikuingia kwenye phase one. Hifadhi kama ya Kituro na Katavi ziweze kufaidika na mradi huu. Kwa kufanya haya itarahisisha programu ya phase two ya The hidden place of Tanzania kuja kufanya kazi vizuri kwa sababu muda huo tutakuwa tumeishajiandaa vizuri kutambua na kuainisha vivutio vya Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaombi kwa TANAPA Serikali iangalie namna ya kuwaongezea bajeti TANAPA. Kwa sababu wakati wana hifadhi 16 TANAPA walikuwa wanapata bilioni 104. Sasa hivi hifadhi imeongezeka ziko 22 wanapata bilioni 111, lakini hitaji halisi la Bajeti ya TANAPA ni bilioni 222 unaweza ukaona hapo ni fifty percent tu ya wanayoipata kutokana na hitaji lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TAWA, TAWA mapori yameongezeka lakini bajeti ni ndogo. Serikali iangalie namna ya kuwaongezea pesa ili waweze kufungua njia au barabara kwenye mapori hayo lakini vilevile wawaongezee watumishi. Baada ya kumaliza hiyo Nyanda za Juu Kusini, sasa napenda nizungumzie utalii wa fukwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inabidi sasa ifanye mikakati mikubwa ya kuhakikisha ya kwamba tunaendeleza utalii wa fukwe. Tunazo fukwe nzuri lakini Serikali bado hawajazifanyia kazi. Ukienda Seychelles wamefanikiwa sana katika utalii wa fukwe na wanafanya vizuri, kwa sababu wao wana mamlaka maalum ya kusimamia fukwe na hiyo mamlaka iko chini ya Bodi ya Utalii. Kazi ya mamlaka hiyo kuandaa mipango ya matumizi ya hizo fukwe vilevile kusimamia utekelezaji wa mipango ya hizo fukwe, pia wanakazi ya kuratibu na kuzitangaza fukwe hizo kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwa mikakati hii madhubuti ndiyo maana Seychelles imefanikiwa sana kuuza katika utalii wa fukwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa kwa Serikali, jambo la kwanza Serikali inatakiwa irudishe fukwe ziwe chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Serikali ikirudisha hizi fukwe kuwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaweza ikapeleka kwenye Taasisi kama ya malikale. Vilevile irudishe na Visiwa vyote viwe chini ya Wizara ya Malisili na Utalii na hivi Visiwa vinaweza vikasimamiwa na Jeshi USU kule maliasili wana Jeshi USU kwa ajili ya sababu za kiusalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo Serikali inatakiwa itoe fursa kwa wawekezaji, wananchi waweze kujenga hotel ili kuiongeza idadi ya vyumba. Hivi sasa tuna vyumba 132,667 ukilinganisha na competitive wenzetu hawa hapa Kenya maana hao ndiyo washindani wetu wakubwa, wanavyumba zaidi ya milioni moja. Kwa hiyo, Serikali ione umuhimu wa kuangalia jambo hili na kulifanyia kazi ili tuweze kuongeza mapato katika sekta ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la pale Kilwa, yale majengo ya kale, Serikali ione umuhimu wa kuyakarabati ili kuanza kufungua utalii na watalii waendelee kwenda zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuzungumzia masuala la migogoro. Migogoro ya binadamu na wanyama, migogoro ya ardhi kati ya Hifadhi na Vijiji. Nilikuwa naiomba Serikali, Wizara hii ya Maliasili na Utalii ifanye kazi kwa ukaribu na Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Mifugo, Wizara Kilimo ili kuweza kutatua na kuweza muda mwingine kuepusha migogoro isiyokuwa na sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni ile Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pale Mvomero, imejengwa ndani ya muda mfupi, lakini pale kuna mgogoro kwamba wanyama wanakwenda, wanapita mpaka kwenye baadhi ya vijiji pale, lakini inawezekanaje Ofisi ya Serikali wanapewa hati, wanapewa kibali cha kujenga, mipango inafanyika katika Wizara ya TAMISEMI, wanaelekeza ijengwe pale na baadae inakuja kuona kwamba imejengwa katika maeneo ambayo wanyama wanapita! Nafikiri kuna haja sasa Wizara hizi za Serikali zote kabla hamjafanya matumizi ya ardhi mkae kwa pamoja, mshauriane ili muweze kufikia muafaka muone je hili jambo linalofanywa ni sahihi ama litakuja kuleta madhara baadaye? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sasa hivi kuna programu inaendelea ya BBT, Wizara ya Kilimo kule kwa Kaka yangu Hussein Bashe, ninataka kujua yale mapori, mashamba waliyoainisha ya kuweza kufanya hizo programu za BBT wamewasiliana na Wizara ya Maliasili? Isije ikawa baadaye tena waanza kulima mazao yamekua tembo wanaingia wanaanza tena kulalamika kwamba tembo wanapita, isije ikawa wameweka hizo programu zao katika maeneo ambayo yanaushoroba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiria ni wakati muhimu sasa wa kuangalia umuhimu wa kujua matumizi ya ardhi katika sehemu sahihi kwa wakati sahihi ili baadaye isije kuleta migongano na migogoro hii hifadhi, vijiji, Wanyama na binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)