Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu subhanahu wata’ala kwa kutujalia uhai, uzima na salama lakini pia nikimshukuru sana Mheshimiwa Rais ambaye ni mhifadhi namba moja kwa jitihada ambazo amekuwa akizichukua katika kuendeleza masuala mazima ya uhifadhi wa maliasili Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Kwa kweli amechukua ofisi hii muda mfupi uliopita lakini jitihada zake zinaonekana wazi kwamba anakwenda kufanya kitu. Jitihada tumeziona na mimi juzi wakati anazungumza kwenye semina pale niliwaambia wenzangu naona Mheshimiwa Waziri hii tune ambayo ameizungumza hapa leo, hii ndiyo tune ya maliasili. Maana yake kuna tune ambayo unaweza ukaiongea mahali pengine lakini kuna tune nyingine hiyo ndiyo ya kuiongelea kwenye Maliasili na ndiyo ile Mheshimiwa Waziri uliyozungumzia ukamalizia pale kwenye semina juzi, ile ndiyo tune ya kuizungumza katika uendelezaji wa maliasili popote duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia mambo manne kama muda utaruhusu. Jambo la kwanza ninazungumzia kuhusu suala la uendelezaji wa hifadhi zetu. Kama inavyofahamika kwamba hifadhi zetu zimeongezeka kutoka hifadhi 16 mpaka kwenda kuwa hifadhi 22, eneo la hifadhi limeongezeka kufikia karibu kama sijakosea kilometa za mraba sasa hivi 105,000 hivi kama. Eneo ni kubwa lakini bajeti haikuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulizungumzia hili hapa hali kadhalika wakati tunatoa ripoti ya nusu mwaka Kamati pia ilipendekeza kwamba lazima tuangalie uwezekano wa kuongeza bajeti katika hifadhi zetu ili ziweze kukidhi changamoto ambazo zinatokea kwenye uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwaka jana wakati ana-conclude speech yake hapa aliahidi kwamba hifadhi atazipatia bajeti ya miezi miwili kwa utangulizi ili bajeti moja ibakie kama spare in case ikitokezea dharura za moto, dharura za uhifadhi zote zile itatumika lakini utatuzi huu haukusaidia sana. Hifadhi zetu bado zinateseka na tatizo la kibajeti na zinahitaji mchango mkubwa kwenye bajeti. Kwa hiyo mimi napendekeza kama alivyozungumza Mheshimiwa Hawa Mwaifunga hapa kwamba pamoja na changamoto za retention ambazo zilipelekea retention kuondoshwa, mimi naomba tena retention tuirejeshe hata kwa asilimia siyo ile iwe pungufu lakini retention ni muhimu katika masuala ya uhifadhi. Hiyo ni kama utaratibu wa kidunia. Masuala ya uhifadhi lazima kuwe kuna retention ambayo inatumika kwa sababu ukifuata utaratibu wa kawaida wa kibajeti basi hutozisaidia sana kwa sababu mambo mengi ya kidharura yakitokezea hutoweza kuyashughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ningependa kuzungumzia kuhusu mwenzangu ambaye amechangia kuhusu Msomera. Nahisi kama tunakwenda kusahau changamoto ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Tulipelekea kufanya maamuzi yale tuliyopelekea watu waende Msomera kwa sababu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iko hatarini, hizi hatari zilizungumzwa hapa na watu wakafika mpaka kutoa machozi kutokana na tatizo la Mamlaka ya Ngorongoro lakini sijui ni utaratibu wetu au utamaduni wetu watanzania, jambo tunaweza tukalichukua kwa kasi kubwa lakini baadae tukapoteza mood.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi mood ya Ngorongoro imeanza kupungua. Sasa nilichangia hapa katika ripoti ya Kamati ya nusu mwaka nikazungumza kwa sababu wenzetu wameshafanya utafiti wamesema wakipata shilingi bilioni 200 basi hii kazi inakwenda kuisha. Nikazungumza kwamba kwa sababu makusanyo ya Mamlaka ya Ngorongoro yenyewe tu yanakaribia shilingi bilioni 200, sasa kama hatuna fedha basi Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuwaruhusu wenzetu wa Ngorongoro wanachokikusanya wakitumie ili tuondoshe hili tatizo, lakini kama kuna uwezekano mwingine basi tuwakopee, tutafute mahali tukope hili jambo tulimalize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waswahili wanasema, “Mchuzi wa mbwa unywewe ukiwa wa moto.” Sasa suala la Ngorongoro tulimalize likiwa liko moto moto, tukikaa hapa miaka mitatu, minne, mitano tutapoteza dira nzima ya masuala ya Ngorongoro ambayo tilishakubaliana nayo hapa. Kwa hiyo niombe Wizara na zaidi Waziri wa Fedha tuwapatie wenzetu Mamlaka ya Ngorongoro, tuwapatie wenzetu wa Maliasili fedha kwenda kumaliza hili suala. Tusifanye kazi zetu kwa vipande vipande, tunafanya kazi nusu, nusu inabakia mwaka mzima, matokeo yake tuna vipande vipande dunia nzima hatuendi hivi. Kwa hiyo mimi naomba hili tukalisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni kuhusu Jeshi USU ambalo pia mwenzangu hapa amelizungumzia, sasa hivi limepandishwa daraja limekuwa Jeshi la Uhifadhi. Tunalo tatizo kubwa kuhusu suala zima la Jeshi la Uhifadhi maslahi yao siyo mazuri. Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa na alikuwa anakaribia kutoa machozi, Jeshi la Uhifadhi wanapata shida sana. Wanakufa, wanauliwa, wanajeruhiwa lakini maslahi yao hayaendani na kazi wanayoifanya. Watu wa Jeshi USU au Jeshi la Uhifadhi wako kwenye mapambano mwaka mzima, wawe mitaani mwaka mzima anaingia kazini bismillah kwanza ana mapambano na wanyamapori lakini ana mapambano na majangili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuende tukarebishe maslahi ya Jeshi la Uhifadhi na hili mimi nilitegemea, kwa sababu tunaambiwa kwamba watu wa utumishi ndiyo wanalishulikia hili suala, kuna suala sijui waraka tayari umeishapelekwa wapi? jamani tusifanye kwa mazoea hebu tukifanya mambo tuyamalize, hawa watu wanauhitaji. Hapa nitoe ombi maalum vijana wetu wanaomaliza Olmotonyi, Mweka ambao ndiyo tunategemea tuwaajiri kwenda kuwa Jeshi la Uhifadhi, kwa sababu hatuajiri kila mwaka tunakaa miaka miwili, miaka mitatu wanapitwa na umri, sasa hili suala la umri Mheshimiwa Waziri hebu liangalie hili, tusiwaache hawa vijana ambao tayari wameishamaliza chuo na wana vigezo vyote, lakini suala la umri linakwenda kuwasumbua. Kwa hiyo ningeomba tu suala la umri ingawa lipo kisheria, hebu tukaliangalie kwamba wanafunzi wote ambao hawajaajiriwa wanachuo wetu basi ikitokea nafasi wawe na nafasi sawa ya kuomba kuweza kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ni kuhusu suala la hewa ya ukaa. Nimshukuru sana Mheshimiwa Jafo amepiga hatua kubwa kwa kutayarisha mwongozo wa suala zima la biashara ya hewa ukaa, lakini bado hatuendi kwa hatua kubwa hasa katika uelimishaji. Kwa sababu inaonekana kwamba biashara ya hewa ya ukaa ni kama vile Serikali ndiyo itaongoza kila kitu. Hii ni biashara huria isipokuwa Serikali inatakiwa iweke vigezo na kuwaruhusu wadau kuingia kwenye hii biashara. Kwa hiyo, tuende tukatoe elimu kwa sababu ina faida kubwa katika uhifadhi wa misitu yetu hii ni incentive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa uharibifu wa misitu ni mkubwa sana kwa Tanzania. Tunapoteza karibu hekta laki nne kila mwaka, sasa watu wanafikiria kwamba ukishakuwa na msitu tayari wewe uko eligible kuweza kupata fedha za hewa ya ukaa. Kupata fedha za hewa ya ukaa ni incentive ya uhifadhi, umehifadhi kwa kiwango gani? kwa hiyo, kile kiwango ambacho kinaongeza (additionality permanence) ya uhifadhi ndiyo inayokwenda kukupa credit ya biashara ya hewa ya ukaa. Kwa hiyo, twende tukatoe elimu kwa wananchi wetu, tukawambie kwamba kuwa na msitu ni jambo moja lakini suala la kuulinda, kuhifadhi usichomwe moto, usikatwe hovyo, usiharibiwe ndiyo utakwenda ku – add value wewe kupata fedha za hewa ya ukaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala zima la utafiti. Tuna taasisi zetu za utafiti za TAFORI na TAWIRI lakini nazo hizi zina tatizo kubwa la kibajeti na tumelizungumzia hapa, ukienda TAFORI kwa mfano, inafika wakati hata kuweza kulipa umeme hawawezi, ile kulipa umeme hawawezi inamaana inabidi wachangishane ofisini wakalipe umeme wa ofisi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeliomba Mheshimiwa Waziri, tukazingalie hizi Taasisi za Utafiti, kwa sababu hakuna nchi ambayo itaendelea bila utafiti, hakuna eneo ambalo utalifanyia kazi bila utafiti, ili wafanye utafiti vizuri lazima tuendeleze kibajeti. Sasa ningeliomba tu angalau fedha ambazo zilikuwa zinatengwa tuwaongezee ziongezeke kidogo kadhalika na fedha zenyewe zipatikane kwa wakati, siyo fedha zinatengwa asilimia 100 lakini wanapata asilimia 26 mwaka ukimalizika, hii haitusadii sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)