Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii na namshukuru Mbunge mwenzangu kwa kunipa fursa hii ya kuchangia dakika zake tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili tu, la kwanza ni suala linaloendelea hapa Bungeni mara kwa mara, Wabunge wengi wakichangia na hasa wa maeneo ya Kusini wanajaribu kuonesha kwamba Kaskazini kumeendelea sana. Sasa hofu yangu dhana hiyo inaweza ikapoteza mwelekeo wa Serikali katika kupanga keki ya Taifa, kwa kuamini kwamba Kaskazini kumeendelea kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizungumzia Kanda ya Kaskazini unazungumzia Tanga, ukienda kwenye Majimbo ya Tanga kuhusu barabara utapata shida, sasa ikioneshwa kwamba Kaskazini kumeendelea, maana yake ni kwamba hayo Majimbo yote yana barabara nzuri za lami, yanapitika vizuri, kitu ambacho siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda Manyara ni Kaskazini, maeneo ya Wamasai, hayapitiki; kwa hiyo, hoja ya kwamba Kaskazini kumeendelea pia siyo ya ukweli kama inavyozungumzwa hapa Bungeni. Ni jambo jema kufikiri kwamba kama kuna maeneo hayajaunganishwa mkoa kwa mkoa likatekelezwa hilo, kwa sababu ni sera ya Serikali. Yale ambayo yalishaunganishwa mkoa kwa mkoa yaunganishwe wilaya kwa wilaya, yale ambayo Wilaya zilishamalizika yataunganishwa Kata kwa Kata na hatuwezi kwa pamoja katika nchi hii, kuendelea kwa kiwango cha aina moja kwa wakati mmoja, tunapogawa resources za Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tukubaliane tu kwamba kwenye Bunge hili, sote katika nchi hii kama walipa kodi na wachangiaji wa Pato la Taifa tunapaswa kugawana keki ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kaskazini reli ya Tanga mpaka Arusha, hapa ni wimbo, ukijiuliza ni kwa nini reli hiyo mpaka sasa iko katika hali ile, wala kabla hatujafikia upembuzi yakinifu bado ile reli ingefaa kutumika na ikainua sana uchumi wa Kanda ya Kaskazini. Hata hivyo, reli ile mpaka sasa haifanyi kazi, lakini bado kuna dhana kwamba Kaskazini kumeendelea. Ukienda kule Kilimanjaro ukienda Upareni utasikitika, bado unaambiwa Kilimanjaro kumeendelea au Kaskazini kumeendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hilo ili kuweka rekodi sawa, kwamba Taifa hili lina uhitaji unaofanana katika mahitaji yote ya barabara, mahitaji ya reli na mahitaji mengine yoyote yanayohusu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri alivyoleta bajeti yake, ni lazima aiangalie Kaskazini kama anavyoiangalia Kusini na Magharibi na Mashariki mwa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongee suala la pili kuhusu TRL na RAHCO. Mpaka mwaka 2002, Shirika la Reli (TRC) lilikuwa na uwezo wa kufanya kazi yake vizuri. Mpaka mwaka 2002 Shirika la TRC lilikuwa na vichwa 68, mpaka mwaka 2002 Shirika la TRC lilikuwa na mabehewa 1,500 mpaka mwaka 2002 Shirika la TRC lilikuwa na uwezo wa kusafirisha tani 1,500,000; kwa hiyo, mgawanyiko kati ya TRC na RAHCO, ndiyo umeleta shida katika Shirika la Reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana ni makosa ya Serikali kuingia kwenye mkataba ambao haukuwa mzuri, kati yake na kampuni ya wenzetu wa India, ndiyo uliosababisha hali hii iliyojitokeza. Sasa rai yangu kwa Serikali, ni lazima hapa leo tutoke na azimio katika Bunge lako Tukufu la kuunganisha RAHCO na TRL, ni lazima tutoke na tamko hilo, vinginevyo maeneo mengi yaliyokuwa yakifanya vizuri kipindi cha TRC yatakuwa ni magofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TRC ilikuwa na karakana nzuri, ilikuwa inahudumia reli yake vizuri, lakini leo maeneo yote hayo hayafanyi vizuri kwa sababu ya TRL kunyimwa nguvu na Shirika la RAHCO ambalo ukiangalia kwa nini lipo hupati majibu yaliyokamilika. TRL haina uwezo wa kukopa, kwa sababu haina dhamana, lakini TRL ndiyo inayoangalia mabehewa yake, vichwa vyake na reli kwa wakati mwingine, naomba sana, muunganishe TRL na RAHCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.