Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, inaelekea Waheshimiwa Wabunge wanataka twende kwenye Kamati ya Matumizi moja kwa moja, lakini kwa kuwa kuna masuala waliuliza na waliyachangia basi kwa heshima na taadhima na kwa kibali chako ningependa kujielekeza kwenye baadhi ya hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe shukrani kubwa sana kwako na shukrani kubwa na nyingi kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii kwa kuzungumza na kwa maandishi. Tumefarijika sana kwa sababu michango ni mizuri sana, michango iliyotupa elimu kubwa, iliyotuhamasisha, iliyotutia moyo, iliyotuelimisha, iliyotufikirisha. Kwa hiyo tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kweli kwa kuitendea haki hoja yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waliochangia ni wengi, wamezidi 70, nadhani ni rekodi katika hoja za hivi karibuni, na hatutaweza katika muda huu tulionao kutoa majibu yote na kwa wote; ila tumefanya jambo kidogo tofauti kwamba mkienda kwenye visimbuzi vyenu tayari hivi ninavyozungumza majibu tumeshayatoa kwa Waheshimiwa Wabunge wote. Nimshukuru pia Naibu Waziri naye kwa kunisaidia na kusaidia kujibu baadhi ya hoja vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nijielekeze kwenye baadhi ya mambo yaliyozungumzwa na Wabunge wengi kwa makundi. Kwanza ni kuhusu suala la LNG. Hili ni jambo kubwa sana, na sisi tumefarijika kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumzia. Katika bajeti yetu hii, kutokana na nchi yetu kuingia kwenye mradi huu Bajeti ya Wizara ya Nishati inatazamwa na Dunia ya Nishati. Kwa sababu Mradi wa LNG Tanzania ni mradi wa usalama wa nishati duniani; ni Global Energy Security Project. Kwa sababu hii gesi inapelekwa kwenye masoko ya nchi kubwa zenye viwanda zilizoendelea zenye njaa ya nishati, kwa hiyo uhakika wa upatikanaji wa gesi hii ni suala linalotazamwa na wengi. Kwa hiyo wenzetu dunia nzima walikuwa wanatazama Tanzania tunasemaje kuhusu huu mradi?

Mheshimiwa Spika, lakini siyo bajeti yetu tu, hata michango ya Wabunge ilikuwa na yenyewe inatazamwa. Je, hao wawakilishi wa wananchi na wenyewe wanasemaje? Huu mradi wanauchukuliaje? Naomba niwape mrejesho kwamba wenzetu wamefarijika sana kwamba kuna hamasa kubwa, kuna uelewa mkubwa na kuna hamu kubwa miongoni mwa viongozi wa nchi yetu, kwa sababu ninyi ndio viongozi, kuhusu mradi huu. Kwa hiyo tumefarijika sana kwa mchango wenu na umetupa nguvu sisi tunaosimamia mradi huu kwamba si mnaona? Mradi huu una support ya wananchi kupitia wawakilishi wao. Kwa hiyo tunapenda niwashukuru sana kwa hilo na tutapenda pia kuwaomba katika hatua zinazokuja ikiwemo sheria mahususi ya mradi huu; kwa sababu kama nilivyoeleza kwenye hotuba yetu tutatengeneza project law ya LNG tutaleta Bungeni hapa sheria mahususi ya mradi ili muone vitu gani vitasaidia kuendesha mradi huu ili uwe na tija na manufaa na maslahi kwa nchi. Kwa hiyo Bunge litakuwa na nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba pia tutakapokuja wakati huo pia moyo mliouonyesha katika hatua hii pia muendelee kwa sababu wataendelea kutazama. Kwa hiyo nawashukuru sana sisi tumeyapokea ushauri mlioutoa kwamba tuharakishe utekelezaji, na tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la kukatika katika kwa umeme. Hili Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza, na labda niseme tu kwamba suala hili ni changamoto ya muda mrefu. Kwenye bajeti yetu lilizungumzwa pia na siku za nyuma pia limezungumzwa. Tunafarijika kwamba sasa hivi ni kwa maeneo mahususi. Kwenye bajeti ya mwaka jana ni Wabunge wengi zaidi lilikuwa linawagusa katika maeneo yao, lakini kadiri muda unavyoenda maeneo yanapungua, hatusemi tumemaliza lakini maeneo yanapungua.

Mheshimiwa Spika, hili suala ni la kihistoria, labda nichukue muda kulieleza kidogo. Utakumbuka kwenye miaka ya 1990 nchi yetu iliingia kwenye hamu ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Na ikawa ikiamuliwa kwamba shirika libinafsishwe linawekwa kwenye kundi la makampuni yanaitwa specified na linakuwa gazetted kabisa. Na ikishaamuliwa hivyo, Serikali inasimamisha uwekezaji katika shirika hilo na inasimamisha hata ajira. Kwa hiyo moja ya shirika mwaka nadhani 1993/1994 lililowekwa kwenye kundi la ubinafsishaji ilikuwa ni TANESCO miaka hiyo. Baada ya uamuzi ule kufanyika ajira zilisimama, uzalishaji wa umeme ulisimama, ujenzi wa miundombinu ulisimama, ukarabati wa miundombinu ulisimama kwa sababu tulikuwa tunasema tutalibinafsisha.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya uamuzi wa kulibinafsisha ukachukua muda mrefu, takribani miaka 10 haukufanyika. Baadaye uamuzi ulipofanyika ulikuwa hatubinafsishi tena, libaki shirika la umma. Lakini katika kipindi ambacho uamuzi huo ulikuwa unatafakariwa, ni kipindi ambapo uchumi ulikuwa una kua kwa kasi sana, idadi ya watu inaongezeka, tumefungua uchumi wetu kwenye dunia na wawekezaji wanakuja. Kwa hiyo katika kipindi ambacho uzalishaji wa umeme umesimama, ujenzi wa miundombinu umesimama ndipo ambapo nchi ilikuwa inaenda mbele kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ile historia ya miaka 10 ya kutokuwa na ukarabati, uwekezaji wala uzalishaji malipo yake ndiyo tunayalipa sasa. Ndiyo, kwa hiyo lazima historia tuwe nayo sahihi. Sasa kwenye umeme, kama nilivyosema, kuna uzalishaji wa umeme, kuna usafirishaji kwenye yale mawaya makubwa na kuna usambazaji. Hivi vitu vyote lazima viwe sawa ili uweze kupata umeme wa uhakika. Tukiwa wakweli wa nafsi zetu, na kwa sababu sisi ni viongozi tuna wajibu wa kusema ukweli, hatukuwa na umeme wa kutosha. Nchi yetu yenye watu milioni 60, sisi tunao safiri duniani ukiwa Waziri wa Nishati swali la kwanza vipi mna megawati ngapi na kule wanatumia gigawatt, 1,800 wanasema 1.8 gigawatt.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nchi yetu tunasema tuna umeme 1.8 gigawatt. Mimi huwa nawaambia watu wangu tusitumie neno gigawatt, tutumie neno megawatt angalau zionekane nyingi, 1,800. Kwa sababu kwenye nchi nyingine umeme wa nchi yetu 1.8 gigawatt au megawatt 1,800 ni umeme wa sehemu kama Kisesa, mtaa sio umeme wa nchi. Sasa kwenye nchi ambayo ina malengo makubwa ya maendeleo kama yetu, watu wanaongezeka kwa kiasi kikubwa, shughuli zinapanuka, lazima tuondoke katika hali hii. Na katika uamuzi wa kijasiri uliowahi kufanyika katika nchi hii ni uamuzi uliofanywa na Rais wa Awamu ya Tano ya kujenga Bwawa la Julius Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ule utatupunguzia aibu ya kusema 1.8 gigawatt. Na ilani yetu imetuelekeza kwamba ifikapo 2025 walau tuwe tumefika 5,000; 5.0 gigawatt. Bado, bado. Na sisi sasa hivi tunadhani tuna umeme wa kutosha, lakini ni kwa sababu; ninaenda kwenye jambo la pili la usafirishaji na usambazaji; umeme huu tunaona unatosha kwa sababu haujawafikia wote wanaouhitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo tunaingia jambo la pili, la miundombinu. Leo hii tukiweza kutimiza mahitaji ya Mheshimiwa Dotto Biteko na wamezungumza Wabunge wa Geita, Wabunge wa Kahama rafiki zangu Kassim na Cherehani na Dada Rose pale. Tukiweza kuipa migodi yote inayotumia diesel leo umeme ni megawatt 1,200 kwa mpigo. Naomba nirudie. Tukiweza kuipa migodi yote nchini sasa hivi inayotumia diesel tukiweza kuipa umeme itatumia umeme sawa na umeme wote tulionao siku ya leo, mwaka huu katika kipindi hiki. Maana yake ni kwamba bado hatujawafikia Watanzania wengi wanaohitaji umeme, acha kwenye nyumba hata kwenye maeneo ya kilimo, uzalishaji na migodi.

Mheshimiwa Spika, usambazaji; umeme unaenda kwenye mitaa yetu na kwenye wilaya zetu. Na kitaalamu umeme wa usafirishaji una nyaya zake, umeme wa usamabzaji una nyaya zake. Nyaya za umeme wa usambazaji ni za bei nafuu, za usafirishaji ni za bei ghali. Sasa ili huko nyuma tuweze kupeleka umeme kila mahali, tukawa tunasafirisha umeme kwa njia za usambazaji. Matokeo yake Mheshimiwa Simbachawene pale, line inayotoka hapa Zuzu inaenda Mpwapwa, inaenda Kongwa, inatokea Gairo inaenda Kiteto ni line hiyo hiyo moja kilometa zaidi ya 1,000 wakati ilipaswa kwenda kilometa 100 tu.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba nguzo ikianguka hapo Mvumi huko kwenda umeme unakatika mpaka Kiteto. Sasa ndiyo changamoto tuliyonayo na ndio ukweli wenyewe na ni maeneo mengi. Tabora pale mji mzima wa Tabora una waya mmoja tu mrefu, mpaka Urambo, ulikuwa ni waya huo huo mmoja kilometa 1,200. Sasa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita alivyoingia madarakani akatupa hii kazi umeme ukawa unakatika tukaanza kunyoshewa vidole, ni yule Bwana Kipara pale ndiye anakata umeme. Ni Bwana Maharage pale ndiyo anakata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tulichofanya tukakaa tukajifungia na wataalamu wale mnaowaona tukawaambia hebu tuambieni ukweli. Maana kulikuwa na dhana kwamba ni hujuma. Mimi siamini kabisa mtu ameajiriwa TANESCO ahujumu kukata umeme kuzima umeme kwa sababu ndiyo maisha yake. Ndipo wakasema wakuu, unajua Serikali tunaitana wakuu. Wakasema mkuu, nikwaambia hebu acheni mambo ya mkuu, hebu semeni tu kinachoendelea. Ndipo tukapewa uchambuzi wa hali ilivyo, na sisi tukapendekeza mpango mahususi mkubwa, unaitwa Grid Imara, wa gharama kubwa sana wa kubadilisha nyaya za zamani kuweka nyaya nene zaidi. Pia kuvalisha nguo zile nyaya, kubadilisha transformer, kujenga na line nyingine mpya. Tukauita Mradi wa Grid Imara wa trilioni 4.4 tukaenda kwa kiongozi wetu Mheshimiwa Rais tukamuwasilishia ule mpango akasema sawa nitawaanzia na shilingi bilioni 500, tukaja Bungeni mkatuidhinishia. Tukaenda tukaanza awamu ya kwanza tukatafuta wakandarasi 26 sasa hivi miradi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,Hii ni safari. Sitaki kuwadanganya kwamba umeme utaacha kukatika mwakani au mwaka unaofuatia. Ambacho nawaahidi tumeweka jitihada kila mwaka tutakuwa tunapunguza changamoto hii. Mpaka mpango huu ukamilike. Hakuna watu wanaoumia kunapokuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme kama sisi tunaosimamia sekta kama wataalamu kule TANESCO. Kwa hiyo tunafahamu madhara kwa uchumi, kwa vifaa vyetu kutokana na kukatika kwa umeme ila naomba muiamini Serikali. Na mimi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, mara moja alielewa, mara moja aliridhia, mara moja aliidhinisha na Bunge hili tunalishukuru kwamba mara moja na nyie mlielewa na mara moja mliridhia na mkaidhisha ule mpango.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa, mwaka huu tumeomba zaidi shilingi bilioni 400 zaidi kwa kuendelea na ule mpango. Kwa hiyo sasa sisi hapa nchini ili umeme uwe imara walau kila wilaya iwe na kituo cha kupozea umeme (substation). Ninyi mnatoka huko wilayani, nchi nzima kuna vituo 46 tu, wilaya 46 tu ndizo zina vituo katika wilaya zetu zote. Tumekuja na mpango mwingine wa kujenga substation kwenye kila wilaya.

Mheshimiwa Spika, safari ya kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa ni safari siyo tukio, ni safari. Tunachoomba ni subira na uvumilivu; na wakati mwingine tupeane nafasi.

Mheshimiwa Spika, siku moja hapa umeme umekatika Bungeni kulitokea hitilafu, ghafla bana fukuza Waziri, fukuza TANESCO. Kumbe kuja kuchunguza wala; umeme umekatika kwenye uwanja wa mpira, fukuza Waziri, fukuza TANESCO, kumbe ni mambo mengine. Kukiwa na mkutano watu wakichezea chezea huko umeme ukikatika fukuza. Jamani si wakati wote ni TANESCO na si wakati wote ni Wizara. Sisi tutachukua wajibu wetu pale linapotokea na moja ya hatua ni kuimarisha shirika lenyewe linalofanya kazi hii ili liwe na weledi. Na mmeona mliotembelea pale mabadiliko makubwa yanayoendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye hili la kukatika kwa umeme tutapunguza, lakini sitaki kuwaambia kwamba kesho itaisha. Wote tutawapa na tutaweka dash board muingie muone maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Grid Imara. Tutawapa link muone wapi tumebadilisha, wapi hali imebadilika, wapi tatizo lipo ili muweze na ninyi kufuatilia, ili na nyie mtusaidie kusema kwa wananchi. Hilo tutalifanya katika kipindi cha miezi miwili ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Julius Nyerere ni mradi wa kihistoria kama nilivyoeleza na umezungumzwa sana hapa na tunawashukuru sana kwa kuunga mkono. Tulileta ile teknolojia ili muone maendeleo kwa sababu walau inaitwa virtual reality yaani unakaribiana na ukweli wenyewe. Naomba nitoe tangazo hapa kwenye Bunge kwa ridhaa yako, sisi tuko tayari, si tu kusafiri kutokea hapa Bungeni kwa kuvaa miwani, kwa ratiba Mheshimiwa Spika atakayoweka, kwa logistics zitakavyokuwa tuko tayari kuwasafirisha Waheshimiwa Wabunge wote kwenda kwenye mradi mkauone wenyewe wakati wowote ili tusiishie hapa; na hilo tutaongea na Ofisi ya Mheshimiwa Spika ili tuweze kuliweka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kuna suala la mradi umechelewa, mradi umechelewa, mradi umechelewa, kwa nini hatujamkata mkandarasi limezungumzwa. Miradi hii ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ina ukubwa tofauti. Huu ni mradi mkubwa katika ukanda huu. Mkataba wa kwanza ulikuwa miaka mitatu ya ujenzi lakini ukiangalia miradi mingine, ukienda Kihansi, Mtera, Hale, Pangani Falls hamna mradi kati ya hiyo na ni midogo megawati 80, megawati 200, 180 hakuna uliojengwa chini ya miaka mitano. Naomba nirudie, mradi wa megawati 80 hapa Mtera umejengwa miaka sita.

Mheshimiwa Spika, mradi wa Julius Nyerere sisi tulipanga kuujenga; fikiria ni megawati 2,000; tulipanga kuujenga kwa miaka mitatu. Sasa CAG alitusema kwamba hakukuwa na ukadiriaji sahihi wa muda wa ujenzi wa mradi, na alikuwa sahihi kabisa. Hakuna mahali popote unaweza kujenga megawati 2,115 kwa miaka mtatu, hakuna. Kwa hiyo ndio ukweli. Mchungu lakini ndiyo ukweli. Sasa muda umeongezeka, muda ukiongezeka mkataba uliowekwa una namna za kushughulikia mambo hayo ndani ya mkataba. Hadi leo hatujavunja mkataba kwa sababu hata hiyo nyongeza imeelezewa ndani ya mkataba itafanyikaje.

Mheshimiwa Spika, kuna habari kwamba watu wanakwenda mahakamani si kweli. Na kuhusu malipo kwa hiyo nyongeza. Kuna hoja hapa kwa nini hamumkati mkandarasi kwa kupitisha muda. Hiyo dhana ya kumkata siyo sahihi kwa sababu fedha tunazo sisi si kwamba anazo yeye, tunazo sisi. Sasa haki ya kubaki nazo hatujaipoteza. Naomba nirudie, haki ya kubaki nazo hatujaipoteza. Ilikuwa ni suala la busara, tu kwamba je, ile Juni mwaka jana mradi ukiwa asilimia 60 ndipo ufanye fujo wakati ule? Au utumie busara usiipoteze haki yako mradi usonge mbele hadi huko mbele? Kwa sababu hupotezi ile haki mpaka siku ya mwisho.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna baadhi ya watu hapa wanasema hakuna kamata hao, zuia, zima, ondoa, leta mwingine. Mnajua mobilization ya mkandarasi mpya pale inavyokuwa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wakati mwingine maarifa, weledi, mkakati unahitajika kusimamia hii miradi mikubwa. Mradi leo uko asilimia 87 haikutokea kwa ajali imetokea kwa maarifa, kwa weredi na kwa mkakati, hakuna hata siku moja kazi imesimama pale na mambo yanaendelea. Kwa sababu tumeamua kutofautisha, kushughulikia mikataba na kusimamia mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu pia ulianza pia kama sehemu ya mahusiano kati ya nchi na nchi, marais wawili walizungumza, kwa sababu ni mradi mkubwa. Mkandarasi kutoka Misri, haiwezekani mkandarasi kutoka Misri wa mradi mkubwa kama kuu viongozi wasiwe na mahusiano katika kuuzungumzia. Kwa hiyo pia mradi huu unalelewa na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi zetu mbili Misri na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu mimi nimeingia katika nafasi hii Mheshimiwa Rais wetu amekutana na Rais wa Misri mara tatu na mimi nikiwepo. Mheshimiwa Rais wetu ametuma Mjumbe maalum Misri kwa barua maalum kuhusu mradi na Rais wa Misri ametuma Mjumbe maalum hapa kuhusu mradi huu. Kwa hiyo mradi huu pia unalelewa na mahusiano kati ya nchi zetu mbili, hauwezi kufeli. Na katika kushughulikia mradi huu lazima tulizingatie na hilo, hatuwezi kuliacha; ndiyo maana hamna mambo ya Mahakamani haitotokea. Juzi tu tumepokea mjumbe maalum pia mwingine wa Rais wa Misri kuhusu mradi huu. Kwa hiyo naomba mtuamini, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeweka sayansi ya usimamizi wa miradi, tunaizingatia, tumefika pazuri sana, mradi huu utakwisha salama kwa kibali cha Mwenyezi Mungu na tutawapeleka mkaone, mtafurahi na mtapata fahari ya uwezo wa Watanzania wenzenu kufanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mambo ambayo yanapaswa kutuunganisha Watanzania ni huu mradi. Hii dhana kwamba kuna watu wanataka kuhujumu, kuna watu hawautaki, kuna watu wamefanya kosa hapa, kuna watu nini na nini; mimi naomba huu mradi tusiutumie kupata sifa ya siasa kabisa. Kwamba mimi ndiyo mbabe zaidi, ndiyo naweza kuusimamia kuliko watu wote waliyopewa dhamana ya kusimamia mradi huu. Naomba siasa iwekwe pembeni na mradi huu kabisa, mradi huu ni mkubwa wa heshima na wa bei kubwa sana kwa fahari ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu CSR imezungumzwa hapa ni sehemu ya makubaliano ya mradi huu. Tulikubaliana wakati tunausaini kwamba asilimia 3 itatumika kwa miradi ya kijamii, lakini tukimlipa kwa wakati kwa miaka miwili tutapata asilimia moja ya ziadi, kwa hiyo imekuwa asilimia 4 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 262. Sasa zile fedha kwenye yale makubaliano kulikuwa na makubaliano zitumike wapi? elimu na afya lakini baadaye ukafanyika uamuzi kwamba hapana tujenge uwanja wa mpira na barabara.

Mheshimiwa Spika, sasa tukakorofishana na mkandarasi kwa sababu yeye alisema siyo mkataba. Kwa hiyo kile kipindi cha mabishano kilikuwa kirefu mno na hatukufikia mwisho ndiyo maana miradi hii imechelewa kwa sababu kuna sababu mbona hamjafanya? mbona mmechelewa? kwa sababu sisi wenyewe tuliamua kuamua tofauti. Kwa hiyo tukabishana tukaenda mbele, nyuma baadaye busara ikatamalaki kwamba jamani ee pia afya na elimu ni muhimu. Kwa hiyo turudi kwenye makubaliano ya awali, hapo muda ulikuwa umeisha kwenda pia vilevile.

Mheshimiwa Spika, baada ya pale sasa vikaanza vikao, na kwa sababu ni elimu na afya sisi tukatafuta vikao na wenzetu, kwamba jamani nyie sekta ya elimu, sekta ya afya vitu gani muhimu kwenu ili tuweze ku-finance huu mradi? Tukaletewa vyuo vya juu vya ufundi na maeneo tukaletewa na kwa sababu yalikidhi haja na kwa sababu katika vyuo hivi watasoma vijana wote wa Kitanzania kutoka kila kona ya Tanzania. Sisi suala la pahala hatukuliona ni suala kubwa, kiwe Rufiji, kiwe Dar es salaam, kiwe Morogoro kama chuo cha UDOM hapa kipo Dodoma lakini asilimia ngapi ya watu wa Dodoma wanasoma hapa? Watanzania wote wanasoma pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukaona kwamba tusiingie kwenye changu, changu, leta kwangu na nini? ila kitu ambacho tunakili ni kwamba wenzetu ambao mikoa yao, wilaya zao, maeneo yao yapo kwenye mradi wanao wajibu mahususi, wanayo majukumu mahususi. Kwa hiyo pia tutazingatia hilo vilevile. Pamoja na kwamba imeamuliwa kwamba tujenge hivi vyuo vikuu vitatu vya juu vya ufundi siyo VETA juu ya VETA very technical lakini tutafanya Morogoro, Pwani na kwingineko tutafanya vitu kwenye afya na kwenye elimu kwa sababu hatuwezi kutoka hapo. Kwa hiyo katika fedha upya tumewasikia Mheshimiwa Kalogeris tuandikieni, Waheshimiwa Pwani vilevile nimemuona Kuchauka naye anasema Liwale pia ni Rufiji sawa na yeye tumepokea, tumepokea kuhusu miradi mingine ya elimu na afya katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba hii fedha ya CSR imeliwa, imeibiwa si kweli, fedha ipo kwenye mkataba na ipo na tayari chuo cha kwanza Lindi tumeishaona mahala, watu wameishakwenda, watu wameishapima, michoro imeishafanywa na Mungu akijalia mwezi wa saba tutaweka jiwe la msingi pale na kazi itaanza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi kama nilivyosema Mheshimiwa Rais alipokea Mjumbe maalum wa Rais wa Misri akiwa na barua maalum kutoka kwa Rais wa Misri na moja na ya mambo tuliyozungumza ni utekelezaji wa Miradi ya CSR. Kwa hiyo liko hata kwenye ngazi ya juu litafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la nishati ya kupikia sisi tunafarijika sana kwamba tumefanikiwa. Kama Bunge kama Serikali kupika na namna ya kupika inachukua takribani asilimia 30 ya mazungumzo ya Bajeti ya Nishati. Hiyo haijapata kutokea. Kwa sababu siku zote tukizungumza nishati, tunazungumza mafuta, umeme, gesi. Sasa ukiweza kuingiza ajenda mpya inayowagusa watanzania kwenye masuala ya Serikali umefanikiwa jambo kubwa. Wakati tunaanza sisi ilikuwa ni mashambulizi jambo gani hili na nini? lakini tume – force mpaka nishati ya kupikia ni mjadala sasa hivi. Kwa hiyo tumeanza mjadala, tumekuja tafakuri sasa tunaenda kwenye hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tumefurahi sana kwamba Waheshimiwa Wabunge wamehamasika, wameelewa, wameibeba ajenda hii kwa sababu inagusa watu wao. Na pia tumepanua wigo wa masuala sisi wanasiasa ya kuzungumzia kuhusu wanawake, kwa sababu nyuma ilikuwa ni unyanyasaji wa kijinsia, uwezeshaji wa kiuchumi, maji. Kwa hiyo masuala ya wanawake tulikuwa tunazungmza siasa na kwenye majukwaa ilikuwa ni narrow, sasa tumeongeza jambo jipya juu ya nishati ya kupikia ambalo tukilifanya vizuri wote tunapata manufaa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Lakini pia tunamwezesha mtoto wa kike na yeye kufikia pale anapostaili kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili jambo ni gumu, si jepesi ni gumu. Substation tutajenga, umeme tutaweka mkandarasi atapeleka vijijini sijui bwawa litajengwa ni mambo ya kiufundi ukiwa na hela, ukiwa na mkandarasi linaenda. Suala linalohusu tabia, linahusu mazoea, linalogusa kila nyanja siyo jepesi kwa sababu linahitaji elimu sana, uwekezaji mkubwa, mabadiliko ya sera, mtazamo na kadhalika. Kwa hiyo siyo jepesi, linahitaji sisi sote tuunganishe nguvu. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais alivyoamua kuongoza jambo hili sisi tumepata Faraja, na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge na nyie mlipo libeba tumepata faraja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa tumeamua kufanya jambo hili kwa sababu hiyo hiyo, kwamba ni gumu. Wakati mwingine unaamua majambo siyo kwa sababu ni mepesi bali kwa sababu ni magumu ili kupima kiwango na nguvu yenu kama Chama kama Serikali ya kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii. Kwa hiyo hili ni kipimo chetu kuchukua jambo ambalo ni it intellectually challenging ni challenging kisera, kiutamaduni lakini linaleta ustawi wa watu. Kwa hiyo ningependa Waheshimiwa Wabunge tulibebe wote ili tuweze kuwasaidia akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na kumpongeza kwa sababu yeye ndiye Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kitaifa ya kufanya jambo hili. Ametuongoza, tumekaa vikao vinne. Sasa hivi tunayo rasimu ya mwisho ya dira, tunayo rasimu ya mwisho ya mpango mkakati unao elezea hatua kwa hatua nani afanye nini na kwa wakati gani ili tufike kwenye yale maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ndani ya miaka 10. Sasa moja ya mathalani tuliyofanya tunataka, tutagawa nishati hii mitungi, tutafunga mifumo ya kupikia kwenye Taasisi zetu mbalimbali hatuoni aibu, hatuogopi kuwapa Waheshimiwa Wabunge nyenzo ya kuhamasisha. Kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wana ushawishi. Ukitaka jambo lako lifike nchi nzima kwa wakati mmoja wape Wabunge kwa sababu wanafanya mikutano na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulisema hata kwenye bajeti mwaka jana, tulitenga na fedha hapa hapa mkapitisha ya mitungi laki moja. Hii tuliyowapa ni sehemu ya mitungi laki moja tuliyoipangia kwenye bajeti. Na utaratibu wa manunuzi umefanyika watu wameshindanishwa. Mtapata mitungi, kama msambazaji wa Kanda ya Ziwa ni fulani na anauwezo na kanda ile tutafanya, kwa wengine watagawiwa na mtu nyanda za kusini kama kampuni fulani ni u-strong upo. Kwa hiyo wale waliyokuwa wanasema hakuna maeneo ya ujazaji yapo kwa sababu waliyoshinda katika maeneo yenu ni wale wenye mtandao wa usambazaji katika maeneo yenu; kwa hiyo limefanyika, kwa hiyo tutaendelea leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la wafanyakazi wa TANESCO limezungumzwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa. Naomba niseme tu kwamba Shirika linapitia katika mabadiliko. Kuna masuala ambayo TANESCO tunaka ifanye, kuna matarajio tuliyonayo juu ya TANESCO, lakini vilevile kuna mahitaji ya uchumi mpya ya teknolojia mpya. Sasa, haya mabadiliko niseme wazi hapa hayana nia ya kupunguza mtu, hatutapunguza mtu, hatutapunguza mtu kazi TANESCO. Ila tutawahitaji wawe tayari kupokea ujuzi mpya na majukumu mapya yanayoendana na mahitaji ya dunia mpya vilevile, waondoke katika comfort zone kwasababu dunia ya huduma inabadilika, umeme ni huduma. Kwa hiyo tutawa-retrain, tutawawezesha lakini tutakuwa nao. Mtu ataacha kazi kwa kutaka yeye mwenyewe, hatoondelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wao wanajua wafanyakazi wa TANESCO, kwa mara ya kwanza katika miaka 17 tumewapandishia mshahara juzi. Miaka 17 hatukupandisha mshahara, sasa hivi tunapimana kwa matokeo, na jam ndiyo dunia ya kisasa, tunapimana kwa matokeo. Kwa hiyo naomba msiwe na wasi wasi mambo yatakuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu vinasaba tumelisikia lipo Serikalini linashughulikiwa, tutahakikisha kwamba suala hili linakaa mahala ambapo litakuwa na tija na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, umeme vitongojini. Waheshimiwa Wabunge hili ni jambo kubwa vilevile, ndoto yetu sisi ni kupeleka umeme kwenye kila kona ya nchi yetu. Mnafahamu vijiji vyote tutamaliza, vimebaki vijiji 2,000. Kila kijiji kina mkandarasi na kazi inaendelea. Lakini kama mnavyofahamu kila kijiji kina wastani wa vitongoji vitano. Kwa hiyo tunaposema tumepeleka vijiji vyote ni maana katika kitongoji kimoja katika vitongoji vitano kwenye kila kijiji. Sasa mtu atakupa kura kwa kumletea umeme karibu na alipo. Kura ukimwambia bana ule palee you know usiwe na wasi wasi umeuona ule tumefanya kazi nzuri; Hapana, lazima uwe pale, na huo ndiyo mwelekeo. Uwekezaji wa kuusogeza ili tuupeleke kwenye vitongoji kwa sababu lazima utue kijijini ili usambae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa sana imefanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Nne ya Tano na ya Sita, kazi kubwa sana imefanyika lazima tujisikie fahari kwamba tumemaliza vijiji lakini kazi kubwa ipo mbele yetu. Sasa sisi tulifanya utafiti tulipoingia tu kwenye nafasi hii, ni nini kinahitajika kupeleka umeme vitongoji vyote? fedha, vifaa, muda, rasilimali watu; tukapata huo uchambuzi tukatengeneza mpango lakini kwa kujua kwamba hatuwezi kwenda Hazina kusema haya hiyo tupeni fedha, tukaja pia na maarifa ya chanzo cha kugharamia pia huo mradi. Tukajadiliana ndani ya Serikali na kuchakata na kuangalia mahitaji mbalimbali. Tulikuwa tuanze mwaka huu wa fedha unaokuja lakini busara ikatamalaki kwamba chanzo kile kitumike jambo jingine, mambo mengine muhimu zaidi na sisi tuanze program yetu mwaka kesho kutwa unaofuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninapenda niwape Waheshimiwa Wabunge faraja kwamba mpango wa kupeleka umeme vitongoji vyote haujafa tumeuharisha kwa mwaka wa fedha unaokuja tutaenda kwenye mwaka unaofuatia. Ila sasa tumeona basi walau tuwape starter (appetizer) ndiyo maana ya vitongoji vipo kumi na tano. Tunajua havitoshi, lakini sisi vitatusaidia kuangalia utaratibu na namna bora zaidi tutakapofanya ule mradi mkubwa ya kufika. Imani yetu ni kwamba katika vitongoji 15 tutachagua maeneo yenye mahitaji zaidi, maeneo ya huduma, maeneo ya uzalishaji mali, maeneo ya uchumi kwenye minara ya simu na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii ya vitongoji 3,000 kwa ujumla ukipiga si vidogo kwa sababu mahitaji ni sawa na yale yale ya nyuma ya kupeleka umeme katika vijiji. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge naomba tukubali kwamba tutaendelea na utaratibu wa kujiandaa kwa mwaka unaofuatia. Bahati nzuri sisi tuko tumeishaweka mipango yote ikiwemo namna ambavyo vifaa vitapatikana, namna ambavyo vitasambazwa, utaratibu mpya wa manunuzi tutakapokuja kwenye huo mradi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni masuala mbalimbali ambayo ni mahusisi yaliyozungumzwa. Watu wa Mtwara tumewasikia Msimbati, Madimba kwa kweli tutaleta maendeleo pale kwa sababu hakubaliki kwamba panatoa gesi halafu pako vilevile. Ule mtambo tuliyoahidi kwenda Mtwara umeishafunguliwa mafundi wako Mtwara kazi inaendelea. Wahadzabe Mheshimiwa Flattey nimeona umesema weka historia wapelekee Wahadzabe umeme. Niseme tu kwamba kabla ya Desemba tutawapelekea umeme wa solar uko waliko. Tutaanza na solar kwanza tuone, kwa hiyo tutawapelekea solar. Mheshimiwa Cherehani timu nzima na Mheshimiwa Iddi Kassim timu nzima ya TANESCO na management itakuja Kahama na kukaa na Uongozi wa Mkoa na Wilaya kuangalia mahitaji mahususi ya pale. Cable Zanzibar tutaweka cable mpya Zanzibar ya kutoa umeme Bara na kupeleka Zanzibar. Tunafanya upembuzi yakinifu ili kuongeza uwezo wa umeme kutoka Zanzibar. Naomba nirudie; tutaweka cable mpya ya kupeleka umeme Zanzibar chini ya Bahari. Mheshimiwa Bidyanguze tumepokea, tumesikia waambie watu wako wasiwe na wasi wasi greed Katavi inakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho tu niseme kwamba Waheshimiwa niongee na Wananchi wa Tanzania moja kwa moja kupitia Mheshimiwa Spika kwamba mmewasikia Wabunge wenu na kwa bahati mbaya hapa sikuweza kuwajibu wote ila naomba niwahakikishie kwamba tumewajibu Waheshimiwa Wabunge wenu kwa majibu yanayotatua changamoto walizozisema kwetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama Waheshimiwa mnatusikiliza, mmemsikia Mheshimiwa Mbunda pale amezungumza umeme, Kapinga kule Mbinga kwa sababu sijamtaja lakini nimemjibu na nimemueleza lini umeme utafika. Kwa hiyo majibu hayo tumeshawafikishia, kwa hiyo msiwahukumu Waheshimiwa Wabungwe wenu kwamba mbona Waziri kasimama hajakutaja. Muda hautoshi ila tumewajibu Wahehsimiwa Wabunge wote.

Mheshimiwa Spika, mwisho kulikuwa na maneno mengi ya faraja kwetu katika mjadala huu; yametutia moyo, tumeyapokea, tumefurahi. Hatukutegemea kwamba Bajeti yetu ingekuwa na hamasa na shamra shamra na pongezi kiasi hiki, tumefurahi. Tumesikia maneno Mheshimiwa Mzee wangu Mzee Deo Sanga, mdogo wangu Mheshimiwa Tauhida kwamba hayo maneno yanayosemwa msiyasikilize kabisa.

Mheshimiwa Spika, sisi tunayasikiliza. Naomba nitofautiane nao, tunayasikiliza kwa sababu yanatusaidia. Tunayasikiliza, hayatutoi relini ila tunayasikiliza. Tunayasikiliza kwa sababu kwanza yanatuongezea umakini. Unajua mtu akiwa anakusema kwa maneno ya uongo, anakusingizia mambo, mnakaa na wenzako jamani mnaona haya. Hebu tusije tukafanya mambo ya hovyo halafu ikaja ikaonekana ni kweli. Kwa hiyo tunashikana, na inatusaidia kuwa makini. Unajua ukiwa unamulikwa unakuwa makini. Kwa hiyo haya maneno yanatufanya saa zote tuwe macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili haya maneno yanatuongezea hamu na hamasa ya kupata matokeo. Sisi hamasa yetu ni imani ya Mheshimiwa Rais kwetu, hamasa yetu ni matokeo ya kazi yetu kwa uhai wa chama chetu, hamasa nyingine ni kuwasaidia Watanzania kwa majukumu tuliyopewa. Lakini hamasa ya mwisho ni maneno haya, kwa sababu si unataka upate matokeo? Mtu akikusema wewe hufai, maana yake unajitahidi ili uonekane unafaa. Kwa hiyo haya maneno yanatusaidia ndio maana tunayasikiliza. Lakini pia haya maneno yanatusaidia kwa sababu yanawaamsha wanaotupenda na wanaotutakia kheri ili watuombee dua na sala. Kwa sababu ukisemwa sana, rafiki zako, ndugu, jamaa watasema Mungu msaidie, msaidie, wanaamka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii pia inatusaidia sala na dua zinaongezeka. Kwa hiyo tunayapenda. Lakini mwisho yanatusaidia kwa sababu yanatufundisha kuwa na subira, yanatufundisha kuwa na ukomavu, yanatufundisha kuwa na uvumilivu ili tuwe viongozi bora zaidi. Maneno haya yanatusaidia kwa sababu yanatufundisha ukomavu, yanatufundisha kuwa na subira, yanatufundisha kuwa na uvumilivu na yanatujenga kuwa viongozi bora zaidi. Kwa hiyo sisi tunasema waendelee kwa sababu yanatusaidia.

Mheshimiwa Spika, sisi kisasi chetu ni matokeo, ndio mwisho. Naomba nirudie, hatutabishana, hatutatupa maneno, hatutajitetea, tutalipa kisasi kwa matokeo. Na tunaomba Mwenyezi Mungu atupe afya na uhai tuendelee kuruzukiwa na imani ya Mheshimiwa Rais na tutapata matokeo, tutakuwa tumetimiza mchango wetu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.