Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, awali nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania kwa uzalendo mkubwa sana na hasa namna anavyojali na kupeleka fedha nyingi kwenye Wizara ya Nishati.

Pili, nikupongeze wewe Mheshimiwa Spika wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi kubwa na nyeti ya kuwa Rais wa Bunge la IPU. Mimi nikuombee heri na mafanikio makubwa kwenye hatua hiyo.

Tatu, nimpongeze sana Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba kwa kazi nzuri wanayoifanya akisaidiwa na Naibu wake Mheshimiwa Stephen Byabato, hakika kazi yao ni njema, nami nawatakia heri katika kufanikisha malengo waliyoaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo utajikita kwenye malalamiko au masikitiko yangu makubwa sana juu ya hali ya kusuasua ya utekelezaji wa mradi wa REA Mkoa wa Rukwa. Namba ya Mkataba ni AE/008/2020 -21/HQ/W/31 – LOT 24; Mhandisi Mshauri ni Mercados Aries International; msimamizi ni TANESCO Ltd Mkoa wa Rukwa; Mkandarasi ni M/s JV Pomy and Qwihaya Partnership; muda wa utekelezaji ni miezi 18; gharama za mradi ni shilingi 36,549,180,653.61; wigo wa kazi kwa mkoa mzima.

Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa kwa ushirika wa kampuni ya Pomy na Qwihaya, kwa taarifa za nyuma Qwihaya ni kampuni ya nguzo ila kwa sasa ni mkandarasi wa umeme pia, Pomy ni mkandarasi wa umeme tangu kipindi cha nyuma hadi sasa. Mkandarasi Pomy alishawahipewa kazi ya mradi wa umeme kwa mkoa wa Tabora, alitekeleza mradi huo kwa kiwango kisichokubalika na hakumaliza, lakini adhabu na lawama ilielekezwa kwa wafanyakazi wa TANESCO akiwemo Meneja wa Mkoa.

Mheshimiwa Spika, mwaka uliofuata baada ya kazi ya Tabora kutoisha na kuwa na mgogoro na kukawa na miradi mingine iliandaliwa na REA kwa mikoa mbalimbali ikiwemo Rukwa, sasa wakati wa mchakato huo watumishi wa REA walikataa kumpa nafasi ya kupata mradi mwingine baada ya kuona Tabora kazi iliharibika na maneno ni mengi, hata hivyo alipenya na baadae akapewa mradi kwa Mikoa ya Rukwa na Kagera zikiwa ni lot mbili tofauti. Kwa mkoa wa Kagera vijiji vilivyokwishawashwa umeme ni 36 kati ya vijiji 137 kwa mkoa mzima na kwa mkoa wa Rukwa ni jumla ya vijiji 49 kati ya vijiji 140 kwa kipindi chote hadi mwisho wa mwezi wa nne mwaka huu ikiwa ni miezi minne zaidi ya mkataba wake wa awali.

Mheshimiwa Spika, tangu anaanza mradi huu wa Rukwa kwa kushirikiana na Qwihaya, kumekuwa na migogoro kati yao isiyoisha na kusababisha mradi kutokwenda kwa wakati na kuwa na dalili zote za kutokamilika na huenda mgogoro ukawa ni sawa na kilichotekea Tabora. Tutambue kuwa mradi huu wa Rukwa ulianza kutekelezwa tarehe 9 Julai, 2021 na mwisho wa mradi huu ilikuwa ni tarehe 8 Januari, 2023 na alikuwa amefikia asilimia 38, REA wakaongeza muda wa miezi minne hadi tarehe 30 Aprili, 2023 ili kukamilisha mradi, lakini hadi mwisho wa mwezi wa nne utekelezaji wa mradi ulifikia asilimia 41. Kwa sasa REA wameongeza muda wa kutekeleza mradi huu hadi tarehe 31 Oktoba, 2023.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu sana juu ya maendeleo ya mradi huu ambao unatupa wakati mgumu sana kwa wapiga kura na nimebaini mambo mengi ya kusikitisha. Pamoja na TANESCO kufanya vikao mbalimbali vya maendeleo ya mradi, lakini hakuna juhudi zozote za makusudi kuhakikisha mradi unakamilika, isipokuwa nilichobaini Mkandarasi Pomy (Eva Fumbuka ambaye ni Mkandarasi Mkuu) kuwa na maneno ya kufajiri bila ya utekelezaji, sababu anazotoa ni kuwa Covid-19 imeathiri upatikanaji wa vifaa, REA hawawalipi na wanaibiwa vifaa site.

Mheshimiwa Spika, TANESCO Rukwa kama msaidizi wa mradi wamekuwa na vikao vya kikazi na mkandarasi kuhusu mradi huu, lakini kwa upande wa mkandarasi mara nyingi wamekuwa wanahudhuria mainjinia tofauti tofauti tena wasio na mikataba ya kazi kwa mujibu wa mkataba wa mradi, kikubwa zaidi ni kuwa Meneja wa Mradi hapatikani eneo la kazi na hata vikao si mhudhuriaji.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuona usumbufu mkubwa sana na kelele ya wananchi kuwa kubwa niliomba mpango kazi na maelezo toka kwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Rukwa ambaye alini-brief kwamba kuna kikao kiliitishwa tarehe 27 Aprili, 2023 kujadili tatizo hilo la Mkoa wa Rukwa na kilifanyika Ofisi ya REA Makao Makuu Dodoma, na Menejimenti ya REA ilikuwa Dar es Salaam hivyo iliwakilishwa katika kikao. Waliohudhuria ni wawakilishi wa Menejimenti ya REA, Mshauri wa Mradi, TANESCO Rukwa na Makao Makuu, Mkurugenzi wa Pomy na Mkurugenzi wa Qwihaya.

Mheshimiwa Spika, katika kikao hicho cha tarehe 27 Aprili, 2023 walijadili changamoto zinazopelekea mradi kusuasua, kama ifuatavyo; mgogoro wa ndani kati ya Mkurugenzi wa Pomy na Mkurugenzi wa Qwihaya katika mambo mbalimbali na kusababisha mgawanyiko wa kiutendaji kama vile suala wa wafanyakazi, usafiri (transport), kugawana vijiji, mvutano wa kufikisha vifaa eneo la kazi, mvutano wa kimaslahi na mvutano wa kimaamuzi.

Mheshimiwa Spika, mgongano wa kimaslahi kwa kuwa mmoja wa Wakurugenzi (Eva Fumbuka) kuwa ni Meneja wa Mradi na kusababisha kuwepo na mgongano wa kimaslahi na wa kimaamuzi, kwenye mkataba kama huu hasa kunapotokea wenye kampuni kutoelewana, Meneja wa Mradi hayupo eneo la kazi ingawa ni mmoja wa Wakurugenzi ni shida mno kupatikana hata kwa njia ya simu, na hashiriki vikao vya kazi kwa mujibu wa mkataba, pamoja na mgawanyiko uliopo wa kiutendaji bado hali ya mradi si nzuri, kubwa zaidi ni kuwa hakuna mawasiliano mazuri kati ya wafanyakazi (wahandisi) wa Pomy na Qwihaya na kupelekea TANESCO pia kuwa na sintofahamu ya mradi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na hali ya kubadilisha au kuacha kazi kwa wafanyakazi (wahandisi waliochini ya Pomy anaowaweka kama joint venture) bila taarifa yoyote na inapelekea kuharibu mwenendo wa mradi.

Mheshimiwa Spika, baada ya uwasilishaji huo na kuwa na mjadala juu ya hoja hizo, REA walikiri kupokea hoja hizo na kuzifanyia kazi na kwa vile Menejimenti ya REA iko Dar es Salaam basi watawasilisha na kuandaa ripoti ya kikao kwa yale tuliyoyajadili, lakini mpaka leo hii ni mwezi umepita hatuoni chochote kinachoendelea kwani mkandarasi alikuwa kafikia asilimia 41 ya ukamilishaji wa mradi na alikuwa ameomba haraka haraka kwa sababu ya kikao hicho nyongeza ya muda hadi mwisho wa mwezi wa nane, lakini REA kwa sasa wameshatoa nyongeza ya muda hadi tarehe 31 Oktoba, 2023 hii ikiwa ni pamoja na kuongezewa kazi zaidi, nyongeza ya kazi ya kilometa mbili kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Spika, jambo la kumuongezea huyo mkandarasi muda (extension of time) kila wakati pamoja na ukweli wote huo wa kusuasua na usumbufu huo wote bado linatupatia jeraha kubwa Wabunge wa Mkoa wa Rukwa. Binafsi sikuona sababu tena za kumuongezea mkandarasi wa aina hii kilometa mbili nyingine kwa kila kijiji kwani ni msumbufu sana na uwezo wake ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe kwa kumshauri Mheshimiwa Waziri ambaye pia nitamuomba aje Rukwa kwa mara nyingine kujione hali hii. Kwa kifupi mkandarasi Pomy amekuwa ni tatizo kubwa kutekeleza mradi na ni dhahiri kuwa muda wa mradi utaisha hata hiyo Oktoba, 2023 aliyopewa na kazi haitakuwa imekamilika.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri awaagize REA kuupitia mkataba wa mradi na kuona mapungufu yaliyopo na kufanya mabadiko stahiki kwa kuangalia matakwa ya kimkataba, lakini uwepo na utoshelezi wa timu iliyoko Rukwa na Kagera na yote yanayohitajika, kuwataka Wakurugenzi waajiri Meneja wa Mradi kwa upande wa Rukwa na Kagera kama mkataba unavyotaka, ikiwezekana na kwa vile Qwihaya amekwishaona ni tatizo na anachafuliwa na Pomy na anajutia kuingia kwenye hii joint venture na Pomy na kwa sasa kulazimika kuwa na timu yake na kutekeleza mradi, basi timu ya Qwihaya itekeleze mradi kwa Mkoa wa Rukwa na timu ya Pomy itekeleze mradi kwa Mkoa wa Kagera, kuliko ilivyo sasa maana wanalaumiana pia kuwa mmoja anamchelewesha mwingine kuendelea na mradi kwa sababu fulani hajakamilisha kipande fulani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na nawasilisha, ahsante sana.