Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Nishati, Wizara ambayo Wabunge takribani wote hapa tumekiri wazi kwamba ni Wizara ambayo ni ya muhimu kabisa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwanza na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na hata leo napata nafasi ya kuchangia kwa ajili ya mambo muhimu kabisa yahusuyo nishati. Lakini la kwanza nikupongeze wewe kwa uthubutu wako na kuamua kugombea nafasi hii katika Bunge la IPU. Nataka nikuhakikishie sisi Wabunge tutaendelea kukuombea wakati wote ili mradi haya aliyoyazungumza Mheshimiwa Matiko kama mjumbe wako kuhakikisha kwamba na sisi maombi yanaungana pamoja na nyinyi kuhakikisha kwamba unapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo unaokuja.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba nimpongeze Mheshimiwa January Makamba Waziri katika Wizara hii ya Nishati kwa namna ambavyo amekuwa akifanya kazi nzuri ya kuisimamia Wizara hii; na mabadiliko makubwa katika kipindi chake cha uongozi sisi wenyewe tumekuwa mashuhuda na Watanzania wamekuwa mashuhuda katika mapinduzi makubwa ambayo umekuwa ukipambana wakati wote ili kuhakikisha kwamba azma ya Watanzania na Serikali inaweza kufikiwatena katika kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Spika, nimpengeze sana Mheshimiwa Byabato ambaye ni Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji katika Wizara hii. Pia naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wilaya yangu ya Kishapu kwa namna ambavyo wamekuwa wakisismamia vizuri suala zima la umeme katika Wilaya yangu ya Kishapu na Mkoa mzima wa Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, kuna kampuni hii ya Suma JKT ambaye ndiye mkandarasi anayesambaza umeme katika Wilaya yangu ya Kishapu. Naomba nimpongeze kwa sababu kwa kweli kazi inayofanyika ni kubwa na changamoto ilikuwa ni kubwa kwa sababu tulikuwa na idadi kubwa ya vijiji ambavyo havikuwa na umeme kabisa, na sasa tunaona mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta hii muhimu katika Jimbo langu la Kishapu.

Mheshimiwa Spika, na moja kwa moja naomba niunge mkono hoja kwamba bajeti hii yenye thamani ta trioni tatu iweze kupita kwa asilimia 100 kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, la kwanza katika mchango wangu naomba Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana kwa kusimamia suala zima la Mradi wa Umeme wa Jua ambao tarehe 29 Mei tumeweza kusaini mkataba huu na kuushuhudia sisi Wabunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya Nishati ya Bunge kwa namna ambavyo mradi huu unakwenda kuwanufaisha Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Mradi huu upo katika jimbo la kwangu la kishapu katika Kata ya Taraga Kijiji cha Ngunga; na tunakwenda kuzalisha megawatt tano na mradi huu ni wa thamani ya zaidi ya bilioni 275. Kwa kweli mradi huu ukishakuwa umekemilika hizi megawatt tano zinaweza kuongezwa katika Grid ya Taifa, na kwa hali hito tunaenda kupunguza pakubwa sana tatizo la umeme hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, ninaomba tu niseme kwamba mradi huu ni mradi mkubwa wa kwanza, na kwa maana hiyo tunatarajia makubwa yatakuwa yanakuja kwa sababu Mkoa wa Dodoma nao unaenda kupata bahati ya mrado huu mkubwa wa Umeme wa Jua. Sasa kwa msingi huo naomba niipongeze sana Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa jitihada kubwa anazozifanya kuhakikisha kwamba Watanzania tunaondokana na changamoto kubwa ya umeme katika Taifa letu.


Mheshimiwa Spika, lakini jambo kubwa ambalo naliona katika mpango huu wa umeme huu wa jua ambao katika Wilaya ya Kishapu tunaenda kunufaika nao; kwanza tunaenda kupata service levy kwa ajili ya Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kishapu ambayo tunakwenda kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri yetu kwa sehemu kubwa sana. Lakini tunashuhudia kwamba tunakwenda kupata CSR ambayo itakwenda kusaidia sana maeneo muhimu. Kwa mfano, tunakwenda kunufaika na ujenzi wa hospitali ambayo itajengwa katika eneo hilo, tunaenda kunufaika na ujenzi wa bwawa kubwa litakaloenda kujengwa eneo hilo, na pia kuna ujenzi wa shule ambao tunarajiwa utafanyika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, yako mambo mengine mengi ambayo tumekaa kwa pamoja na mikakati imeshaanza kusimamiwa na Mheshimiwa January kuhakikisha kwamba miradi hii inayokwenda kusaidia wananchi inaanza kufanya kazi vizuri; haya ni manufaa makubwa ambayo tunaenda kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na changamoto kubwa ya kukatika umeme katika Wilaya yetu ya Kishapu; na kwa sababu tuna Mgodi wa Almasi wa Mwadui, lakini tuna migodi katika Mkoa wetu wa Shinyanga, kwa maana ya migodi iliyopo Wilaya ya Kahama. Haya matatizo ya kukatika kwa umeme baada ya suluhisho hili mimi naamini kwamba sasa tunaenda kuondokana na changamoto hizo. Na kwa hali hiyo ninaomba nikutakie kila la kheri ili usimamizi katika utekelezaji wa mradi huo uende vizuri na manufaa tuyaone kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie eneo la REA. Wilaya ya Kishapu mpaka sasa kwa mwaka wa fedha huu ambao tunakwenda kumalizia tumeweza kuwasha vijiji 13, na hii kazi imesimamiwa na SUMA JKT. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa jitihada kubwa ambayo wamekwenda nayo.

Mheshimiwa Spika, lakini bado tuna vijiji 28 kati ya vijiji 51 ambavyo vilikuwa havijapata umeme; vijiji 28 bado havina kabisa umeme. Kwa hiyo, naomba kasi hii iweze kuongezwa, na SUMA JKT chini ya Engineer Meja Mohammed nawaomba waongeze kasi ili suala la kuwasha umeme katika maeneo haya yaweze kuafanyika. Nimeshuhudia nguzo zimesambazwa katika vijiji vyote na tulikuwa tunasubiri nyaya ndiyo changamoto kubwa. Naamini kwamba kama hili nalo litasimamiwa maeneo haya yote yanaweza kupata umeme kwa wakati. Mimi naomba sana SUMA JKT muongeze kasi ili mradi suala hili liweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu niyataje baadhi ya maeneo ambayo hayana kabisa, ni kata ambazo hazina kabisa umeme, ambazo ni Kata za Lagana, Mwasubi, Mwamashele pamoja na Bunambiu. Hizi ni kata nne ambazo hazina kabisa umeme. Kwa hiyo, nilikua naomba hata mkandarasi atazame kwa macho maeneo haya muhimu na hasa ile Bunambiu na Mwasubi kwa sababu ni maeneo ambayo maji yanapita mengi na ikifika nyakati za masika inawezekana changamoto ikawa kubwa sana, hivyo waongeze kasi kuhakikisha kwamba wanaharakisha katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ninaomba nipongeze sana kwa jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Waziri umekuwa ukisimamia suala zima la mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tumeshuhudia kabisa kwamba sasa imefikia asilimia 80. Kazi hii ni kubwa unayoifanya; na mimi naomba nipongeze hata Kamati yenyewe ya Nishati kwa namna ambavyo mnasimamia kuona kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati na hivyo Taifa liweze kuondokana na changamoto ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala zima la vitongoji, nina zaidi ya vitongoji 145 katika Wilaya ya Kishapu. Vitongoji ambavyo tayari vimeshapata umeme ni vitongoji kama 55, vitongoji zaidi ya 90 bado vina changamoto kubwa ya umeme. Pamoja na kuongezewa idadi hii ya vijiji 15 ambao ni mpango ambao unakwenda kutekelezwa lakini bado jitihada zinatakiwa ziongezewe ili kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapata umeme. Maeneo haya Watanzania wamekubali kubadilika, na kasi ya wananchi wanavyojitokeza kujisajili kwa ajili ya kuwekewa umeme ni mkubwa sana. Ninaomba Serikali, kwa maana ya Wizara, Mheshimiwa January ongeza kasi ili vitongoji vyote tuweze kupata umeme kabla ya mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya pekee, sasa naomba nizungumze mambo machache ambayo ni changamoto nikishauri kwamba tuweze kusaidia katika maeneo haya. La kwanza, ni eneo la usafiri. Jimbo la Kishapu na Wilaya ya Kishapu ina tatizo kubwa la usafiri, lakini la pili ni watumishi, naomba eneo hilo na lenyewe litazamwe. Tuna tatizo kubwa la watumishi katika eneo hili; panapotokea emergency tatizo linakuwa ni kubwa sana kwa ajili ya kutatua matatizo ya aina hii.

Mheshimiwa Spika, ninakushuru sana kwa kunipa nafasi naunga asilimia mkono hoja 100, ahsante sana. (Makofi)