Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa hii na mimi kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukupongeza kwa kweli. Mimi ni mjumbe wa IPU, kwa hiyo kwa kipekee kabisa nikupongeze kwa nia lakini kwa dhamira ya dhati ya kuwaza kwenda kugombea Urais wa Mabunge ya Dunia na niwaambie tu Watanzania wenzangu pamoja na Wabunge kwa kweli tukuombee dua. Tukuombee dua kubwa kabisa ili njia iweze kufunguka na uweze kuwa endorsed hata kwa asilimia mia; kwa sababu tumeshaona kule IPU ulikuja kwa muda mfupi tu tukakuamini na tukakufanya ukawa Rais wa Ukanda wa Afrika, na sasa hivi tunaenda kukupandisha uwe Rais wa Mabunge ya Dunia. Kwa kweli kwa asilimia kubwa kabisa Wabunge wa Mabunge ya Dunia wanakukubali. Kilichobaki ni kutoa rai tu kwa Watanzania wakuombee lakini pia najua kuna Watanzania ambao hawako humu Bungeni lakini wana connection na Wabunge wa Mabunge mengine wakipata fursa basi waendelee kutuombea kura. Mwisho wa siku ni pride kwa Bunge hili lakini kwa nchi yetu kama Tanzania na kwa Afrika na zaidi kwa wanawake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia. Kwanza kabisa kipekee ninakwenda ku-acknowledge, kwa Mkoa wetu wa Mara vijiji vyote vimefikiwa na umeme kwa asilimia mia moja, kwa hiyo hapa ninatoa complement kwa Wizara na kwa REA. Lakini bado kwa upande wa vitongoji tuko chini. Vitongoji vimefikiwa kwa asilimia 47 tu, kwa hiyo bado takriban asilimia 53 hawajafikia.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa najaribu kupitia nikaona takwimu za NBS 2019/2020 of course walionesha kwamba ufikaji wa umeme ulikuwa ni asilimia 69 lakini uunganishwaji ni asilimia 24 tu. Hili ndilo tatizo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea hapa. Kweli utatoa takwimu kwamba umeme umefika lakini bado inabidi tuweke mtandao kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huu umeme. Sasa tumeona mpango mkakati wa Wizara hapa ameainisha kwamba ili kuweza kukamilisha REA ikamilike ndani ya miaka mitano na sio miaka 20 basi atahitaji kupata vyanzo vingine zaidi kuliko ambavyo tunavipata sasa hivi. Mojawapo aka-suggest kwamba ikiwezekana sasa na Bunge lako Tukufu likiweza kuona tuweze walau tuongeze ile waweze kupokea kutoka shilingi mia ambayo tunapokea sasa hivi iongezeke iende 150 na hata ingewezekana iende hata 200 ili tuweze kumaliza.

Mheshimiwa Spika, tukiweza kuimarisha na umeme ukapatikana vijijini kwanza tunaongeza kuchechemua uchumi huko vijijini lakini pia usalama utakuwepo, pia na kupandisha hadhi wawekezaji wengi waweze kwenda wa kuweza kuwekeza. Tunashuhudia wote kwamba huko vijijini kwenye vituo vya afya au kwenye taasisi mbalimbali tunatumia vibatali au hivi vi-solar vidogo hata wamama wanataka kujifungua inakuwa ni shida sana. Kwa hiyo kwa kweli mimi ningetoa rai Serikali ione ni jinsi gani, huu mpango mkakati wa kuhakikisha umeme unapatikana kwenye vitongoji uweze kupatikana kwa uharaka Zaidi; hata isiwe hiyo miaka mitano, ikiwezekana iwe miaka mitatu au miwili, ambayo kwa kweli inakwenda kusaidia na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi dunia, lakini hata kwa Tanzania, tulimwona Mheshimiwa Rais aliweza kuzindua mpango mkakati wa kwenda kwenye nishati safi. Sasa hii nishati safi haiwezi kufikiwa kwa ukamilifu kama Watanzania hawatafikishiwa kwa huduma ya umeme ambayo itapelekea urahisi wa kuweza kutumia majiko sanifu ambayo yanaweza kuonekana yana nafuu zaidi kuliko majiko banifu na njia zingine za kuweza kupikia kwa nishati safi. Ukiangalia takwimu kwa wanaopata umeme hasa kwa mijini asilimia 40 watu wanaumeme lakini hawatumii nishati ya umeme kupikia. Tumeona kwamba asilimia tano wanatumia gesi, asilimia tatu tu ndio wanatumia umeme lakini asilimia 32 wanatumia hizi nishati ambazo ni chafu, na kati ya hizo asilimia 26 ni mkaa, na mkaa wa Tanzania ambao unavunwa asilimia 75 unakwenda kwa matumizi ya watu wa mjini ambao wana umeme; na asilimia 60 anayosema ni wanatumia kuni.

Mheshimiwa Spika,sasa hapa ina trigger kwamba kuna vitu vingine vya ziada tunatakiwa tufanye ili kujua kinachosababisha ilhali tuna umeme na tuna gesi, huku gesi ikiwa inatumika kwa asilimia tano na umeme unatumika kwa asilimia tatu. Hapa inaonekana kuna elimu ya matumizi bado haijatolewa; elimu haijatolewa ya kutosha ili uweze kuainisha kwamba ukitumia kwa mfano jiko sanifu unapunguza gharama kwa kiasi gani.

Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru nilipata fursa ya kuweza kuhudhuria, walikuja watu wa TaTEDO na SESCOM sijui, na wakatupa semina baadhi ya Wabunge hapa, Wabunge wa Bunge lako kupata semina. Ikaonesha mfano kama unapika maharagwe kwa jiko hili la pressure ya kutumia umeme, inarahisisha mara tano zaidi kama vile ambavyo ungetumia mkaa. Kwa hiyo kama ungetumia mkaa ungepika labda kwa dakika sitini ukitumia lile jiko unakuta unatumia dakika kumi na mbili kuweza kuivisha hicho kitu. Lakini pia inarahisisha mara nne zaidi kama ambavyo unatumia gesi. Ina-serve muda lakini pia ina-serve na gharama. Sasa kama Watanzania ambao wana umeme wakielekezwa kwamba tukitumia hili jiko tuta-serve muda, tuta-serve fedha lakini pia itaturahisishia kuweza kuhakikisha kwamba hata zile nutrients kwenye chakula zinakuwa hazipotei kwa wingi wake.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mambo kadhaa ambayo kama Serikali inahitaji kufanya. Moja ni hiyo ya kutoa elimu. Tunaweza tukapeleka umeme kwa Watanzania wote lakini bado wakaendelea kukata miti, kuchoma mikaa kwa sababu watu hawajapata elimu ya kutosha. Kama tunataka tufikie hiyo target ya 2033 ya kuweza kufikisha asilimia 80 Wizara mnajukumu la kutoa elimu ya kutosha hasa kwa hawa wananchi ambao tayari wana umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini kingine tuhakikishe tunatoa incentives zingine. Kwa mfano Uganda bei ya umeme kwa ambao wanatumia majiko imepunguzwa. Umeme umepunguza ile tariff. Kwa hiyo ni incentive ya kuweza kuwavutia watu waweze kutumia haya majiko. Lakini pili tuweze kuhakikisha kwamba tunatoa kodi. Hizi kodi zitasaidia kuweza kupunguza bei ya kuweza kununua majiko sanifu ili Watanzania wengi waweze kuwa nayo lakini hata taasisi ambazo zinapika kutumia kuni na mkaa waweze kutumia hii, ambayo pia itasaidia kwenye ku-protect mazingira yetu. Tukiendelea kuacha wanakata miti tutaendelea kupata mabadiliko ya tabianchi ya hewa ukaa ambayo inazidi kudidimiza, na tutakuwa tunaenda kinyume na Paris Agreement, lakini pia tunaendelea kuhakikisha kwamba hata upatikanaji wa mvua tukikata miti sana tunakuwa hata hatuwezi kupata mvua wakulima wataathirika na wafugaji wataathirika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nilikuwa nashauri, tuhakikishe tunatoa hizo incentives (ruzuku), tunatoa kodi ili Watanzania waweze kwenda kutumia haya majiko sanifu. Pia tusi-rely sana kwenye umeme wa maji tu. Natambua wametoa mkakati hapa, lakini twende kwenye Biothermal, joto ardhi, twende kwa kiwango kikubwa sana kwenye umeme wa jua na kwenye umeme wa upepo. Na tukiwekeza pia huko kwa zaidi huu umeme wa maji unakuwa kama ni balancing tu. Umeme wa jua hata gharama yake sio kubwa. Nina acknowledge ambavyo tumeshawekeza kwa kiwango kikubwa kwenye maji, tuji-balance sasa twende na kwenye hizo source zingine ambazo zitatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, ukiaangalia madhara mengine ya kuendelea kutumia hiyo nishati chafu sote tulielezwa, lakini kuna takwimu ambazo zimetoka ambazo unaangalia siyo tu vifo kwa kupelekea upumuaji au TB lakini kunakuwa kuna carcer, kuna ku-premature, mimba zinatoka lakini pia ulemavu. Kwa hiyo kuna madhara mengi sana ambayo ukifanya cost and benefit analysis kama Taifa ni lazima tuwekeze kuhakikisha kwamba Watanzania sasa tunatoka kwenye kutumia kuni na mkaa tunakwenda kutumia kwa kiwango kikubwa majiko sanifu na banifu ili kuhakikisha kwamba tunalinda afya yetu lakini tunaweza kuwa productive; kwa sababu ukiwa unaumwa hata huwezi kwenda kuzalisha.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia sasa, kuhusu luku, niko na mwekezaji hapa. Kwenye plot ulivyoleta hizo luku tunakata hiyo kuweza kulipia kodi ya ardhi. Tulisema mita moja kama ni plot ndiyo itakayotumika kulipia. Lakini unakuta labda sehemu hiyo plot moja au kiwanja kina mita takriban 11 sasa kila mita inachajiwa tena elfu kumi na mbili kwa mfano wawe wanachaji elfu moja moja, kila mita 12,000. Hili liangaliwe, huu ni wizi. Ina maana if you multiply 12,000 mara 11 yaani mimi plot yangu unanilipisha laki moja na kitu ilhali nilitakiwa nilipe 12,000. Kwa hiyo hili mlipitie muweke kama luku mama iwe moja kwenye plot, kwamba hii ndiyo iwe inalipa hiyo chaji ili hata kama Salome hapa huyu Mheshimiwa Mbunge anayewekeza kwenye vitu vya apartment kama anawapangaji hao wengi mapangaji mmoja atakuwa anam-refund hiyo 12,000 hao wengine wasiwe wanachajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)