Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kukushukuru kwa kunipatia nafasi nami ya kuweza kuchangia kwenye Wizara yetu nyeti ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini pia nimshukuru Rais wetu, mama yetu kipenzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwapigiania Watanzania, anakesha kila kukicha kuhakikisha wananchi wake wanaboreshewa miundombinu.

Mheshimiwa Spika, nipende tena kumshukuru kaka yangu, Mheshimiwa January; mdogo wangu, Mheshimiwa Byabato pale, kazi mnayofanya siyo ya kitoto, tunaona mambo mengi sasa hivi yamekuwa mazuri. Lakini bila kuwasahau viongozi wangu wa mkoa Eng. wangu Khadija pale Engineer wangu wa Kanda na Engineer wangu wa wilaya, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Wanatupa ushirikiano wa kutosha kiukweli hata tukiwapigia simu wana-respond kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, baada ya hizi salamu nianze mchango wangu kwa kuanza na REA. Ni kweli REA wanafanya kazi vizuri sana, sasa hivi hata ukipita huko kwenye maeneo yetu unaona kabisa taa zinawaka waka na mji unabadilika. Kwa kweli tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu na Wilaya yetu ya Kaliua tuna vijiji vipatavyo 100 lakini katika vijiji hivi 100, vijiji 82 tu ndivyo vina umeme lakini vijiji 18 bado. Kati ya hivyo vijiji 18 nina vijiji vyangu mimi kumi ambavyo havijapata umeme kabisa. Nina Kijiji cha Unsungwa, Silambo, Kabanga, Mwamashimba, Tupendane, Imagi, Busubi, Uhindi, Mpagasha na Lusanda. Mheshimiwa Waziri hivi vijiji kiukweli ndivyo vijiji ambavyo vina nibeba mimi kama Rehema na vinawapiga kura wengi sana. Hivyo niombe sasa harakati za kupeleka umeme kule na wakandarasi waharakishe ili wananchi wangu wasione tu umeme unatokea kwenye maeneo mengine. Taa wanaziona maeneo mengine, tunataka nao wawashe taa.

Mheshimiwa Spika, lakini tatizo kubwa la REA ni tatizo la uhaba wa nguzo. Hizi nguzo ni chache sana. Unaambiwa kilometa moja moja wanatoa nguzo 22 hazitoshi. Matokeo yake wanatwambia nguzo ni bure. Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe tu brother, yaani tunaomba mtuambie ukweli hivi hizi nguzo ni bure au vipi. Nikiwa kama mimi ni Mbunge nilishanunua nguzo 350,000. Mimi kama mimi Mbunge nimenunua 350,000, hivi kwa nini sasa msiweke wazi kabisa wananchi wakajua kwamba hizi nguzo badala ya kuwaambia bure mkaweka bei elekezi. Kwamba labda kuanzia mita ngapi kutoka kwenye chanzo labda iwe laki moja au elfu hamsini. Watu wanatamani umeme wanatamani kuweka, mkiweka bei elekezi ya hizi nguzo na mkawa wazi. Mimi ninaimani wenye uhitaji watajichanga na kuweka umeme kwenye nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, lakini leo tunawaambia 27,000, hizi ni ela ndogo sana, wananchi wetu wana uwezo, akiuza kuku wake wawili tu ameshapata fedha ya kuweka umeme; lakini shida ni nguzo. Mheshimiwa Waziri nikuombe nakujua wewe kijana sana mchapa kazi, hili suala naomba ulichukue, hebu wekeni wazi sasa bei ya nguzo. Mkae mfikirie mfanyie bei tu elekezi ili hawa wananchi wetu wenye uhitaji waweze kujichangachanga waweze kufikisha nguzo kwenye maeneo yao wapate umeme, na si tu kila siku kuona umeme kwenye maeneo ya jirani.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu umeme kukatika katika; suala la umeme kukatikakatika bado lipo kubwa sana. Mbaya zaidi umeme unakatika kwenye maeneo ya wananchi wetu na hawapewi taarifa. Zamani kulikuwa na siku maalum ya kufanya matengenezo ndipo wananchi wanapewa taarifa kwamba umeme utakatika lini; lakini sasa hivi umeme unakatika mno na mgao upo wa kutosha. Kaka yangu kwa hiyo nikuombe, huku kukatika kwa umeme wananchi wetu wanaharibiwa vitu vingi sana, hawapewi taarifa. Tuombe sasa wananchi wawe wanapewa taarifa lakini hata ikitokea kuna tatizo basi wananchi waambiwe na lisichukue muda mrefu hili kushughulikiwa. Nimeona kuna kata yangu ya Uyowe kule vijiji vya Mnange, Kashishi wapi kule takribani mwezi mzima wananchi wangu wamekaa gizani lakini tunashukuru process zinaendelea. Tunaomba hizi harakati ziendelee, maintenance yafanyike kwa haraka ili wananchi watoke gizani.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu kumtua mama kuni kichwani. Nikupongeze kaka yangu Mheshimiwa Januari, tumeona hizi hatua za mwanzo. Tunaenda kupeleka majiko ya gesi kule vijijini kwetu. Hii ni approach nzuri sana. Lakini napenda nishauri jambo kidogo hapa. Mwananchi tunampelekea gesi lakini akishamaliza ile gesi hakuna filling station kule. Vijijini kwetu kule hata maduka ya kubadilisha gesi hayapo. Nadhani sasa kuna haja ya Wizara mkae chini mfikirie namna gani ya kuweza kuwaboreshea hao watu wa majiko bainifu lakini na hii mikaa jadidifu.

Mheshimiwa Spika, kuna tafiti mimi nimefanya kidogo, inaonesha kwamba mtu anayekata mkaa anatumia miti tani kumi mpaka kumi na mbili ambapo akichoma mkaa anapata mkaa wa kawaida tani moja tu. Tunaona namna gani wanavyoharibu mazingira na miti inakwisha. Kwa hiyo nikuombe sasa either twende kuanzisha mashamba darasa ya kupanda miti inayokua haraka, kama walivyofanya watu kwenye BBT. Tuanzishe mashamba kuna miti inaota haraka sana. Kuna miti inaitwa mianzi, mabingobingo yale ndani ya miezi sita mpaka mwaka unatosha kabisa kutaka kutengeneza mikaa hii bainifu na mikaa ambayo ni sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ningeweza kupendekeza hapa. Hii gesi ishuke bei badala ya kuwapandishia naamini kabisa mwananchi hata akiuza mayai mangapi ataweza kwenda kunua gesi kuliko tukiacha gesi ilipo halafu tumewapa majiko, itakuwa useless; kesho tutakuta wameweka chuma chakavu. Nikuombe kaka yangu tupunguze hii bei ya gesi na hao wananchi wetu waweze kununua.

Mheshimiwa Spika, kwenye hiyo gesi ninafikiria sasa tuanzishe yale majiko ya kama mtu anavyokwenda kutumia luku. Tulifanyiwa semina kule tuliona; yaani mtu atumie gesi kulingana na uwezo wake na si mtu mtungi wa kilo kumi na tano ambao hawezi kununua kwa wakati. Tukiweka kama vile matumizi ya luku mtu ana buku anapika maharagwe na maisha yanaenda. Lakini kuachia mtungi wa 60,000 ishirini na ngapi wananchi wetu hawawezi kutumia hizi.

Mheshimiwa Spika, tumeona Serikali bado haijatenga bajeti. Tumeona asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa. Kwa hiyo kama wanatumia mkaa tuweke bajeti kuhakikisha kwamba hao wadau wetu wabunifu wadogo wadogo wanaweza kuingizwa kwenye mpango wa kutengeneza mkaa ambao unatumiwa na watu wengi. Kuna majiko mbadala, tumetoka kununua kule. Kwa hiyo kama tutawawezesha hawa wadau wetu wazawa wa ndani, na kule kwenye mabango yako kule kwenye mabanda tumewaona, hebu tuwatengee bajeti hawa, nina uhakika kabisa ile azma kaka yangu Mheshimiwa Januari uliyonayo ya kuwafanya wakina mama wawe wasafi wakipika yani wasichafue masufuria mazingira yawe safi nafikiri itatimia. Hilo nikuombe kaka yangu panga bajeti vizuri mambo yako yatakuwa safi. Leo sitarajii kushika shilingi mambo yako yamekaa vizuri. Lakini, kama umeme hautafika kwangu kule nitashika shilingi, lakini leo sijadhamiria kwa sababu mambo yako makubwa nimeyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru umenitengenezea sub-station pale kutoka Tabora mpaka Ulyankulu, tunatumia peke yetu. Pale mwanzo tulikuwa tunatumia Tabora, Kaliua na Ulambo. Kwa hiyo kaka yangu nikushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)