Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii. Kwanza kabisa naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hoja hii. Na mimi naomba niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Januari, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hiyo. Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyoifanya katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuweza kusimamia na kuweza kuiwezesha Wizara kuweza kufikia mahali walikofikia katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kuishukuru Serikali kwa ajili ya Mkoa wa Kigoma. Kwa muda mrefu Kigoma tulikuwa hatuko kwenye grid ya Taifa, lakini tangu mwaka jana umeme wa grid ya Taifa uliwashwa katika Wilaya nne na Wilaya tatu zilikuwa zimesalia, lakini niipongeze Serikali kwa Mradi wa Rusumo – Nyakanazi, kilovoti 400 zilizopatikana na ninaamini Wilaya zilizosalia kwa maana ya Kigoma Vijijini, Kigoma Mjini na Uvinza zitaweza kupatiwa umeme. Hivyo, ninaishukuru Serikali na ninaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika miradi ya REA wapo wakandarasi ambao wamefanya vizuri na wengine ambao hawajaweza kufanya vizuri. Na kwa sababu kwa mwaka huu Serikali iliahidi kwamba wananchi wote watakuwa wamepata umeme katika vijiji vyote, lakini bado umeme haujawafikia wananchi. Ninaomba Serikali iwasimamie wakandarasi wote wale ambao hawajaweza kukamilisha miradi hiyo ili waweze kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na hatimaye vijiji vyote viweze kupatiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Kigoma katika mradi wa umeme awamu ya kwanza hatukuwa tumepata umeme wa REA. Katika awamu ya pili hatukuwa tumepata umeme wa REA, lakini tumekuja kupata umeme wa REA katika awamu ya tatu. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri asimamie wakandarasi hao ili umeme uweze kufika katika vijiji vingi lakini pia katika vitongoji. Kwa sababu ukiangalia maeneo mengi vijiji vichache ndivyo vimepata umeme na penyewe kwenye center, lakini vitongoji havijaweza kufikiwa na umeme. Tunaomba kwa sababu tumeshatoa ahadi kwa wananchi, wananchi wote wafikishiwe umeme hadi kwenye vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini zipo shule zetu za msingi na shule za sekondari nazo bado hazijapata umeme, vilevile na taasisi. Tunaomba Serikali ihakikishe umeme unawafikia wananchi, uwafikie wenye taasisi ili waweze kunufaika na umeme wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sana wapo wakandarasi ambao wengine wamefanya vizuri na wengine hawajafanya vizuri. Nirudie kusema kwamba Serikali iangalie wale ambao ni wababaishaji iwachukulie hatua na ikibidi wasiongezewe mikataba mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)