Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Na mimi, kama ilivyo ada, kuna usemi unaosema kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Nafahamu wengi wameongea kwa maana ya suala lililoko mbele yako lakini naamini kwa kuwa ni wengi wanalizungumza hilo tunarejea kwamba sauti yao ni sauti ya Mungu na mimi naikunja mikono yangu ikiamini Mwenyezi Mungu atatenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo nimshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Januari, kwa maana ya Waziri, Naibu Waziri lakini na watendaji wote kwa kazi ambazo wanaendelea kufanya. Shukrani nyingine za ziada nizielekeze kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa inayoendelea.

Mheshimiwa Spika, ulitutahadharisha tusitaje nchi moja moja kwa maana ya kuepuka migogoro ya kiitifaki na mambo mengine ya namna hiyo lakini mimi nikuombe…

SPIKA: Ngoja niiweke sawa. Ukiwa unataja kama mfano wa jambo zuri linalofanyika huko, ambalo sisi tunapaswa kujifunza ama kuiga ni sawa. Lakini kama wana changamoto yao hiyo ndiyo inayokuwa changamoto kwenye kuitaja nchi hapa ndani. Ahsante sana.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mimi nitaliweka kwenye sura kwamba haya yote mazuri tunayofanya ndani ya nchi basi changamoto zinazoifika nchi nyingine kwetu iwe ni somo. Nilikuwa naomba niliweke kwenye sura hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa maana ya utekelezaji wa vipaumbele vya mwaka 2022 na 2023 ni upelekaji wa mradi mkubwa wa kuimarisha grid ya Taifa kwa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera. Lakini hilo Mheshimiwa Waziri amelirudia tena, kwa maana pia ndio vipaumbele vya 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi kwa ujumla wake kuna wimbi kubwa la kuongezeka kwa miradi; na sisi pale Mpanda uzalishaji ambao tumekuwa tukiendelea nao ni uzalishaji kupitia majenereta haya ambayo yanatumia mafuta. Niishukuru Serikali kwa hilo, na najua tulikuwa na jenereta nne, kwa msaada wa Mheshimiwa Makamu wa Rais tukaongezewa jenereta moja, na watts ambazo tumekuwa tukipata kwa kipindi chote ilikuwa ni megawati 6.25 kwa majenereta matano. Lakini kwa maana ya ongezeko kubwa la miradi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, kuna mambo mawili, nikiamini kwa maana ya suala zima la grid ya Taifa njia ya msongo wa kv 132 kutoka Tabora Kwenda Katavi mpaka sasa hivi kwa mujibu wa taarifa za Mheshimiwa Waziri iko asilimia 26.7.

Mheshimiwa Spika, rai au ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri. Kasi ya maendeleo ya wananchi ni kubwa na yeyote akija Mpanda akija Katavi atakubaliana na mimi katika eneo hilo. Tumuombe Mheshimiwa Waziri, wakati tukisubiri huu umeme wa msongo mkubwa atusaidie, lengo ni kupeleka mbele maendeleo ya watu wetu. Nimuombe sana katika hilo. Waliweza kutusaiida jenereta, najua ni kipindi cha mpito kwa usikivu wake ndugu yangu Mheshimiwa Makamba tuliangalie hilo; wametusaidia hapo katikati. Na wakati wengine wakilalamika najua kuna suala la kukatika kwa umeme lakini mimi nishukuru walau kwa jitihada hizo zilizofanyika, maana unaposema ahsante hata ukiomba unafikiriwa kwa hiyo naomba mnifikirie katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo. Nimezungumzia habari ya mashine hizo na ongezeko la wawekezaji, na nimesema suluhu kwa kipindi hiki ni hiyo grid ya Taifa. Kuna mradi wa REA; mimi nimebakiwa na vijiji vitano. Vijiji hivyo ambavyo kwa mujibu wa taarifa wanasema mpaka ikifika mwezi Juni kwenda Agosti 2023 umeme utakuwa umewashwa katika maeneo hayo, vijiji hivyo ni vya Kamakuka, Mkokwa, Nguvu Mali, Nseso na Mkwajuni. Nimuombe Mheshimiwa, maeneo yote hayo ambayo nimeyazungumza kilimo kinafanyika, uzalishaji ni mkubwa na kuna viwanda vidogo vidogo vya ukoboaji wa mazao. Kwa hiyo tukiwapelekea umeme tunakwenda kuwasaidia na nikiamini upatikanaji huo wa umeme utasukuma mbele jitihada hizo za wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini nikitoka hapo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri; tuna mradi mwingine tuna takribani milioni 260 ambazo tunakwenda kupeleka umeme kwa ajili ya kusukuma pump kwa ajili ya Vijiji vya Society na Kakese, lakini pia kwa maana ya Zahanati ya Mwamkulu na Kakese, tumepewa takribani milioni 260, nishukuru sana kwa suala hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo yote nishukuru pia kwa ajili ya mradi wa ujazilizaji mzunguko wa pili (b), tunaambiwa vitongoji 1,686 na Katavi ikiwemo vitanufaika. Kwa hiyo mimi nishukuru kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya shukrani hizo maelezo yangu ya jumla natamani niione TANESCO, au shirika kwa ujumla wake ambalo kwa kiwango kikubwa Serikali imekuwa ikililea shirika hili, ikilipa nguvu shirika hili basi tufike sehemu tuone huyu mtu ambaye amaelelewa kwa kiwango kikubwa amefika sehemu anaweza kusimama.

Mheshimiwa Spika, nalisema hilo kwa sababu gani, kati ya maeneo ambapo huwezi ukalalamika uwepo wa wateja ni pamoja na eneo hili la TANESCO, wateja wapo tu ni wa kufikia. Labda nilichokuwa naomba au kushauri, tubadilishe mtazamo tuachane na ile biashara ya mazoea. Kama wateja ndio wanaolalamika tunaomba huduma, tunaomba huduma maana yake suala la soko siyo tatizo. Kwa hiyo tukiachana na biashara ya mazoea, TANESCO kwa jitihada wanazofanya, na wakabadilika; kuna taasisi nyingine mnaona kila kukicha inafanya mabadiliko; kawaangalie TANROADS na TARURA wanafanya mabadiliko kila kukicha. Na mimi natamani TANESCO waachane na biashara ya mazoea tunagalie sura hiyo kwamba ni soko la uhakika lakini kwa nini watu walalamike kila siku? Maana yake kuna kitu wanatakiwa wabadilike, na wakibadilika, mimi naamini haya yote ambayo yanazungumzwa, ukiangalia kwa maana ya nchi hii yenye fursa kibao, kwa maana ya kutekeleza miradi ya nishati jadilifu ikiwemo joto ardhi, tungamotaka, upepo na jua pamoja na matumizi bora ya nishati yanawezekana. Na nchi yetu njema, fursa zote zipo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naongea na jirani yangu hapa Mheshimiwa kuna sehemu moja kama unaenda Moshi, unaambiwa jihadhari upepo mkali, hiyo ni fursa. Kama tunaambiwa tunapita kwa magari kwamba jihadhari upepo mkali, hiyo ni fursa, na maeneo mengine yote ni fursa. Lakini moja kubwa haya yote hata kama tutatumia vyanzo vyote hivi kuviingiza kwenye grid ya Taifa, tusiache, kama nilivyozungumza pale mwanzo, kuchukua tahadhari. Sitamani siku moja tukaona migawo hii ikiendelea eti kwa sababu kuna jambo moja hatukufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa unyenyekevu mkubwa naunga mkono hoja.