Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie kwenye bajeti ya nishati. Pamoja na kukushukuru lakini tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu katika safari hiyo uendako Mwenyezi Mungu akujalie upate ushindi na ushindi ulio mnono. Watanzania wote sasa hivi dua zetu zielekee kwa Mheshimiwa Tulia, inshallah na Mwenyezi Mungu atakujalia katika hilo. Wanaokwenda Kanisani, wanaokwenda Msikitini kwa sababu hili jambo litaleta heshima katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naanza kuchangia, na ninaanza na hao wenzetu wa REA. Ni kwamba kazi ya REA ni kubwa sana katika nchi hii. Wamefanya miradi mingi mizuri sana katika hii miradi ambayo imefanyika. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, tumepita nafasi ya kuangalia miradi, kwa kweli imefanyika kwa ustadi mkubwa, na Wizara tunaishukuru sana, wamekuja na jambo la kupeleka ma-engineer kila Wilaya ambao wanakwenda kusimamia miradi ya REA na kutoa taarifa Serikalini na kwa sisi Waheshimiwa Wabunge. Tunaipongeza Wizara kwa ubunifu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika jambo hili nikwamba mwanzo ni mgumu sana, sasa katika mwanzo huu tunataka Wizara waje watueleze hapa katika majumuisho yao.

Mheshimiwa Waziri ni kwamba hawa mainjinia walioko kule wamejiegesha katika ofisi za TANESCO. Maeneo mengi ofisi za TANESCO ni za kupanga ambavyo wana vyumba vyao na watumishi wao. Sasa hawa Mameneja ambao mliowapeleka wa REA wanakuwa wameelea. Hadhi ya kumuita injinia ambaye ni Meneja wa REA katika eneo hilo inakosekana.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni kwamba hawana usafiri hata kwa kuanzia pamoja na bajeti zetu ndogo hizi pikipiki boxer ni 2,700,000, na kama zitatolewa ushuru hizi pikipiki zinaweza zikawa msaada mkubwa sana katika kutembelea na kuona miradi ya REA inayoendelea, na ninyi kama Wizara mtapata taarifa mnazozitaka kwa haraka, kwa sababu tayari waratibu mnao katika makao makuu yote ya wilaya nchini. Lakini la pili ni wakandarasi wanaofanya kazi. Ni kwamba mnao wakandarasi wengi, wako wakandarasi wazuri wanaofanya kazi tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, Lakini kuna mkandarasi Mheshimiwa Waziri, ungenisikiliza, kwa sababu huyu mkandarsai anafanya kazi katika Mkoa wa Tanga na Wilaya jirani ya Korogwe na Lushoto. Huyu mkandarasi tumekwenda kule Kwenda kuangalia kazi yake, ni kwamba amepewa fedha kwa ajili ya kufanya kazi Korogwe, Mkinga pamoja na Pangani.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sisi wanasiasa ni kwamba hili tunaloliona, huyu mkandarasi pamoja na kwamba alifanya kazi nzuri huko nyuma za miradi mikubwa na akapata hii kazi na akachukua advance zaidi ya bilioni tatu na kitu, sasa tunaomba aanze kukatwa penati kuanzia muda alioacha kukamilisha mradi ule. Na kwa sababu kesi za kuishitaki nchi zinakuwa nyingi nendeni naye kwa utaratibu mzuri, kaeni vizuri sana kisheria, apigwe penalty yule, na hizo penati ni takriban milioni 33 kwa siku. Tangu sisi tumetoka kule nafikiri sasa hivi huyu anakaribia kufikia asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, m-terminate contract yake, lakini isiwe sababu ya kuilaumu REA kwa sababu REA imesimamia miradi mingi kwenye kandarasi zaidi ya 60, mkandarasi mmoja si sababu hiyo. Kwa hiyo tunaomba watu wa REA wawe makini katika kuangalia wakandarasi tena wa aina hii, na huyu mkandarasi, kwa sababu tayari anapofanya kazi ni kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na huyo Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati, Mheshimiwa Kitandula, anapita kusimamia miradi yetu kila kitu.

Mheshimiwa Spika, leo hata kwa kwenyewe Mwenyekiti nako kumepata mkandarasi wa hovyo, sasa inakuwa ni tatizo kubwa. Tukija humu ndani ya Bunge lazima tuwe wakweli, tuseme, Mwenyekiti hawezi kusema lakini sisi tunaoyasimamia haya mambo tunayaona, sasa lazima tuseme. Kwa hiyo sisi tunawapongeza sana REA kwa kazi nzuri wanayoifanya, wapo wanaoweza kuangalia huyu mkandarasi mmoja kati ya wakandarasi 60, mtu kama huyu anataka kaharibu sifa. Lakini tunaipongeza sana REA kwa kazi na miradi mikubwa.

Mheshimiwa Spika, katika hili tunaomba sasa REA umeme huu unaopelekwa vijijini, kuna watu masikini. Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumza hapa, huu umeme wa jua mnaouona huu shilingi 27,000 shilingi labda 50,000 akifanya na installation ndani takriban inafika shilingi 100,000. Kule mngeenda Guangzhou Mheshimiwa Waziri, maonesho ni tarehe tano mwezi wan ne takriban mpaka mwezi wa sita. Kaangalieni, kule kuna taa za sola nzuri, kuna watu hawahitaji huu umeme wa kuchoma welding wanataka umeme wa taa, friji na Tv. Tumieni umeme wa jua kwenda kuwapelekea hawa watu.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali inatoa ruzuku kwenye kuunganishia mtu umeme, toeni sasa hiyo ruzuku ifanye kazi kwenye taa za sola na wakipelekewa watu masikini huko vijijini watashukuru na kuliombea Taifa hili hakuna mfano wake, na wao waonje ladha ya keki ya nchi hii, kwa sababu huu umeme wa jua hauhitaji gharama kubwa za kiasi hicho. Juzi tumeenda kuweka saini wewe mwenyewe Mheshimiwa ulikuwa shahidi, umeme wa upepo. Umeangalia gharama kuna megawatts 50 gharama zake zile ni tofauti. Japo gharama za kwanza zitakuwa ngumu lakini badaye tunaanza kunufaika.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala ambalo Mheshimiwa Iddi hapa amelizungumza, suala la hawa vijana wetu. Vijana wanamaliza katika vyuo na wamesomea umeme. Sasa hawa vijana wakiwa wanakosa kazi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwenye Ilani tunataka ajira milioni 10 tutazipata wapi ilhali kuna ajira manzifunga? Hawa vijana tayari wangepata leseni hawa wenzetu wa EWURA usajili CRB. CRB wanasajili wakandarasi wa ujenzi class seven mpaka class one, sasa hawa EWURA wangesajili hawa vijana wangepewa class, kama ni class seven waanzie huko.

Mheshimiwa Spika, hawa vijana wakafanye kazi ya installation, mmewafundisha umeme, watashindwa kutengeneza umeme vijijini wa taa tatu au taa nne? Kwa hiyo kila kazi itafanyika kwa class yake. Hawa vijana mngewapa na gharama zikawa ndogo za kulipa. Kama mnakwenda kujenga vituo vya mafuta vijijini mnashindwaje kuwapa leseni hawa vijana wakaenda wakafanya kazi? Wapo ma-engineers wengine wamemaliza vyuo, hawa ma-engineers waliomaliza vyuo nao wanatakiwa kusaidiwa. Wangefanya kazi hizi ambazo zinakuwa ni nyepesi na mnapunguza gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Spika, muhuri shilingi 50,000, fundi shilingi 100,000 bado installation ya umeme. Mtu akinunua installation ya umeme anunue mita, socket breaker, tayari inafika kama shilingi laki tatu na zaidi, hizi gharama zinakuwa kubwa kwa hiyo ziangalieni hizi gharama. Huyo mtu akimaliza kufanya kazi haitaji muhuri, yeye mwenyewe awe ni muhuri, anagonga muhuri wake. Na kwa sababu ana leseni anapeleka TANESCO wanakwenda kutoa. Mheshimiwa Waziri hili haliwezi kukushinda. Nafikiri hili na tulilishauri mpaka kwenye kamati. Kwenye majumuisho, uje ulisemee kwa sababu litakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TBS. Hawa wenzetu wa TBS ni wachanga wamepewa kazi ya kuweka kinasaba katika magari. Ushauri wetu sisi tunachosema ni kwamba waongeze jitihada na juhudi katika kazi; tunajua ni wachanga. Aliyekuwepo pale TFI alifanya kazi kwa miaka 11 ndipo akawa giant, sasa hili ni shirika la Serikali lipunguzieni milolongo. TBS apewe fedha ili anunuee magari, aweke katika kanda, asaidiane na EWURA hii kazi ili tupunguze dumping ya mafuta nchini.

Mheshimiwa Spika, lakini automation machine tulielekeza sisi kwenye tenda zake sasa anazokuja kufanya sasa hivi TBS aje kwa automation machine ili yale magari yaweze kuwekewa kule. Lakini kuna kelele na minung’uniko midogo midogo, TBS amalize, aweke session mbili. Asubuhi wawepo wafanyakazi watakaofanya kazi saa mbili mpaka saa kumi na wawepo watakaofanya saa kumi mpaka saa nne usiku, ili magari yasilale depo yanapakiwa mafuta. Kila gari iliyopakiwa depo iwekewe mafuta, ikishawekewa kinasaba ifungwe seal. Lazima TBS naye afunge seal yake ili kusudi hiyo gari ifungwe seal ya deport na itafungwa seal ya TBS. Tumpe uwezo TBS aweze kufanya kazi. Taifa hili liweze kuokoka na mafuta ya dumping nchini.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; ninaomba dakika moja tu. Ni kwamba katika Jimbo langu umeme unakatika, Mheshimiwa January mwenyewe alikuja ukaona, na akatueleza kabisa kwamba anatengeneza line nyingine kutoka Mpovu Geita kuja Sengerema. Wananchi wa Sengerema wamenituma katika jambo hili na umeme visiwani, niletewe umeme visiwani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana…

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: … hongera sana Mheshimiwa January Makamba baada ya kutoka hapa basi uniambie sasa lini Sengerema tunapata umeme? Ahsante sana.