Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze na mimi kukupongeza kwa makusudi kuamua kugombea nafasi ya Uspika. Tuna imani kubwa na wewe, tuna amini kwamba utakwenda kushinda. Kwa namna ya Rais wetu alivyoitangaza Tanzania na namna anavyoonesha ujasiri na uwezo mkubwa wa mwanamke wa Tanzania tunaamini hii itakuwa kwako ni kampeni tosha ya kukufanya urudi na ushindi. Mwenyezi Mungu atakujalia utashinda. Ila ufahamu, ushindi wako ni fahari ya Wabunge Wanawake wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo nichukue fursa hii kumpongeza Waziri na Naibu wake Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuleta mabadiliko kwenye Wizara ya Nishati.

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Tauhida kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe.

TAARIFA

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba wanawake ni fahari ya wanaume na ushindi wako utakuwa ni fahari ya Watanzania wote na wanaume kwa ujumla. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tauhida unapokea taarifa hiyo?

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, niseme kwamba nimeipokea taarifa. Nianze kwa hapo kaka yangu tuacheni wanawake kidogo tujidai wa Tanzania, msiwe na wivu kwenye hilo. Huu ni wakati wetu wa kujidai, kujivuna na kuringa. Tupeni fursa kidogo na sisi turinge wanawake wa Tanzania. Tunaheshimu na tunatambua msaada mkubwa mnaotupa mpaka tukafika hapa tulipofika. Wanaume wa Tanzania mmetuunga mkono na mmetu-support vya kutosha. Ila kuna muda tuacheni na mkituona tunasema jueni tu kwamba ni wakati wetu wa kuringa acheni turinge kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maringo hayo ya wanawake wa Tanzania na wewe utaenda kuionesha wanawake wa Tanzania wana ringaje miaka hii, tunaamini utaenda kushinda. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu Waziri. Mheshimiwa Waziri una Naibu Waziri mzuri, msikivu na mfanyakazi hodari. Mwenyezi Mungu kakujalia umepangiwa Naibu Waziri hana machachari ambaye anafanya kazi vizuri kama unavyofanya wewe mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri tumepanga kwa makusudi Wabunge wa Zanzibar kila atakayesimama tukupongeze kwa punguzo lililoenda kushusha umeme wa Zanzibar. Mwaka jana kila Mbunge wa Zanzibar aliyesimama alikuwa analalamikia bei ya umeme iliyokwenda Zanzibar. Binadamu ukitendewa mema basi ukumbuke na kushukuru. Kama hukuweza kushukuru kwa binadamu mwenzio unayemuona ni ngumu kumshukuru Mja wako aliyekuumba ambaye humuoni. Tunakushukuru na tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukujalia kuweza kukupa nguvu na uwezo na hekima na akili ya kuweza kufanya kazi kwa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wamepunguza umeme Zanzibar na bei imepungua. Tumuombe, bado dhana na dhamira ya Wabunge wa Zanzibar tulilozungumza hapa na kupiga kelele aliloenda kulitimiza, kuondosha bei ya umeme kupunguza lakini bado kwa wananchi haijashuka vizuri. Tunaomba; ninaelewa vizuri kwamba hii si Wizara ya Muungano; lakini ninapata shida kutenganisha maji na mafuta. Unapoizungumza Tanzania tayari umezungumza Zanzibar na Bara. Mheshimiwa Waziri tukuombe kwa unyenyekevu mkubwa tulete maombi yetu kwako haya ni maombi. Sisi tukiwa kama Wabunge wa Zanzibar tukuombe tunaomba hebu kaa kitako na Waziri wa Zanzibar uone maeneo gani yana shida kiasi kwamba huku umeme umeshuka halafu kule bado bei ya wananchi iko pale pale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la madeni ambalo linatukabili ambalo hilo deni ni kubwa linahitaji kulipwa ili tuweze kuendesha nchi yetu vizuri. Hatulikatai Mheshimiwa Waziri, tunaodaiwa, tutalipa, tunakuahidi wananchi wa Zanzibar tutalipa. Lakini tunaomba mtumie akili na uwezo aliyokupeni Mwenyezi Mungu kuona deni tunalipaje, mkae na Waziri msaidiane kuona deni tunalipaje lakini vile vile kuona mwananchi wa Zanzibar anapata umeme sawa na Mtanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme ndiyo kila kitu kwa sasa. Ili Mwananchi wa Zanzibar aweze kunufaika lazima naye nishati ya umeme kwake imwendee bei ikiwa nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wetu wa Zanzibar ni msikivu, Rais wetu wa Zanzibar anasaidia wananchi wa Zanzibar. Tunaomba ona Waziri ukizungumza nae wa Zanzibar mtataka lipi kwenye lipi? muone mnaongea na viongozi wetu kuweza kufanya sasa. Dhamira njema uliyoifanya Serikali yetu ya Muungano ilioifanya kushusha bei ya umeme imfikie mwananchi wa chini wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, mimi nikisimama hapa namuongelea mwanamke wa Tanzania ninamzungumza mwanamke wa Tanzania ndiyo anayenifanya nije hapa Bungeni, kwa hiyo kila nitakaposimama sina ajenda zaidi ya kumzungumza mwanamke wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri. Wakati picha za mwanzo naanza kuziangalia alianza kupeleka majiko ya gesi vijijini, aliwapelekea wanyonge vijijini. Alifanya jambo hili na anastahili kupongezwa. Hakuanza mikoa ambayo ni ya mjini, alikwenda vijijini, alienda kwa dhana ya kusema kwamba mwanamke wa Tanzania kubeba kuni kichwani iwe basi. Mheshimiwa Waziri atembee kwenye dhamira ya aliyemteua, dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu kumuona mwanamke wa Tanzania anaishi Tanzania akiwa hana matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muda huu tuliyokuwa nao tunataka tutumie vizuri fursa hii tushikeni. Endeleeni kutushika mkono fanya vizuri kaka, fanya vizuri, mwanamke wa Tanzania mfikirie. Anakwenda shambani tena anakwenda na mume wake wanalima lakini muda wa kurudi mwanamke amejitishwa kuni kichwani, mtoto mgongoni, baba anafanya kazi moja ya kuburula baiskeli. Akifika nyumbani akiutua mzigo wa kuni anapanga jiko kupika ugali watoto wale na baba ale. Sasa, mwanamke huyu wa Tanzania atapumzika lini? atajisikia lini? Tumwombe Mheshimiwa Waziri, kwamba katika hili aongeze jitihada za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la umeme tunajua kuna msemo unasema kawia ufike. Kwenda mwenyewe kwa taratibu na mipango yake atafika vizuri. Na kuna muda nimshauri Mheshimiwa Waziri, kuna mambo mazuri anayoyafanya, kaka yangu amezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tuko Dodoma Wabunge tunakwenda kuona bwawa la kufua umeme, niambie Mheshimiwa Waziri kama haya yangekuwa wazi, kila kitu kikawa wazi wananchi wa Tanzania wangekuwa wanafahamu nini kinaendelea? itumie Wizara yako kwa wale ambao wana nafasi, mara kwa mara fanyeni vipindi lawama na manung’uniko ya watanzania yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna maendeleo watu wanalala siku moja ndani ya nchi wakaamka maendeleo yakawa yamekuja, maendeleo ni safari ndefu. Kuna muda mwingine unaweza kutoa mfano hata wa familia yako, angalia muda mlioutumia kupiga hatua, kutoka kwenye ujenzi mpaka mnapomaliza mnakwenda hatua kwa hatua. Maendeleo haya yataleta maneno na maneno yake Mheshimiwa Waziri na Naibu wake yasiwarudisheni nyuma, maneno hata kwenye kanga yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwetu Zanzibar kuna mtu ambaye anatengeneza kanga, ukipeleka maneno hayo ukafikisha maneno mia moja unapewa zawadi ya kanga. Kwa hiyo maneno hayafanyi mtu asifanye jambo lake, maneno ndiyo yamekufanya wewe kufanya ukue zaidi na ufanye kazi zaidi. Kiongozi level uliyofikia wewe si wa kusikiliza maneno, sikiliza Watanzania wanyonge wanataka nini? Hakuna mnyonge anayepiga kelele, hakuna mnyonge anaesema maneno ya hovyo, kila siku mnyonge kazi yake anamuomba Mungu, kusema Mungu tupatie, tuletee, tupe, hiyo ndiyo kazi ya mnyonge. Aliyeshiba na aliyepata mafanikio ndiyo mwenye kelele na mwenye maneno. Kwa hiyo nimpe moyo Mheshimiwa Waziri kaka yangu aendelee kufanya kazi, atimize kiu, ndoto na malengo ya Mheshimiwa Rais wetu. Kama atalifanya hilo atatutendea haki wanawake wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja; atoka siku moja na gari, apite, akifika maeneo ya Chalinze kwa Mheshimiwa Ridhiwani mpaka unapandisha Kibaha aangalie ndugu zake wanaobeba boda boda na mkaa, amuangalie yule boda boda anavyoumia na mkaa, hafanyi vile kwa kutaka. Anafanya kwa kutafuta riziki yake, tunataka tunapotoka na magari yetu tuwakute wamebeba mitungi ya gesi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa haya, ahsante sana.

MHE. TAUHIDA CASSIAN. GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)