Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. KABWE Z. ZITTO: Mheshimiwa Spika, leo na kesho tunajadili bajeti ya Wizara ambayo inabeba asilimia 46 ya Bajeti yote ya maendeleo ya nchi yetu.
Yaani katika fedha za Bajeti ya Maendeleo ambazo zinaombwa na Serikali mwaka huu, trilioni 10.5, trilioni nne point nane ni ya Wizara inayoongozwa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Naamini kabisa kwamba, wakati tunapanga siku za kujadili hatukuwa tumezingatia hili, ilipaswa Wabunge wapate muda mwingi zaidi kwa kuwa na siku nyingi zaidi za kuijadili Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, Wizara hii inaongoza taasisi ambayo kwa mujibu wa Taarifa ya PPRA ndio taasisi ya pili kwa thamani ya manunuzi nchini, TANROADS, baada ya TANESCO. Kwa hiyo, ni Wizara ambayo ni nyeti sana na naamini kabisa kwamba, Waheshimiwa Wabunge wataitendea haki na Serikali itaweza kutoa majibu yanayostahili kwa ajili ya hoja mbalimbali ambazo Wabunge wataweza kuzi-raise. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda nisisitize hoja ambazo Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Waziri Kivuli wa Miundombinu, amezi-raise ziweze kupatiwa majibu na hasahasa hoja ya MV Dar-es-Salaam kwa sababu, ni hoja ambayo inakimbiwakimbiwa na ni muhimu tuweze kuona suala la MV Dar-es-Salaam likichukuliwa hatua, ndiyo tutaamini kweli kuna nia ya dhati ya kupambana na ufisadi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Nsanzugwanko na Wabunge wengine wa Kigoma watakaopata nafasi watazungumzia barabara za Mkoa wa Kigoma. Tuna kilometa 258 ambazo zitaunganisha Nyakanazi na Manyovu kwa maana ya kutokea Kabondo – Kabingo – Kibondo – Kasulu mpaka Manyovu, kilometa 258.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na Waziri wa Fedha walitwambia kwamba, mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Katika vitabu vya bajeti hatuoni, siyo tu ni lini mradi huu utaanza, hatuoni fedha zimetengwa kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kuna confusion ya project number kwa sababu, barabara iliyokuwa inatoka Sumbawanga mpaka Nyakanazi ilikuwa na Project Number hiyo. Sasa hivi project number nyingine kwa Nyakanazi mpaka Manyovu kwa maana ya kwamba, Wizara ya Ujenzi bado haijarekebisha jambo hili. Kwetu sisi Kigoma, mkoa pekee ambao haujaunganishwa na mkoa mwingine wowote kwa lami moja kwa moja, barabara ya Nyakanazi ni barabara muhimu, ni barabara ya kimkakati na ndiyo siasa za Kigoma. Kwa hiyo, naomba jambo hili Waziri aweze kulitolea ufafanuzi wa kina, hasa hasa inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara inayounganisha Tabora na Kigoma kuna takribani kilometa 200 pale kama 204 hivi ambazo bado hazijakamilika. Kwa hiyo, naomba Waziri aweze kutueleza taratibu, tumeona Urambo – Kaliua itaanza mwaka huu, lakini pale Kazirambwa mpaka Chagu hatujajua inaanza lini. Kwa hiyo, naomba mambo haya Waziri aweze kuyatazama ili Mkoa wa Kigoma uweze kuunganishwa. Pili, barabara ya kutokea Uvinza kwenda Mpanda na barabara ya kutokea Uvinza kwenda kwenye Daraja la Malagarasi, tunaomba tupate commitment hapa ya Serikali, inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hasa tumeambiwa kwamba, barabara ya Mpanda mpaka Uvinza inaanza kilomita 30 kuanzia Mpanda. Naomba nimshauri Waziri kwamba, tuwe na Mkandarasi ambaye ataanzia Mpanda kuja Uvinza na tuwe na Mkandarasi ambaye ataanzia Kanyani mpakani kwenye njiapanda ya kwenda Uvinza mpaka Uvinza ili tuweze kuhakikisha kwamba, barabara hii inakamilika vizuri kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la reli. Kama ilivyo kwa barabara, reli kwa Kigoma ndiyo siasa na siyo Kigoma peke yake, kwa mikoa yote ambayo inategemea reli ya kati, reli ni kiungo muhimu sana cha usafiri. Hapa napenda nirejee maoni ambayo yalitolewa asubuhi kama swali na Mheshimiwa Sabreena na baadaye tukawa tumeyazungumza na majibu ambayo Waziri ameyatoa; kuna haja kubwa ya kuchukua hatua za haraka kuondoa ulanguzi wa tiketi katika Stesheni ya Reli, Kigoma. Ni jambo ambalo linaumiza sana watu, watu wanatoka mbali na njia pekee ni njia ya uwakala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata ukisema tunatumia digital, tunatumia simu, bado simu zitatumia mawakala kwa sababu, ni lazima TRL iweze kukubaliana kuingia makubaliano na kampuni binafsi kama zile ambazo zinatumika kwa ajili ya uwakala, kwa hiyo, huwezi kukwepa uwakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jambo hili watu wa TRL waweze kulitazama, lakini jambo la msingi sana katika eneo hili, lazima sasa tufahamu kwamba, RAHCO ndiyo TANROAD ya reli. RAHCO inapaswa kuachia assets zote ambazo hazihusiani na ujenzi wa reli, kuiachia TRL ili TRL iweze kuwa na balance sheet iliyo nzuri kwa kuweza kupata fedha za uendeshaji wa reli, kwa hiyo, naomba jambo hili liweze kutazamwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, tuangalie namna gani ya kutumia Stesheni za Reli kama maeneo ya biashara; stesheni zetu za reli zote kuanzia Dar-es-Salaam mpaka Kigoma zimelala! Hamna shughuli yoyote inayofanyika! Kwa hiyo, naomba TRL waweze kupewa kibali maalum cha kuendeleza Stesheni za Reli ambazo sasa hivi ziko chini ya RAHCO. Kwa hiyo, naomba mabadiliko hayo yaweze kutazamwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kupata maelezo ya Serikali kuhusu kipande cha reli kutokea Kigoma kwenda Tabora na Uvinza – Msongati kwa ajili ya standard gauge kwa sababu, naona sasa hivi mwelekeo wa Serikali ni kupeleka reli Isaka mpaka Kigali na mmesahau kabisa suala zima la Uvinza – Msongati na jambo hili kwetu ni siasa kwa sababu, tunataka Uvinza iwe ni hub kwa ajili ya maeneo ya Maziwa Makuu. Kwa hiyo, naomba jambo hilo liweze kutazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza, naomba ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri kuhusu Uwanja wa Ndege wa Kigoma kwa sababu, tulizungumza na alikuja Kigoma na aliona. Ametenga fedha, lakini naomba nifahamu kiwango gani ambacho kinakwenda kupanua runway na kiwango gani ambacho kinaenda kujenga jengo la abiria kwa sababu, kwenye bajeti yake hakufafanua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya mambo ambayo yame-miss katika bajeti; la kwanza, ni Bandari ya Ujiji kwa sababu tulishakubaliana na Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Ndogo ya Ujiji na Mamlaka ya Bandari Tanzania wamesema wanaanza mwaka huu. Sasa sijaiona hiyo kwenye bajeti! Sasa ni kwa sababu, iko kwenye Bajeti ya Maendeleo ya Mamlaka ya Bandari ama namna gani? Naomba nipate maelezo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, ni suala zima la Bandari ya Kigoma. Bandari ya Kigoma ndiyo Mji wa Kigoma! Bandari ya Kigoma ikilala mji unalala kwa sababu, biashara zinakuwa hazipo! Sasa hivi Bandari ya Kigoma inaendeshwa na Mamlaka ya Bandari, lakini huwezi ukafanikiwa kuiendesha Bandari ya Kigoma kama huna biashara kutokea Kongo, kama huna biashara kutokea Kalemii. Kwa hiyo, Serikali inapaswa kuwa strategic kuhusu Bandari ya Kigoma.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Kigoma inapaswa kuendeshwa na taasisi ambayo inao uwezo wa kupata mzigo kutoka Kongo. Kwa hiyo, Waziri naomba jambo hili alitazame, tulilizungumza Kigoma, tulijadiliana Kigoma, lakini sasa hivi kuna ushindani mkubwa sana, vinginevyo reli tunayojenga itakuwa haina maana yoyote kwa sababu, haitapata mzigo kutokea Kongo. Kwa hiyo, naomba jambo la uendeshaji wa Bandari ya Kigoma waweze kulitazama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, MV Liemba, naomba jambo hili tuweze kulimaliza, tumelizungumza muda mrefu sana. Waziri Mwakyembe anakumbuka, tulizungumza mpaka na watu wa Ujerumani, alikutana na Waziri wa Usafirishaji kutoka Ujerumani wakati akiwa ni Waziri wa Wizara hii. Jambo hili la MV Liemba yasije yakatokea mambo yaliyotokea kwa MV Bukoba! Kwa hiyo, naomba MV Liemba, kama meli ya kihistoria, iweze kutazamwa na iweze kushughulikiwa kwa namna ambavyo inatakiwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, nakushukuru sana.