Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo ndiyo inafanya Taifa letu liwe na mwanga kila saa.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa jinsi ambavyo unaongoza Bunge letu na niseme tu kwa moyo wa dhati kwamba wewe ni Spika ambaye nimeona na nadhani kwa sababu ya taaluma yako ya sheria ndio maana unatuongoza vizuri katika Bunge hili. Kwa kweli Mungu akubariki sana. Lakini nikutakie kila la kheri katika safari yako ya shughuli iliyoko mbele yako. Mungu akutangulie na naamini utashinda kwa sababu una uwezo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme pia nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaongoza Taifa letu na kusimamia kila Nyanja ya Taifa letu kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, lakini nitakuwa mwizi wa fadhila nisipompongeza pia Mheshimiwa Waziri, Ndugu yangu Makamba pamoja na wasaidizi wake Naibu Waziri pamoja na Wizara nzima kwa ujumla wataalamu ambao wanamsaidia. Kwa kweli mnachapa kazi na mnajitahidi pamoja na changamoto nyingi ambazo mnakabiliana nazo. Mwenyezi Mungu aendelee kuwatia nguvu ili muendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais akatekeleze majukumu haya na wananchi waendelee kumwamini, na In Shaa Allah Mungu akijalia aendelee kuongoza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza mimi niseme tu kwamba bajeti hii nimefarijika na ninaipongeza kwa sababu moja tu; nikiangalia jinsi ambavyo bajeti hii ni ya shilingi trilioni tatu na bilioni karibu 48 na point juu; lakini ukiangalia Wizara imekuja na kwamba ujenzi wa miundombinu ni asilimia 97.1. Hiyo tu peke yake mimi ilinifanya nione kwamba hawa watu wako committed, kwamba kweli wanataka kupunguza changamoto za wananchi. Matumizi ya kawaida ni asilimia 2.9 tu. Hapo peke yake imenionesha kwamba kwa kweli Wizara hii iko kwenye mazingira ambayo ya kujisikia kwamba ingetaka kuondoa matatizo yote ya umeme katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tujuavyo, changamoto zinakuwepo tu kwa sababu ya resources tulizonazo, kwamba hazitoshi. Na kwa sababu hazitoshi ndiyo maana sasa unaona tunaendelea kuzungumza katika Bunge hili kuiomba Serikali sasa ione ni jinsi gani inaweza kuhakikisha kwamba changamoto zilizopo za upatikanaji wa umeme katika maeneo yetu, katika vijiji, kata na vitongoji viweze kuwepo umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi; mimi nina kata 27, vijiji 86, vitongoji 268. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kusema kwamba atatupatia vitongoji 15 kwa kila Jimbo; lakini katika vitongoji mia mbili karibu 68 ukitoa vitongoji, 15 hebu fikiri kwamba hali itakuwaje huko kwenye jimbo? Kwa hiyo bado tunaiomba Serikali ione ni jinsi gani itahakikisha kwamba inatupunguzia adha hii sisi Wabunge kwa sababu tunapokuwa majimboni, tunapokuwa kwenye ziara mbalimbali changamoto kubwa wananchi wanatudai umeme na wanasema mbona umeme hakuna? Tunajaribu kwaambia Serikali imeanza mchakato wa kuhakikisha kwamba kila kijiji inapata umeme halafu tutakuja kwenye kitongoji. Sasa katika bajeti hii vitongoji 15 bado tunaona kidogo Serikali ingeangalia, na hasa Wizara ingeangalia namna ambayo itatufikisha.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi katika vitongoji vingi, ambavyo siwezi kuvitaja, lakini kata ambazo mpaka sasa vitongoji vyake havina umeme ni vya Bwawani, Oljoro, Nduruma, Musa, Mwandeti, Oldonyo Sambu kwa maana ya Kata ya Otoroto, Mlangarini, Sambasha, Oldonyo Sambu, Oldonyouwas, Lengijabe, Lemanyaka, Kimnyak. Vitongoji vya hiyo kata hizi zote ambazo nimezitaja bado havina umeme; na wananchi wetu katika kata hizo nilizozitaja hawako mbalimbali, kwa maana hawako scattered, wako karibu karibu kabisa; kwa hiyo wanahitaji umeme kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na unajua umeme ni sehemu kubwa sana ya maendeleo. Kama ni kuchaji simu, uchomeleaji, kusaga mahindi, na kufanya mambo mengi basi wananchi wanategemea kupata huduma ya umeme ili mwisho wa siku basi waendelee kufurahia huduma kutoka kwenye Serikali yao. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo moja gumu mno, na ugumu wake miundombinu yake jinsi ilivyokaa ramani yake imekaa vibaya, na hivyo niombe sana kwa kweli ujaribu kutusaidia kwa sababu wananchi wanahitaji umeme.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna suala la uimarishaji wa TANESCO. TANESCO inahitaji kuimarishwa. Niwapongeze Wizara kwa sababu mmefanya mabadiliko makubwa hivi karibuni katika hiki kipindi cha mwaka mmoja, naona kama kuna mabadiliko makubwa ndani ya TANESCO kiasi fulani lakini bado mnahitaji kufanya kazi kubwa kurekebisha TANESCO; lakini pia TANESCO isaidiwe kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ukiachilia madai makubwa, yale ambayo yametajwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nikiangalia mfano taasisi za Serikali. Taasisi za Serikali hazilipi bili za umeme, ni kwa nini? Ukisoma ripoti ya Kamati, taasisi za Serikali tu peke yake inadaiwa zaidi ya bilioni 334, hazilipi. Naomba hili nalo liangaliwe, TANESCO ipewe nguvu. TANESCO bado haina nguvu kwa upande wa madeni makubwa, lakini pia Serikali na taasisi za Serikali zinavyotumia umeme hailipi ina maana gani? Kwa hiyo naomba kama taasisi hizi kwenye bajeti zao zimeweka ulipaji wa bili ya umeme kwa nini wasilipe? Mheshimiwa Waziri TANESCO wasaidiwe wawakatie umeme. Wakiwakatia nafikiri watashtuka na watalipa bili. Hii siyo sawa, tutakuwa tunawaonea TANESCO lakini hatuwasaidii.

Mheshimiwa Spika, Namshukuru sana Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Arusha kwa sababu anajitahidi sana. Ukimpigia simu saa yoyote maskini ya Mungu anapokea, ana-deal na mambo makubwa makubwa magumu. Kwa kweli nampongeza sana na ninashukuru sana kwa sababu ni mtu msikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la uunganishaji wa umeme. Uunganishaji wa umeme bado hatuelewi vizuri kama Wabunge na hata Watanzania hawaelewi; kwamba, ni wapi ambapo ni shilingi 27,000, ni wapi ambapo labda inatozwa nguzo moja shilingi laki tatu karibu na 60, ni wapi inakuwa sijui ngapi? Hili nalo Mheshimiwa Waziri inabidi Wizara iliangalie sana na itoe kabisa schedule ambayo nchi nzima itajulikana. Kama maeneo yametofautiana basi iwekwe vizuri. Kuna wananchi unakuta nguzo imefika mpaka kwake, Serikali imefikisha nguzo pale lakini insahindwa kuvuta umeme kwa sababu ya gharama kubwa. Kwa hiyo hebu tuangalie ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu hawa waweze kuendelea kufurahia matunda ya nchi yao na hasa kuhakikisha kwamba siku zijazo Chama cha Mapinduzi kinaendelea kung’ara ndani ya nchi yetu na kuendelea kutawala vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)