Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa January Makamba na Naibu wake, wajomba zangu wale wote wawili, kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wa mijini na vijijini wanapata huduma hii muhimu ya nishati ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini, nina vijiji 24 ambavyo vinahitajika kuwashwa umeme. Vijiji tisa kati ya 24 ndivyo vimewashwa umeme, vijiji 11 bado vinaendelea, mkandarasi yupo site anaendelea na kazi; vijiji vinne bado kabisa havijafikiwa kuwashwa umeme. Kwa maelezo ya mkandarasi amezungumza mpaka kufikia Desemba vijiji vyote 24 vya Mtwara Vijijini vitakuwa vimewashwa umeme. Kwa hiyo nimuombe mkandarasi ambaye anashughulika na suala hili katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini aongeze speed ili mpaka kufikia Desemba basi vijiji vyote viwe vimekamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, gesi hii inatoka katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini katika Kijiji cha Msimbati, lakini kwa masikitiko makubwa sehemu ambayo inatoka gesi asilia umeme unawaka maeneo ya barabarani, ukiingia ndani hakuna umeme. Vijiji na vitongoji vingi umeme hakuna katika Kijiji hiki cha Msimbati ambapo gesi hii asilia inatoka. Kwa hiyo hii ni aibu, ni aibu kubwa sana. Niombe sana Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu sana, nikuombe Kaka yangu tuhakikishe vijiji hivi vinapatiwa umeme haraka sana kutokana na umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vijiji ambavyo vina shida ya umeme ni Kijiji cha Mnuyo katika Vitongoji vya Mnamba, Bumbwini, Lianje pamoja na Vitongonji wa Najibu na vitongoji vingine vingi sijavitaja. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana, sehemu hii ni sehemu muhimu, sehemu hii ndio sehemu ambako gesi inatoka. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri wananchi hawa waweze kufurahia huduma hii ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sehemu ambayo gesi inachakatwa, Madimba, maeneo mengi na vijiji vingi navyo hakuna umeme. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, nayo sehemu hii kwa umuhimu wake naomba umeme ufike kwa haraka kwenye vijiji pamoja na vitongoji. Kwa mfano Vitongoji vyote vya Mahiva, Uvikwani, Litembe, Miembeni, Namnaida B, Namindondi pamoja na Mitambo Shuleni hakuna umeme. Hii ni aibu kubwa kweli kweli kwa sababu maeneo haya sehemu ambayo gesi ipo, sehemu ambayo inachakatwa gesi umeme hakuna. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, na nikushukuru Mheshimiwa Waziri, kwa moyo wangu wa dhati kabisa, nilizungumza na wewe nikakueleza juu ya changamoto hizi, nashukuru Mheshimiwa Waziri jitihada ambazo umezichukua zinaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ninavyozungumza…

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa inatokea wapi? Aah! Mheshimiwa Shamsia Mtamba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Soud.

TAARIFA

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba tu kumpa taarifa Mheshimiwa Shamsia kwamba ni utaratibu ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeuwekwa kwamba wale ambao either kama ni source ya maji au ni ya umeme basi kwanza waanze kupata umeme wao kabla ya kusambaza katika maeneo mengine. Kwa hivyo kama kweli kuna maeneo ambayo gesi inapita lakini hao hawanufaiki nayo basi nafikiria Mheshimiwa Waziri lazima ajitahidi awa support hao.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Shamsia Mtamba unaipokea taarifa hiyo.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ninaipokea tena kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Spika, sehemu hii ya Msimbati na Madimba ni sehemu muhimu sana, na nimekuwa nikisema katika Bunge hili; barabara mbovu hakuna, huduma ya nishati ya umeme ndio kama hivyo hakuna, miundombinu ya watu wale maskini ya Mungu ni duni. Kwa hiyo, sehemu kama hii ni sehemu ya kuiangalia sana, sehemu kama hii inahitaji miundombinu ya shule nzuri ziwepo, maeneo haya shule nzuri hakuna, miundombinu ya afya, huduma za afya nzuri katika maeneo haya inahitaji ziwepo lakini miundombinu hiyo hakuna. Kwa hiyo ninaipokea taarifa ya Mheshimiwa kwamba maeneo haya ni lazima wayaangalie kwa macho mawili kutokana na umuhimu wake. Watu wale wanaweza wakahujumu kule. Kwa hiyo lazima Serikali muone umuhimu wa Vijiji vya Msimbati na Madimba, muwawekee mambo mazuri ili wananchi wale basi wafurahie na neema hii waliopewa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwisho kabisa ni kusisitiza. Mheshimiwa Waziri, kwanza tunakushukuru kwa unyenyekevu wako na usikivu wako. Tumekaa kikao na wewe sisi Wabunge wa Mtwara, na Wabunge wa Mtwara kwa kweli tuna changamoto kubwa sana ya umeme. Tuna changamoto kubwa wananchi wetu wanalalamika, wananchi wetu vitu vyao vinaungua, wanapoteza vitu vyao kila siku kutokana na changamoto ya umeme ya kukatika katika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana tuliyoyakubaliana kwenye kikao yafanyike kwa wakati na uamuzi mzuri uliouchukua wa kuhakikisha unakuja kutatua changamoto ya umeme katika Mkoa wetu wa Mtwara ndani ya siku 90 basi Mheshimiwa Waziri tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uweze kutimiza hili ili wananchi wa Mtwara waweze kufurahia huduma hii bora, huduma hii muhimu ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo mengi kwa kweli yamesimama, mambo mengi hayaendi, viwanda vingi sasa hivi wawekezaji wanashindwa kuja Mtwara kutokana na umeme kutokuwa wa uhakika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe, wewe ni mtu msikivu wewe ni mtu ambaye unafikika, wewe ni mnyenyekevu njoo umalize tatizo la umeme katika mkoa wetu haraka. Njoo umalize tatizo la umeme katika Mkoa wa Mtwara kwa uharaka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo, ninakushukuru sana. (Makofi)