Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; na mimi kwa kweli kama mwanamke na tunaoamini uwezo wa wanawake tuna kila sababu ya kuku-support; na In Shaa Allah, unaipeperusha bendera ya Taifa vizuri, uwezo wako si wa kutilia shaka, tunakutakia kila la heri. Ushindi wako ni ushindi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwanza kabisa, Mheshimiwa January my brother na Naibu wake, naomba tu niwambie kwenye Jimbo la Bunda Mjini umeme umefika takriban vijiji vyote, lakini bado speed ya kuunganisha ni ndogo kufikia nyumba za watu, kufikia taasisi bado ni ndogo sana. Bunda umeshakuwa mji wanahitaji maeneo yote yawake umeme. Kwa hiyo, hilo nilisema na niliweke wazi.

Mheshimiwa Spika, kwanza Watanzania wote tumeona fahari ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, hilo tunakubaliana kabisa. Lakini tunatamani uendeshaji wake, ukamilishaji wake uendane pia na thamani ya fedha ya Watanzania iliyowekezwa pale kwa sababu ni fahari ya nchi. Kwa sababu tunaamini ukikamilika on time utaweza kusaidia changamoto ya umeme hapa nchini, hilo hatubishi.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nina maswali yangu, natakiwa nipate majibu ya kutosha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba ambao mmeingia na mkanadarasi unataka Mkandarasi akichelewa kukamilisha Mradi anapaswa kutozwa tozo. Sasa huu mradi umechelewa kwa sababu ulitakiwa kukamilika mwaka 2022. Hata hivyo unatakiwa ukamilike mwaka huu, ambapo zimebaki siku 13; na taarifa zilizopo hautakamilika on time, utakwenda mpaka mwakani sijui tarehe 7 Juni. Je, kulikuwa na sababu za kutosha za mkandarasi kushindwa kutozwa tozo. Kwa nini TANESCO mpaka sasa hivi hawajamtoza mkandarasi tozo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutokukamilisha tu mwaka 2022 alitakiwa atozwe bilioni 329. Waheshimiwa wabunge, Serikali imekuwa ikichelewa tu kumlipa mkandarasi inatozwa tozo. Ukienda kwenye miradi ya barabara, ukienda kwenye miradi ya maji, kwa nini sisi tunapata kigugumizi kwa kuchukua pesa yetu? kwa nini TANESCO wanashindwa kuchukua hii tozo? Tunajua hata kama huko mbele walikosea lakini mwaka jana walishindwa kukamilisha mradi on time, mwaka huu mradi haukamiliki on time; kigugumizi gani kinakuwepo mkandarasi asitozwe tozo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hili tunawafanya wakandarasi waone Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu, na kwamba wanaweza wakafanya wanavyotaka. Nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jesca hapa, kwamba, mtu amekiri amepewa shilingi bilioni tatu halafu mambo yanaendela. Ni kwa sababu ya sisi kushindwa kusimamia mikataba yetu kwenye maeneo ambayo yanatu–favor.

Mheshimiwa Spika, na hii kwa upande wa TANESCO haijaanza leo, ukienda kwenye Symbion, ukienda kwenye IPTL ukienda kwenye SONGAS tunashida gani? Leo tena tunaona fahari ya kuwa na mradi wa Bomba la Gesi hatutaki haya yajirudie na ndiyo maana tunasema. Lazima tujifunze pale tunapojikwaa; hilo moja.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere alipaswa kujenga miradi mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii ya zaidi ya bilioni 200. Sasa mpaka sasa hivi mradi ambao unaenda kumalizika hatujui hizi huduma za kijamii zimefika wapi? Na ni haki yetu na aliji-commit, wakati haya yanaendelea yeye nasikia kwa mujibu wa mkataba, kwamba tulikubaliana anaweza tu akaongeza bei ya gharama ya mradi, na tuna taarifa ya kwamba anampango wa kufungua kesi; hili Mheshimiwa Waziri lazima utuambie limekaaje?

Mheshimiwa Spika, yeye hataki kutimiza masharti ya mkataba halafu huku yeye kwenye hicho kipengele ambacho kwa kweli mimi nakisema kibovu bado nasikia anataka kwenda kufungua kesi Mahakamani adai nyongeza wakati huku ameshindwa ku-meet vigezo vya mkataba. Tunajua kuna mitambo mingine inatakiwa ije mapema, inaingia tarehe nne mwezi August halafu bado ana-guts za kutaka kwenda kufungua kesi, hizi ni pesa za Watanzania.

Mheshimiwa Spika, na tunaamini kati ya mkandarasi anayelipwa vizuri on time ni huyo wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kaka yangu umepewa dhamana, tunaamini tusirudie kule tulikotoka, lazima tuwasimamie hawa ili waweze kututendea haki Taifa letu na waheshimu Taifa hili lina wenyewe lina Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hizi fedha zitalipwa na walipakodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuwa na Shirika la TANESCO ni fahari, tuna miradi mikubwa, Shirika hili lisipokuwa stable hawataweza ku-manage hii miradi ambayo tuna-invest. Tuna taarifa Shirika linadaiwa sana, Shirika linadai sana, speed ya kuhakikisha hili Shirika linakuwa stable iko wapi? Nitapenda kujua, kuna deni la muda mrefu la Serikali zaidi ya tirioni mbili, kuna deni la bilioni 720 la TPDC, lakini ukisoma taarifa mbalimbali Shirika hili la TANESCO lenyewe kuhimili madeni ya muda mfupi ni shida.

Mheshimiwa Spika, tunatambua jitihada za Serikali za ku-invest kwenye miradi mikubwa, miradi ya umeme inayohitaji uwekezaji wa kutosha lakini lazima tuwe na Shirika la TANESCO imara. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakiksha Shirika la TANESCO linakuwa imara, linaweza kujiendesha likatengeneza faida? ni aibu kukaa humu Bungeni kuimba TANESCO inatakiwa iwezeshwe, TANESCO inatakiwa iwezeshwe kimuundo, iwezeshwe kimtaji, zaidi ya miaka kumi bado tunaenda ku-invest halafu Shirika ni hohehahe? Yaani ni sawa unanunua furniture kwenye nyumba ya udongo, furniture kali lakini nyumba ina ufa.

Mheshimiwa Spika, lazima hivi vitu vinaenda sambamba tuna-invest kwenye miradi tunahakikisha Shirika letu linakuwa stable.

Waheshimiwa Wabunge yasije yakatukuta kama ya Afrika ya Kusini, leo wana mgao mkali kwa sababu gani? Shirika lao limeyumba, Shirika lao haliko stable. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, hii miradi tunayowekeza mikubwa ya gharama nafuu lazima Shirika letu litakaloenda kusimamia miradi hii liwe na uwezo wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, Kingine Mheshimiwa Waziri tunaomba utupe status ya umeme nchini ikoje? nilikuwa kwenye kamati Lindi, zaidi ya mara kumi umeme ulikatika. Umemskia Mbunge wa Kahama, umesikia taarifa iliyotolewa na Mbunge wa Mkoa wa Songwe, shida ipo lazima kama Taifa tuambiwe tatizo liko wapi maana kuna manung’uniko; ooo uchakavu wa mitambo, sijui nini;

Mheshimiwa Spika, sasa lazima kama Wabunge Wawakilishi wa Wananchi tupate maelezo sahihi status ya umeme nchini ikoje. Tunafurahi sasa hivi mkakati wako wa gesi lakini bado spidi ya uunganishaji wa gesi kwenye viwanda ni ndogo sana. Tunataka tujue kwenye viwanda peke yake zitatumika kiasi gani kujenga miundombinu ya gesi ili sasa viwango vyetu viwe na uhakika wa kupata umeme wa kutosha na waweze kuchangia uchumi kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.