Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, niendelee kukushukuru sana lakini pia mimi niendelee kukuombea sana kwa Mwenyezi Mungu jambo lako ambalo liko mbele yako uweze kufanikiwa na upate ushindi mkubwa kuiwakilisha Tanzania; na kama mwana mama uendelee kuandika historia kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,mimi niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wanachi wa Jimbo la Ushetu kwa kutujali kwenye suala la umeme. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani Ushetu ilikuwa na kata saba tu zilizokuwa zimeshafikiwa na umeme. Leo Mheshimiwa Rais yuko madarakani kata zote 20 zimeshafikiwa na mtandao wa umeme. Lakini pia kwenye vijiji wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani tulikuwa na vijiji ambavyo vimefikiwa na umeme vilikuwa vijiji 20 lakini leo tunavyoongea vijiji 71 kwenye Jimbo la Ushetu tayari vimefikiwa na umeme. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais lakini pia kipekee niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Januari Makamba, Ushetu sasa inaendelea kuneemeka, Ushetu sasa inaendelea kung’aa. Niendelee kukuomba; vijiji ambavyo vimebaki kwa wananchi wa Ushetu sasa ni vijiji 41 ambavyo havijafikiwa na umeme kabisa. Niendelee kukuomba uendelee kumbana mkandarasi. Mkandarasi wako anaenda taratibu sana.

Mheshimiwa Spika, jiografia ya eneo la Ushetu na Halmashauri ya Ushetu ni kubwa sana akaze buti. Ukiangalia tu majimbo yetu yote matatu na Halmashauri tatu ukijisemea Kahama Manispaa, Msalala pamoja na Ushetu akimbize. Hata kipindi fulani niliuliza swali hapo nyuma la nyongeza kwamba Mkandarasi anaenda kwa kusua sua msukumeni sasa akimbize. Tunaona mabadiliko sio kama ilivyokuwa mwanzo,na Imani kazi imefanyika akimbize. Vijiji vinahitaji umeme, shule zinahitaji umeme, hospitali zinahitaji umeme na zahanati zetu kwenye vijiji vyetu ambazo amezijenga Mheshimiwa Rais zinahitaji umeme. Akimbize akamilishe hivyo vijiji 41viweze kufikiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini nimeona jana amesema kila jimbo angalau kupata vitongoji 15 kwa ajili ya kuwapatia umeme. Ndugu yangu Januari nikuombe Mheshimiwa Waziri, Ushetu ina vitongoji 561, sasa unaposema tu vitongoji 15 unaacha kipi na unachukua kipi? Tumia hekima yako tumia busara yako. Najua wewe ni kijana unahitaji kesho kubwa pambana ili wananchi wangu wa Ushetu na vitongoji angalau viongezeke kwa sababu ya wingi.

Mheshimiwa Spika, unajua tunatofautiana vitongoji unakuta kuna Halmashauri nyingine ina vitongoji 200 nyingine 300; lakini angalia vitongoji 561 na kitongoji kimoja ukubwa wake unaweza ukadhani ni vijiji viwili kwa hiyo niombe hili Mheshimiwa Waziri ulichukue utalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri aiangalie Kahama kwa macho mawili. Mwaka jana tulilia sana, tulisema hapa na Mheshimiwa Idd pamoja na Profesa Kishimba. Kahama ilivyo inahitaji mkoa wa ki-TANESCO. Kwa nini Kahama usiipe mkoa wa ki-TANESCO kwa upande wa Umeme. Ukingalia wenzio TRA tayari wana Mkoa wa ki-TRA kwa sababu ya makusanyo yaliyopo pale Kahama. Ukiangalia NSSF wana Mkoa wa ki-NSSF kwa sababu ya makusanyo yaliyopo pale Kahama. Ukiangalia hata kwenye upande wa kilimo wenzetu wa tumbaku wana mkoa wa ki-tumbaku Kahama kwa sababu ya kazi na ukubwa wa eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hali ya umeme ya Kahama ni mbaya. Kahama ambayo ina viwanda zaidi ya 422 umeme unakatika kwa wiki, umeme unamaliza wiki haupatikani Kahama. Kahama ambayo inawafanyabiashara, eneo lillotengwa na Manispaa ya Kahama; kuna eneo maarufu linaitwa Dodoma lina vijana waliojiajiri zaidi ya 1,700 umeme vijana wanashinda wamekaa umekatika Kahama. Hii Kahama ambayo ina benki zaidi ya 12 umeme unakatika katika. Kahama ambayo ina hoteli nyingi, ina wageni wengi, ina mzunguko mkubwa, ina kusanya kwa mwezi zaidi ya bilioni nne na milioni mia tano umeme ni wa kusua sua. Kahama ambayo kwa miezi mitatu imeweza kukusanya zaidi ya bilioni 13; Kahama imekusanya bilioni 13 kwa miezi mitatu lakini umeme bado ni wa kusuasua. Yaani Kahama biashara ya generator ni kubwa kuliko biashara ya umeme unavyopatikana.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri aiangalie Kahama kwa jicho, aiangalie Kahama na ukubwa wake. Wananchi wa Kahama wanalalamika hakuna umeme, wafanyabiashara wa Kahama wanalalamika hakuna umeme…

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Cherehani, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Stella Fiyao.

TAARIFA

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa Mheshimiwa Taarifa kwamba, tatizo lililoko Kahama ndio tatizo lililoko Songwe ambalo ndilo lango Kuu la SADC. Umeme unakatika kila mara wananchi tunakosa majibu.

SPIKA: Mheshimiwa Cherehani, unaipokea taarifa hiyo?

EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Mbunge kwa sababu inaongezea nguvu kwenye miji mikubwa inayokusanya fedha nyingi kwenye mapato makubwa, Serikali ipeleke umeme igeuze na ibadilishe maeneo yale ambayo yana makusanyo makubwa ya fedha yapewe nguvu na yapewe mikoa.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, maeneo ambayo anapata nguvu, anapata fedha nyingi aelekeze nguvu; Serikali ya Mheshimiwa Rais inahitaji fedha; na jana Mheshimiwa Waziri ametuonesha; mimi sijafika kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, mimi jana nimeliona pale Dodoma, nimeliona, ukigeuka huku unaona Mtumbwi, ukigeuka huku unaona unasogelewa na Samaki. Sasa kwa nini ashindwe kufanya miji inayokua kwa kasi aibadilishie kukatikakatika kwa umeme iwe historia?

Mheshimiwa Spika, mimi nalia na Kahama, eneo la Kahama ukiliwekea mkoa Msalala ambayo ina madini, ina vijana ambao wanahangaika, ina wachimbaji wakubwa itaneemeka na hawatasumbuka na umeme. Kahama ukiipa mkoa, Ushetu wakulima wetu watawekeza viwanda. Ndiyo maana hata juzi wawekezaji wetu wanunuzi wakubwa wa tumbaku wameshindwa kuwekeza kwa sababu hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, mimi niendelee kukuomba, na niendelee kukupongeza sana, kazi unayoifanya ni kubwa sana, lakini hebu angalia kwa macho mawili miji inayokuwa kwa kasi ipe mkoa. RCC Mkoa wa Shinyanga imeshakaa ikamaliza na ikatoa mapendekezo, leo ni zaidi ya miaka mitatu mmekaa tu. Fanyeni ziara muone jiografia ya maeneo. maeneo mengine Mheshimiwa Waziri wamefanya kazi vizuri sana, wanadhibiti mapato. Lakini wanashindwaje kwenda kujiridhisha maeneo ambayo yanakusanya? Kama kwa mwezi mmoja tu, mfano mwezi wa pili Kahama imekusanya bilioni 8,323,140,550.36 kwenye makusanyo ya umeme wilaya hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimpongeze Tumaini Chonya ambaye ni meneja wa Wilaya, yule bwana halali, anafanya kazi. Akipigiwa simu Msalala anakimbia, Ushetu anakimbia, na sisi tukiwa kwenye mkutano wa hadhara wananchi wakilalamika tu tunamuunganisha hapo tunaweka loud speaker, analalamika, anasema anachopata ni sawa na wilaya nyingine kama zilivyo. Sasa hauwezi kuilinganisha Wilaya ya Kahama na wilaya nyingine halafu ukailinganisha matumizi na kuipelekea hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha suala la Kahama liwe na majibu ya kipekee. Tunahitaji Kahama ipate mkoa. Na kama RCC imekwishapitisha ninyi wizara mnashindwa nini? Niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri; kuna kata zangu hazina umeme. Kata ya Igwamanoni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Emmanuel, kengele ya pili imeshagonga, malizia sentensi.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, Kata yangu ya Igunda, Kata ya Igwamanoni, Kata ya Chona ni maeneo ambayo vijiji vyake vingi havijapata umeme. Mheshimiwa Waziri, naomba aangalie Mkandarasi, amsukume kwenye kata zangu hizi ili ziweze kupelekewa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja.