Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia sekta hii muhimu sana ya uchukuzi, barabara, reli na kadhalika. Kwanza niwape hongera sana timu ya Profesa na mwenzake kwa kazi mnayoifanya.
Mheshimiwa Spika, nataka nijielekeze katika mambo matatu. Suala la kwanza ni suala la kisera. Tumeshakubaliana na kwa mujibu wa Sera za Chama cha Mapinduzi kwamba tutajenga barabara za lami kuunganisha mkoa na mkoa, ndivyo tulivyokubaliana. Nilikuwa najaribu kuangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hiyo sera hamuizingatii. Mnaanza kuhamisha rasilimali na resources kuhangaika na barabara za Kata kwenda Kata na Wilaya kwenda Wilaya. Kwa nini tusianze kujenga barabara za kuunganisha mikoa kwa mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Mkoa wa Kigoma, nashukuru nimeona kuna juhudi inafanyika kwa barabara yetu ya Tabora – Kigoma kwamba kuna vipande vipande bado vinafanyiwa kazi na nimeona kuna mweleko mzuri. Hopefully flow ya fedha itakwenda vizuri ili barabara ile ikamilike; lakini bado sisi hatujaunganishwa na Tabora, hatujaunganishwa na Katavi, haijaunganishwa na Kagera, haijaunganishwa na Mwanza, haijaunganishwa na Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha anieleze, kwa nini wanatapanya resources wakati tumeshakubaliana kwamba mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano iunganishwe kwanza kabla ya maeneo mengine? Hilo ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nizungumzie suala la uwiano. Jamani hii nchi ni yetu wote. Hakuna wa Tanzania bora kuliko Watanzania wengine, Watanzania wote ni sawasawa. Ukiangalia mtandao wa barabara za TANROADS na unaweza ukaenda tu ukapata picha ukurasa 279, ukiangalia zile barabara za changarawe kwa mfano, inakupa picha ya moja kwa moja kwamba kuna mikoa ambayo ina mtandao mkubwa kuliko mikoa mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, ni mpya katika awamu hii na bahati nzuri Jimbo lake ni Ikulu, hana Jimbo la uchaguzi, naomba waanze kwenda na utaratibu kuwe na uwiano, ikibidi wa-employ concept ya slow match na quick match. Wale waliotangulia sana, wasubiri wenzao. Haiwezekani unakuwa na mkoa una mtandao wa kilometa 300 wengine wana mtandao wa kilomita 600 wengine 900 wengine 800; that is very unfair. Twende kwa utaratibu mzuri (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, sisi Mkoa wa Kigoma tumeomba barabara kupandishwa hadhi kutoka barabara za Wilaya, Halmashauri, kuwa barabara za Mkoa kwa maana ya TANROADS. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alizingatie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kule Kasulu kuna barabara muhimu sana, inatuunganisha kati ya Kasulu, Kabanga, Msambala, inakwenda Mwanga mpaka Wilaya mpya ya Buhigwe, kwenda border yetu na Burundi. Barabara hiyo tunaomba, Mheshimiwa Waziri kwa kibali chake tumeshapitisha kwenye RCC, inangoja timu yake ile na Kamati yake ili barabara hiyo waweze kuipandisha hadhi. Tutaomba sana! Siyo hiyo tu, ziko barabara tatu, nne za Mkoa wa Kigoma ambazo tumeomba zipandishwe hadhi na hiyo tafsiri yake itatuongezea mtandao wa barabara angalau za changarawe. Hilo lilikuwa la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, ni barababara yetu ya kihistoria ya muda mrefu nimeona imetengewa fedha, shilingi bilioni 70 Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 32 ameeleza vizuri kwamba kipande cha Kidahwe – Kasulu kuna mkandarasi yuko pale na kimetengewa fedha; na kipande cha Kabingo - Nyakanazi, nacho kimetengewa fedha, lakini hapo katikati, kuna kilometa zaidi ya 200 za Kabingo – Kibondo – Kasulu - Manyovu Border na Burundi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ameandika kwenye kitabu chake kwamba kilometa 258, amezungumza kwenye kitabu chake kwamba hiyo inafadhiliwa na fedha za African Development Bank. Sasa tungependa kujua, ameishia hapo tu na akaweka na nukta kubwa, maana yake nini? Hizo barabara zinaanza lini? Kwenye vitabu vyake vyote viwili haonyeshi bajeti au hizo fedha za ADB zitatoka lini na ni kiasi gani kwa barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, hiyo maana yake nini? Maana yake ni kwamba, hiyo barabara kubwa ya kihistoria ya Kigoma - Kidahwe - Nyakanazi itakuwa haijakamilika, kama hicho kipande hakijakamilika, sisi tunaotoka Kidahwe, Kasulu itakuwa imekamilika. Nilimshukuru Mheshimiwa Waziri, nilimwona akiwa Kijiji cha Kasangezi anahangaika na barabara ile. Yule Mkandarasi juzi nimemuuliza mwenyewe akaniambia amepewa fedha. Hiyo ni assuarance ya watu wa Kigoma, kwamba hiyo barabara ya kihistoria sasa inajengwa. Tunaomba flow ya fedha iendelee, barabara hiyo ni muhimu sana, kwa sababu ni barabara ya kihistoria na ni barabara ya siku nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo naomba pia nizungumzie barabara ambayo ameitaja kwenye kitabu chake, hii barabara ya Sumbawanga - Mpanda - Nyakanazi, shilingi bilioni 77. Sasa nataka kujua Mheshimiwa Waziri, hii barabara maana yake kutoka Sumbawanga ukaja mpaka Katavi - Mpanda, ukaja mpaka Uvinza - Border, ukaja mpaka Kanyani - Kasulu kwenda Nyakanazi, hiyo ni barabara ndefu sana. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuelewe, hizi fedha ambazo wamezitenga, shilingi bilioni 77 zinajenga sekta ipi? Maana yake ukitoka Mpanda mpaka Uvinza, unazungumza habari ya kilometa 600 ni mbali sana! Sasa napenda kujua, hizo shilingi bilioni 77.5 zinajenga sekta ipi katika barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, nakumbuka kulikuwa na mkakati wa kujenga barabara itoke Katavi kwa maana ya Mpanda kuja Uvinza border, ije mpaka Kanyani - Kasulu - Nyakanazi inakuwa ina-link ile barabara. Sasa tungependa kujua hizi fedha huyo mkandarasi atakuwa anaanzia wapi, anaanzia Kanyani kwenda Uvinza au anaanzia Uvinza kwenda Mpanda, kwa maana ya Mkoa wa Katavi? Mheshimiwa Waziri ningependa kuelewa kwa sababu hiyo ni barabara ndefu sana na inapewa jina refu sana, kilometa zaidi ya 600, ni barabara ndefu na ningeomba kupata maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine dogo tu, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 75 amezungumza ujenzi wa block train kwenda Kigoma na Mwanza kwa kuhudumia wafanyabiashara wa Kigoma – Mwanza – Tabora – DRC - Burundi - Uganda na kadhalika. Amezungumza habari ya vichwa vya treni, kuundwa. Yeye unajua Kiswahili; yeye ni mtu wa Zanzibar, kuundwa maana yake nini? Wanaunda vichwa vya treni au wananunua vichwa vya treni? Sijui kama ni lugha maana wanazungumza kuunda vichwa vya treni, sasa kuunda maana yake nini? Kama wanaviunda, basi napenda clarity tu, labda ni lugha, lakini ninachojua kama wanachozungumza ni kununua vichwa vya treni naweza nikaelewa. Naomba hilo jambo aliweke makini.
Mheshimiwa Spika, ukurasa 72 nafikiri nayo ni error, anazungumza habari ya ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma, lakini anazungumza habari ya matawi yake ya Tabora – Mwanza. Mheshimiwa Waziri hiyo jiografia imekosewa; hakuna ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma ukawa na matawi ya Tabora kwenda Mwanza. Halafu anazungumza habari ya tawi la kwenda Minjingu na matawi ya kwenda Engaruka, angalieni jiografia hiyo msije mkajichanganya katika utekelezaji wa miradii hii ya reli, hiyo iko ukurasa wa 72.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, juhudi ni nzuri, Mheshimiwa Waziri endelea, tuna matumaini makubwa na naunga mkono hoja. Ahsante sana.