Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa dhati kabisa kwa namna ambavyo umeongoza na kusimamia vyema majadiliano haya ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2023/2024.

Pia nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge wote kwa usikivu, kwa uchangiaji wenu makini uliofanywa kwa kuzungumzwa moja kwa moja katika Bunge hili Tukufu pamoja na kwa njia ya maandishi. Naomba niseme kwamba, tunatambua na kuthamini dhamira na nia njema ambayo mnayo ambayo kimsingi inalenga kuboresha mikakati na mbinu za kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya NUU chini ya Mheshimiwa Mwenyekiti Vita Rashid Kawawa pamoja na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Vincent Mbogo na Wajumbe wote kwa jinsi ambavyo walivyoweza kuwasilisha Taarifa ya Kamati iliyosheheni na yenye maelekezo na ushauri mzuri. Nao niwaahidi kwamba ushauri huo tutauchukua na kuufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja za Wabunge ni nyingi na waliochangia ni wengi. Naomba nizijibu hoja hizi, zile ambazo nitaweza kuzijibu sasa hivi kuzifafanua bila kuorodhesha majina tuweze kuzijibu kwa pamoja kutokana na wingi na wengi wake. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo ameweza kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kabla yangu mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru tena kwa mara nyingine tena Waheshimiwa Wabunge kwanza kwa kuthamini jitihada kubwa sana za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Hii inadhihirisha kwamba Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais na Serikali yake tunazungumza lugha moja, tunacheza wimbo mmoja, tunatembea pamoja. Tunashukuru sana kwa kuunga mkono jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Rais amekuwa akizifanya toka ameingia madarakani za kuhakikisha kwamba anashughulikia changamoto za Askari na vyombo vya usalama katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Kiongozi Mkuu wa nchi yeye amekuwa ndio mpambanaji namba moja wa kuhakikisha kwamba vyombo hivi vya usalama vinatekeleza majukumu yake katika mazingira mazuri na kwa weledi. Nadhani sisi tunapaswa kufuata nyayo zake. Waheshimiwa Wabunge mmelionesha hilo katika michango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa jinsi ambavyo wametupongeza na wamependezwa na vyombo hivi vinavyofanya kazi zake vizuri, lakini hawajasita kuonesha maeneo ambayo wanadhani ni vyema yakafanyiwa kazi ili tuweze kuviimarisha vyombo vyetu vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii sasa kuweza kutoa ufafanuzi wa mambo hayo, lakini kabla sijafanya hivyo, kuna hoja moja naomba nianze nayo ambayo nimeona siyo sawa nianze ufafanuzi bila kuizungumzia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waheshimiwa Wabunge wamezungumza kwa uchungu na hasira kutokana na jinsi ambavyo wanaona kuna haja ya kufanya jitihada zaidi za kuweza kuimarisha vyombo na Askari wetu. Katika mazingira yoyote yale, hakuna namna ambavyo tunaweza kuhalalisha rushwa, hakuna namna ambavyo tunaweza kuhalalisha uzembe, hakuna namna ambavyo tunaweza kuhalalisha uonevu, hakuna namna ambavyo tunaweza kuhalalisha kupora haki ya watu kwa kisingizio chochote. Iwe kwa maslahi madogo, iwe kwa kucheleweshwa kwa haki hizo na maslahi hayo. Kwa hiyo, hili naona nilizungumze likae kwenye rekodi na nina hakika Waheshimiwa Wabunge nao pia wanaamini kama ambavyo ninaamini mimi kwamba tuna haja ya kuhakikisha kwamba tunawatendea haki wananchi wa nchi hii kwa kuepuka vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili na uadilifu kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Hilo niliona nilizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, ndiyo maana kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tutaendelea kuhakikisha tunachukua hatua za kisheria kwa yeyote yule, iwe Askari, iwe mtumishi raia katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye atakiuka maadili mema ya utendaji kazi wake lakini hatutaacha kuwapongeza wale wote ambao wanafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi. Leo kuna Askari mmoja mwenye cheo kidogo tu alifanya kitendo cha kishujaa na cha kupigiwa mfano. Tulimleta hapa Waheshimiwa Wabunge mmemwona na tumemtambulisha kwenu na baadaye jioni tukitoka hapa tuna tafrija, yeye pamoja askari wengine waliofanya vizuri kwenye kata, tukiona kwamba ni utaratibu mzuri wa kuweza kutoa motisha kwa Askari wengine; naamini waliofanya vizuri ni wengi, lakini tutaendelea kufanya hivi kila mwaka ili kuweza kutoa motisha kwa Askari wengine ili watambue kwamba tunathamini juhudi za Askari waadilifu, tunathamini juhudi za askari ambao wanafanya kazi zao kwa kujituma na kwa ubunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwa uchungu kabisa ni nyingi. Wamezungumzia kwa mfano masuala ya vitendea kazi. Wako waliozungumzia masuala ya usafiri, magari, boti, vitendea kazi vingine mbalimbali kama pikipiki, hata helicopter naongezea hiyo, lakini wako Waheshimiwa Wabunge walizungumzia juu ya changamoto ya vituo vya Polisi katika maeneo yao, nyumba za makazi ya Askari. Kuna masuala ya stahiki na madeni ya muda mrefu ya Askari Polisi, masuala ya mafunzo, masuala ya vitendea kazi vya kisasa, mifumo, TEHAMA, vifaa, zana, sare na kadhalika. Mambo mengi yamezungumzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kutokana na dhamira njema ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tokea ameingia madarakani, amefanya kazi kubwa sana ya kuboresha vitendea kazi katika vyombo vyetu vya usalama. Ndiyo maana katika bajeti hii ambayo tunamaliza nayo, ambayo imetekelezwa kwa zaidi ya 80% na ni historia katika Wizara hii kutekeleza bajeti za Mambo ya Ndani kwa zaidi ya 80%, kuna ziada ya zaidi ya Shilingi bilioni 300. Amekuta bajeti ya shilingi bilioni 900 kufikia Shilingi trilioni 1.1 na mwaka huu tumeongezeka kidogo. Kwa hiyo, dhamira ya Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu inadhihirishwa kutokana na namba zilizopo katika bajeti yetu. Namba hazisemi uongo. Kwa hiyo, hili Waheshimiwa Wabunge nataka niwahakikishie kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais tokea ameingia madarakani ni dhamira ya dhati na dhamira ya vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika suala la ulipaji wa madeni na stahiki mbalimbali, katika mwaka huu wa fedha, shilingi bilioni 82.52 zimetolewa kwa ajili ya kazi hiyo. Ni fedha nyingi, najua fedha hizi zinaweza zisiwe zimekidhi kuweza kutatua matatizo au changamoto ya miaka mingi sana ya madeni ya Askari na kadhalika, lakini angalau kuna kazi na hatua imepigwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunachukua maoni yenu na kufanya jitihada zinazowezekana kupunguza madeni haya ya askari kwa kadiri ya hali ya kiuchumi itakavyoruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo linadhihirisha juu ya dhamira ya dhati ya Serikali katika kwenda sambamba na dhamira ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayo ni kwamba katika kipindi cha mwaka huu tunaomaliza nao, tumeweza kutekeleza miradi 23. Nimekuwepo katika Wizara hii kwa muda mrefu. Ni kwa miaka mingi sana katika kumbukumbu yangu ambapo miradi 23 imekamilika. Miradi hii imekamilika; nazungumza kwa taarifa zilizopatikana mpaka mwezi huu. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuna miradi kadhaa ambayo inafikiwa katika hatua ya mwisho, kabla ya mwisho wa mwaka huu kumalizika itakuwa imekamilika na hivyo kuongeza hata idadi ya miradi 23 na kuwa miradi mingi zaidi. Miradi hiyo nimeitaja kwa kina katika hotuba yangu, sina haja ya kuirejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia stahiki za Askari, unazungumzia mambo mengi. Kuna masuala kwa mfano ya upandishwaji vyeo. Kumekuwepo malalamiko ya muda mrefu ya Askari kutokupandishwa cheo lakini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, watumishi zaidi ya 1,696 wamepandishwa vyeo, lakini mwaka huu ambao tunazungumza nao hali kadhalika tunatarajia kupandisha vyeo askari wengi zaidi. Askari hao ambao wamepandishwa vyeo ni miongoni mwao ni wale Askari ambao tumewapeleka katika kata, wenye vyeo hivi vya ukaguzi na ambao wanaendelea kufanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika ajira, tumeweza kutoa ajira kwa watumishi 6,608 katika kipindi hiki, katika mwaka ambao unamalizika; na mwaka huu ambao tunaomba bajeti muipitishe, tunatarajia kutoa ajira kwa askari 3,117. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunapunguza mzigo wa Askari wetu ambao wanatekeleza majukumu makubwa wakiwa na idadi ndogo. Askari wengi wanastaafu lakini Askari kwa muda mrefu walikuwa hawajaweza kuajiriwa hivyo pungufu hilo sasa linaenda kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo niliona nataka nilizungumzie ni kwenye eneo la mafunzo. Suala la mafunzo ni suala la msingi sana kwa vyombo vyetu vya usalama na katika hili nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake mahususi aliyotoa ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyapongeza ya kuhakikisha kwamba Askari ambao wanakwenda mafunzo hawakatwi posho yao. Hili limefanyika katika mwaka wa fedha huu ambao unamalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusisitiza tena, katika mwaka huu wa fedha maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba hakuna Askari hata mmoja anakatwa posho yake ya aina yoyote kwa ajili ya mafunzo. Ndiyo maana katika bajeti yetu ya mwaka huu tumetenga zaidi ya Shilingi bilioni 29 kwa shughuli hiyo. Kwa hiyo, hakuna sababu yeyote kwa askari yeyote kukatwa posho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hakuna sababu yeyote kwa askari yeyote kukatwa posho. Lakini nipongeze wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wanaimarisha mafunzo vyuo vyetu vya kuwafundishia askari, na niipongeze vilevile Serikali kupitia Mheshimiwa Rais wetu kwa kutenga bajeti nzuri ya kuimarisha miundombinu ya vyuo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetoa mfano wa Chuo cha Zimamoto na Uokoaji mwaka huu wa fedha tunavyozungumza tuna takribani bilioni 1.1 lakini kazi nzuri inaendelea kukamilika katika Chuo cha Raphael Kubaga cha Uhamiaji kule Tanga vilevile, na upande wa Jeshi la Polisi halikadhalika. Kwa hiyo katika eneo la mafunzo kuna jitihada kubwa ambazo zinaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika eneo la uimarishaji wa miundombinu ya usafiri, nimezungumza katika bajeti hii kuna fedha ambayo tumetenga takriban milioni. Kwanza nizungumze, katika bajeti iliyopita mtakumbuka kwamba nilieleza bilioni 15 ilitengwa na kufedha ambayo tayari imeishatolewa kununua magari hayo, na mwaka huu wa fedha tunatarajia kununua magari mengine 24 zaidi kwa shilingi bilioni 7.6. Lakini magari ambayo yako njiani kufika ni magari 101 366 ni pikipiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu umuhimu wa kuimarisha usafiri katika ngazi za chini za Kata. Lakini si katika suala la usafiri tu, mwaka huu tumekuja na mpango kabambe. Mheshimiwa Naibu Waziri alizungumza hapa, kwa mwaka jana mtakumbuka tulizindua mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba tuna kabiliana na changamoto ya usafiri, makazi ya askari kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama ambapo lengo lilikuwa ni kuja na nyumba na vituo vya polisi 51,760. Tumefanya mpango huo kwa mafanikio makubwa kwa mwaka huu mmoja. Hata hivyo tumeona kuna haja ya kuupitia tena mpango huo na kujikita zaidi katika ngazi ya chini. Baada ya kuona mafanikio makubwa ya Askari Kata katika kata zetu ambapo wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana, wamekuwa wakifanyakazi ya kutoa elimu na kuelimisha, wamekuwa karibu na wananchi na kuweza kuyakabili matukio kwa haraka yanapotokezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge kwahiyo nawapongezeni sana kwa jinsi ambavyo mmeona juu ya umuhimu wa kuwawezesha askari wetu kata hawa, ambapo kata hizi zipo katika majimbo yenu yote. Ndiyo maana tukapewa maelekezo na Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba si tu tunapeleka magari katika wilaya lakini tupeleke pikipiki katika kata zote ambako kuna askari kata. Na gari na pikipiki hizi ambazo ziko njiani zitakapofika tutaanza kuzitawanya katika kata na Wilaya hizo. Si tu pikipiki na magari, hata mafuta yatakwenda sasa moja kwa moja kwenye kata na Wilaya, hayatabakia Mkoani. Na ukiangalia bajeti hii imeonesha kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya mafuta kimeongezeka kwa kiwango kikubwa sana (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi, kwa eneo hili la kata tumeweza kufanya maboresho makubwa sana ya Mfuko wetu wa Tozo na Tozo. Kama mnvyotambua Mfuko wa Tuzo na Tuzo umekuwa ukifanya kazi kubwa sana ya kuchangia jitihada za kuimarisha vituo vya polisi na nyumba za askari ili kutoa msukumo zaidi na nyongeza ya kazi kubwa ya fedha ya bajeti ya Serikali inayotengwa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu nichukue nafasi hii kumpongeza IGP kwa kuweza kutoa msaada mkubwa sana katika kufikisha azma hii ya kuleta maboresho makubwa katika matumizi ya mfuko wetu wa Tozo kwa kushirikiana na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi. Tunakwenda kufanya maboresho makubwa ambayo yatapelekea sasa kuhakikisha tunapata fedha za kujenga vituo vya polisi vya kata zote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wabunge mbalimbali ambao walizungumza hapa, nimeandika majina yao, wale ambao walikuwa wamezungumzia kuhusu habari ya vituo vya polisi kata. Walisema wameishaanza hizo kazi za kujenga vituo vya polisi kata katika kata zao lakini vimeshia njiani kabla ya hata mpango huu. Niwapongeze, najua na wengine hamjapata nafasi ya kusema, lakini mmefanya kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge hawa nitakao wataja wamefanya. Mheshimiwa Chaya, Mheshimiwa Iddi, Mheshimiwa Vicent, Mheshimiwa Jah People haa hili jina nadhani halina shida Mheshimiwa, Mheshimiwa Nicholas, Mheshimiwa Munira, niliwasikia mkizungumzia habari ya vituo vya kata. Nataka niwahakikishie, kwamba tutakapoanza kutekeleza mpango huu najua yatahitajika mabadiliko ya sheria, lakini tutaharakisha. Tunadhani katika kipindi kisichozidi miezi sita tuanze utaratibu huu. Tutaanza na kata zenu na tutaanza na kata zile za Waheshimiwa Wabunge ambao watakuwa wameenda kwakushirikiana na wananchi wao kuanza jitihada za kutafuta maeneo na kuanza kazi za awali. Hilo nataka niwahakikishie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nadhani tutakapoweza kufanikiwa kuweka miundombinu imara katika kila kata katika nchi hii hali ya usalama itaendelea kuimarika katika maeneo yenu na hatimaye katika Taifa kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya Magereza ameyazungumza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa hiyo mengine ambayo niliona niyachangie ni kwamba, kuna hoja ambazo zimezungumzwa kuhusiana na suala la uhamiaji haramu, lakini wengine wakalinasibisha jambo hili na msongamano wa mahabusu. Wamesema kwamba wahamiaji haramu hawa wako wengi, hususani hawa ambao wanatoka nchi ya Ethiopia, wamekuwa wakijaza magereza na hivyo kusababisha msongamano. Sitaki nikatae, changamoto ya Wahamiaji haramu hususani wa Ethiopia kwa kwakweli ipo, ingawa imepungua kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nieleze takwimu mpya ambazo tunazo sasa hivi tunavyozungumzwa. Wahamiaji haramu waliyopo sasa hivi katika magereza ni 1,600. Tumefanikiwa kuwaondosha wahamiaji haramu 3,100 katika siku za hivi karibu. Tumefanya hivyo kwa jitihada na ushirikiano na msaada kwanza wa Shirika, nichukue fursa hii kulishukuru sana Shirika Uhamiaji la Kimataifa (IOM) kwa kuweza kutusaidia kuwasafirisha wahamiaji haramu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nipongeze jitihada ambazo zimeendelea kufanyika kwa ushirikiano wa Idara yetu ya Uhamiaji pamoja na Ubalozi wa Ethiopia hapa nchini kwa kuhamasisha ndugu wa hao wahamiaji haramu katika nchi yao kuweza kutoa fedha za kuwaondoa. Jambo hili limetusaidia sana kama Serikali kupunguza gharama za kuwasafirisha watu hawa ambazo hazina sababu yeyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mna uchungu sana, kwamba watu hawa wakikaa magerezani wanakula bure. Lakini watu hawa vilevile tukitoa hela za wananchi ambazo zingeenda kujenga shule, zingeenda kujenga hospitali, tukawasafirisha watu ambao waliyokuja hapa kwa hiyari na yenyewe vilevile ni kutumia rasilimali vibaya. Ndiyo maana tukaamua kutuma jitihada hizi; jitihada za kuhakikisha kwamba tunazungumza na Shirika la IOM watusaidie kuwaondosha na wamefanya hivyo na kuzungumza na ndugu zao ambao wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la muhimu zaidi ni nini ilhali unaweza ukawaondosha leo wakaja wengine kesho? Jambo la muhimu ni kuhakikisha kwamba tunatafuta ufumbuzi wa kudumu la tatizo la kudumu la Wahamiaji haramu ususani ambao wanatoka Ethiopia ambao ni wengi. Katika kufanya hivyo, katika Hotuba yangu nimesoma imeeleza kwamba, tumefanya marekebisho ya kanuni na kuiondoa nchi ya Ethiopia kutoka katika listi ya nchi ambazo zinatumia viza rejea. Sasa hivi raia wa Ethiopia anaweza akaja na passport yake akaingia kwenye mpaka, akatoka bila ya bughudha yeyote. Jambo hili limesaidia sana kutupatia ufumbuzi wa kudumu. Najua ni mapema mno kuweza kusema tunajivunia kwa kiasi gani. Lakini tunavyozungumza sasa hivi takwimu zinaonyesha kwamba tunapata wahamiaji haramu kutoka Ethiopia kwa mwezi hawazidi 40, wakati ilikuwa kwa mwezi wahamiaji haramu zaidi ya 300 wanaingia nchini. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba utaratibu huu umeweza kusaidia na pengine utaweza kusaidia zaidi kuliondosha kabisa kama siyo kulimaliza tatizo la wahamiaji haramu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la msongamano wa Mahabusu lina mambo mengi; na ndiyo maana nataka nichukue fursa hii tena, mimi leo sisemi mnyonge maana Mheshimiwa Rais hawezi kuwa mnyonge; nitasema tumpe haki yake Amiri Jeshi Mkuu kwa jinsi ambavyo anaguswa na changamoto za vyombo vyetu lakini na wananchi wa nchi hii ambao wanahitaji huduma kwa vyombo hivi. Kitendo chake kwa kuunda Tume ya Haki Jinai ambayo hivi karibuni itawasilisha ripoti tunategemea Tume hii itakuja kutupa mapendezo mengi ikiwemo hayo mliyoyazungumza, maboresho ya haki na stahiki za askari, masuala ya mafunzo ambayo nimeelezea na mengineno, lakini hata utaratibu wa jinsi ambavyo mifumo na miundo ya Taasisi zetu za Haki Jinai. Kwa mfano katika jambo moja ambalo lilikuwa lina changia ongezeko la Magerezani kuwa na msongamano, kama ambavyo mnajua, kuna idadi kubwa ambayo inakaribia idadi ya wafungwa ya mahabusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unaweza ukakabiliana na tatizo la kuondosha wafungwa ambalo tunakwenda nalo vizuri. Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa ya kutoa msamaha kwa wafungwa nimetoa Takwimu, wakati ambapo nawasilisha taarifa yangu. Amefanya kupitia Katiba katika Ibara ya 45(1)(c) cha Katiba kimempa Mamlaka Mheshimiwa Rais ya kutoa msamaha wa wafungwa ambao katika kipindi kilichopia wafungwa 12,515 wameweza kutolewa, kwa mwaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hizi taarifa zisiingie kwenye Hansard lakini nataka tu mtambue tu kwamba kuna Idadi kubwa ya wafungwa katika kipindi cha kuanzia miaka hiyo ambayo tangu utaratibu huu umeanza wa wafungwa kuachia. Pia kana kwamba hii haitoshi kupitia Sheria ya Bodi ya Parole Sura Na. 400 inazungumzia wafungwa 1,046 ambao wameachiwa lakini kwa huduma ya jamii inazungumzia wafungwa 5,339 ambao wametumikia vifungo vya nje pamoja na kufaidika na huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utaona, takwimu hizi zinaonyesha jinsi ambavyo sheria hizi; Sheria ya Bodi ya Parole, Sheria ya Huduma ya Jamii pamoja na Sheria ya Kifungo cha Nje, pamoja na Mamlaka ya Mheshimiwa Rais Kikatiba inavyosaidia kutupungumzia msongamano wa wafungwa magerezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii haigusi maabusu. Kwa hiyo lazima kuna haja ya kuangalia namna ya kufanya ili kuhakikisha kwamba tunawaondoa na kuwapunguza mahabusu katika Magereza; na ndiyo maana nimezungumza hapa suala la Tume ya Haki Jinai ambayo naamini kabisa itakuja na mapendekezo ambayo pengine yatatusababishia tuweze, sitaki nilisemee, lakini najua, kwa sababu hata sisi kuna mambo ambayo tumeyaona na tumeyatolea maoni na tutaendelea kuyatolea maoni ili yaweze kuingizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni namna ambavyo utaratibu wa jinsi mifumo na miundo yetu itakavyoharakisha masuala ya upelelezi, kuepusha mianya ya kutokuwa na upelezi usiokuwa na mapungufu. Wakati mwingine unaweza kusema sasa hivi tumejitahidi sana, Jeshi la Polisi limejitahidi. Kwa mfano ukienda Magereza leo hakuna hata mahabusu mmoja ambao upelelezi wake haujakamilika, lakini bado kuna msongamano. Kuna mahabusu ambao pengine bado wako ndani kwa sababu tu ya sheria zetu zilivyo, kuna mahabusu ambao wako ndani pengine wamekosa dhamana kwa kushindwa kutimiza vigezo vya dhamana, kuna mahabusu pengine wapo ndani leo kwa sababu wanamakosa ambayo kwa mujibu wa sheria hawapaswi wapate dhamana. Kuna mahabusu wapo ndani kwa utashi wao tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo haya yanahitaji ufumbuzi wa pamoja, na ndiyo maana nichukue fursa hii kupongeza sana ile Kamati ya Haki Jinai, ambayo iko chini ya DPP ambayo imekuwa ikipita kwenye Magereza mbalimbali na kupitia kesi za mahabusu moja baada ya nyingine na kusaidia wale ambao pengine walikuwa wanahitaji msaada wa kisheria, msaada wa mawazo, na wengine ambao kwa sababu ya uelewa mdogo wameshindwa kuzifahamu haki zao; na mahabusu wengi wamekuwa wakiachiliwa kwa utarabu huo. Kwa hiyo niliona nizungumzie hizo ni kama sehemu ya jitihada ambazo tunazichukua za kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuimarisaha Magereza yetu. Wakati nchi hii inaundwa idadi ya watu walikuwa ni wachache sana, sijui kama bado walikuwa wanafika milioni 12. Sasa unazungumzia watu milioni sitini na kitu. Kwa hiyo lazima maeneo haya haya ambayo tumerithi kutoka kwa wakoloni tukubaliane ukweli kwamba hayawezi kutosha kulingana na idadi ya watu walio hapa. Na ndiyo maana katika bajeti yetu mwaka huu tumeongeza. Mwaka jana tulitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Magereza sita na fedha yote hiyo imetoka na kazi inaanza, mwaka huu tumeongeza Magereza 12. Tunaamini kabisa tutakajenga Magereza mengi zaidi na kuongeza mabweni si tu itasaidia kupunguza msongamano lakini itasaidia dhamira tuliyokuwa nayo katika kuhakikisha kwamba kwenye hii hoja ya maboresho tuanayoendelea nayo katika Wizara ya kuangalia utaratibu wa urekebu ili tuhakikishe kwamba wafungwa wanaotoka magerezani hawarudii makosa. Na moja katika jambo ambalo linasaidia kuwa na urekebu uliyo bora ni mazingira mazuri ya wafungwa hawa wanapokaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukiwa na magereza ya kutosha yenye nafasi utaweza kutenganisha wafungwa kulingana na uzito wa makosa yao, usugu wa uhalifu waliyokuwanao umri na kadhali. Kwa hiyo hoja hii ya ujenzi wa Magereza ni hoja ya msingi na hoja endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limezungumzwa vilevile, naomba niliunganishe hapa hapa; hoja ya kuimarisha vitendea kazi. Hakuna namna ambavyo tunaweza tukaimarisha usalama wa nchi katika karne hii bila kuwa na vyombo vya kisasa; ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Zimamoto na Jeshi la Uhamiaji. Na ndiyo maana niungane sana na Waheshimiwa Wabunge ambao mmezungumza kwa uchungu sana kuhusu eneo la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Mmezungumza kwamba Jeshi hili limesahaulika, Jeshi hili linaonewa, wako ambao waliofikia wakasema kwamba kuna haja ya turudishe kwenye Halmashauri, wamesahau changamoto zilizotokea wakati huo ambazo zilikuwa zinasababisha ikaletwa kwenye Jeshi. Lakini najua mmesema hivyo kwa sababu ya uchungu mlio kuwanao, ambapo mko sahihi kabisa, wala mimi siwezi kuwa Waziri ambaye nasema uongo hapa mbele ya Bunge, nikasema kwamba eti Jeshi la Zimamoto letu liko vizuri, lina vifaa vya kutosha; nitakuwa ni Mbunge mwongo, Waziri mwongo na siwezi tena kuingia kwenye rekodi hiyo. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nakubaliana na ninyi juu ya kilio chenu hicho. Lakini Waheshimiwa Wabunge nataka niwaambie kitu kimoja; kwamba mkipitia bajeti yangu niliyoisoma mtagundua kuna maeneo mawili ambayo nimeyaeleza na maeneo hayo nadhani yanakwenda sasa kutupatia suluhisho la kudumu kwenye matatizo ambayo ninyi yanawaumiza kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa jambo la kwanza, kwamba tunatarajia kupata magari ya Zimamoto 12 hivi karibuni kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Austria. Nadhani hii nyimbo ya mkopo huu wa Austria ni ya miaka mingi sana, na ninyi Waheshimiwa Wabunge mtakuwa ni mashahidi. Hakuna siku nilivyokuwa Naibu Waziri katika miaka yangu mitano sikuwa nimeimba mwimbo huu; lakini leo santuri hii inafikia mwisho, hayo magari yapo njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi ni kwamba, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Serikali inakamilisha mkopo mwingine wa masharti nafuu. Nichukue fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais, kwanza kwa kuimarisha demokrasia ya uchumi. Ndiyo maana leo tunazungummzia mikopo hii mizuri kabisa ambayo haitakuwa mzigo kwa Watanzania, lakini inakwenda kutoa na kuongeza thamani ya maisha yao na uhai wao, maana uhai uwezi kununua kwa hela na pia inakwenda kuokoa mali zao. Kama mlivyosema Waheshimiwa Wabunge mlio wengi; kwamba leo hii nchi imefunguka, wawekezaji wanaongezeka. Mmeona takwimu nilivyoisoma kwenye Uhamiaji, jinsi idadi ya watu wanaoingia, jinsi vibali vya class A vilivyozidi kiwango, inadhihirisha kwamba sasa kuna wimbi kubwa sana la uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na uwekezaji mkubwa halafu tuwe na Jeshi la Zimamoto kama tulilo nalo sasa hivi. Lakini kupitia mkopo huu ambao nina imani kabisa upo katika hatua za mwisho tutakuwa na Jeshi la Zimamoto la kisasa. Kama tulipata shida sana kuzima moto uliokuwa unawaka Mlima Kilimanjaro sasa hivi tutakuja kuleta helkopta kwenye Zimamoto mkopo huu ukikamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeliona hilo na Insha Allah kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu jambo hili litakwenda vizuri na litakwenda kuondosha changamoto ambazo Wabunge wamezieleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi, najua nimeletewa hapa note kwamba nimalizie, lakini nataka nizungumzie uraia pacha. Hili nililizungumza juzi, majibu yangu yanabakia vile vile kwamba waheshimiwa ni Watanzania wenzetu ambao wako nje, tunawathamini sana, michango yao ni muhimu, hapa ni nyumbani kwao japokuwa wameamua kwenda kuchukua passport nyingine kwa sababu zozote waliokuwa nazo, tunawahitaji sana waweze kuja kutoa michango kwa uchumi wa nchi hii. Ndio maana Serikali kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, ilifanya majadiliano nao na wakaona kwamba kwa sasa na kulingana na uhitaji uliopo, wanaweza wakatimiza azma yao hiyo kwa kuweza kupewa hadhi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana katika hotuba yangu hii nimeeleza juu ya mpango wa marekebisho ya sheria nyingi ikiwemo Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 ambayo inalenga kwenda kutibu tatizo na kero moja kubwa ya watu hawa, ili kuwa wanaingia hapa kama wageni, lakini sasa kama jambo hili litapita, basi wataingia hapa bila visa, wataingia hapa kama anavyoingia Mtanzania mwingine. Kwa hiyo hiyo ndio kauli yangu, nasisitiza katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona amenitoa katika mstari nilikuwa nataka nieleze kitu kimoja cha muhimu sana, kwamba hii dhana ya maboresho na kuwa na vyombo imara, nikisema hapa nizungumze mipango na mikakati ambayo aidha imeshafanyika au inaendelea kufanyika nahitaji muda mwingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo nataka niyagusie ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyazungumza kabla sijamaliza. Wamezungumzia hoja ya kuwa na umuhimu wa kuwa na mifumo ya kisasa ya kubaini kushughulikia, pamoja na kuzuia uhalifu ikiwemo kuweka mifumo ya miji salama. Nimezungumza katika hotuba kwamba tunaenda sasa kuweka kamera kwenye miji yetu mitatu kwa kuanzia, lakini nimezungumza najua kuna Waheshimiwa Wabunge wana changamoto hata Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti kwenye Kamati alikuwa analizungumza sana hili na tatizo pamoja na Mheshimiwa Aida kule Nkasi kwenye Maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda juzi kwa Mheshimiwa Chege, tatizo hili la vifaa, boti kwenye Maziwa yetu kwenye Bahari, kwenye bajeti hii kuna boti 10 tunaenda kununua. Kwa hiyo mambo ni mengi, lakini kwa sababu muda ni mchache naomba nimalizie labda jambo moja tu ambalo nisingeomba niliache kutokana na jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza kwa hisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la NIDA. Ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa kwenye upatikanaji wa vitambulisho na changamoto hiyo ilitokana na sababu nyingi. Kwanza, ilikuwa, hatukuweza kununua kadi ghafi za kutosha kwa wakati, lakini sababu ya pili ilichangiwa na kutokea mambo ya UVIKO, tuliweka fedha kwa ajili ya kuomba hizi kadi na mlolongo wa foleni ya mahitaji ulikuwa mkubwa, ikawa tumechelewa kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wanaonisikiliza hapa, kwamba fedha zote za kadi na ziada zimeshalipwa, yaani sasa hivi hatuna deni la kadi hata moja. Kwanza tulitoa bilioni 28 ambazo kadi zake ziko njiani na nyingine zimeshaanza kuingia nimeambiwa mpaka mwezi huu kuna kadi zimeingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakwenda kukata mzizi wa fitina. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati amezungumza vizuri, tunakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kulieleza vizuri Mheshimiwa Vita Kawawa. Shilingi bilioni 42.5 na hii ndio fedha ambayo tulitenga kwenye bajeti ya mwaka jana kwa ajili ya ununuzi wa kadi. Maana yake ni kwamba tumetumia fedha ya ziada vile vile kupata kadi nyingi zaidi. Hivyo itakavyofika mwezi Desemba mwaka huu, tunategemea kadi zote zilizokuwa zimeshalipiwa zitakuwa zimefika na hivyo kuanzia wakati huo hatutarajii hata Mtanzania mmoja kuwa hana kitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nisisitize kitu kwamba kwa hivi tunavyozungumza kwa wale Watanzania wenzetu ambao hawana ID hizi za NIDA. Najua wanazo zile namba za utambulisho waendelee kutumia namba hizo, namba hizo zinatambulika, namba hizo ni halali. Hakuna sababu yoyote ya kumkosesha haki yake Mtanzania yeyote popote pale alipo eti kwa sababu hana kipande kile cha NIDA. Kwa sababu namba hii inatumika na inaendelea kutumika kwa taasisi za Serikali, kuendelea kutoa taaluma na kuzitumia ili wananchi waendelee kupata huduma zao mpaka pale tutakapotarajia ambapo ni Desemba mwaka huu, kuwa tutaweza kufikisha kadi kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana tukasema sasa tunataka tupeleke mwelekeo wetu kwenye ule utaratibu wa kuwa na kadi moja. Najua mchakato wake siyo mwepesi, lakini tutaanza nao. Tusingeweza kusema hivyo kama hata watu kadi zenyewe hawana. Inaleta matumaini sasa kadi watakuwa nazo, hivyo hata tukija na mpango kwa baadaye kwamba sasa tupunguze gharama za Serikali, za kuwa na rundo la makadi kwenye kipochi na kumsumbua mwananchi kupata huduma, tuwe na utaratibu huo wa kuwa na kadi moja kwa ajili ya matumizi ya huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa fursa hii. Naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.