Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru wewe kwa kuendesha vizuri sana kipindi hiki cha hoja yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya na kutuwezesha kukutana hapa leo ili kujadili hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kama Msaidizi wake kwenye nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninamshukuru Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu, Waziri wangu Mheshimiwa Injinia Masauni kwa miongozo bora kabisa wanayonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Pia ninawashukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Vyombo na Wasaidizi wao kwa msaada ambao wamekuwa wakinipa katika utekelezaji wa majukumu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru familia yangu kwa msaada na watoto kuvumilia wakati mwingine nakuwa nao mbali. Zaidi niwape shukrani za pekee wananchi wa Butiama kwa kuendelea kunivumilia ninapokuwa natekeleza majukumu haya, wakati mwingine nakuwa nao mbali na hasa siku ya leo wanapomhifadhi katika nyumba yake ya milele aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo niliyepokea nafasi yake, Mheshimiwa Nimrod Mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa, lakini mtoa hoja atakuja ayaguse mengi. Mimi mdogo wake niguse yale machache ambayo yametajwa na Waheshimiwa Wabunge. Moja ni kuhusu miundombinu ya majengo ya ofisi, makazi ya Askari wa vyeo tofauti kwa vyombo vyote vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wangu imesemwa bayana kabisa namna ambavyo dhamira ya Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kushughulikia changamoto zinazokabili vyombo vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwa uchache tu nikiwarejesha Waheshimiwa Wabunge katika ukurasa wa 50 wa Kitabu cha Bajeti mpaka 65, imeelezwa kwa kirefu namna ambavyo Jeshi la Polisi kwenye miradi yake ya maendeleo imegusia ukarabati wa ofisi, makazi pamoja na kujenga vituo vipya vya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba, mtakumbuka mwaka uliopita, Mheshimiwa Waziri wangu alizindua mkakati wa ujenzi wa nyumba 1,760 kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Sekta ya Usalama wa Raia na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa majengo, imetajwa hapa na Waheshimiwa tofauti tofauti kuhusu Magereza na Polisi. Nilitaka niwatajie maeneo machache ambayo tumefanya kazi kubwa. Kwenye upande wa Magereza imeelezwa vizuri sana kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wangu kwamba yako maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza yalikuwa hayajamilikiwa rasmi kwa maana ya kuwa na hati lakini katika bajeti hii, zaidi ya shilingi bilioni 1.778 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia, kulipia upimaji wa viwanja na kukabidhi hati kwa ajili ya vyombo vyetu hivi hasa Magereza. Ukurasa wa 19 mpaka 21, aya ya 31 mpaka 34 kwenye bajeti yetu imeeleza bayana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya maeneo hayo kwa mfano, nitaje Chuo cha Kiwira kitanufaika, Chalinze, Namtumbo, Nanyumbu, Hanang’, Muleba, Liwale, Kalambo, Mlele, Ikungi, Bahi, Wazo Hill, Kimbiji, Namvuti, Chamwino na Kaliua. Kote huko maeneo yameshalipiwa, kinachofuata ni ujenzi na hati tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi, zaidi ya shilingi milioni 210 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia ili hatimaye jeshi hili limiliki maeneo hayo ili fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi ziweze kujengwa na kuepusha migogoro iliyopo kati ya wananchi na vyombo vyetu. Uhamiaji kadhalika wametengewa zaidi ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya kulipa fidia. Polisi wametengewa zaidi ya shilingi milioni 554.8 kwa ajili ya kulipia fidia maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezwa juu ya uimarishaji wa Magereza, Magereza chakavu na mengine yanahitaji kujengwa upya. Niwakumbushe kwamba imeelezwa katika hotuba ya Waziri wangu kwamba mwaka huu unaokuja, Magereza 12 yafuatayo yatajengwa na kukamilishwa yale yanayoendelea kujengwa; Gereza la Msalato, Kaliua, Kakonko, Karatu, Kilosa, Kyabakari, Gairo, Kingurungundwa, Mpimbe na Sengerema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ujenzi maeneo ya Zimamoto na Uokozi imeelezwa kwa ufasaha na Mheshimiwa Kichiki Neema Lugangira. Tumesema katika eneo hilo zaidi ya shilingi bilioni 2.3 zimepokelewa ili kuendeleza ujenzi eneo la Songwe, eneo la Simiyu, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Njombe na ujenzi unaendelea kutekelezwa na kwa mwaka ujao zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa majengo ya mikoa hiyo saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitendea kazi kwenye upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, zaidi ya shilingi bilioni tatu zimetengwa kwa ajili hiyo na kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri mmesikia majadiliano yanayoendelea na moja ya nchi wahisani ili kupata zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa madhumuni tu ya kuimarisha vitendea kazi kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hususan magari na vifaa vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza Mheshimiwa Mbunge kutoka Manyoni juu ya nini tufanye? Nimhakikishie Mheshimiwa, katika Wilaya yake ya Manyoni tumetenga gari. Atapewa gari la lita 1,000 kwa ajili ya ku-support shughuli za Zimamoto na Uokozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Uhamiaji, mwaka 2022/2023 wamepata zaidi ya shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya kununua magari 30 kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao. Mwaka ujao tumetenga shilingi bilioni 3.8 kununua magari 23 kusaidia utendaji hasa misako na doria ambayo imelalamikiwa kwa kiwango kikubwa hapa na baadhi ya Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usalama barabarani. Imetolewa hoja hapa na Mheshimiwa Shabiby kuhusu umuhimu wa kuzingatia ratiba za magari yale badala ya kutegemea tu speed governor na vitu kama hivyo. Pamoja na kutumia hizo teknolojia, ushauri wake tunauchukua na tunaanza kuufanyia kazi. Baraza la Taifa la Usalama Barabarani eneo hilo ni eneo linalosisitizwa sana ili ratiba inayotolewa na LATRA izingatiwe na mabasi yote na basi litakalo-overspeed kwa maana ni mwendo hatarishi hata kwa usalama wa abiria na wenye mali, wadhibitiwe ili waende kama ratiba zao zinavyoonyeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa kwamba baadhi ya Askari wetu wa Usalama Barabarani wanapungukiwa maadili na kufanya vitendo vinavyokiuka nidhamu na maadili ipasavyo. Niweze kusema IGP kupitia Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, kwa kweli amekuwa madhubuti sana kusimamia nidhamu ya Askari wa Usalama Barabarani. Mtakumbuka IGP alivunja ile Kamati inayohusika na utoaji wa leseni za udereva na kuiunda upya baada ya kuonekana wanakiuka maadili. Nikwambieni, IGP amewaondoa baadhi ya Askari wasio na maadili kwenye kikosi hiki na kupeleka wengine ili kuhakikisha kwamba nidhamu inakuwa nyenzo namba moja katika utendaji wa jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mmoja amezungumzia juu ya uhakiki wa leseni. Mheshimiwa nimekuona. Leseni zile zinahakikiwa kwa sababu uvunjwaji wa kile Kikosi cha Leseni cha Jeshi la Polisi ni baada ya kubaini kwamba zipo leseni zilizokuwa zinatolewa kinyume cha taratibu na wengine walizipata bila hata ya kufanya mafunzo.

Mheshimiwa Mewnyekiti, nikwambie, katika leseni zaidi ya 29,000 zilizohakikiwa katika muda huu mfupi, tumebaini uwepo wa leseni zaidi ya 2,000 ambazo hata wenye nazo walikiri kwamba hawakuzipata kwa utaratibu unaokubalika. Sasa ukishakuwa na watu wanaendesha vyombo vya moto, wanabeba abiria, hawakuhudhuria mafunzo yoyote na ukabaini, lazima uchukue hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo tuvumiliane. Hatuna dhamira ya kumnyang’anya mtu leseni aliyeipata kwa njia za halali na ni mtu ambaye anajua hiyo kazi ya uendeshaji wa magari. Kwa hiyo, nikuondoeni shaka kwamba, wale ambao watakuwa na leseni zao, hawatanyang’anywa kama wamepitia mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)