Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi kubwa wanayofanya ya kulinda raia na mali zao. Hata hivyo nina mambo kadhaa ya msingi sana ya kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu kuwajumuisha polisi kutumia kikokotoo kama watumishi wengine wa Serikali tofauti na askari wengine wa majeshi mengine. Yapo malalamiko makubwa miongoni mwa askari kutoridhika na utaratibu huo. Askari hawa wa Wizara hii wanaona ni vyema utaratibu unaotumika kutoa mafao au kikokotoo kinachotumika kwa askari wengine mfano toka Wizara ya Ulinzi utumike na kwao pia kwani mazingira yao ya ufanyaji kazi yanalingana na askari wengine, lakini pia hawana muda wa kufanya mambo yao wanapokuwa katika ajira ukilinganisha na watumishi wengine wa umma, hivyo hawana muda wa kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya kustaafu kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia viinua mgongo vyao au pensheni zao kwa walio wengi sio kubwa, hivyo, kutumia kikokotoo cha asilimia 33 hakiwasaidii kujiweka vizuri kwa maisha ya kustaafu, na pia umri wao wa kustaafu ni tofauti na wastaafu wengine wa kada nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni vyema kwa ufanisi bora wa majukumu yao wakiwa na afya nzuri ya akili wawapo kazini na baada ya kustaafu, tunaiomba Serikali ilipe uzito jambo hili la kutumia utaratibu wa kuwalipa mafao kama askari wengi wa Wizara ya Ulinzi na sio kikokotoo hiki cha asilimia 33 kama kinavyotumika kwa watumishi wengine wa umma ili kuweka heshima sawa kwa askari wetu wote na kuimarisha usalama wa raia na mali zao.

Pili, Serikali iweke mpango mahususi kwa kutumia nguvu kazi yake wakiwemo wafungwa na mahabusu kuhakikisha inaboresha makazi ya askari. Mfano makazi ya askari polisi ndani ya Jimbo la Iringa hayaridhishi. Hata makazi ya askari polisi wa Dodoma Kituo Kikuu cha Polisi Iringa Road hayaridhishi, ni aibu kwetu kama viongozi kuridhika kuwa na makazi duni namna hii ya askari wetu ambao ndiyo wanalinda mali na wananchi wetu wote yakiwemo mahoteli makubwa, maghorofa na roho zetu Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, wenza au wanawake wa askari polisi waangaliwe kwa namna ya kipekee katika kuwawezesha kiuchumi ili kusaidia ustawi wa familia za askari wetu. Kwa kuwa mara nyingi kupata ushirikiano wa kukopeshwa kwenye vikundi mitaani inakuwa ni changamoto kutokana na kazi za wenza wao. Uwepo mpango mahsusi wa kuzisaidia familia za askari kiuchumi kwa kuwawezesha wenza wao.