Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Rashid Abdalla Rashid

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Niungane na wenzangu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mafungu ndani ya bajeti za Wizara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Engineer Masauni pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa anazozifanya na hasa Engineer Masauni, nimwambie kwamba ana Naibu Waziri wa kazi sana, ameshatembelea katika maeneo yetu na kuona matatizo mbalimbali ikiwemo Kituo cha Polisi Kengeja. Kaenda kukishuhudia mwenyewe na kuona kwamba kituo hiki kina hali ngumu sana. La kushukuru ni kutuambia kwamba ndani ya mwaka huu wa bajeti zimetengwa kiasi cha shilingi milioni 247 ili kwenda kuanza ujenzi wa kituo kile ambacho kimejengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nije katika upande wa Polisi Jamii, Polisi Jamii katika jimbo langu wamefanya jitihada kubwa na jitihada hizi zilifanyika kwa sababu ya kuahidiwa na RPC wa wakati huo ndani ya miaka 10 iliyopita na tukaweza kama wananchi kujenga zizi pale na sasa limefikia hatua ya kuezekwa na tayari hili nimeshaliombea sana tangu akiwa Mheshimiwa Simbachawene ambaye aliniahidi kwamba tutatumia Mfuko wa Tuzo na Tozo kwenda kukuezekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Masauni pia ameshaniahidi kwamba ujenzi huu wa Polisi Jamii tutakwenda kumaliza kuezekea, lakini mpaka sasa hivi ninapozungumza hakuna kinachoendelea. Nimwombe sana Mheshimiwa Masauni akanimalizie jengo langu hili la Polisi Jamii katika huu Mfuko wake wa Tuzo na Tozo ili wananchi waweze kuona umuhimu wa nguvu zao walizozitumia pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kingine ni Kituo cha Polisi Mkoani, ni kweli kituo hiki sasa hivi kinaendelea kujengwa, lakini nadhani changamoto zake Mheshimiwa Waziri anazijua kwamba amepata fedha tangu mwezi Desemba, 2022 na ujenzi wake umekwenda kuanza juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha akatuambia alikumbwa na tatizo gani hata kituo hiki kutoka Desemba hadi ujenzi umeanza Mei na ujenzi wenyewe nimwambie Mheshimiwa Waziri unahitaji usimamizi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamejengwa lakini ukuta umekaa upande, jana ukuta wameubomoa, nadhani Kamishna wa Zanzibar na yeye yupo hapa, afuatilie aone ni kwa nini huyo Engineer anaendeleza ujenzi huo pasi na umadhubuti, pesa milioni 700, ni pesa za kutosha kwa ajili ya huo ujenzi, lakini inaweza kutokea kwamba fedha zisitoshe kwa hali hiyo ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Ofisi ya NIDA, Wilaya ya Mkoani, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba NIDA, Wilaya ya Mkoani hakuna Ofisi kuna kaofisi kadogo, kachumba, kastoo wameazimwa pale wilayani, shughuli zote zinafanyika humo humo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili ni afadhali atoke mwenyewe aje akague ile ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, kuna suala zima la Ofisi ya Uhamiaji ambayo inaendelea kujengwa katika Wilaya ya Mkoani. Ofisi hii mkataba wake wa ujenzi kati ya Wizara na mkandarasi unamalizika Agosti, 2023. Ujenzi bado uko katika hatua nzuri, lakini niombe mkandarasi wampatie fedha ili aweze kumaliza ile ofisi kwa wakati ili wananchi wa Wilaya ya Mkoani tuweze kupata huduma kutoka katika Jeshi letu la Uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo makubwa katika Jeshi letu la Polisi Mkoa wetu wa Kusini Pemba. Jeshi linafanya kazi vizuri, lakini pesa za Other Charge kwa maana ya OC hawapati fedha za kutosha. Tunajua kule tuna Viongozi Wakuu wa Serikali ambao wanaenda Pemba na huduma ambayo inatakiwa kutoka Jeshi la Polisi ni kuongoza misafara na mambo mengine, lakini inapotokea hizo shughuli kwa kweli ma-RPC wale tunawapa wakati mgumu sana wa kuona namna gani misafara ile wataiongoza kwa sababu fedha hawana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, hili suala la OC Mheshimiwa Waziri alifanyie jitihada za kutosha kwa hawa ma-RPC, wanapata shida kubwa kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni kwamba, tunaomba tupate usafiri kwa patrol za hawa askari wetu. Askari wanafanya kazi za kutosha, lakini wakati mwingine wanaenda kwa miguu au watumie usafiri wa hizi bodaboda za kawaida, haipendezi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani sana kuona askari wetu wa kule Pemba au Zanzibar kwa ujumla wanafanya kazi za doria kama ambavyo wanazifanya askari wenzao wa huku bara. Inapendeza na inatia moyo, lakini unamkuta askari anatembea kwa miguu kufuata mhalifu ni shida. Hilo naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, bodaboda milioni tatu, milioni tatu na nusu, Waziri atupatie angalau bodaboda 12 kule Pemba, kila mkoa upate bodaboda sita ziweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)