Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Viongozi wote Wakuu wa Majeshi walio chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza Wabunge mbalimbali ambao wameweza kueleza maeneo mbalimbali katika majeshi yetu na kazi wanazozifanya, lakini naomba tu niwaambie majeshi yetu haya yanafanya kazi nzuri sana, sisi tunaosimamia Kamati tunajua umuhimu, Jeshi la Polisi wanafanya kazi saa 24 kwa siku saba na ndio maana leo tuna amani katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linalinda usalama wa raia na mali zake, lakini tuna Jeshi la Magereza linahifadhi wale ambao wanakuwa wakorofi na wanawahifadhi vizuri na wanarekebishwa. Tuna Jeshi la Uhamiaji ambalo linakaa, lipo mipakani mwetu, linafanya kazi masaa 24 siku saba au wiki, kuangalia kila mtu anayeingia nchini na linaruhusu watu wanaokuja waliokuwa wema, waliokuwa wabaya wanaondoka, ndio maana nchi yetu leo hii inaendelea kuwa na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna budi kuyapongeza majeshi yetu haya. Tuna Jeshi la Fire basi ikitokea moto, linakuja kuzima, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge tutambue majeshi yetu haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tulibahatika kutembelea na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani tulitembelea nchi moja sitaweza kuitaja, nchi hiyo hakuna amani. Tumefika nchi ile pale tumewekwa sehemu moja na tunatakiwa twende sehemu nyingine, umbali wa kutoka hapa mpaka Morogoro lakini kwa gari ni siku nne, umbali wa kutoka hapa mpaka Morogoro, siku nne na njiani humo kuna vikundi vitatu, kila kikundi kinafanya kazi yake ya uhalifu, kwa sababu hakuna amani. Kwa hiyo tulishindwa kwenda kwa chini na tukashindwa kwenda kwa kuruka kwa sababu hakuna amani. Kwa hiyo sisi hatuna budi kuyapongeza majeshi yetu na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri inazozifanya za kulinda amani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kwa kukubali na kuridhia maombi ya Wizara chini ya Mheshimiwa Engineer Masauni, kuridhia kutoa shilingi bilioni 42.5 kwa NIDA, Taasisi yetu ya Vitambulisho vya Taifa kwa ajili ya kuchapisha vitambulisho milioni 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii NIDA imeshapokea fedha hizo na imesha-order vitambulisho, kwa hiyo tunachosubiri ni ujio wa vitambulisho ghafi na kuanza kuzalishwa milioni 13. Naamini kabisa maneno yote ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Taasisi ya NIDA ikikamilisha, kelele zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mategemeo yetu kwa Taasisi yetu hii ya NIDA ikisimamiwa vizuri chini ya Wizara na ikafanikisha zoezi hili la kuzalisha vitambulisho milioni 13, tutavuka hapa tulipo kwa sababu vitambulisho ni jambo muhimu sana kwa Taifa letu, lakini pia na kwa dunia yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haja ya kuboresha sheria ili kuona taasisi zetu muhimu zinazohusika na utambuzi kwa watu wetu na kwa ajili ya shughuli za kimsingi za kijamii na kiuchumi zisiachwe nyuma kutokana na vitambulisho hivi vya NIDA, kwanza ni vitambulisho janja kwa maana vina smart card, vina chip ndani yake ambayo inahifadhi taarifa zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunafanya kazi ya duplications katika taasisi mbalimbali ya utambuzi wa watu, lakini ushauri wangu ni kwamba lazima tuwe na uniform au tunakuwa na universal identity data bank kwa ajili ya vitambulisho vyetu vyote ili kupata taarifa zilizo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano leo tumesikia hapa kwa Mheshimiwa mkongwe Maida kwamba kuna mtu aliumwa, akapelekwa Zanzibar, alipofika Zanzibar akafariki na alipofariki baada ya mwaka akaletewa barua ya kuambiwa amestaafu na anatakiwa arudishe vifaa vyote vya Jeshi la Polisi. Hii yote ni kwa sababu ya kukosa mfumo unaounganika pamoja ulio sahihi. Kwa hiyo tuuboreshe mfumo huu wa NIDA, tukipewa vitambulisho vyote watu wote wakapata tujitahidi sana taasisi zetu zote ziunganishe mfumo uwe mmoja kwenye mfumo huu wa NIDA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)