Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nikushukuru kwa kunipatia nafasi jioni hii ili kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu katika nchi yetu. Pili, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliompongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoiongoza nchi yetu kwa umakini na kwa ufasaha zaidi. Mimi pamoja na wapigakura wangu wa Jimbo la Tumbatu, tunamwombea dua Mwenyezi Mungu amjalie afanye kazi zake kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu pamoja na Naibu wake kwa namna walivyotayarisha hotuba yao na baadaye kuiwasilisha kwa umakini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu leo naenda katika michango ifuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, viongozi wetu wa Wizara hii ni miongoni mwa viongozi wasikivu sana, wanasikiliza maoni ya Wabunge tunapokwenda na kutuelekeza. Kinachotakiwa katika hili ni sisi Wabunge kuwa wasitahimilivu tu lakini ukiwa unakwenda unaomba, unakwenda unaomba, unajibiwa vizuri, basi ustahimili tu unaloliomba utalipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2016 nimekuwa nikisimama hapa kuiomba Wizara hii kujengewa Kituo cha Polisi katika Jimbo langu la Tumbatu. Kwa muda wote wa miaka mitano nimekuwa nikionana na viongozi hawa, majibu yao yalikuwa ni mamoja, nayo ni kuniambia kwamba Mheshimiwa subiri itafika siku Insha Allah na wewe tutakujengea Kituo chako cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeweza kustahimili, na nimestahimili nikijua kwamba mahitaji ya nchi hii katika kujenga vituo hivi ni makubwa, siyo kwangu mie tu, lakini katika nchi nzima mahitaji ya kujenga vituo hivi ni makubwa sana. Sasa unapokwenda kuomba kitu kwa mwenzako lakini asikukatalie anakwambia subiri, basi ni vyema ukasubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima naishukuru Serikali hii kwa kupitia Wizara hii kwamba ombi langu hili limekubaliwa na Kituo cha Polisi katika Jimbo langu la Tumbatu ujenzi umeshaanza. Kwa hiyo nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali yangu inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna ombi langu hili lilivyokubaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba mambo mawili katika hili, masafa kutoka Mkokotoni mpaka Tumbatu, jiografia yake ni lazima u-cross bahari, sasa basi maaskari wetu pale watakuwa wanakwenda Tumbatu kwa kutumia vidau au viboti vya wananchi. Naiomba Serikali na ni vyema itafutie boti maalum kwa ajili ya maaskari wetu ambao wanakwenda kule Tumbatu, kuwe na boti maalum kwa ajili ya maaskari ambao wanakwenda katika Kituo chetu cha Tumbatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika kutatua hili ni vyema pamoja na kituo cha polisi ambacho kitajengwa kule pia tunaomba maaskari wetu kule wajengewe makazi ili waweze kufanya kazi kule kule. Sisi wananchi wa Tumbatu kwa kushirikiana na Ofisi ndogo ya utawala kule Tumbatu tumeshatenga eneo maalum kwa ajili ya kuwapa Serikali wajenge makazi hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili ambalo linafanana kabisa na hili ni kuhusu Kituo changu cha Mkokotoni. Mwaka 2018 nilisimama hapa kutoa masikitiko yangu makubwa kwa namna ya kituo kile kilivyokuwa, lakini nashukuru Serikali imechukua juhudi kituo kile sasa hivi kipo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kutoa mfano, niliwahi kusema ule ukweli ulivyo kwamba, kipindi kile maaskari wetu walikuwa wanafanya kazi, inaponesha mvua wana-shift, kutoka ofisini kwao wanafanya kazi katika chumba cha mahabusu lakini alhamdulillah hali ni nzuri, wanafanya kazi vizuri na jengo liko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililokuwepo pale ni moja ambalo ni kubwa, kuhusu makazi ya maaskari pale Mkokotoniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hija, malizia, muda wako umeisha.

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)