Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Nimpongeze sana amepambana sana na panya road na sasa hivi Tanzania yetu imetulia, majangili wamepungua. Kwa hiyo nimpongeze sana kaka yangu Masauni, endelea kufanya kazi sisi tunakuamini na Taifa linakuamini pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara yote kwa ujumla, hakika mnafanya kazi nzuri sana, nawapa pongezi sana. Lakini niwapongeze sana sana Wizara kwa kuanza ujenzi wa kituo changu cha Wilaya Mkoani. kituo hiki kilikuwa kimezungushwa mabati tangu mwaka jana lakini huu mwezi wa tano sijui kwa ajili ya bajeti ya leo tayari kimeanza msingi na tayari kimeanza kufanyiwa kazi. Niombe Serikali, itakapo pita bajeti hii kile kituo basi kiendelee pia na ujenzi wake usije ukasita. Iendelee na kile kituo pale kimalize kwa sababu kituo hiki ni kituo muhimu, ndicho kituo ambacho kimezungukwa na Bandari ya Mkoani pale, kwa hiyo ni kituo muhimu sana. Ujenzi wake naomba uendelee na uharakishwe zaidi kwa sababu ni kituo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na kituo hiki, niombe nyumba za Wilaya Mkoani, Waheshimiwa Wabunge karibu wote wamezungumzia hapa suala la nyumba. Suala la nyumba limekuwa ni tatizo kwa Tanzania nzima. Niombe basi Wizara iweze kuangalia upya suala la nyumba ya makazi ya askari hawa. Hasa ukiangalia mazingira ya Pemba. Mazingira ya Pemba si rafiki askari kukaa uraiani. Ukiangalia mwaka sasa hivi tulionao tunapitisha bajeti ya 2023/2024. Mwaka kesho tu kuna uchaguzi. Si mazingira rafiki kwa askari wetu kukaa katika nyumba za uraiani. Niombe sana Serikali iweze kuangalia upya suala la nyumba za mapolisi, naamini Serikali yangu ni Sikivu.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mheshimiwa Saashisha taarifa ya tatu leo inatosha hiyo. Mheshimiwa Mnura endelea na mchango wako.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala la nyumba hili Serikali yangu Sikivu itasikia na itafanyia kazi. Mheshimiwa Waziri tunakuamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la dawati la jinsia. Nipongeze sana. Serikali kwa kuamua kwa makusudi kuunda hili dawati la kijinsia la watoto ndani ya Jeshi la Polisi. Kwa kweli mmetusaidia wazazi na hili dawati linafanya kazi nzuri sana. Lakini niombe Serikali, dawati hili liwe na kamisheni, liweze kujitegemea lenyewe na liwe na bajeti ya kutosha. Hatuwezi dawati hili kulichanganya ndani ya askari jamii kwa sababu dawati hili linafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri akae aangalie dawati hili lina wasaidia watoto. Mimi binafsi nimeshaenda kulitembelea dawati hili, linatoa elimu, linawasaidia akina mama, linafanya kazi zake vizuri. Dawati hili linatakiwa liweze kujitegemea. Kama ilivyo kwa askari jamii ndivyo dawati hili linatakiwa lijitegemee lenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kumaliza suala la udhalilishaji kwa watoto basi ni lazima kuweza kuwapa kamisheni iweze kujitegemea wenyewe lakini pia dawati hili lipatiwe fedha ya kutosha ndipo litaweza kufanya vizuri. Kwa sababu sasa hivi tunapokwenda kuna mambo mengi ya udhalilishaji wa kijinsia kama tutalisaidia dawati hili, yale masuala mengi ya ukatili wa watoto naamini yatapungua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munira ahsante sana muda…

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba niunge mkono hoja.