Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naona watu wa Igunga walikuwa wana-test mitambo lakini imeshindikana. Mambo yanakwenda vizuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii nami niweze kuchangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya ya Ndani ya Nchi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kuunda Tume ya Haki Jinai nchini. Ukifuatilia kwa haraka haraka, ukifanya utafiti, hii Tume ya Haki Jinai, asilimia takribani 60 ni wanufaika wa taasisi na vyombo vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maana ya taasisi zote zilizopo chini ya Wizara, asilimia 30 ya wanufaika ni Wizara ya Katiba na Sheria na asilimia 10 ni taasisi nyingine. Tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona, tunaamini tume hii italeta mabadiliko makubwa sana kwenye vyombo vyetu vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Engineer Masauni, kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya kwenye hii Wizara pamoja na Naibu wake, kaka yangu, Mheshimiwa Jumanne Sagini. Hongereni, mmeendelea kuaminiwa, mnaendesha vizuri Wizara, mnatoa mwongozo mzuri, nasi kama Wabunge tupo nanyi, tunawaunga mkono na kuhakikisha yale yote ambayo mmepanga yanatimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Nampongeza Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Afande IGP; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji; Kamishna Jenerali wa Magereza; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na pia niwapongeze Maafisa wa Bunge, wale ambao wanahudumia Jeshi la Polisi na Magereza ambao wako hapa Bungeni, wanatupa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha mambo yetu yanakwenda vizuri. Nami kwenye bajeti nimeona Gereza langu la Igunga litakamilishwa, kwa kuwa mwaka 2022 nilitoa fedha pale kwa ajili ya cement kama Mbunge, na mwaka huu nashukuru Serikali mmetuunga mkono, mtalikamilisha gereza letu tuwe na gereza la kisasa kwa sababu Wilaya ya Igunga ni ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie maeneo matatu, manne, lakini kabla ya kuchangia, niseme naunga mkono hoja Taarifa ya Mheshimiwa Waziri na Taarifa ya Kamati ambayo pia mimi ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Jeshi la Polisi. Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea suala la makazi, sitalisema, mimi napenda kusemea Chuo cha Polisi pale Moshi, kuna miundombinu imechakaa, namwomba Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele katika kuhakikisha anaifanyia maboresho. Ni chuo cha kisasa, kimekuwa cha muda mrefu. Kuna mabweni pale tulijengewa na wahisani kwa kupitia Wachina pale, lakini pia na sisi sasa tuweke jitihda kuhakikisha tunaboresha bwalo letu pale la chakula na yale mabweni kwa ajili ya wanafunzi kwa maana ya maafisa wetu wanapokwenda kozi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, jambo lingine ambalo napenda kuchangia jioni hii ni sare la Polisi. Tumefika pale tukaona kwa sasa tunazalisha sare zetu wenyewe. Imewapa heshima sana kama Wizara, hongereni. Kwa hilo, ni hatua kubwa. Zamani tulikuwa tunakutana na Askari Polisi, unakuta uniform imechanika, lakini kwa sasa wanazalisha pale kwa ustadi mkubwa, kwa ufanisi. Afande IGP pamoja na wasaidzii wake walituonesha na sisi tumeridhika. Mabadiliko haya sasa yaende pia kwenye majeshi mengine yaliyoko chini ya Wizara hii ili tuweze kuendelea kuzalisha uniform zetu nchini. Uniform zinazalishwa vizuri, zinatoka mpaka na majina na vyeo vya Askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia jioni hii ni kuhusu vyombo vya usafiri na doria na patrol. Mheshimiwa Waziri, mama yetu Amiri Jeshi Mkuu, ametenga fedha kwa ajili ya kununua magari. Nasi Jimbo letu la Igunga tunaamini litakuwa miongoni mwa majimbo ambayo yatapewa kipaumbele katika kupata haya magari kwa ajili ya kuimarisha patrol. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru OCD wa Igunga, anatupa ushirikiano mkubwa sana. Mwaka 2022 mimi kama Mbunge niliwachangia matairi, mwaka huu nimeona Serikali inatupatia gari mpya. Basi tunasema Insha’Allah, mama anaupiga mwingi, vijana wanasema apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mwongozo wa ujenzi wa hivi vituo vya polisi vya kwenye kata (police posts); sisi pale tumeanza jitihada pale Jimboni kwetu Igunga, nilipewa fedha kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi pale sehemu moja inaitwa Mwanzugi eneo ambalo lina uchumi mkubwa sana na mzunguko wa fedha. Naomba na ninyi Serikali basi mtuingilie muongeze nguvu tuweze kukamilisha kile kituo cha Mwanzugi ili tuweze kupata na kuhakikisha raia na mali zao zinakuwa salama. Lakini pia Kata ya Igurubi ambayo ni makao makuu ya tarafa, kule kuna uchimbaji mkubwa wa madini, pia tuna kituo pale cha polisi cha nguvu za wananchi ambacho kimeshafikia hatua ya kupauliwa. Naomba mtuongezee fedha kama Serikali tuweze kukikamilisha mtuletee askari wetu pale waendelee kutusaidia kulinda wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukweli mnafanya kazi nzuri, tunawapongeza kwa hilo. Lakini pia kuna huu utaratibu wa polisi kata mmesema mnawapatia pikipiki. Ilikuwa ni hoja niliyotaka niijenge hapa, kwamba tuweze kuwasaidia usafiri ili angalau basi wawe huru ili wanapokuwa wanafanya shughuli zao kwenye hizi kata waweze kutembea sehemu moja kwenda nyingine. Mmejitahidi sana polisi kata wanatupa ushirikiano hata sisi tunapokuwa kwenye ziara zetu Waheshimiwa Wabunge tunapata ushirikiano mkubwa Mheshimiwa Waziri tunakushukuru kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi kwenye Jeshi la Polisi ningependa kuchangia pia kamera. Muweke sasa, kama mlivyosema, kwamba mtaweka kamera za usalama barabarani ili zinapotokea ajali au uhalifu mweze ku-track kirahisi. Hili namkumbuka hata Mheshimiwa Kenethy Nola alinisisitiza, akaniambia asubuhi kuwa yeye hatapata nafasi ya kuchangia lakini aliomba niweze kulichangia. Hongereni lakini tunawapa msisitizo miji yetu imekuwa kama Makao Makuu ya Dodoma sasa inahitaji kamera kwa ajili ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimaliza Jeshi la Polisi, naomba niende Jeshi la Uhamiaji. Niongelee suala la Chuo pale cha mafunzo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ngassa muda umeisha, naomba malizia.

MHE.NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa pamoja na yote niliyoongelea ningependa kuchangio la mwisho, upande wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa. Mheshimiwa Waziri naomba nishauri, muwapatie fedha za kutosha ili waweze kukamilisha waweze kununua card ghafi ili wananchi waweze kupatiwa vitambulisho vya Taifa. Lakini pia ukijaribu kufatilia suala la vitambulisho vya Taifa linasaidia utambuzi wa walipa kodi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru sana, naunga mkono hoja.