Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika Taifa letu, pili nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja ninachangia kuhusu changamoto katika Mkoa wangu wa Katavi. Katika Mkoa wangu wa Katavi Jeshi la Zimamoto tuna takribani zaidi ya miaka 12 katika Mkoa wetu wa Katavi hatuna gari la uhakika la zimamoto. Mkoa wetu unakua, Serikali imewekeza vitu vingi sana ikiwepo bandari, lakini Mkoa wetu wa Katavi pia ni Mkoa ambao unapokea wafanyabiashara wengi kutokana na biashara ya kilimo. Hivyo, niiombe sana Wizara hii kupitia Mheshimiwa Waziri katika Mkoa wetu wa Katavi gari letu tulilokuwa nalo lilipata ajali mwaka 2012 likaenda kufanyiwa matengenezo, lakini mpaka hii leo ninapoongea gari hilo halijaweza kurudi katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini katika Mkoa wetu wa Katavi gari ambalo wanasema tunalitegemea ni gari dogo na ambalo liko airport. Sasa unajiuliza ikitokea ajali ya moto na ndege wakati huo inatua, je, gari hilo litaweza kufanya kazi ya kuzima moto? Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, Mkoa wetu wa Katavi tuna uhitaji mkubwa sana wa gari hilo ukizingatia Mkoa wetu unakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalopenda kuchangia jioni hii ya leo nitachangia katika upande wa Jeshi la Magereza. Jeshi la Magereza linafanya kazi nzuri, lakini katika Mkoa wetu wa Katavi tumekuwa na msongamano mkubwa sana wa mahabusu na wafungwa. Mfano katika gereza letu pale Wilaya ya Mpanda Mjini ambapo ndiyo gereza linalochukua almost wafungwa wote katika Mkoa, gereza lina uwezo wa kupokea wafungwa 100, lakini ukiangalia kwa sasa kuna takribani wafungwa zaidi ya 400. Wafungwa hawa wamesongamana, hivyo tujiulize je, ikitokea mlipuko wa magonjwa nini kitatokea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niombe sana Wizara, katika Mkoa wetu wa Katavi tumeshaleta maombi yetu na tumeshatenga eneo ambalo liko Mpimbo katika Kata ya Useja, tuna eneo kubwa lenye ekari za kutosha kwa ajili ya kujenga magereza. Tunaomba sana Wizara muweze kutukumbuka. Katika Mkoa wetu wa Katavi almost tuna kama magereza moja tu ambayo ni ya maana pale mjini, tunaomba sana tuweze kujengewa magereza hiyo, ili kuweza kuepusha huu msongamano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalopenda kuchangia ni kuhusiana na Shirika la Magereza la Uzalishaji (SHIMA). Mheshimiwa Waziri, shirika hili hapo nyuma lilikuwa halifanyi kazi vizuri, tunalipongeza kwamba kuna improvement ambazo zimeongezeka kidogo, shirika hili tunataka lije na mkakati, mfano, ukiangalia katika Mkoa wetu wa Katavi katika Mkoa wetu wa Rukwa tuna mashamba ambayo ni makubwa sana, ambayo ni mashamba yanamilikiwa na Magereza, lakini mpaka hivi sasa shirika hili limeshindwa kutumia resource hizo kwa kulima chakula cha kutosha ili kuweza kuipunguzia Serikali adha ya kuhudumia wafungwa ambao wamekuwa na upungufu mkubwa sana wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara waweze kulisimamia Shirika hili la SHIMA liweze kufanya kilimo, ikiwezekana kilimo cha umwagiliaji ili waweze kuendana na nyakati. Wakitumia kilimo ipasavyo hawatakuwa na upungufu mkubwa wa chakula. Ni aibu kwa Taifa kama hili ambalo lina maeneo makubwa sana kushindwa kutumia ardhi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kulima chakula cha kutosha, matokeo yake kuipa Serikali mzigo wa kwenda kuwahudumia wafungwa kwa kusema kwamba, chakula hakitoshi magerezani. Wanayo nguvu kazi ya hawa wafungwa, waweze kuitumia, lakini waweze kutumia resource tulizopewa na Mwenyezi Mungu waweze kupata chakula cha kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tunaomba shirika hili lirudi nyuma ikiwezekana lifuge, pia liweze kupata mifugo ambayo itasaidia, kuna akinamama ambao wako Magereza, kinamama waliofungwa na watoto wadogo, wale watoto hawana hatia, shirika hili tukiweza kufuga mifugo wakaweza kupata maziwa hata wale watoto wadogo wataenda kupata maziwa. Tuombe sana Wizara waweze kulisukuma shirika hili liweze kufanya kazi vizuri kwani wale watoto waliopo kule magereza hawana hatia yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia jioni hii ya leo ni kuhusiana na makazi ya Askari Polisi pamoja na Askari Magereza. Ukiangalia makazi yao kwa kweli, yanasikitisha na unaweza ukalia machozi. Tuwape heshima Askari hawa kwani ndio wanaotulinda, kama wanatulinda ni kwa nini tusiboreshe mazingira yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweze kuwapatia vifaa vya kufanyia kazi, lakini upande wa magari, hawana magari, ikiwezekana tuweze kuwabadilishia uniform zao mara kwa mara ili waweze kuwa nadhifu na waweze kuipenda kazi yao. Niiombe sana Wizara muweze kuangalia mfano nyumba tu za maaskari ukiziangalia kwa kweli unaweza ukalia machozi. Hawa watu ni muhimu katika Taifa letu, wanatulinda, wanasababisha tunakuwa na amani ni kwa nini tusiweze kuwatetea watu hawa waweze kupata mazingira mazuri katika kufanya kazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningependa kuzungumzia suala la Polisi Jamii. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo Polisi Jamii inafanya kazi katika Kata zetu. Sote ni mashahidi tulivyokuwa likizo iliyopita tuliona Polisi Jamii ikifanya kazi kila Kata wakituhusisha sisi akinamama wa UWT, ninaipongeza sana Serikali. Ili Polisi Jamii waweze kufanya kazi vizuri katika nchi yetu ni lazima kuhakikisha kwamba, Serikali tunajipanga kuhakikisha tunajenga vituo vya Polisi kila Kata, pia ni lazima tuwapelekee vitedea kazi. Mfano watu hawa hawana vitendea kazi, sasa watafanyaje kazi hiyo? Kazi wanayoifanya ni kubwa na ukizingatia uhalifu mkubwa unafanyika katika Kata zetu, tukiwaboreshea mazingira wakafanya kazi vizuri tutaweza kukomesha uhalifu kuanzia kwenye ngazi za Kata na hivyo kupunguza uhalifu mkubwa sana katika Wilaya zetu na level za Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni kuhusiana na wao kuweza kutenga pesa kwa ajili ya kutoa elimu. Tukiangalia katika maeneo yetu mengi, ukiangalia ni kweli wananchi wengi hawana uelewa kuhusiana na masuala ya ukatili, lakini kupitia Polisi Jamii tukitenga pesa kwa ajili ya elimu, hususan vijijini, wananchi wengi watapata uelewa kuhusiana na mambo yanapotokea ni wapi waende kushtaki na badala yake waache kuficha mambo yanayokwenda kufanya uhalifu katika maeneo yetu. Mfano, masuala ya ulawiti kwa watoto wetu, masuala ya ubakaji na ukatili wowote ule wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuongelea ni kumpongeza RPC wangu wa Mkoa wa Katavi kwa jinsi ambavyo anafanya kazi nzuri, kazi iliyotukuka. RPC wangu wa Katavi napenda kumpongeza sana kwa namna jinsi alivyo-deal na vijana wanaoitwa damu chafu, walikuwa wanatusumbua sana wananchi wa Katavi, lakini nampongeza kwa jinsi ambavyo ame-deal na vijana wale ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaenda kupata amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na ninawatakia utekelezaji mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)