Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita kwenye jambo moja tu la kujaribu kuelezea Sekta ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry). Sekta hii ilianzishwa huko Ulaya miaka mingi iliyopita, lakini ilianzishwa baada ya kuwa na sheria zake zote na kanuni zake ndipo wenzetu wale wakaanzisha hii sheria. Sekta hii ya ulinzi binafsi hapa kwetu Tanzania imeanza mwaka 1980 yaani miaka 43 iliyopita na hapakuwa na sera wala sheria wala GN.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii inafanya kazi chini ya mwamvuli wa ulinzi wa raia na mali zao na wakishirikiana na Jeshi la Polisi, lakini sekta hii inafanya kazi zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ulinzi wa watu (man guarding), kusindikiza hela (cash in transit), ulinzi wa mitambo (security installation) kama tunayoiona hapa Bungeni, huduma za zimamoto (fire rescue), upelelezi binafsi (private investigation), lakini na ulinzi wa watu binafsi ambao unaitwa bodyguard au kifupi bouncers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta sasa imeajiri ajira karibu 450,000 nchi nzima na hili ni jeshi kubwa sana. Linasaidia sana kupata kodi, lakini pia limesaidia ajira kwa vijana wetu. Sasa yako makampuni elfu mbili na zaidi, wakati ilipoanza mwaka 1980 ilikuwa na kampuni mbili tu, lakini sheria inazotumia ni za kiraia yaani sheria ile ya BRELA ya Usajili wa Makampuni, lakini Sheria ile ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zote hizi mbili ni za kiraia na hazifai kutumia kwenye sekta ya ulinzi binafsi kwa sababu sekta ya ulinzi binafsi ni karibu jeshi. Kwanza wanavaa kijeshi, lakini vile vile wanafanya kazi zile zile kama za polisi yaani kulinda raia na mali zao, lakini wanavaa sare za kijeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilianzia wapi hii sekta ya ulinzi binafsi? Ilitokana na ombwe mwaka 1980 wakati Mheshimiwa aliyekuwepo, IGP Philemon Mgaya alipomwomba Mheshimiwa Rais wakati ule Mheshimiwa Mwinyi, ili wapate fursa ya kulinda mali ambazo zilikuwa zimetaifishwa na Azimio la Arusha, wakarudishiwa wenyewe mwaka 1980 na kuondoa mgambo au polisi waliokuwa wanalinda mali hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pakawa na ombwe kubwa sana hakuna sasa walinzi na kwa vile ilikuwa haraka haraka Mheshimiwa Rais Mwinyi akatoa ruhusa ya kuanzisha sekta ya ulinzi na ndipo yakaja makampuni mawili la Group Four na Ultimate Security. Tangu hapo makampuni yamekua na kuendelea kufanya kazi ambazo nimezitaja hapo juu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa limejitokeza, yako mapungufu makubwa na mengi kwa sekta hii binafsi kuendeshwa bila sheria, kanuni wala miongozo. Kwa hiyo hatuna sheria wala mamlaka, kule nje kuna mamlaka (Private Security Industry Authority) kama vile EWURA au TCRA na kadhalika. Kwa kukosekana mamlaka hizo Private Security Industry Authority (PSIA), kampuni za ulinzi hazina madaraja. Ukitangaza kazi kampuni yoyote inaomba kazi bila madaraja. Tofauti na wakandarasi. Wakandarasi lazima uwe daraja la kwanza mpaka la saba, lakini makampuni haya hayana madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya ya ulinzi hayatambuliwi na mashirika ya kigeni yanayokuja hapa kwa sababu hayana certification, hayana uthibiti. Kwa hiyo makampuni haya yanazurura tu na yanapata tabu sana ikitokea kazi, kwa mfano, kwenye gesi kwenye oil, lakini pia kwenye migodi, lazima yajiunge na kampuni nyingine ya nje ili yapate kazi huko na imekuwa hasara kubwa sana na huduma kwa kampuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako matukio mengine mabaya sana katika sekta hii kutokana na kutokuwepo kwa sheria, kwa mfano, walinzi kushtakiwa kwa mauaji. Watu wamevamia lindo na askari ana bunduki, akipiga akaua jambazi anashtakiwa kwa mauaji, wakati polisi wakipiga jambazi wanapongezwa na kupewa vyeo, lakini wote wanafanya kazi zile zile. Hili ni pungufu moja kubwa sana. Bahati nyingine wakati fulani hawa askari walinzi binafsi walitoka kwenye Jeshi la Polisi au Jeshi la Wananchi. Wana vyeo vikubwa wale walinzi kuliko wale walinzi ambao wako pale pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wateja wa sekta kuumizwa na kukosa pa kukimbilia. Kwa hiyo wako watu sana waliajiri walinzi, lakini wakaumizwa. Walinzi kugeuka majambazi, wakawaibia wateja wao, lakini pia walinzi kuwadhulumu wateja kwa mfano, wizi wa Tawi la CRDB Azikiwe, mabilioni yalichukuliwa kwa mpango wa kupanga, lakini pia kesi ya Kasusula mnaifahamu, alitumwa kwenda kuchukua dola 2,000,000 akaondoka nazo kutokea Airport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wizi wa NBC Moshi mabilioni yalichukuliwa. Walinzi wa shule ya sekondari ya wasichana huko Tabora mchana wanalinda, usiku wanaenda wanawaibia wasichana, wakampiga mlinzi akafa, lakini walinzi kuuawa malindoni huko Temeke, walinzi waliuawa pamoja na mlinzi mmoja wa polisi na mlinzi mmoja aliyekuwa Sajenti Mstaafu wa sekta ya ulinzi binafsi. Mambo mabaya yalitokea pale. Yule Polisi aliyekuwa junior staff akazikwa kwa bendera ya Serikali huyu wa sekta binafsi akatupwa kama maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tiba ya kasoro hizi ni kuwezesha sekta ya ulinzi binafsi iwe na sheria yake. Iwe na mamlaka yake Private Security National Authority na hii itatokea tu kwa kuleta sheria ndani ya Bunge lako. Nilileta sheria ya sekta hii hapa mwaka 2016 na Serikali iliipenda sana ikaichukua sheria hiyo kwa mategemeo kwamba wangeiletea haraka iwezekanavyo lakini nashangaa mpaka leo haijaja. Kwa hiyo nimwambie Waziri nina mpango wa kukamata shilingi niende nayo Uyui aifutae huko Tabora Uyui ili atueleze, nataka tu commitment ya Serikali, Serikali itoe ahadi lini sheria hii itakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nakushukuru sana kwa muda wako. (Makofi)