Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii ya kuweza kuchangia mchana wa leo katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, pia kwa jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Waziri amezizungumzia hapa; kutafuta fedha mbalimbali katika kuhakikisha kwamba wanaboresha mifumo kwenye Jeshi letu hili la Polisi na majeshi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya. Mimi kama mdogo wako, nina imani kubwa sana na wewe na uwezo wako ulionao. Wewe pamoja na Naibu Waziri wako. Nataka nikusihi jambo moja tu Mheshimiwa Waziri kwamba utaandika kitabu chenye historia nzuri sana kama utafanya mabadiliko na mapinduzi makubwa sana katika kuliboresha Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi kwa sasa ukienda kwenye mawanda ya ajira utaona kabisa imepewa kipaumbele cha mwisho katika kutafuta ajira ama kuombwa ajira. Uki-compare na hapo mwanzoni Jeshi la Polisi lilivyokuwa lilikuwa na heshima kubwa sana. Leo hii tuna baadhi ya Maafisa wa Polisi wakubwa tu akiwemo IGP mwenyewe Wambura, wakiwemo akina Msangi, akina Mkumbo nimemwona hapo na wengine, akiwemo RPC wangu wa Shinyanga Mama yangu, ni mfano ulio bora kwa maafisa wenye weledi, wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kadiri siku zinavyokwenda Mheshimiwa Waziri mwenyewe umeona kumekuwa na sintofahamu ndani ya Jeshi la Polisi. Nidhamu, weledi, rushwa na mambo mengine. Haya yote kama alivyosema kaka yangu Mheshimiwa Shabiby hapo, ni kwa sababu maslahi ya Askari wetu ni mabaya mno. Askari ambao wanatulindia mali zetu, Askari ambao wana-risk maisha yao, leo hii Askari anayefanya kazi miaka 60, anapostaafu, anaondoka na Shilingi milioni 18. Hivi hata kama ni wewe Mheshimiwa Waziri, usingefurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hata pension utaona, mtu aliyetumikia Taifa kwa miaka zaidi ya 60 anaondoka na Shilingi 40,000. Ndiyo maana nikatanguliza kukuomba kaka yangu, utaandika kitabu kizuri sana kama utaenda kusimamia vizuri kwa weledi maslahi ya hawa watu ili waweze kufanya kazi kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye Jimbo langu la Msalala. Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu, lakini Halmashauri hizi kwa maana ya Ushetu, Msalala na Kahama Manispaa; Msalala tuna OCD, lakini OCD yule hana gari, OCD mwenyewe anakwenda kukagua tukio kwa bodaboda, akishuka pale amejaa vumbi, hata haeleweki. Nakuomba kaka yangu kwa uchungu mkubwa, maeneo yetu hasa sisi tunaotoka kwenye mazingira ya mgodi, cha kushangaza, hawa hawa ndio Askari ambao wanaenda kulinda mali, migodi mikubwa hii. Hivi Mheshimiwa Waziri unashindwa kufanya kikao hata na hawa wawekezaji wakubwa kwenye maeneo yetu kama Barrick kuwaomba walau wachangie magari kwa ajili ya maaskari wetu ambao wanalinda mali zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia askari hawa wamekuwa wakidharaulika kwenye maeneo mengine. Leo hii wanaacha kufanya kazi ya uaskari, kwenye maeneo yetu utakuta askari ndiyo mchimbaji anaingia kwenye duara. Kwa nini? Kwa sababu maisha ni magumu, hajielewi. Boresha maslahi Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia habari ya rushwa. Rushwa inatokea kwa sababu ya mazingira magumu. Nenda kaimarishe mifumo kwenye Jeshi la Polisi. Siyo kila kitu kinaweza kikafanywa na watu wenyewe. Leo tunazungumzia habari ya tochi. Kwani hakuna mfumo, hakuna system ambayo unaweza ukaifunga Mheshimiwa Waziri? Cameras au kukawa na checking point walau kutoka hapa kwenda Dar es Salaam kukawa na checking point mbili? Funga camera, funga vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kuonesha kwamba vinaweza kulinda usalama wa barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nizungumzie habari ya magari. Naomba sana, kwenye Jimbo la Msalala, Halmashauri ya Msalala, Halmashauri ya Ushetu, tusaidie magari. Bado mpaka sasa utaona, hata kwenye misafara hii, magari yaliyoletwa yale ya Land Cruiser wanazotumia ma-OCD, ma-RTO bado zimechoka mno. Unakuta Land Cruiser iko kwenye msafara, tairi inatembea inacheza inakatika, inakatika, inakatika. Naomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii, pia peleka maombi kwa Mheshimiwa Rais aone namna ya kuweza kusaidia kununua magari mapya kwa ma-OCD wetu kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumze habari ya vituo vya Polisi. Nampongeza sana RPC wangu wa Mkoa wa Shinyanga. Huyu mama anafanya kazi kubwa sana. Nimekuwa nikilia hapa toka mwaka 2022 kupatiwa vituo vya Polisi maeneo yetu hayo ni maeneo hatarishi sana maeneo ya migodi. Mama ameweza kufanya jitihada nami mwenyewe nimemchangia, sasa hivi tunanyanyua vituo vitatu vya Polisi Isaka, kituo kimoja kinanyanyuka na bado hakijakamilika. Naomba kwenye bajeti hii upeleke fedha tukamalize Kituo cha Polisi cha Isaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunanyanyua kituo kingine cha Polisi Kata ya Ngaya, tumeezeka, tunatakiwa tumalizie. Naomba muunge mkono RPC wako wa Shinyanga tukamalizie Kituo cha Polisi hiki. Tunajenga Kituo cha Polisi kingine Kata ya Mwaluguru kitahudumia kata tatu. Tayari kiko kwenye lenta. Nakuomba peleka fedha twende tukamalizie vituo hivi. Huyu mama ameona aanze jitihada mwenyewe binafsi kuhakikisha ya kwamba tunakuwa na vituo vya Polisi kwenye maeneo yale ili tuweze kulinda usalama wa raia na mali zao kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hali ya vituo vya Polisi kwenye maeneo baadhi, ni mbaya mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kata ya Busangi tuna kituo cha Polisi lakini kimebomoka upande. Askari wamekaa mle ndani kwenye gofu. Muda wowote linaweza likadondoka. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uone namna ya kupeleka upeleke fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie habari ya NIDA.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hili la mwisho. Suala la NIDA, bajeti iliyopita ya mwaka 2022 nilizungumza hapa, nikasema suala la NIDA ni changamoto kubwa mno na nikatoa mfano nikasema mnazidiwa hata na Klabu ya Yanga! Leo hii kwenye maeneo yetu hakuna jambo lolote linaloweza likafanyika mpaka mtu awe na kadi ya NIDA. Mmefeli wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe ni rafiki yangu, ni kaka yangu, lakini kwenye hili mimi nashika shilingi. Mheshimiwa Shangazi uko hapo, uniandike. Nashika shilingi ya mshahara wako mpaka uje unieleze, mna mkakati gani wa kuhakikisha ya kwamba mnatatua tatizo la kadi za NIDA?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)