Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakuu wote wa vyombo vya usalama kwa kazi nzuri wanazofanya, lakini nami leo nina michango yangu tu midogo midogo. Nitaanza na Uhamiaji. Pale Gairo mlisema tuwatafutie kiwanja kwa ajili ya kujenga ofisi. Kiwanja kipo, tunasubiri ofisi ije uhamiaji. Mwakani nikija, nakuja kivingine, naomba hiyo ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni masuala ya Zimamoto. Nataka kujua tu, hivi ninyi Mawaziri mnavyopewa hivyo vyeo, mnakuwa waoga, mnakuwa kama sisi tu huku hatuongei na kwenye Mabaraza ya Mawaziri, mnakuwa wenzetu au mnakuwa vipi? Mimi unajua sielewi kabisa! Hili suala la Zimamoto liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Ukijenga jengo, yako majengo yanatoa mpaka Shilingi milioni 40, Shilingi 30, Shilingi milioni tano, wanalipia Zimamoto hata jengo hujaanza kujenga. Kwenye magari, kuna kodi ya Zimamoto, lakini ukiangalia kwenye miji yetu, magari ya Zimamoto hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikupe mfano wa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi ina majengo mapya mengi, majengo marefu mengi, ukienda kuangalia pale vigari vya zimamoto vile, hata moto ukiwasha na nyasi havizimi. Tatizo ni liko wapi kwenye upande wa Zimamoto? Ukienda kule Mtumba kuna majengo ya Serikali. Hata kama yale majengo yamewekewa vifaa vya Zimamoto, lakini yako wapi magari ya Zimamoto? Hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Dar es Salaam, ukienda kule Tegeta, wapi, hakuna. Sana sana utayakuta magari ya watu binafsi. Kuna shida gani na fedha ziko nyingi za zaidi ya kununua magari ya Tanzania nzima? Mfano, pale Gairo, amekuja Mheshimiwa Rais, ameongea na wananchi pale, amesema Gairo ijengwe Mahakama, imeshajengwa. Gairo yajengwe madaraja, yamo kwenye bajeti; Gairo ijengwe mfereji wa kuzuia mafuriko, imeshajengwa; Gairo iletwe gari la Zimamoto kwa sababu ni katikati ya Dodoma na Morogoro kwa ajili ya accidents zinazotokea pale barabarani, lakini mpaka leo hata mpango hamna. Mmeleta watu wa Zimamoto zaidi ya sita. Sasa mnataka wazime na mikono?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mtuambie basi, mtupe course wenyewe tu, hamna haja ya kuweka watu wa Zimamoto pale. Kama watu wa Zimamoto wako sita, wanapewa mshahara, lakini hakuna chombo chochote cha kufanyia kazi. Hilo ni agizo la Rais. Mheshimiwa Waziri, nataka ukija uwe na majibu ya kutosha, kwa sababu wakati ule alikuwa Waziri, Mheshimiwa Simbachawene. Sasa sifahamu kila akija Waziri mpya na mambo yanabadilika? Nilikuwa naliomba sana hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la accidents zinazotokea hasa kwenye magari yetu, mabasi. Mimi ni msafirishaji wa zaidi ya miaka 27 sasa, nafanya hiyo kazi. Kuna vitu vingine hamtaki kushirikisha wadau. Mkiita wadau, mnaita wapiga debe, wale wadau wahusika kabisa hamtuiti tuwapeni ushauri. Toka enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere, akaja Mheshimiwa Mwinyi, akaja Hayati Mkapa, mpaka leo, ukienda LATRA kuchukua leseni ya usafirishaji; kwa mfano, kama unatoka Dar es Salaam kuja Dodoma unapewa na kitu kinaitwa time table kwamba gari itatoka Dar es Salaam saa ngapi, itafika Chalinze saa ngapi, itafika Morogoro saa ngapi, itafika Gairo saa ngapi, na itafika Dodoma saa ngapi? Zile time table zinawekwa kulingana na speed ambayo unatembea, unawekewa na kituo, ukiingia dakika tano, utoke, yaani kila kitu inaeleza kwamba gari inatakiwa ifike saa ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye mkaleta speed governor, zimefanya kazi, zikafeli kwa sababu madereva wanazichezea, wanaweka switch, hazina kazi yoyote. Zimefeli speed governor. Sasa hivi mmeleta VTS. Nayo kuna kipindi inafanya vizuri, kuna kipindi nayo inachezewa. Sasa tena nimekusikia Waziri tena unarudisha tena speed governor ambayo ilifeli mwanzoni. Msifanye mchezo jamani. Nani atanunua kila siku? Eti mtu una gari 60 ukanunue speed governor shilingi 1,800,000 kwa magari 60 ambayo ilishafeli na unajua kabisa dereva ataichezea. Kwa nini msiweke utaratibu wa kufuata time table?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mweke speed 95. Haya magari ya sasa hivi siyo speed 80 na hata ukiangalia Sheria ya Traffic, speed 80 haiko kisheria. Inasema iwapo TANROADS kama wataweka kibao cha speed 100 ndiyo hizo hizo, lakini sisi tumeweka kichwani kwamba ni speed 80. Wekeni speed 95. Magari ya sasa hivi hayatumii breki tu, yanatumia na umeme ambapo ni kitu kinaitwa retarder kuwa kama breki. Wekeni speed 95, fuateni time table, gari ikitoka Dar es Salaam, Chalinze imewahi weka pembeni gari, piga faini. Inakuja mpaka Morogoro, gari imewahi, piga faini, weka gari pembeni isiondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi hapa niliona mabasi yamekamatwa pale Same. Askari wa Same walikuwa wanafanya kazi vizuri sana, lakini kuna baadhi hata ya Wabunge hapa wakaanza kupiga kelele, wananchi wanateseka. Siyo wanateseka, Polisi wafanye kazi yao bila kufuata watu wa siasa. Gari imewahi, time table inapokuonesha, weka pembeni piga faini. Dereva baadaye atapigwa na abiria, akionekana anawahi wahi tu, mwishowe abiria watambadilikia. Watampiga. Hiyo ndiyo kumaliza accidents. Sasa kama tuna Polisi kila kona na wanashindwa kuangalia time table na time table za kila gari wanazo, haiwezekani kitu kama hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masuala ya kikotoo. Kwenye Jeshi la Polisi, tunapata taabu, tunawaona ndugu zetu, jamaa zetu, wako kama pale Gairo, wako sehemu nyingine. Kikokotoo wanachotumia cha mafao ni kikokotoo cha watumishi wa Umma. Kwa nini wasitumie kikokotoo kama wanachotumia JWTZ au TISS? Leo Askari anamaliza kazi yake, amefanya kazi miaka 30 anakwenda anakuwa masikini wa kutupwa, anakufa hata kabla ya siku zake. Hiyo lazima tufanye haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata uhamisho. Utakuta kwenye uhamisho miaka 10 mnahamisha Askari hapa, mnapeleka pale, miaka 10 hamjawalipa. Wako wanaodai mpaka Shilingi milioni 100, wako wanaodai mpaka Shilingi milioni 80. Kwa hiyo, kwenye Wizara mnazidi kuongeza mzigo. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, taarifa kutoka kwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe tu taarifa, licha ya kwamba wanapewa kwa kama watumishi wengine na siyo kama JWTZ, lakini pia hata hayo mafao yao kwa maana ya michango wanacheleweshewa kupeleka. Wakistaafu wanaenda kufuatilia mafao yao wanaambiwa, hawawezi kupewa mafao mpaka watoe riba. Yaani wakatwe wenyewe ile adhabu ambayo wanatakiwa walipie waajiri wao ambao ni Serikali, wanalipa wao wenyewe. Kwa hiyo, unakuta Askari hawa wengine mpaka wanafariki hawajapewa mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe tu hiyo taarifa iwe kwenye kumbukumbu yake.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Shabiby, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nilikuwa naitaka hiyo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa Askari saa nyingine mnasema wanakula rushwa, hata mimi ningekuwa Polisi ningekula, kwa style hii. Ndiyo ukweli huo. Lazima mafao yao jamani wapate. Unajua kuna vitu vingi sana tunachangia tu, tunachukia, lakini tunaangalia kuanzia mishahara yao? Tunaangalia kuanzia maslahi yao? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AHMED M. SHABIBY: Hiyo ni kengele ya mwisho Mheshimiwa?

MHE. AHMED M. SHABIBY: Ni kengele ya pili?

MWENYEKITI: Ndiyo.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Dah, haya bwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono. (Makofi)