Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kulifanyia Taifa letu na mojawapo ya sehemu ya kazi nzuri ni kututeulia viongozi makini kama Waziri wetu wa Mambo ya Ndani pamoja na Naibu wake na timu yake nzima kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kazi inakwenda vizuri kwenye Wizara hii mchango wangu utakuwa mfupi. Nimetazama majukumu ya Wizara hii chini ya Government Notice ile namba 383 na namba 385 ya mwaka 2021 kama ambavyo imeboreshwa na Government Notice namba 334 ya Julai, 2021. Majukumu ya Wizara hii ni mapana sana, lakini yako summarized pale kwamba ni utekelezaji wa sera za usalama wa umma (implementation of policies on public safety).

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hili si jukumu dogo kwa sababu ni jukumu ambalo wateja wake kuanzia mwanzo mpaka mwisho ni binanadamu. Kama ambavyo watu wanasema kazi ya kuongoza binadamu siyo kazi ndogo, wakati mwingine kuongoza vitu ambavyo havina utashi au haviko hai ni rahisi zaidi kuliko kuongoza binadamu. Kwa hiyo taasisi zote hizi ukianzia Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto zote zinashughulikia binadamu, tena binadamu wenye changamoto au binadamu walioko katika changamoto za matukio mbalimbali. Kwa hiyo si jambo ambalo ni rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukubali kwamba juhudi zote hizi za uchumi za kukuza uchumi na ustawi wa jamii ambazo Serikali inaendelea nazo bila Wizara hii kukaa sawa sawa hatutaweza kufaidi matunda yake. Tutaomba madarasa yatajengwa lakini vibaka watakuja wataiba madirisha ya kisasa. Tutaomba dawa zitakuja wezi wataiba, mateja wa madawa ya kulevya watavuruga Nchi. Kwa hiyo, Wizara hii ina umuhimu mkubwa sana tofauti ambavyo tunadhani kwamba labda kazi yao ni kukamata na kuachia watu. Mambo yote ya msingi haki za binadamu zinaanzia Wizara hii, haki jinai zinaanzia Wizara hii. Sijui kufanya siasa, hata sisi kufanya si lazima Wizara hii ikae sawa sawa ili tuweze kufanya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mpira, Yanga wasingecheza vizuri jana kama kungekuwa hakuna usimamizi wa Wizara hii. Tuende mbele hata suala la sovereignty, uhuru wa Nchi ambaye inakupa right to govern na responsibility to protect (haki ya kutawala na wajibu wa kulinda). Bila kuwa na Wizara hii makini ikalinda watu wako huwezi ukahesabiwa kama ni nchi huru kama watu wanakufa na kuuwawa kila siku kama kuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la kujiuliza hapa ni kwamba hawa tunaowakabidhi dhamana kubwa nanma hii hali yao ikoje? Hali yao kibajeti kwa mfano iko namna gani? Kamati imeeleza hapa kwamba ukienda kwenye miradi ya Wizara hii stress ni msongo wa akili imeeleza taarifa ya Kamati kwamba tumekwenda Handeni kule kwenye kile chuo cha pale Chogo kwa kweli kinatia msongo. Hali siyo nzuri kwa sababu hakuna kinachoendelea pamoja na bajeti kutengwa. Ukienda kituo pale ofisi za uhamiaji pale Babati hakuna kinachoendelea, ukienda kile kituo cha uhamiaji kule Kichakamiba halafu kina nafuu kidogo lakini bado, ukienda Chuo chetu cha Polisi Moshi bado, ukienda gereza kule Kilosa bado, hata ukija kwenye Gereza la Jimbo langu la Mwanga bado hali hairidhishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninachokiomba sana ni kwamba fedha zinazotengwa za miardi ya maendeleo kwa Wizara hii ziende tena ziende kwa wakati, vinginevyo tunajiingiza kwenye mazingira ambayo sio mazuri. Hali ikoje kimaslahi, malalamiko juu ya stahiki za askari yamekuwa mengi sana, kila siku wapo kwenye maswali na majibu tunayaona. Hili suala linahitaji kutazamwa sana kwamba tusibaki tubakakia na askari wetu ambao wanaishi kwenye malalamiko kila siku. Suala lingine ambalo ni la muhimu katika taasisi za Wizara hii ni suala la mafunzo na vifaa, taasisi zilizoko chini ya Wizara hii kama nilivyosema zina-deal na wahalifu zina-deal na wageni zina-deal na majanga. Sasa ili uweze kushughulika na mambo kama haya na bado utimize sheria lazima mafunzo na vifaa uwe navyo vya hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweka umuhimu mkubwa sana katika suala la haki jinai ndiyo maana akaunda na Tume ambayo ina wabobezi inazunguka kufanya kazi nzuri, lakini masuala yote yanaanzia kwenye Wizara hii. Mahakama haziwezi kufanya vizuri kwenye mambo ya uhalifu kama Wizara ya Mambo ya Ndani haifanyi vizuri. Tutaweka watu ndani, Magereza watatoka bado majambazi kama suala la urekebu halifanyiki vizuri. Kwa hiyo, tunapokuja kwenye suala la bajeti katika Wizara hii kwa kweli ni vizuri tukatilia kipaumbele kama ambavyo tunatilia kipaumbele Wizara zingine ambazo labda matokeo yao yanaonekana kwa macho, maana ukisema kilimo utaona mashamba kwa macho na chakula utakiona, ukisema madini utaona madini yanachimbwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa wanashughulika na jambo ambalo pengine halionekani kwa macho lakini lina umuhimu mkubwa sana ili hao mengine yaweze kufanyika. Liko suala ambalo limesumbua, Tanzania tu lakini limesumbua hata Dunia hasa Nchi za Afrika na Afrika Mashariki kwa sasa. Ni juu ya suala la hizi taasisi za dini pamoja na NGOs ambayo zinafanya mambo ambayo kwa lugha ya mtaani tunasema ni ya hovyo, lakini tuseme ni mambo ambayo ni kinyume cha sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo pamoja na mengine ambayo yapo lakini tatizo moja wapo ni suala zima la kuchuja hizi taasisi wakati wa usajili. Tunafahamu kwamba sheria inataka kabla taasisi haijasajiliwa idhaminiwe na taasisi nyingine ambayo tayari iko inafanya kazi. Sasa udhamini huu uko wa namna gani, siyo suala tu la kusaini form tu ambalo nadhani ndiyo linalofanyika. Umefika wakati sasa udhamini huu uende na uwajibikaji kwamba wacha niitolee mfano dini yangu mimi ili ni rahisi zaidi. Kama mimi nakuja nataka kusajili taasisi ya kikristo, nafikiri umefika wakati sasa Wizara ku-rank zile taasisi za kikristo ambazo tayari zipo, zile ambazo zimeshadumu miaka mingi na zina sifa ya kudhamini taasisi mpya ndiyo zipewe wajibu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhamini unakuaje? Lazima kusaini form ya kusema mimi so and so wa taasisi fulani nimesoma Katiba ya mwombaji na mafundisho yake, Constitution and Doctrines, nimeridhika kwamba kwa Katiba hii na kwa mafundisho haya huyu mwombaji anaweza akaendesha taasisi au kanisa whatever la Kikristo. Sasa akishasaini hivyo tukakubaliana siku naye akianza kuficha watu porini tutamuuliza, atakuwa ni sehemu ya kutusaidia katika ushahidi na katika kuiwajibisha hii taasisi kwamba mbona wewe katiba yako ilisema unafanya haya na haya, haya ya kupeleka watu porini ya kushindisha watu njaa, mbona yalikuwa hayapo katika katiba yako wala kwenye doctrines zako. Usipofika hapo tutaendelea kupata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina fahamu kwamba utaratibu huu unafuata katika maana ya udhamini lakini hauendi deep kwenye kuhakikisha kwamba yule anayedhamini ni nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakati tunaingia Council of Legal Education tuwe Mawakili ilikuwa lazima upate referee, lazima upate udhamini wa Wakili lakini siyo kila Wakili, ni Wakili ambaye amefikia level fulani ya seniority ambayo Mahakama inamuani kwamba huyu akituambia huyu kijana anafaa mruhusuni afanye mtihani wa uwakili anaweza, siyo kila mtu tu. Kwa hiyo, hili tunahitaji kuliangalia kwa makini sana lisije likatuvurugia Nchi kama ambavyo tumeona sehemu zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo lakini nisisahahu kupongeza taasisi zilizoko chini ya Wizara hii. Nikianzia Jimboni kwangu Mwanga, Polisi pale Mwanga jengo lao wamelikarabati kwa kuchanga kutoka kwenye mishahara yao na kuwakamata wadau wengine kama sisi, lakini wamelikarabati vizuri. Wananchi wa Jimbo la Mwanga hasa Tarafa ya Usangi wameungana wakajenga Kituo cha Polisi cha kisasa kabisa na hili nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba baada ya kukupitishia bajeti yako twende ukakitazame kile kituo ili tujenge na vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho pia niwapongeze Idara ya Uhamiaji, mradi mmojawapo ambao unafanya vizuri ni kile Chuo pale cha Kichakamiba taarifa ni kwamba walianza kwa kukatana mishahara wachange wao wenyewe kutoka mishahara yao kuanza kujenga na ndiyo maana ile taasisi iko vizuri sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono hoja na nawapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)